6/13/18

MAGADI YA ZIWA NATRON NA MAZINGIRA -1

‘WANAOPINGA UCHIMBAJI MAGADI WANATUMIWA’
na Salehe Mohamed

SIKU chache baada ya wadau wa mazingira kupinga mpango wa Serikali kuchimba magadi katika Ziwa Natron, kumeibuka tetesi kuwa wadau wanaopinga mradi huo wanatumiwa na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo waliopo nchini Kenya.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, vinaeleza kuwa wafanyabiashara hao wanahofia endapo Tanzania itaanza kuchimba magadi kuna kila dalili watu wa Kenya nao wakaanza kudai eneo lao lenye madini hayo linalomilikiwa na Waingereza.
Wadau hao inaelezwa kuwa waligharamiwa safari ya kuja Dar es Salaam kupinga uanzishwaji wa mradi wa kuchimba magadi kwenye mdahalo ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), uliokuwa ukilenga kupata maoni ya wadau kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo.
Vyanzo hivyo vinasema fedha zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa magadi ni zaidi ya zile zinazopatikana katika sekata ya madini hivi sasa na Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani.
Viliendelea kubainisha kuwa watu wanaopinga uanzishwaji wa mradi huo kwa madai kuwa utasababisha mazalia ya ndege aina ya Lesser Flamingo (Korongo Wadogo) kupotea, hiyo ni danganya toto kwani nchini Kenya wanachimba na bila kuharibu mazingira ya ndege husika.
Korongo wadogo
Miongoni mwa wataalamu wa mazingira ambao wanapenda kuona mradi huo ukitekelezwa hapa nchini ni Dk. Boniface Mbiyu, ambaye alisema nchi za Kiafrika zimekuwa maskini kwa sababu ya kuwasikiliza wahisani ambao wana lengo la kuzinufaisha nchi zao.
Alisema kama Tanzania itaweza kuchimba madini hayo inakadiriwa kupata zaidi ya sh bilioni 600 ambazo ni zaidi ya fedha wanazozipata katika sekta ya madini na itakuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani.
Alisema Kenya ilianza kuchimba magadi tangu mwaka 1910 na hakuna madhara makubwa ya kimazingira kama ambavyo watu wamekuwa wakipewa taarifa tofauti kuhusu uanzishwaji wa mradi huo.
Kenya ni miongoni mwa makoloni yaliyokuwa yakitawaliwa na Uingereza na mpaka hivi sasa Waingereza bado wanamiliki eneo linatoa magadi hayo na wameweka vikosi vya kijeshi eneo hilo kwa kushirikiana na askari wa Kenya.
“Huu mradi utakuwa na thamani kubwa sana kwa Watanzania na itakuwa mkombozi wa kiuchumi kwani fedha zitakazopatikana ni zaidi ya zile za dhahabu, makaa ya mawe na almasi,” alisema Mbiyu.
Alisema ni vema Watanzania hasa watu wanaoishi katika eneo la jirani ambalo linatarajiwa kuchimbwa magadi wakawa makini na kuepuka ahadi ndogo ndogo pamoja na maneno ya watu wasiopenda maendeleo ya Tanzania kiuchumi.
Kauli hiyo ya Dk. Mbiyu inaungana na ile aliyoitoa Waziri wa Malisili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kuwa serikali haitasitisha mpango wake wa kuchimba magadi katika Ziwa Natron lililopo katika Mkoa wa Manyara pamoja na kelele kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka mradi huo usitishwe.

MAGADI YA ZIWA NATRON, MKOMBOZI WA UCHUMI TANZANIA
Salehe Mohamed

TANZANIA ni moja ya nchi zilizobarikiwa duniani kuwa na rasilimali nyingi lakini pia ni moja ya nchi zinazoongoza kwa umaskini, kwa sababu ya kutokuzisimamia vema.
Dhahabu, tanzanite, almasi, makaa ya mawe, mbuga za wanyama na vivutio vingi ambavyo kama vingetumika ipasavyo vingeweza kuiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tajiri zaidi duniani.
Madini ni miongoni mwa sekta ambazo kila kukicha imekuwa ikipigiwa kelele kuwa inawanufaisha zaidi wageni kuliko wazawa kutokana na mikataba iliyoingiwa na wazawa wasio kuwa na uchungu na rasilimali za nchi yao.
Hivi karibuni kumezuka mashindano ya hali ya juu kati ya watunza mazingira, jumuiya za kimataifa na Serikali ya Tanzania kuhusu azima ya Tanzania kutaka kuchimba magadi yaliyopo katika Ziwa Natron lililopo mkoani manyara.
Wadau wa mazingira na jumuiya ya kimataifa wanasema eneo hilo ni tengefu kwa ajili ya kuhifadhi ndege aina ya lesser flamingo ambao hupatikana katika maeneo machache hapa duniani na wapo hatarini kutoweka.
Wakati wahisani na wadau wa mazingira wakisema hayo, Tanzania imesema itaendelea na mradi huo kwani utasaidia kupunguza umaskini kwa wakazi wa eneo hilo na kukuza uchumi wa nchi.
Mpango wa Serikali ni kuchimba tani 500,000 kwa mwaka kwa muda wa miaka 200 na tayari Kampuni ya Tata Chemical ya nchini India inakamilisha taratibu za mwisho kabla ya kuanza kwa mradi husika.
Zaidi ya dola za Marekani milioni 800,000 zinakadiriwa kupatikana endapo mradi huo utafanya kazi vizuri kama ilivyopangwa pamoja na kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa watu wanaofanya kazi katika mradi husika.
Kampuni ya Tata Chemical ndiyo ambayo hivi sasa inaendesha mradi kama huo katika Ziwa Magadi lililopo nchini Kenya na kwa kiasi kikubwa wametambua faida ipatikanayo na magadi ndiyo maana wameamua kuja kuwekeza Tanzania.
Kampuni hiyo imeahidi kuajiri zaidi ya watu 500 katika ajira ya kudumu na zaidi ya watu 2,000 watapata vibarua huku nyumba zaidi zikitarajiwa kujengwa kwa ajili ya wafanyakazi.
Reli ya kutoka eneo la mradi mpaka Tanga kwa ajili ya usafirishaji tayari ipo katika mchakato wa ujenzi, umeme nao utafika mradini pamoja na barabara itakayopitika kipindi chote cha majira.
Kimsingi mradi huu utawanufaisha watu wengi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa ambapo ni watu wachache hunufaika na fedha zinazopatikana kutokana na utalii.
Magadi ni aina ya madini ambayo yanapatikana kwa wingi katika Ziwa Natron na asili yake ni kulipuka kwa Volcano hai ya Mlima Oldonyo Lengai uliopo katika Mkoa wa Manyara.
Magadi yana matumizi mengi kwa binadamu, yakiwemo kutengenezea karatasi, viwanda vya ngozi, kusafisha maji, dawa, vitu vya kulipuka na vingine vingi.
Inakadiriwa kuwa nishati ya petroli, madini ya tanzanite, makaa ya mawe na madini mengine yakijumuishwa pamoja hayawezi kufikia fedha itakayopatikana kutokana na uchimbaji wa magadi.
Kimsingi magadi kama yakitumika ipasavyo yanaweza kuiletea Tanzania faida kubwa zaidi kuliko inavyofikiriwa na watu wengi ambao kwa namna moja au nyingine wamekosa uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa madini haya kwa uchumi wa Tanzania.
Kenya ina eneo linalojulikana kama nchi ya magadi, ambayo yalianza kuchimbwa mwaka 1910 na hutoa zaidi ya tani 600,000 kwa mwaka na inakadiriwa hupata zaidi ya dola milioni 41, fedha ambazo huwafaidisha zaidi Waingereza.
Eneo yanapopatikana madini hayo hulindwa na vikosi vya Kenya na Uingereza, ambayo wakati ikitoa uhuru kwa watu wa Kenya iligoma kutoa eneo hilo kutokana na umuhimu wake.
Mwaka 2001 jumuiya ya kimataifa, hasa wanaojiita wana mazingira walipitisha makubaliano ya kulinda maeneo chepechepe na yenye viumbe ambavyo vinaweza kutoweka ikiwemo eneo hilo la Ziwa Natron.
Lesser flamingo ndio ndege ambao jamiii ya kimataifa inataka wasipotee katika eneo husika ilhali jumuiya hiyo haitazami namna Tanzania inavyoathirika kiuchumi kama haitachimba madini hayo.
Jumuiya hiyo inaonyesha nia ya kutoa shinikizo la kutoipatia Tanzania misaada ya kifedha kama Tanzania itaendelea na mradi wake wa kuvuna magadi katika Ziwa Natron.
Inataka ilete masharti kama ya Mto Nile ambapo nchi zinazozunguka mto huo hutakiwa kuwasiliana na Misri ndipo ziweze kuyatumia maji ya mto huo.
Mtaalamu wa mazingira, Dk. Boniface Mbiyu alielezea umuhimu wa Tanzania kuchimba madini hayo kwa kipindi hiki ni mkubwa zaidi kuliko vipindi vilivyotangulia kwani nchi haiwezi kuendeshwa kwa kutegemea misaada ya wahisani.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ili nchi ifaidike zaidi ni lazima kuwapo na mgawanyo mzuri wa rasilimali hiyo kabla ya kuingia mkataba na wawekezaji ili yasije yakatokea yale ya madini.
Alisema mwekezaji na Serikali wanapaswa wapate asilimia 40 katika mradi huo huku asilimia 20 ikienda kwa wakazi wa eneo la mradi ambao wana hofu ya kupoteza fedha wanazozipata kutoka kwa watalii.
Kuwapo kwa ndege hao kumekuwa kivutio kikubwa zaidi kwa watalii ambapo inakadiriwa zaidi ya dola za Marekani 500,000 hupatikana sambamba na wananchi wa Kijiji cha Ngarisero kunufaika kwa kuwatembeza watalii.
Marekani ni nchi ambayo magadi hupatikana lakini ni lazima yachimbwe mita 400/600 kwenda chini, tofauti na Tanzania ambapo hata jembe la mkono linamtosha mtu kuchimba magadi.
Urahisi wa uchimbaji magadi katika Ziwa Natron utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara hiyo ambayo inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kukua kwa uchumi wa Tanzania.
Uchimbaji wa magadi katika ziwa hilo ndiyo mwelekeo mwema wa kufanikisha malengo ya kukuza uchumi wa Tanzania na kutimiza azima ya serikali ya kuboresha maisha ya wananchi.

Chanzo cha habari hii: Gazeti la Tanzania Daima, 29/01/2008

Nitazijadili hoja hizi kwa undani.

No comments: