6/13/18

Mgao wa Umeme, utaishaje?

Mgao wa umeme
Historia inaonesha kwamba mgao usio wa kawaida wa umeme kwa nchi yetu kwa miaka ya karibuni ulianza mwaka 1992, kufuatia ukame wa muda mrefu ambao uliikabili nchi kwa sehemu kubwa, ukizingatia kwamba kwa kipindi hicho, sehemu kubwa ya umeme uliokuwa ukitumika hapa nchini ilitokana na nguvu ya maji (hydropower) na mafuta mazito (Heavy Fuel Oil – HFO). Kwa kipindi hicho, umeme utokanao na gesi asilia ulikuwa bado haujaanza kuzalishwa kwa kuwa miundombinu ya uzalishaji na usafirishaji wa gesi ilikuwa haijajengwa.
Mahitaji makubwa ya umeme kwa sasa hayaendani kabisa na kasi ya uwekezaji katika miundombinu ya uzalishaji wa umeme, suala hili limesababisha kiwango kidogo cha umeme unaozalishwa kugawiwa kwa wateja wachache kwa muda fulani, hivyo kuleta kitu kinachoitwa mgao wa umeme. Kabla hatujaingia katika mjadala wa namna ya kuondokana na mgao, ni vema tukaangalia historia 'fupi' ya mgao wa umeme tulionao.
Nilichoandika hapa chini nimechukua kutoka katika vyanzo mbali mbali, ikiwemo katika machapisho ya shirika la Tanesco, makala za magazeti, makala za mtandaoni na mahojiano binafsi na watendaji wa shirika hilo na mahojiano na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati.
**************************************************************************
Historia Kidogo
Kati ya mwaka 1996 na 2006 kilikuwa ni kipindi cha ubinafishaji wa mashirika ya umma kwa nchi yetu. Katika kipindi hiki mashirika mbali mbali ya umma yaibinafsishwa kwa wawekezaji mabepari ili kuyaendeleza. Katika orodha ya mashirika ya kubinafsishwa, Tanesco ilikuwemo. Ili kuiandaa Tanesco kubinafsishwa, serikali 'Haikuwekeza' rasilimali katika shirika hili, hivyo vitu vya msingi kama vile miundombinu ya uzalishaji umeme, usafirishaji na usambazaji, kuajiri nguvukazi mpya kila mara havikufanyika. Vitu hivi ni vya msingi sana katika suala zima la uhai wa shirika.
Ikumbukwe kuwa katika kipindi hicho, uchumi wa nchi ulikua kwa kiwango cha asilimia 7 kwa mwaka na kiwango hicho kiliendana na uwekezaji mkubwa katika migodi, kampuni za simu, kukua kwa sekta ya ujenzi (wa majengo ya kibiashara), kufunguliwa kwa mashamba makuwa yenye viwanda vya kusindika mazao, na kukua kwa sekta ndogo na za kati kiuchumi (small and medium sized enterprises). Sekta hizi ni watumiaji wakubwa wa umeme, hivyo waliongeza idadi ya wateja wakubwa wa umeme. Hadi kufikia mwaka 2002, shirika hili lilikuwa halijabinafsishwa, na kama nilivyotaja hapo awali hakukuwa na uwekezaji mkubwa tangu mwaka 1996.

Ujio wa Net Group Solutions
Mnamo mwaka 2002 serikali iliamua kuliweka shirika hili chini ya menejimenti kutoka nchini Afrika Kusini (Net Group Solutions) ili kukusanya mapato ya wadaiwa wakubwa na kuliandaa shirika na kubinafsishwa. Kampuni hii ilifanya kazi katika shirika hili hadi mwaka 2006 ya kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa wakubwa kama vile taasisi za serikali, jeshi, serikali ya Zanzibar na viwanda vikubwa. Ufanisi wa utendaji wa kampuni hii bado unatiliwa mashaka na wadau wengi, kwani haikusaidia kuondoa matatizo yaliyokuwa yakikabili shirika la umeme. Hatimaye mnamo mwaka 2006, serikali iliamua kutolibinafisha shirika lake. Mpaka hapo ikawa miaka 10 imeshapotea, ndani ya kigugumizi cha ugumu wa maamuzi ya 'Tubinafsishe' ama 'Tusibinafsishe'?.

Uwekezaji mpya kwenye umeme
Baada ya mwaka 2006 ndipo zikaanza juhudi za uwekezaji katika miundombinu ya umeme, mpaka sasa. Kwa mujibu wa ripoti ya mwezi Januari ya Tanesco, mahitaji ya umeme ni kiasi cha megawati 833, na mpaka mwezi huo shirika lililikuwa likizalisha kiasi cha megawati 1006 kutoka vyanzo mbali mbali kama vile maji, gesi na mafuta mazito. Katika kiwango hicho cha uzalishaji, umeme unaopatikana muda mwingi ni megawati 650 tu, hivyo hautoshelezi mahitaji. Ongezeko la mahitaji kila mwaka ni kati ya megawati 100 na 120. Hadi mwezi Juni mwaka 2011 ni megawati 145 tu ndizo ambazo zimeingizwa katika gridi ya taifa, hivyo suala la upungufu wa nishati hii bado ni kitendawili.

Hatua za dharura za uzalishaji umeme
Kimbilio kubwa la serikali katika kutatua janga la mgao imekuwa ni suluhisho la muda mfupi, la kutumia mitambo ya dharura ya kukodi ili kuzalisha umeme. Mitambo hii ambayo hutumia mafuta mazito na/au gesi na hutugharimu pesa nyingi kama taifa hivyo kuzorotesha uchumi. Hili ni pigo kwa uchumi wetu ambao bado ni mdogo. Suluhisho hili la muda mfupi la uhaba wa nishati haliwezi kutupeleka mbali, zaidi ya kutuongeezea umasikini. Kiwango cha gesi kinachopatikana sasa kwa ajili ya uzalishaji umeme ni kidogo, kwa sababu ya ufinyu wa miundombinu ya usafirishaji wa gesi kutoka mahali inapozalishwa kisiwani Songosongo hadi mahali inapotumika, Dar Es Salaam. Hivyo, hata kama mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi itanunuliwa na kufungwa leo, bado hatuwezi kupata umeme kwa sababu tuna upungufu wa gesi ya kuendeshea mitambo hiyo.


Tufanyeje kuepukana na mgao?


Utashi wa kisiasa
Kwa hili, kwa mtazamo wangu, kwanza kabisa kunahitajika utashi wa kisiasa (political will) wa wale tuliowakabidhi jukumu la kutuondolea umasikini. Utashi wa kisiasa ndio unaofanya kuwe na kigugumizi au maamuzi ya wapi tuweke rasilimali nyingi na wapi tuweke chache kulingana na vipaumbele vyetu vya taifa. Hatujawekeza rasilimali za kutosha katika utatuzi wa muda mrefu wa janga la upungufu wa nishati, hasa umeme. Kwa ulimwengu wa dijitali tulio nao, suala la upatikanaji toshelevu wa nishati linatakiwa kuwa ni kipaumbele namba moja. Huwezi kuongelea kilimo cha kisasa cha kuongeza thamani ya mazao kupitia usindikaji, iwapo huna umeme wa kuaminika. Huwezi kuongelea suala la kukuza sekta ya madini iwapo huna umeme wa kuaminika. Huwezi kukuza viwanda iwapo huna uhakika na umeme. Hakuna mwekezaji atakayekubali kupoteza rasilimali zake kwa kuwekeza mahali ambapo umeme si wa uhakika.

Uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati
Binafsi, sijaona mipango MADHUBUTI na INAYOTEKELEZEKA kwa rasilimali tulizonazo, ya kufanya uwekezaji mkubwa katika suala la nishati, hasa kwenye nishati jadidifu. Mpango wa serikali wa hadi mwaka 2015 ni kuzalisha megawati karibia 3000 na kuingiza katika mfumo wa gridi ya taifa. Mipango hii inategemea sana hisani ya wafadhili na mikopo. Binafsi sio mchumi, lakini natilia shaka sana mpango huu, kwa sababu kama taifa hatujaweka jitihada za kutosha kutoka vyanzo vya ndani vya mapato kugharamia miradi hii. Nimesoma bajeti za serikali kwa mwaka 2010/2011 na 2011/2012, bado hakuna mipango madhubuti ya uwekezaji mkubwa kutoka vyanzo vya ndani, kwenye nishati. Kwa miaka ya hivi karibuni, uchumi wa dunia umeyumba sana, na bado mpaka sasa katika nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya Euro uchumi haujatulia. Umoja wa Ulaya pamoja na serikali ya Marekani ndio wafadhili wakubwa wa miradi mingi ya nishati nchini kwa sasa, hivyo mtikisiko katika uchumi wao unaweza kubadili mwelekeo wa sera zao, kutoka kufadhili miradi na kutoa mikopo kwa nchi zinazoendelea na kupelekea kuinuana wao kwa wao kiuchumi, kama wanavyofanya kwa uchumi wa nchi ya Ugiriki unaoyumba. Hili linawezekana. Iwapo hili la kubadili sera litatokea, basi uwekezaji katika miradi ya nishati kwa hapa nchini utayumba na hivyo kuathiri utekelezaji wa mpango wa megawati 3000. Lisemwalo lipo!

Kudhibiti Upotevu na wizi wa umeme
Kwa mujibu wa takwimu za Tanesco kwa mwaka 2010, zilizochapwa katika ripoti iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia (Electricity loss Reduction Study, June 2011) , upotevu wa umeme huligharimu shirika kiasi cha dola za Kimarekani milioni 72. Katika umeme wote unaozalishwa, asilimia 20 ya umeme wote haufiki kwa wateja (kwa mfano, kama zinazalishwa megawati 850, ina maana megawati 170 zinapotea kabla ya kufika kwa wateja). Hiki ni kiwango kikubwa sana cha upotevu. Katika upotevu huu, asilimia 25 inatokana na ubovu na/au uchakavu wa miundombinu na asilimia 75 inatokana na upotevu kwenye mauzo. Takwimu hizi zinasikitisha kwa sababu shida kubwa ya upotevu haiko kwenye miundombinu kama wengi tunavyotarajia, ila kwenye mauzo (udanganyifu na ukosefu wa uadilifu). Iwapo kuna utashi wa kisiasa, asilimia hizo 75 ambazo zinatokana na (mkono wa mtu) zinaweza kudhibitiwa kabisa. Hasara hiyo ya dola milioni 72 inaweza kudhibitiwa na kuongeza kipato katika bajeti ya taifa.

Udhibiti wa mikataba tata ya uzalishaji umeme
Kumekuwa na matatizo kwenye mikataba ya uzalishaji umeme inayosainiwa kati ya serikali na kampuni binafsi. Mikataba mingi imetokana na mpango wa dharura wa uzalishaji umeme, hasa kunapokuwa na shida ya mgao. Mikataba hii imetokana na maamuzi mabovu ya makusudi ya watendaji waliopewa dhamana ya kusaini mikataba hii kwa niaba yetu. Udhibiti wa mikataba mibovu unahitaji utashi wa kisiasa pia, kwa wale tuliowapa dhamana ya kudhibiti utendaji mbovu. Napendekeza kwamba kutungwe sheria (kama haipo), kwamba mikataba mikubwa, kama ile ya uchimbaji wa madini na uzalishaji mkubwa wa nishati, ipitie kwanza bungeni, na iwapo ina maslahi kwa nchi basi iidhinishwe na bunge kabla serikali haijatia saini kwa niaba yetu! Kwa mbinu hii, tutaweza kuwa na uzalishaji mkubwa wa umeme usio na mawaa, kwa kuwa kila kitu kitafanyika kwa uwazi kupitia wawakilishi wetu bungeni.

Hitimisho
Suala la umeme lina maslahi mapana kwa taifa, kiuchumi, kiusalama na kijamii, si la kulifanyia maamuzi ya mzaha na pupa. Uhaba wa umeme unaathiri uchumi wa nchi, kwani uzalishaji katika ofisi, mashamba na viwanda unategemea umeme. Mgao unaathiri sekta nyingine kama vile maji, ambayo husukuwa kwa pampu zitumiazo umeme, kutoka pale yanapotekwa kwenda pale yanapotumika. Tuchukue hatua madhubuti za kuepuka janga hili, kwa maendeleo ya taifa! Tutimize wajibu wetu!

Nimefungua mjadala, tuendelee kuelimishana.

No comments: