6/13/18

MAWE YA ILULA YAZUA MJADALA

Hii ni picha ya eneo la Ilula, mkoani Iringa. Uharibifu wa mazingira umesababisha kilele cha mlima huo kukosa miti. Picha ya Maggid Mjengwa.


UTANGULIZIKaribu katika mjadala ndugu mwanablogu mwenzangu. Niweke wazi kwamba mjadala huu ni mwendelezo wa mada iliyoanzishwa katika blogu ya mwanakijiji Maggid Mjengwa kuhusu mawe yaliyopo katika eneo la Ilula. Mada yenyewe katika blogu hio inasema hivi, nanukuu Kuna mwanakijiji mwenzetu aliyefikiri, kuwa Iringa "IMEBARIKIWA" kwa mawe. Lakini, mlima huo na mingine ya hapa Iringa ilifunikwa na misitu kabla. Kinachoonekana hapo n i uharibifu wa mazingira. Miti yote imekatwa. Kuna vijana wa Iringa wanaokumbuka, kuwa hadi mwaka 1977, waliweza kupanda milima hiyo iliyokuwa na miti mingi. Walikwenda huko na kuwinda ngedere wakiwa na mbwa wao. Binafsi nakumbuka utotoni. Miaka ile ya mwanzoni mwa 70's nikiwa na baba yangu tulisafiri kwa basi la KAMATA toka Igawa Mbeya hadi Iringa. Hapo tulikaa siku kadhaa kwa ndugu yetu mmoja aliyeitwa Merere. Ndugu huyu aliishi Gangilonga, ilijulikana pia kama "Uzunguni". Naikumbuka Iringa iliyokuwa na miti mingi. Mawe hayo ya mlimani sikumbuki kama niliyaona. Nakumbuka Gangilonga yenyewe ilikuwa imefunikwa na miti mingi.Nilipofika tena Iringa miaka ya 90 nikamwuliza mwenyeji wangu nikikumbuka Gangilonga ya utotoni; " Hivi Gangilonga ni wapi ? Niliuliza. " Hapa ulipo ndio Gangilonga!" Alinijibu. Naam. Tunakaribisha mawazo kutoka kwenu, juu ya namna gani tunaweza "kuikijanisha" tena Iringa na hatimaye kuyafunika tena mawe hayo yanayoonekana. Mwisho wa kunukuu.
Kiungo cha mada hio ni http://mjengwa.blogspot.com/2007/08/baraka-au-laana.html
Mtazamo ninaouandika hapa ni wangu, hivyo niko tayari kusahihishwa, kushauriwa ama kukosolewa. Karibuni!

Wanakijiji wanataka huo mlima wa Ilula ufinikwe na mimea kama inavyonyesha picha hii. Inawezekana, tutimize wajibu wetu!
MJADALAUtangulizi huo hapo juu ndio uliozua gumzo na majadala mkali miongoni mwa wachangiaji. Wengi wa wachangiaji walianza na hitimisho kwanza, kuwa ni lazima mimea ipandwe mahali pale ili pawe na ukijani kama ilivyokuwa hapo mwanzo, kama ilivyoshuhudiwa na mmoja wa wanakijiji aliyepita mahali hapo miaka hiyo ya ’70. Shida ilikuwa ni namna gani ya kuanza ’kupakijanisha’ mahali hapo. Na ukiangalia picha hio kwa umakini utaona kuwa kando ya hizo nyumba chini ya huo mlima kuna miti na inaonyesha kuwa ina afya njema tu. Sina uhakika kuwa miti hiyo ni ya kupandwa ama ya asili (nitatembelea hapo mahali na kutoa jibu), lakini kuna dalili zote kuwa hapo mahali miti inasitawi.

HOJA
1. PENDEKEZO LA KUGAWA MITI KWA WANANCHI

Baadhi ya wanakijiji walishauri kugawa miche ya miti kwa wakazi wa Iringa mjini, vyuoni na kwa wanafunzi wote, ili ikapandwe katika mlima wenye mawe pale Ilula. Wazo hili ni zuri, ila kuna wakati huwa halifanikiwi. Suala la kugawa miche ya miti na kuwalazimisha watu kuipanda sio mara zote linafanikiwa. Suala hili linategemea sana mazingira ya eneo husika, mwamko wa watu wa eneo hilo na uhusiano wa mamlaka inayogawa miche na wananchi wa eneo husika. Mfano, kati ya mwaka 1981 – 2000, mradi wa ‘Soil Erosion Control and Agroforestry Project’ (SECAP) ulianzishwa na kuendeshwa katika milima ya Usambara, hususan wilayani Lushoto. Mradi huu ulikuwa la lengo la kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na nyasi katika maeneo mbali mbali ya milima hii ya Usambara. Katika baadhi ya vijiji wanavijiji walipewa miche ya miti na mbegu za majani ya kulisha mifugo, baadhi yao walitupa miche na mbegu hizo na kufanya mradi kutokuwa endelevu. Vijiji ambavyo nilivipitia mwezi Juni mwaka 2005 na walikiri kufanya hivi, (pengine kwa kutojua faida za mti kwa wakati huo) ni Boheloi, Yamba, Mazashai (kata ya Gare) na vijiji vya Mambo, Makose na Mamboleo (kata ya Mtae). Vipara vilivyo katika maeneo haya vinasikitisha sana, hasa ukizingatia kuwa kulikuwa na mradi mkubwa wa utunzaji wa mazingira kwa miaka takribani ishirini. Huu sio uzushi, ila ni hali halisi, kama kuna mtu anatoka maeneo tajwa ama amepita maeneo hayo na kuongea na wenyeji, anaelewa nini ninaongelea hapa. Kuna miradi kadhaa inayofanana na huo wa SECAP ilifanyika katika wilaya ya Mbeya, ambayo ilifadhiliwa na iliyokuwa 'European Economic Community-EEC sasa inaitwa 'European Commission'-EC, ilifanikiwa. Nitatoa makala ya miradi hii siku za baadae kidogo.

2. PENDEKEZO LA KUWA NA SIKU MAALUM YA KUPANDA MITI
Kuna wanakiji walipendekeza kuteuliwa kwa siku maalum ya kupanda miti. Tayari siku hii tunayo, kwani kila ufikapo tarehe mosi mwezi Januari kila mwaka kunakuwa na kampeni za kitaifa za kupanda miti. Ni miti mingi inapandwa katika siku hii na watu binafsi, mashirika, serikali na taasisi mbali mbali. Baada ya kupanda miti suala la ufuatiliaji kujua hali ya mimea hii huwa duni sana, kiasi kwamba mingi ya miti hii huwa inakauka kwa kukosa matunzo. Suala la kupanda miti halina ubaya wowote na ni wazo zuri sana. Lakini sasa, baada ya kupanda, ni nani anajipa shida ya kujua hali ya miti hii baada ya kampeni hizi? Mara nyingi tunapanda miti katika kampeni wakati wa mvua za masika, lakini ni nani anajipa shida ya kufuatilia miti hii mara baada ya mvua za masika kwisha? Nani anakuwa na uhakika kuwa mizizi ya miti hii inakuwa imeshika vyema na ina uwezo wa kufyonza maji sasawasawa wakati wa kiangazi? Ni miji michache sana ambayo hufanya ufuatiliaji wa miti hii mara baada ya kampeni hizi. Kiujumla inatakiwa kila mwananchi awe na mwamko wa kutunza mazingira ya eneo husika, badala ya kusubiri kampeni, ambazo aghalabu huwa ni za zimamoto ama za muda mfupi.

3. MJADALA WA UMILIKI WA ENEO HUSIKA
Niwe wazi kuwa sina uhakika kuwa ni nani anamiliki eneo la Ilula lililoachwa wazi bila mimea. Huenda ikawa ni eneo lililo chni ya mamlaka ya halmashauri ya manispaa, halmashauri ya kijiji ama serikali kuu. Tangu miaka ya nyuma hasa baada ya Azimio la Arusha la mwaka 1967, sehemu kubwa ya ardhi ya nchi yetu ipo/ilikuwa katika miliki ya serikali kuu. Hii inajumuisha pamoja na mambo mengine vitu vyote vilivyomo katika ardhi hiyo, kama vile maji, madini, mimea na wanyama. Ni hivi majuzi tu ambapo maeneo haya yameanza kumilikishwa kwa serikali za mitaa, zikiwemo serikali za vijiji. Suala hili la ardhi kuwa chini ya serikali kuu lilifanya watu kuvamia maeneo haya na kufanya wanachokitaka ikiwa ni pamoja na kuchukua rasilimali zilizomo kama vile kuchimba madini, kurina asali, kuwinda, kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, kupasua mbao na mara nyingine kuichoma moto. Ilikuwa ni ‘Tragedy of the Commons’, kwamba mali ya umma haina hasara. Mara nyingi madhara ya vitendo hivi yametupata hata tusiohusika, kwa hiyo ndio sababu inayotufanya tunapiga kelele. Suala la kuacha kila kitu chini ya serikali kuu siliafiki sana. Tunasema kuwa “Serikali ina mkono Mrefu”, sawa lakini mkono huu una kikomo na kuna maeneo ambayo huwa mkono huu wa serikali kuu hauwezi kufika. Waliowahi kufanya kazi vijijini ambako hata baiskeli hakuna wanaelewa ninachoongelea hapa. Kuna baadhi ya vijiji Tanzania havifikiki kwa magari wala baiskeli, kwa hiyo kusema serikali kuu itafika maeneo hayo na kutekeleza yale wananchi wanayotaka sio kweli. Lazima mambo mengine yaliyo ndani ya uwezo wa serikali za vijiji yaachwe chini ya mamlaka ya serikali za vijiji. Kwa hiyo basi, maeneo kama haya yakipewa umiliki binafsi wa serikali za vijiji yatatunzwa na kuheshimiwa, kwani huku vijijini ndiko serikali inakoanzia na ni wanavijiji ambao ndio waathirika wa kwanza wa moja kwa moja wa athari chanya na hasi za vitendo nilivyoongelea hapo juu, na wengine tunafuata. Kuna wanakijiji wameponda sana suala hili, lakini kamwe hii hainizuii mimi kuendelea kusimamia hoja hii kwa miguu yote. Hatuwezi tu kukurupuka leo na kwenda kupanda miti katika eneo husika eti kwa sababu mvua za masika zinanyesha, bila kujua mmiliki wa eneo husika na bila kujua ana mpango gani na eneo hilo. Huku ni kukurupuka. Naunga mkono suala la kupanda miti, lakini lazima tujue tunapanda miti katika eneo la nani, isije kuwa tunatafuta kesi kwa kuvamia eneo la mtu.

4. MBINU SHIRIKISHI
Pamoja na kwamba kumekuwa na mawazo mbadala kutoka kwa wanakijiji kuhusu hoja hii, lakini pia ina umuhimu wake kwa mazingira ya sasa. Watanzania wa leo huwa wanahoji kila suala, hata kama hawachukui hatua katika suala hilo, lazima wajue nini kinaendelea. Siafiki suala la kuwapita kando ‘by-pass’ wakaazi wa eneo husika. Watanzania wa leo ukiwalazimisha suala ambalo hawalitaki huwa wanasema hapo hapo! Wamebadilika! Kwa hiyo basi, iwapo tunataka kupanda miti eneo la Ilula lililothiriwa, lazima tuwashirikishe wananchi. Narudia kusema kuwa, waliokata miti kwa ajili ya kuni, mbao, ujenzi, uchomaji wa mkaa na kadhalika huenda hawakutoka mbali na hapo, kwa hiyo ni hao hao. Kwa hiyo basi, naunga mkono hoja ya wao kushirikishwa katika kuhuisha mimea ya eneo husika. Nilitoa mfano wa mradi wa “Communal Areas Management Programme For Indigenous Resources” (CAMPFIRE) ulio nchini Zimbabwe, kuwa walitumia mbini hii katika kutekeleza mradi huo na walifanikiwa, kwa nini na sisi tusitumie mbinu hii kama inawezekana? Soma zaidi hapa http://www.resourceafrica.org/documents/1993/1993_campfire_bg.pdf kuhusu mradi huu.
Mfano mwingine wa mbinu shirikishi katika utunzaji wa mazingira unaweza kuusoma hapa, 'http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/9/13/habari33.php' Kitendo cha kufanya mambo ambayo yatawaathiri wananchi hapo baadaye bila kuwashirikisha ni dharau na kinaweza kuleta madhara. Hali kadhalika kitendo hiki kinawaweka wananchi nje ya mradi husika, hivyo wanakuwa hawana uchungu na mradi huo. Ndio hapa vurugu inapoanza, ni katika hatua hii uwindaji haramu hutokea, uchomaji wa mkaa kinyemela hufanyika, ukataji miti bila vibali hutokea na vitendo vingine vinavyofanana na hivyo. Ushirikishwaji wa jamii “Local Level Planning” haukwepeki kwa suala kama la Ilula, kwa hiyo hatuna budi kulipa nafasi yake katika mchakato huu mzima wa kuhuisha eneo husika. Tukidhani kuwa wao hajui mbinu bora za kuhuisha eneo hili tutakuwa tunawakosea haki. Sio vibaya kama tutakumbuka malalamiko ya wananchi wakati wa ‘Operesheni Vijiji/sogeza’ ya miaka ya sabini. Je miradi yote iliyoanzishwa na serikali katika operesheni hii bado inafanya kazi?

5. UREJESHWAJI WA MIMEA ASILIA
Kwa sababu wataalamu wa kwanza na wa kuaminika kwa mtazamo wangu ni wanakijiji wa eneo husika, naamini wao ndio wanaojua ni miti ama mimea ya namna gani ilikuwa inastawi katika eneo husika. Kwa hiyo basi, iwapo wazo ni kurejesha mimea katika eneo husika, sio vibaya kama ile mimea ya mwanzo (original indigeneous species) ikapewa kipaumbele,ndipo mimea mingine hamiaji (exotic species)ipewe nafasi. Inawezekana mimea ya mwanzo isikubali katika eneo husika kulingana na ukubwa wa athari, lakini pia mimea vamizi ina athari zake, na huenda isistawi vyema. Inabidi tuwe makini na hili, kwani tusije kurudi kule kule, leo tunapanda miti na baadaye kidogo tunaambiwa tukate kwa sababu inahatarisha vyanzo vya maji. Hii yote inatokana na kukurupuka. Nadhani tunakumbuka vyema habari ya mikaratusi, kwamba ilipandwa kwa lengo jema kabisa lakini ‘wataalamu’ sijui wa namna gani wakasema miti hii inaharibu vyanzo vya maji. Hoja hii niliipinga wakati fulani bloguni hapa. Nisingependa sana turejee huku miaka kadhaa ijayo.

HITIMISHO
Hatima ya michango ya wanakijiji iwe ni kuhakikisha kuwa eneo tajwa linabadilika kutoka hali ya jangwa iliyopo sasa na kuwa mahali penye mimea. Lakini tisifanye suala hili kwa kukurupuka, kama ilivyo jadi ya Watanzania wengi, tutafeli. Narudia kusema kuwa kijiji (blogu) na wanakijiji kwa ujumla tuna lengo la kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili. Lakini utatuzi huu lazima uwe ‘credible’, vinginevyo tutakuwa tunatwanga maji katika kinu.
Nawasilisha.

No comments: