UtanguliziMnamo mwezi Juni mwaka 2006, niliwahi kuandika makala katika blogu hii kuhusu maeneo tengefu ya RAMSAR. Katika makala hiyo niliandika hivi :
”Maeneo ya Ramsar ni sehemu ya ardhi oevu duniani, (wetlands) ambayo yana umuhimu wa pekee duniani katika suala zima la uhifadhi wa mazingira. Ardhi oevu ni ile ardhi ambayo kwa msimu wote wa mwaka huwa na unyevunyevu. Jina hili "Ramsar" linatokana na mji wa Ramsar nchini Iran ambapo ndipo mkataba wa kutunza maeneo ya ardhi oevu duniani ulisainiwa, mnamo mwaka 1971. Kwa hiyo basi, mwaka 1971 ndipo yalipofanyika maamuzi ya kulinda maeneo ya ardhi oevu dhidi ya uharibifu, ili yaweze kutumika katika shughuli endelevu, kama vile vyanzo vya maji. Mpaka sasa, kuna mataifa 152 duniani yaliyotia sahihi mkataba huu wa kulinda ardhi oevu, ikiwemo Tanzania. Kuna maeneo tengefu 1608 ya Ramsar duniani yanayochukua ukubwa wa hekta milioni 140, kati ya haya Tanzania tuna maeneo manne tu. Maeneo haya ni ardhi oevu ya Muyovozi katika mto Malagarasi-Kigoma (13/04/2000), ardhi oevu ya bonde la Ziwa Natron-Manyara (04/07/2001), bonde la mto Kilombero-Morogoro (25/04/2002) na bonde la Rufiji-Mafia hadi Kilwa-Pwani (29/10/2004). Katika mabano ni tarehe ambazo maeneo hayo yaliingizwa katika orodha ya maeneo tengefu ya Ramsar. Kwa hiyo, maeneo haya yanalindwa na mikataba ya kimataifa, ambapo hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uwindaji na ukataji miti.”
Makala nzima inapatikana katika kiungo hiki: http://jadili.blogspot.com/2006_06_01_archive.html
HOJAKatika makala hii najibu hoja za mwandishi wa makala katika gazeti la Tanzania Daima la tarehe 29/01/2008 kama nilivyonukuu katika makala tangulizi hapo chini.
Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya Tanzania imekuwa na mazungumzo na kampuni ya Tata Chemicals ya India kuhusu uanzishwaji wa kiwanda cha usindikaji magadi katika eneo la Ziwa Natron, ambalo linalindwa na mikataba ya kimataifa, ambayo inazuia shughuli zozote za kiuchumi (ukiondoa utalii) ambazo zina athari kwa mazingira katika maeneo haya. Serikali ya Tanzania imeridhia mkataba wa Ramsar kuhusu ulinzi wa maeneo oevu, hivyo kutaka kulitibua eneo la ziwa Natron kwa kujenga kiwanda ni kukiuka mkataba huo.
HOJA YA MANUFAA YA MADINI
Mwandishi wa makala anasema kwamba madini ya nchi yetu hayajatunufaisha vya kutosha, kwa hiyo tunahitaji kuchimba magadi ili kujinufaisha kiuchumi. Sijaelewa mwandishi alimaanisha nini anapotaja ’madini’ na kuondoa magadi katika kundi la madini. Mimi nasema kwamba, hata magadi ni madini (sodium) ambayo huwepo katika mchanganyiko (compounds and mixtures) mbali mbali ambapo katika taaluma ya kemia yana alama (Na). Sasa basi magadi haya ya ziwa Natron yaweza kuwa ”Sodium Sulphate” (NaSO4), ”Sodium Carbonate” (NaCO3) , ”Sodium Chloride” (NaCl), Sodium Bisulphate NaH(SO3)2 ama Sodium Bicarbonate NaH(CO3)2, na kadhalika. Kwa hiyo aelewe kwamba kama kuna malalamiko ya kimazingira ama ya kipato kidogo kutokana na madini basi magadi hayawezi kabisa kuwekwa kando, kwa sababu nayo ni madini kama nilivyoonyesha hapo juu. Sodium Chloride (chumvi tunayotumia), huchimbwa kule Uvinza Kigoma kwa wingi, je yamenufaishaje taifa kimapato? Anaweza kuanzia hapo kufanya upembuzi, ili kuweza kufikia mwafaka wa manufaa ya madini kwa ujumla.
HOJA YA KIPATOKwamba tunachimba magadi ili kukuza kipato cha taifa sio hoja sana kwa sababu Tanzania inaweza kutafuta vyanzo vingine vya mapato kufidia kile ambacho tutapoteza kutokana na kutochimba madini haya. Suala la mazingira lazima lipewe kipaumbele Iwapo tungekuwa tunaangalia suala la kipato, basi ule mradi wa kamba (prawns) wa kule Rufiji nadhani ungeendelezwa kwa sababu nao likuwa na kipato kizuri tu. Tusisubiri kupigiwa kelele na mataifa makubwa na kushtuka kwamba kweli mradi una athari. Mwandishi wa makala anasema kwamba iwapo tutachimba magadi hayo tunatarajia kuingiza dola milioni 800,000 kwa muda wote wa mradi huo. Hata kama itakuwa ni kwa mwaka, sidhani kwamba itakuwa busara kuchuuza mazingira kwa pesa ndogo namna hiyo. Ambacho haelewi hapa huyu mwandishi ni kwamba ukokotoaji wa mahesabu ya mradi huu hufanywa na mwombaji ama mwendelezaji wa mradi, kwa hiyo lazima avutie kwake ili kutupendezesha na kutushawishi. Katika mfano wake, anasema kwamba Kenya inazalisha magadi kwa wingi sana tangu mwaka 1910, ila fedha ziotokanazo na magadi hayo huwafaidisha Waingereza zaidi kuliko Wakenya! Lahaula! Sasa kama fedha za Wakenya zinawafaidisha Waingereza, je tuna uhakika gani kama hizi za kwetu ambazo tunatarajia kuzipata kutokana na kuchimba magadi hazitaishia kuwafaidisha Wahindi? Ni nani katika serikali kakaa kupiga mahesabu na kupata jibu kwamba ni kweli tutaingiza kipato hicho katika mfuko wetu?
HOJA YA AJIRAKwamba mradi huu utaleta ajira 500 za moja kwa moja na nyingine 2000 zisizo za moja kwa moja sio hoja yenye mshiko ambayo inaweza kusimama na kuhalalisha utoaji kafara wa eneo la ziwa Natron. Suala ni kwamba kuna vyanzo vingine vingi tu vya ajira ambavyo vikipewa kipaumbele vinaweza kuajiri watu zaidi ya hao 2500 kwa muda mrefu ambao watatokana na mradi huu. Kilimo hakijapewa kipaumbele, ingawa kinadaiwa kwamba ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Karibu kila mkoa katika Tanzania unalima zao fulani, je tumechukua hatua gani kuona kwamba kila mkoa unafaidika na kilimo hiki? Iwapo kila mkoa unalima, na chukulia kwamba kila mkoa unatoa wakulima bora 1000 tu katika maelfu ya wakulima wote, tutakuwa na jumla ya wakulima 26,000, yaani mara kumi ya waajiriwa wa huo mradi. Sasa kwa nini tusiendeleze hapa penye ajira nyingi zaidi? Uvuvi nao umesahauliwa. Ni chanzo kizuri sana cha mapato yenye uhakika kwa nchi yetu Tanzania ambayo imejaa maji yanayoruhusu uvuvi kila kona. Kuna Ziwa Nyasa, Tanganyika, Viktoria, Rukwa na kadhalika. Je tumechukua hatua gani kuhakikisha kwamba maji haya yanaajiri watu wa kutosha? Tuna bandari ngapi za kujivunia ambazo zinafanya kazi kwa kiwango cha kuridhisha? Hatujayatumia maji haya vya kutosha katika uvuvi,usafirishaji na matumizi mengine, kwa nini?
KANUNI ZA TATHMINI YA ATHARI ZA KIMAZINGIRA (EIA)
Ufafanuzi wa Mradi
Mpaka sasa, kwa mujibu wa taarifa za serikali, kampuni ya Tata Chemicals bado haijakamilisha suala zima la upembuzi yakinifu kuhusu mradi huu kuangalia kama una madhara ama la, kwa hiyo basi bado kufikia hatua ya kuuweka mradi huu wa magadi ya Ziwa Natron katika miradi salama kimazingira. Taarifa hiyo inapatikana katika tovuti ya baraza la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) katika kiungo hiki, Tangazo la NEMC. ”http://www.nemctan.org/publichearinglnatorn.doc”. Na kwa mujibu wa kanuni za EIA, iwapo mradi husika unazua ”kelele na manung’uniko” toka kwa jamii, basi hicho ni kiashiria kwamba mambo siyo sawia.
RIPOTI YA ”EIA”Binafsi nikiri kwamba, kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu sijaipata na sijaipitia ripoti ya tathimini ya athari za kimazingira ambayo imefanywa na kampuni husika inayoomba kibali cha kuchimba magadi. Pamoja na hayo kama eneo husika linalindwa na sheria za kimataifa, ripoti hii haitakuwa na maana sana kwa sababu tayari eneo la Ziwa Natron haliruhusiwi kuendelezwa kwa shughuli za kiuchumi kwa mujibu wa mkataba wa Ramsar, kwa sababu ya umuhimu wake kwa bioanuwai. Kwamba eneo hili lina ndege aina ya korongo wadogo ”Lesser Flamingo” ambao huishi maeneo hayo na kutegemea eneo hilo kwa maisha yao.
Kwa habari zaidi pitia hapa, hapa na hapaHuo ndio msimamo wangu kama mtaalamu wa mazingira.
No comments:
Post a Comment