6/13/18

WAPINGA KUCHIMBA MAGADI ZIWA NATRON

na Salehe Mohamed

LICHA ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Professa Jumanne Maghembe, kusisitiza dhamira ya serikali kuchimba magadi katika Ziwa Natron, wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi wameupinga mradi huo.
Wadau hao walitoa maoni yao jana jijini Dar es Salaam katika mdahalo wa kupata maoni kuhusu uanzishwaji wa mradi huo, ulioandaliwa na Baraza la Mazingira (NEMC), likihusisha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Wadau hao walisema athari za mradi huo ni nyingi kwa binadamu, ndege, wanyama na upo uwezekano mkubwa wa kukauka kwa ziwa hilo, kama ilivyotokea kwa wananchi wa Kenya, hivyo hawaoni sababu ya kuukubali mradi huo.
Mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya TATA Chemical ya nchini India, ambapo kila mwaka watakuwa wakichimba tani 500,000 na watajenga kiwanda cha kuandaa magadi kwa ajili ya kusafirishwa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Engaresero, ambapo mradi huo utajengwa, Christopher Ndurway, alisema wakazi wa kijiji hicho zaidi ya 5,000 na mifugo yao hawatakuwa na sehemu ya kwenda iwapo mradi utaanza kazi.
“Sisi hatukubaliani na uamuzi wa serikali wa kutaka kuchimba magadi, kwani kuna athari kubwa za kimazingira pamoja na sisi na mifugo yetu,” alisema Ndurway.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Deodatus Mfugale, alisema mradi huo utaharibu mazalia ya ndege aina ya Lesser Flamingo ambao wapo hatarini kutoweka.

Korongo Wadogo
Alisema kuanzishwa kwa mradi huo kunakiuka makubaliano ya kimataifa ambayo yanatamka eneo hilo ni tengefu kwa ajili ya viumbe hivyo.
Mdahalo huo ulitawaliwa zaidi na ubishani mkali baada ya mwakilishi wa NDC, Abdalah Mndwanga, kusema kuwa mwekezaji alibadili eneo la kujenga kiwanda na kusogea umbali wa kilometa 30 zaidi ya eneo la awali.
Mwakilishi huyo alikuwa katika wakati mgumu zaidi pale alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa athari za kimazingira zitakazopatikana baada ya mradi, huku yeye akijibu kuwa alielekezwa kutoa takwimu za kiufundi na si vinginevyo.
Joseph Ng’ida, alisema serikali inapaswa ifanye upya tathmini ya mradi huo badala ya kukurupuka, hatua ambayo inaweza kusababisha majuto siku za usoni.

WAZIRI KITUKO
Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Ana Maembe, alisema maoni ya wananchi hao yatafikishwa kwa Waziri Maghembe ambaye ndiye atakayetoa kibali cha kuruhusu mradi huo.
Maghembe ameshawahi kunukuliwa akisema kuwa watu wanaopinga mradi huo wana sababu binafsi na kama wanataka serikali iachane na mradi huo ni vema wakatoa fedha itakazopata serikali katika kipindi chote cha mradi.

Chanzo: Tanzania Daima 24/01/2008

No comments: