6/13/18

UTETEZI WA MRADI WA MAGADI UNAENDELEA...

Magadi ya Ziwa Natron changamoto ya uchumi
Na Amana Nyembo
MRADI wa uchimbaji magadi katika Ziwa Natroni, mkoani Arusha, ni moja ya miradi ya viwanda ambayo serikali imeipa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) jukumu la kuuendeleza kwa ubia na sekta binafsi.
Mbali na uchimbaji wa magadi, miradi mingine ni uchimbaji wa makaa ya mawe, umeme wa Mchuchuma na chuma cha Liganga - yote ikiwa Arusha.
Akizungumza hivi karibuni Dar es Salaam, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Gideon Nasari, anasema mradi huo utakuwa na faida kwa Watanzania, kinyume kabisa na madai ya wanaharakati kuwa utaharibu korongo (flamingoes), ndege maarufu waishio huko.
Nasari anasema mradi huo utasaidia kuvutia utalii na kuwafanya wananchi wa eneo hilo kufaidika zaidi na baadhi ya miundombinu itakayotengenezwa, kwani hauwezi kuharibu mazalia ya korongo. Wamelichunguza hilo baada ya kutathmini na kutilia maanani mawazo na hofu za wadau.
Kwa sababu waendelezaji wa mradi wameamua kuhamisha eneo la kiwanda lililopangwa kwenda kilometa 32 kutoka Natron na eneo oevu (ramsar site) upande wa mashariki wa ziwa hilo.
Kiwanda kitakuwa mbali na Natron, kwani mazalio ya korongo yapo upande wa kaskazini na kusini sehemu ambayo ndege hao hawatajua nini kinafanyika upande mwingine.
“Hakutakuwa na njia yoyote ya usumbufu kwa korongo hao muhimu na wazuri…si hivyo tu, lakini kuwapo kwa shughuli za wanadamu eneo hilo kutasaidia kuwafukuza wanyama wengine wanyemeleaji,” anasema.
Akizungumzia mfumo wa kemikali katika ziwa hilo, Nasari anasema magadi kutoka ziwani yatavutwa kwa pampu kilometa 32 hadi kwenye mtambo ambako asilimia 23 ya magadi itatolewa na yanayobaki yatarudishwa ziwani.
“Kiwango cha malighafi ya magadi (brine) kitakachovunwa kwa mwaka ni sawa asilimia 0.12 ya jumla ya magadi yote yatakayoingia ziwani kwa mwaka, na hakutakuwa na mabadiliko makubwa yatakayoharibu viumbe hai (cyanobackeria) ziwani humo.
Hata hivyo, anaeleza kuwa mradi huo katika kiwanda hautachukua maji kutoka vyanzo vyovyote vinavyopeleka maji ziwani, kwani mradi una mpango wa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vyanzo vingine vya maji safi na salama kwa ajili matumizi ya binadamu na kiwandani.
“Inatarajiwa kwamba kitachimbwa kisima chenye kina cha mita 100 umbali wa kilometa 30 kutoka ziwani bila kuharibu mfumo wa mazingira…ujenzi wa kiwanda hicho utawahakikishia wananchi maji safi na salama kwa matumizi yao na mifugo,” anasema.
Hata hivyo, mradi wa Ziwa Natron unakisiwa kugharimu dola milioni 450 za Kimarekani, gharama ambazo zinajumuisha kiwanda cha kusindika magadi, pia kijiji cha wafanyakazi wa kiwanda hicho na uimarishaji wa miundombinu na mifumo yake.
Anaeleza miundombinu hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Longido hadi Natron na reli ya Arusha kupitia Natron sehemu ya kiwanda.
“Kutakuwa pia na njia ya kusafirisha umeme kutoka Arusha hadi eneo la kiwanda, lakini pia upanuzi wa Bandari ya Tanga na uimarishaji wa reli ya Tanga hadi Arusha utafanyika,” anasisistiza.
Mradi wa magadi kwa kuanzia utazalisha tani 50,000 za magadi na baadaye kuongezeka hadi tani 100,000 kwa mwaka. Kutokana na kuwapo kwa kiwanda hicho, nafasi za ajira ya kudumu zinatarajiwa kupatikana 500 na nyingine ambazo si za kudumu ni nafasi 2,000.
Anasema mradi huo unatarajiwa kuingiza faida ya dola 300 kwa mwaka kutokana na mauzo ya magadi yanayotoka katika Ziwa Natron.
Kuhusu uharibifu wa mazingira katika eneo hilo, anasema shughuli zote zitakazofanyika kwenye mradi zitaongozwa kwa mapendekezo na maelekezo ya taarifa za tathmini ya kimazingira na kijamii (environmental and social Impact assessment) kama ilivyopitishwa na serikali ya Tanzania.
Anasema hiyo ina maana kila tahadhari itachukuliwa kuhakikisha hakuna uharibifu wowote wa mfumo mpana wa mazingira.
Nasari anafafanua kwamba wananchi waishio katika eneo la mradi watapata nishati ya umeme na hivyo kupunguza kasi ya ukataji miti, vilevile umeme utasaidia usambazaji wa maji safi na salama kwa wananchi wengi. Teknolojia itakayotumika kusamabaza maji pia itadhibiti uchafu wa maji taka, kwani itakuwa ya kisasa na wala haitachafua mazingira na kuhakikisha usalama watu.
Anasema NDC na Tata Chemicals Limited, kutoka India na waendelezaji wa mradi huo kwa makini wanazingatia umuhimu wa kuhifadhi mfumo mpana wa mazingira katika sehemu ya mradi, ndiyo sababu walipokea na kujumuisha mawazo na malalamiko ya wadau kuhusu taarifa ya mazingira
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0784 846907

Chanzo: Tanzania Daima, 8/7/2008

No comments: