Showing posts with label Maisha Mbadala. Show all posts
Showing posts with label Maisha Mbadala. Show all posts

2/3/07

GARI LA MIONZI YA JUA HILI HAPA!


UTANGULIZI

Kumekuwa na usemi kwamba *Tembea uone*. Usemi huu una maana kubwa, kwamba ukiwa mtembezi basi utaona mengi. Pia kuna usemi unaoambatana na huo, kwamba Mtembea bure si mkaa bure, huenda akaokota! Basi katika pita pita yangu hapa na pale, kwa maana ya kwamba nilikutana na habari njema kwa watu wanaojali matumizi endelevu ya nishati na upunguzaji wa hewa chafu duniani. Nilikuta gari moja zuri katika makumbusho, ambalo kwa mujibu wa watu niliowakuta hapo wanasema kuwa lilikuwa linaendeshwa kwa kutumia umeme wa mionzi ya jua. Sababu za kwa nini kwa sasa halitembei ni kwamba hali ya hewa si nzuri sana kuweza kuchaji betri za umeme wa mionzi ya jua kwa mahali hapo, huwa mionzi ya jua si ya kutosha kuchaji betri hadi kuwa na ujazo unaotakiwa.


GARI LENYEWE

Katika boneti la mbele kwa juu kuna moduli kadhaa za kufyonza mionzi ya jua na kuihifadhi katika betri zake sita ambazo huwa zinafunikwa na boneti (sehemu ambayo huwa na radieta, kwa magari yanayotumia mafuta). Betri hizi zimeunganishwa pamoja na kutengeneza umeme mkubwa. Umeme huu hutumika kuendesha mota ambazo ndio husababisha nishati ya mwendo ili gari hili liweze kwenda. Kwa upande wa nyuma, katika buti pia kuna moduli kadhaa ambazo hufanya kazi kama zile za mbele. Gari hili huweza kuendeshwa muda wa masaa sita bila betri kupungua nguvu, kwa wastani wa mwendo wa kilometa arobaini mpaka sitini kwa saa, kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa makumbusho hayo.


Binafsi nilifurahi sana kuweza kuona gari la ukubwa ule linaloendeshwa kwa kutumia mionzi ya jua, kwa sababu teknolojia hii ya kutumia mionzi ya jua kwa kuendesha mitambo si maarufu sana hapa duniani. Pia kuna magari madogo madogo mengi katika nchi zilizoendelea ambayo huendeshwa kwa kutumia betri za magari na mota, ambapo hayatumii mafuta, mara nyingi magari haya hutumiwa na walemavu wa miguu.



Katika ulimwengu huu kwa sasa ambapo tunajadili ongezeko la joto duniani, ni bora tukafikiri kutumia magari ya namna hii kwa safari ambazo ni fupi fupi, ili kupunguza kiwango cha hewa chafu ambayo husababishwa na uchomaji wa mafuta katika mitambo mbali mbali.
Tufikirie dunia mbadala.


1/5/07

MAISHA MBADALA

UTANGULIZI
U hali gani msomaji wa blogu yangu. Kwa leo nakuletea mambo mawili muhimu, hasa kuhusu suala zima la mazingira. Katika mapumziko ya Krismasi na mwaka mpya, nilifanikiwa kuzulu jiji la Copenhagen wao wanaita Kobenhavn, nchini Denmark, na kwa kweli nilifurahi sana.

MADA
MIFUO YA UMEME WA NGUVU YA UPEPO

Katika ufukwe wa bahari kwanza kabisa nilipokewa na msururu wa mifuo ya umeme inayoendeshwa kwa nguvu ya upepo, kwa kweli inaonyesha ni kwa jinsi gani hawa wenzetu wanajali suala la kupunguza ongezeko la joto duniani. Mifuo hii ni mingi sana nchini humu, na kuna watu wanadai kuwa inawezekana kabisa kuwa nchi hii ndiyo inayoongoza kwa kuwa na mifuo mingi ya umeme huu wa nguvu ya upepo.
Mitambo hii wao wameiweka katika ufukwe kwa sababu maalum, kwamba kandoni mwa bahari kuna upepo wenye nguvu sana kutokana na mawimbi ya bahari, kwa hiyo wakaona ni bora watumie nguvu hiyo katika kuzalisha umeme. Kwa upande wa kwetu sisi, bado tupo nyuma ya wakati kuhusu suala zima la kutumia nguvu ya upepo kuzalisha umeme. Tuna ufukwe mrefu sana katika bahari ya Hindi kuanzia Mtwara hadi Tanga, lakini bado hatujafanya matumizi sahihi ya ufukwe huu. Pia tuna maziwa makubwa matatu, nayo ni Tanganyika, Nyasa na Viktoria, ambapo pia ingewezekana kutumia fukwe zake kuzalisha umeme wa nguvu ya upepo, lakini hali si kama hivyo. Mpaka sasa bado sijajua kwa yakini sababu zinazotufanya tushindwe kutumia nguvu hii ya upepo kuzalisha umeme.

ADHA ZA MIFUO HII
Pamoja na hatua hii nzuri ya kuweka mifuo ya umeme, kumezuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanamazingira. Malalamiko haya yanadai kuwa mifuo hii ya umeme huwa inaharibu mandhari asilia ya eneo husika, kwa maana ya kwamba iwapo mifuo hii itawekwa mahali basi sura ya mahali hapo inabadilika, kwa sababu mifuo hii ni mikubwa sana. Kuna mifuo mingine huwa na kimo cha hadi kufikia meta mia moja kwenda hewani na huchukua eneo kubwa sana, kwa hiyo wanamazingira hawa hawajapendezwa kwa kiasi fulani na suala hili. Sababu ya pili ni kwamba, katika maeneo haya na mengineyo ambayo yana mifuo hii huwa kunakuwa na viumbe hai wengine kama ndege ambao huishi katika maeneao hayo, kwa hiyo basi ndege ambao huruka karibu na maeneo haya hupata ajali kwa kugongana na pangaboi za mifuo hii inapozunguka, hasa kunapokuwa na ukungu ama giza wakati wa mchana. Na kama nilivyodokeza hapo juu, mifuo mingi ipo katika fukwe za bahari na kama tunavyojua kuwa katika bahari na pembezoni mwake kuna ndege wavuvi kama batamaji, heroe, furukombe wavuvi, bundi wavuvi na kadhalika, basi ndege hawa wavuvi ndio ninaoongelea katika makala hii, kuwa wanagongana na pangaboi za mifuo hii.
Kwa hiyo pamoja na kwamba tunapata faida ya umeme kupitia mifuo hii, kuna hiyo tahadhari ambayo huwa tunapaswa kuizingatia, hasa tunapokuwa tunapanga mipango endelevu ya kuweka mifuo ya namna hii.

BAISKELI
Suala lingine ambalo ningependa kuliongelea kwa leo ni uwingi wa baiskeli katika jiji la Copenhagen. Kuna baiskeli nyingi sana hapa mahali hadi zinakuwa kero kwa wakati fulani. Kwa upande mwingine, uwingi huu unamaanisha kuwa kiasi kikubwa cha watu huwa wanatumia baiskeli katika safari fupi fupi za mjini hapa. Niliwahi kuliongelea suala hili katika makala zangu zilizopita, kuwa njia moja wapo ya kupunguza msongamano wa vyombo vya moto katika majiji makubwa kama hili ni kutumia usafiri wa kupunguza baiskeli kwa safari ambazo hazilazimu kutumia gari. Suala hili la kutumia baiskeli pia linasaidia kupunguza hewa zenye sumu kutokana na moshi magari. Inawezekana basi ikawa ni mkakati wa serikali katika kupunguza msongamano wa vyombo vya usafiri, kwamba wakasisitiza kutumia baiskeli kwa kiwango kikubwa kama ilivyo mahali hapa.




TUFANYE NINI?
Kwa kutumia mifano hii miwili inatakiwa tutoke na mtazamo mpya kuhusu suala zima la mazingira, kwa sababu kwa namna moja ama nyingine tusipojitahidi kuzuia ongezeko la joto duniani kuna hatari ya kupoteza asilimia kubwa ya viumbe wetu wa asili. Si suala geni kwa kusikia kwa walio wengi sababu kwa sasa tunasoma katika maandiko mbali mbali ya kumbukumbu za kihistoria kuwa hapo zamani kulikuwa na wanyama wanaitwa Dinosaurs na walitokomea kabisa katika uso wa dunia, kutokana na sababu anuwai, kwa hiyo na sisi kama hatutafanya juhudi za kuzuia hali hii basi kuna hatari kubwa sisi pamoja na viumbe wanaotuzunguka kutokomea kabisa katika uso huu wa dunia. Pamoja na kwamba kuna nguvu za asili kama matetemeko ya ardhi na volkano ambavyo huweza kubadili sura ya nchi na uoto wa asili, si vibaya kama nasi tutachukua hatua katika kudhibiti kile ambacho kipo ndani ya uwezo wetu kwa wakati huu. Mambo haya ni pamoja na kupunguza kiwango cha hewa chafu za viwandani, kupunguza kemikali katika maji ambayo huwa tunayamwaga katika bahari zetu, kupunguza kama si kuzuia kabisa utupaji ovyo wa masalia ya nishati nyuklia na la muhimi zaidi ni kupunguza matumizi ya madawa ya kilimo yenye sumu.
Inawezekana kufanya mabadiliko, tutimize wajibu wetu.

11/24/06

MALENGO YA MAENDELEO YA MILENIA - 2: LENGO NAMBA SABA

UTANGULIZI
Katika makala zilizopita niliongelea malengo ya milenia ambayo kwa ujumla wake yapo nane, pia niliahidi kujadili lengo namba saba kwa undani na wasaa huo ni sasa. Lengo hili kwa Kiingereza limeandikwa ‘Ensure Environmental Sustainability’. Kwa tafsiri yangu katika Kiswahili nasema ‘Kuzingatia Uendelevu wa mazingira’. Katika ufafanuzi wake, walioandika lengo hilo wanasema lazima tuingize suala la mazingira katika mfumo wetu wa maendeleo endelevu katika sera na mipango ya nchi zetu na kurejesha rasilmali katika mfumo wake wa asili. Hii ina maana ya kwamba katika suala zima la maendeleo, huwezi kukwepa suala la mazingira, ndio sababu likapewa umuhimu wa pekee katika muktadha wa malengo ya milenia. Kwa ujumla wake, mazingira ni vitu vyote vinavyomzunguka mwanadamu. Ni mara nyingi sana katika shughuli zetu za uzalishaji mali tumekuwa tukichukua rasilmali nyingi katika mazingira yetu bila kurejesha kwa kiasi Fulani kama ninavyofafanua hapa chini.

1. ARDHI
Ardhi ndio mama wa kila kitu kiasi kwamba wataalamu tukaamua kuiita ‘Mother nature’. Bila ardhi hakuna maisha. Tumekuwa tukichukua rasilmali nyingi sana katika ardhi, mara nyingine bila kuzingatia uendelevu wake. Tunachukua mimea, wanyama, maji na madini bila kuchukua tahadhari za kimazingira na kujali madhara yajayo baada ya hapo. Madini yaliyo mengi yanapatikana ardhini na namna pekee ya kuyapata ni kuyachimba toka humo ardhini yalimo. Lakini kwa utovu wetu wa nidhamu tunaacha kufukia mashimo na kurejesha sehemu ya mimea na wanyama walioondolewa mahali hapo kwa makusudi. Tunamkomoa nani? Kwa mtazamo wangu sidhani na sipendi kuamini kuwa tunakuwa hatufahamu tunachokifanya. Matokeo ya madhara haya tunayapata hapa hapa, kwani kumekuwa na upungufu wa maji maeneo mbali mbali duniani, kwani katika shughuli zetu tunaharibu mzunguko wa maji. Pia kumekuwa na upotevu wa viumbe hai sehemu nyingi tu. Kwa kawaida ardhi, mimea na maeneo yenye unyevu yapatapo joto na mwanga wa jua hupumua.Katika kupumua huku mvuke huo huenda angani na kuganda na kufanya mawingu ambayo baadaye hurudi ardhini kama mvua, theluji, barafu na mzunguko huendelea. Sasa basi iwapo sehemu fulani ya mzunguko huu itaathirika kwa namna moja au nyingine basi athari hizi zitasambaa hata katika sehemu nyinginezo za mzunguko huu. Hivi ndivyo mfumo mzima ulivyo. Suala la kilimo pia ni la kuangaliwa. Kumekuwa na matumizi makubwa sana ya mbolea za viwandani katika shughuli za kilimo, hasa katika nchi zinazoendelea. Mbolea hizi,kwa namna moja au nyingine zinachosha sana ardhi, kiasi kwamba baada ya muda fulani ardhu husika inakuwa haina uwezo tena wa kuzalisha mazao mengi kama mwanzo. Wao wenyewe wanaotengeza mbolea hizi wanazipiga vita kwa sasa, sasa sijajua wanamtengenezea nani. Wameshajua kuwa zina madhara, hivyo wanataka kutumia mbolea asilia tu mashambani kwao. Kwa hiyo basi na sisi inabidi tubadilike na kutumia mbolea zinazotengenezwa kiasili kama samadi na mboji ili kulinda ardhi yetu. Licha ya mbolea, suala la kulima milimani ni la kuangaliwa, kwani husababisha mmomonyoko wa ardhi iwapo mvua itanyesha katika maeneo haya. Kuna tovuti kadhaa zimeelezea kinagaubaga suala hili pamoja na lile la kuzidisha idadi ya mifugo katika eneo dogo na kuzidisha madhara katika eneo husika, vitendo ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu ardhi na mazingira kwa ujumla. Kwa hiyo sitayaongelea kwa undani sana masuala haya. Inafaa tu kuyaachia majanga ya asili kama vile volkano na matetemeko ya ardhi yaharibu uasilia wa ardhi, na siyo sisi wanadamu kuiharibu kwa makusudi, kwani kwa kufanya hivyo tunajichimbia kaburi.

2. MAJI
Kumekuwa na kauli mbiu kuwa ‘Maji ni Uhai’. Hakuna ubishi katika hili, bila maji hakuna uhai. Lakini je rasilmali hii tunaitumiaje? Sidhani kama tunafanya juhudi za kutosha katika kuhakikisha kuwa tuna matumizi endelevu ya rasilmali hii. Kwanza, katika kilimo huwa tunatumia mbolea za viwandani. Mbolea hizi si zote huchukuliwa na mimea kwa ajili ya utengenezaji wa chakula. Sehemu ya mbolea hupotelea ardhini na kuchafua hifadhi ya maji katika miamba ijulikanayo kama ’aquifers’. Kitendo hiki kwa lugha ya kitaalamu hufahamika kama ’Leaching’. Hatuwezi kuona kwa macho kwa sababu kitendo hiki hufanyika chini ya ardhi, kwa hiyo huhitaji vipimo vya kitaalamu kujua madhara yake katika maji na maisha ya wanadamu kwa ujumla. Katika kilimo hicho hicho, dawa za kuulia magugu na wadudu waharibifu wa mazao mashambani pia huchangia madhara katika maji kwani dawa hizi mara nyingi huenda katika maji iwapo mvua itanyesha katika mashamba yaliyowekwa dawa hizi. Pili, maji ya bahari ndio yamekithiri kwa uchafu, na ndio humo humo tunapata samaki kwa ajili ya kitoweo. Maji machafu ya miji yote ambayo iko kando ya bahari huishia baharini, maji taka ya viwanda ambavyo hupakana na bahari hali kadhalika huishia baharini. Taka za sumu toka viwandani humwagwa baharini. Hali hii pia iko katika maziwa na mito, ingawa si kwa kiasi kikubwa sana kama baharini. Inasemekana kuwa kwa nchi zinazoendelea kama yetu, baadhi ya wavuvi hutumia mabomu katika shughuli zao za uvuvi. Kitendo hiki si tu kwamba kinaua mazalia ya samaki, bali pia ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa maji. Baruti itengenezayo mabomu ni kemikali yenye sumu, sasa basi iwapo itachangayikana na maji, basi sumu hizi huturudia sisi wenyewe aidha kwa kula samaki waliovuliwa kwa mabomu au kwa kunywa moja kwa moja maji hayo. Lakini kwa tamaa zetu za kupata pesa za haraka, tunasahau madhara ya muda mrefu kama haya na kuishia kushibisha matumbo yetu kwa uvuvi wa mabomu. Tatu, kuna ujenzi na kilimo katika vyanzo vya maji. Kama tunayofahamu, vyanzo vya maji ni muhimu kwa maisha yetu, kwa hiyo iwapo tunachafua hatumkomoi mtu, ila ni sisi wenyewe. Nimeliongelea kwa urefu sana suala hili katika makala zilizopita. Katika hali ya kawaida, inatakiwa tuyasafishe maji yaliyotumika majumbani na viwandani ili yaweze kutumika tena kwa shughuli nyingine, lakini tulio wengi hatuna utaratibu huu. Laiti kama tungezingatia suala hili basi uhaba wa maji kwa maeneo mbali mbali ingekuwa ni hadithi tu. Pia hatuna utaratibu wa uvunaji wa maji ya mvua, kwa maeneo mengi ya nchi zinazoendelea. Maji yanayopotea wakati wa mvua ni mengi sana, iwapo tungeyavuna na kuyahifadhi basi tungetatua suala la uhaba wa maji ambalo ni kubwa sana sehemu mbali mbali duniani. Nne, kama itakumbukwa, hivi karibuni wakati nchi ya Israeli ikiwa katika mgogoro na Lebanon, ilipasua kwa makusudi bomba la mafuta kando ya bahari na mafuta yote yaliyokuwa yanasafirishwa katika bomba hilo yakasambaa baharini na kuua viumbe wengi sana wanaotegemea maji hayo ya bahari. Hali hii ilileta usumbufu pia kwa vyombo vinavyosafiri majini katika maeneo hayo. Kitendo hiki ni cha kulaaniwa sana na kila mtu ambaye anajali usafi wa bahari na mazingira kwa ujumla, lakini cha ajabu hakuna hatua za kinidhamu zinazochukuliwa kukomesha tabia hii.


3. HEWA
Madhara ya uchafuzi wa hewa ni rahisi sana kusambaa kwa muda mfupi katika dunia hii. Hii inatokana na sababu kuwa hewa husafiri haraka sana hasa pale inapopata joto. Si ajabu basi iwapo hewa itachafuliwa katika bara fulani na madhara yakajiri katika bara lingine kwa muda mfupi sana. Tumesikia na kuona madhara ya uchafuzi wa hewa, hasa kuharibika kwa hewa ya ’ozone’. Niliongelea kwa kirefu suala hili katika makala zilizopita. Ikumbukwe kuwa kuna makubaliano yalifanyika katika mji wa Kyoto nchini Japan hasa kwa nchi tajiri, kuhusu kupunguza kiwango cha hewa zenye sumu toka viwandani kwenda angani. Hizi ni nchi za G8 zenye viwanda vingi na vikubwa ambavo huchafua sana hali ya hewa, hivyo ilikuwa ni hatua muhimu sana katika suala ziama la kutunza mazingira. Kama kawaida, Wamarekani hawakusaini mkataba huu wa makubaliano, kwa madai kwamba kusaini mkataba huo ni kukubali kuua uchumi wao ambao hutegemea sana viwanda hivyo. Wakaitwa tena nchini Afrika Kusini, wakakataa kwa mara nyingine tena kusaini mkataba huu. Kwa mara nyingine mwaka huu 2006, mwezi wa kumi na moja wamekataa tena kusaini mkataba huo na kurudisha nyuma kabisa juhudi za kupunguza uchafuzi wa hewa. Nchi nyingine zenye viwanda vingi kama Japan, Sweden, China, Ujerumani, Urusi na Denmark wameshaanza kupunguza kwa kiwango cha kuridhisha, uchafuzi wa hewa.

MIKAKATI ENDELEVU
Kuna mambo kadhaa ambayo yanapaswa kuzingatiwa iwapo tunataka kupata matokeo mazuri ya ya kile tunachokipanga.

SIASA DHIDI UTAALAMU!
Kwanza, tupunguze kama si kuacha kabisa kutatua matatizo ya kiufundi kwa mbinu za kisiasa. Pamoja na kwamba siasa inatawala maisha yetu ya kila siku, lakini si matatizo yote yanaweza kutatuliwa kisiasa. Suala la uchafuzi wa hali ya hewa ni la kiufundi, sasa iwapo tunataka kutatua suala hili kwa mbinu za kisiasa ni makosa makubwa sana kwani masilahi ya kisiasa ni ya muda tu. Matatizo kama njaa, ukosefu wa umeme, ukimwi, ukosefu wa maji, uharibifu wa rasilmali na ukosefu wa maadili ni matatizo ya kiufundi, hayapaswi kutatuliwa kisiasa. Yatatuliwe kiufundi kwani naamini kuna wataamu wengi tu wa utatuzi wa matatizo haya, wapewe nafasi. Umbumbumbu (au ni ubabe?) wa Marekani kukataa kusaini mkataba wa Kyoto wa kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa inatakiwa ukemewe na kila mtu anayependa maendeleo ya muda mrefu na si maslahi ya kisiasa. Nasisitiza tena kuwa siamini wala sifikiri kuwa Wamarekani hawajui wanachokifanya katika hili suala la Kyoto. Nina imani kuwa huenda suala hili likapewa umuhimu wa kipekee na wale waliochukua madaraka nchini humo hivi karibuni, tuvute subira.

MAZINGIRA KWANZA, PESA BAADAYE!
Pili, ningependa kuongelea suala la mirahaba ya madini. Kumekuwa na maelezo mbali mbali kutoka kwa wadau wa madini kuwa tunalipwa mirahaba kutokana na madini yanayochimbwa nchini mwetu. Ni sawa kuwa tunapata mirahaba lakini vipi maslahi ya uhai wa hapo baadaye? Kama nilivyoongelea hapo juu, tusiangalie suala la pesa ambalo ni la muda mfupi ila tuangalie matokeo ya kuacha mahandaki katika machimbo ya madini. Nini kitatokea katika miongo kadhaa ijayo iwapo hali itaendelea kuwa kama hivi? Nani ataathirika? Wanaochimba madini sasa kwa teknolojia za kisasa zisizojali mazingira na uhai wetu watakuwa wameshaondoka na faida na kutuachia mashimo ambayo hayatakuwa na msaada wowote kwa wakati huo ambao vizazi vitakavyokuwepo (huenda hata sisi ) vitakuwa havina maji wala miti. Tuige mfano wa hatua zilizochukuliwa katika kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira , kutokana na uchimbaji wa madini katika msitu wa Balangai wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Sipendi kuonekana naingilia masilahi ya baadhi watu katika jamii kwa kupinga uchimbaji wa madini, lakini naongelea suala hili katika muktadha wa kitaalamu zaidi. Watakaopenda kuongelea suala hili katika muktadha wa kiuchumi wanaruhusiwa pia. Unafikiri ni kwa nini hao wanaotaka kuchimba madini katika nchi yetu hawaendi nchi zingine zenye madini kama sisi? Suala ni kwamba nchi hizi wana sera na sheria endelevu sna kuhusu mazingira.

UTASHI WA KISIASA
Kutatua matatizo yanayoikabili dunia kwa sasa kunahitaji utashi wa kisiasa na si utatuzi wa kisiasa. Katika kutekeleza malengo ya milenia, kinachotakiwa zaidi ni utashi huu ninaouongelea, kwani kwa utashi matatizo haya yanatatulika kabisa. Mpaka sasa inasemekana kuwa hazijaonekana juhudi za makusudi katika kutatua matatizo yaliyoanishwa katika malengo ya milenia, kiasi kwamba huo mwaka 2015 wa matazamio huenda mengi kati ya malengo hayo yasiwe yametimizwa. Wewe masomaji wa makala hii pamoja na mimi inapaswa tutimize wajibu wetu katika kuyafanikisha malengo haya, kwani inawezekana kabisa kuyafikia.
Soma hapa kwa habari zaidi.

10/23/06

NISHATI NA MAISHA

UTANGULIZI
Kwa dhana, nishati ni ule uwezo wa kufanya kazi au kitu fulani. Kuna nishati za aina mbalimbali kama vile joto, sauti, mwendo, mwanga na kadhalika. Kuna uwezekano mkubwa sana wa kubadilinishati hizi kutoka aina moja kwenda nyingine kwa kutumia mbinu na vifaa mbali mbali. Kwa mada hii nitaongelea kwa ufupi sana nishati za mwanga na joto.

UMUHIMU WA NISHATI
Kwa maelezo rahisi ni kwamba hakuna maisha bila nishati. Nishati ni chanzo cha uhai wetu, kwani nishati ya mwanga kama ule wa jua hutusaidia kuona na kufanya mambo mbali mbali, hutuletea vitamini D na pia nishati hii husaidia usanisi wa chakula cha mimea, ambayo nasi tunaitegemea kwa chakula chetu. Nishati ya mwendo hutusaidia kujongea kutoka mahali fulani hadi pengine kwa muda mfupi sana kwa teknolojia ya leo na nishati ya joto hutusaidia kwa mambo mbali mbali kama vile kuivisha chakula chetu, kukausha mazao, kurekebisha hali ya hewa majumbani na kadhalika.
Kumekuwa na mwamko mahali mbalimbali hapa ulimwenguni kuhusu mustakabali wa dunia hasa katika suala nyeti la nishati. Mara nyingi dunia imekuwa ikitegemea mimea, madini (makaa ya mawe na nyuklia) na mafuta kama vyanzo vikuu vya nishati za namna mbalimbali.

KUNI NA MKAA
Katika mimea tunapata kuni na mkaa ambavyo kwa nchi kama Tanzania huchangia zaidi ya asilimia tisini ya mahitaji yote ya nishati kwa taifa. Hiki ni kiwango kikubwa sana, kwa hiyo juhudi za makusudi zinatakiwa ili kupunguza kiasi hiki. Kuni hutumika na mkaa kila mahali katika nchi zinazoendelea katika kufanyia kazi mbali mbali, kuanzia majumbani hadi viwandani. Kuni hutumika kuzalisha nishati ya joto katika viwanda vya chai na tumbaku, hutmika kupikia majumbani na matumizi mengine mengi tu. Kwa nchi zilizoendelea kuni hutumika kuchemshia maji, ambayo husambazwa majumbani kwa mabomba maalum kwa ajili ya kuzalisha joto wakati wa baridi. Ni nishati tegemeo sana kwa nchi hizi hasa wakati wa baridi, kwa kuwa kutumia mitambo ya umeme kuzalisha joto ni ghali kwa kiasi fulani.

MAKAA YA MAWE
Makaa ya mawe kwa miaka ya nyuma yalitumika moja kwa moja viwandani kuzalisha nishati za joto na mwendo kwa matumizi mbali mbali. Mpaka sasa kuna maeneo kadhaa hapa duniani ambapo makaa ya mawe hutumika kuzalisha nishati (kama vile mgodi wa makaa ya mawe kule Ilima/KiwiraMbeya). Makaa pia hutumika katika viwanda vya saruji katika kuzalisha joto la kuyeyushia mawe ili yasagwe na kuzalisha saruji. Lakini kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa, ikaonekana kuwa makaa si nishati rafiki wa mazingira yetu, hivyo kukafanyika mabadiliko makubwa sana ya kuiacha nishati hii kwa maeneo mengi. Lakini bado kuna nchi nyingi tu ambazo hazijaiacha nishati hii, ikiwemo nchi ya China ambayo inakuja juu katika maendeleo ya viwanda duniani. Mwelekeo na mkazo vikawa katika mafuta ya jamii ya petroli ambayo kwa sasa yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha ya mwanadamu.

MAFUTA YA PETROLI
Mafuta haya yanatumika kuendesha mitambo ya namna mbali mbali pamoja na ile izalishayo umeme, maarufu kama jenereta. Magari, ndege, meli, baadhi ya treni, huendeshwa kwa nishati hii pia. Kadri muda unavyosonga, nishati hii nayo imeonekana si rafiki wa mazingira kama inatumika katika mazingira ambayo si muafaka. Moshi unaotokana na mafuta haya yanapotumika katika mitambo huwa na athari sana katika mazingira, kwa kuwa huongeza kiasi kikubwa sana cha hewa ya kaboni dayoksaidi katika anga na kuharibu utando wa ozoni. Matokeo yake ni kuwa kunakuwa na ongezeko la joto katika uso wa dunia, na ongezeko hili limeleta athari nyingi sana katika sehemu mbali mbali hapa duniani (nilishaliongelea hili katika mada zilizopita). hio ni moja, lakini pili ni kuwa iwapo kunatokea ajali majini na chombo kinachosafirisha mafuta kikahusika, mafuta hutapakaa katika maji (na kawaida mafuta huelea majini) na kuathiri viumbe wanaoishi katika maji. Kwa viumbe kama samaki, hushidwa kupumua kwa kuwa mafuta huzuia hewa kutoka na kuingia katika maji. Kwa ndege wanaoshi kwa kutegemea uvuvi, mara wapakaapo mafuta haya katika shughuli zao za uvuvi hushidwa kuruka kwa kuwa mbawa zao hushikamana na kukakamaa hivyo kwa wakati fulani hufa. Kwa sasa kuna mikakati kwa nchi zilizoendelea, kuachana na utegemezi wa nishati hii, lakini itachukua muda sana, ingawa inawezekena (rejea makala iliyopita).

MAJI
Kwa miaka mingi nguvu ya maji imekuwa ikitumika kwa namna mbali mbali. Kwa upande wa nishati, maji yamekuwa yakitumika moja kwa moja kuendesha mitambo ya kusagia nafaka, na kwa upande wa Tanzania bado mifumo hii inafanya kazi mpaka sasa. Kwa mfano, katika kijiji cha Kisiwani wilayani Muheza Mkoani Tanga, kuna mtambo wa kusagia nafaka ambao kuendeshwa kwa nguvu ya maji. Kwa upande wa pili, kutokana na maendeleo ya kiteknolojia, maji yanatumuka kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme, na kwa sasa dunia imekuwa tegemezi kwa nishati hii kwa kiasi kikubwa. Hli si shwari sana kwa upande wetu Tanzania, kutokana na maji kutokuwa ya kuaminika na kutokuwa na mfumo mzuri wa urejeshaji maji katika mabwawa mara baada ya kuyatumia. Pia hali ya hewa hasa suala la ukame limekuwa kikwazo kikubwa kwa uendelezaji wa nishati hii. Miradi mikubwa ya umeme wa nguvu ya maji si rafiki wa mazingira, kwa kuwa hutumia maeneo makubwa sana kuhifadhi maji, kwa hio kunakuwa na uhamishaji wa watu na wanyama na mara kadhaa husababisha mafuriko kwa watu waishio kando yake iwapo milango ya bwawa itafunguliwa kupisha matengenezo, kwa kuwa maji hufunguliwa kwa wingi sana. Pia miradi hii hutumia maji mengi sana, kwa hio viumbe wengine ambao hutegemea maji hayo mbele ya mabwawa hawapati maji kwa uhakika (kumbuka suala la vyura katika mradi wa umeme-Kihansi).

NYUKLIA
Ni moja ya nishati mbadala katika kupunguza tatizo la nishati. Kwa sasa ni nchi zilizoendelea tu ndizo zina uwezo na mamlaka ya kutumia nishati hii, kwa kuwa ni ghali sana. Pia inadhibitiwa sana na shirika na nguvu za nishati la Umoja wa Mataifa liitwalo 'International Atomic Energy Agency' (IAEA), kwa kuwa ni nishati hii hii itumikayo kutengeneza silaha za maangamizi, kwa hio wanahofia kuwa iwapo inaachwa bila ya udhibiti basi inaweza kutumika kwa malengo mengine, na si uzalishaji wa nishati. Kwa sasa nchi kama Japan, Korea Kaskazini, India, Iran*, Marekani, Norway na Urusi zinatumia nyuklia kwa kuzalishia nishati. Nyuklia huhitaji uangalizi wa hali ya juu sana, kwa kuwa ikivuja ina madhara sana kwa mwanadamu na viumbe wengine. Ajali ya kuvuja kwa mitambo ya nyuklia ilishawahi kutokea katika mji wa Chernobyl nchini Urusi mnamo mwaka 1986 na kusababisha madhara makubwa!
*(Vinu havijaanza kufanya kazi Iran)

UMEME WA MIONZI YA JUA
Ni teknolojia mpya kwa kiasi fulani, na ni rafiki wa mazingira. Ni mfumo wa kuvuna mionzi ya jua na kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo maalum ijulikanayo kama 'Photovoltaics'. Uzalishaji wa umeme huu hutegemea sana uwepo wa mwanga wa jua na vihifadhi vya umeme huo kama betri. Umeme huu unafaa sana kwa mazingira yaliyo mbali na umeme wa gridi. Ni teknolojia ghali kwa kiasi fulani ingawa ni nzuri.

Kwa namna moja au nyingine tuendelee kujaribu kutafakari na kutafuta suluhisho la matatizo ya nishati yanayoikabili dunia, ili iwe mahali salama pa kuishi wanadamu.
Nafasi yako ni ipi katika hili?
Jadili!

10/11/06

MAFUTA MBADALA

UTANGULIZI
Kumekuwa na kilio sehemu mbali mbali duniani kuhusu uchafuzi wa hewa pamoja na athari zake ambazo dunia imeanza kuonja makali yake. Kilio hiki kinatokana na kuongezeka kwa kiwango cha moshi wenye sumu katika anga, na kuharibu mfumo mzima wa hali ya hewa. Athari zaidi zinaonekana katika utando wa 'ozone', ambao umetobolewa na hewa hizi za sumu. Kazi ya utando huu ni kuzuia mionzi ya jua yenye athari kutufikia moja kwa moja na kutuathiri. Athari ambazo dunia inazipata kwa sasa ni pamoja na ongezeko la joto duniani na kupungua kwa kiwango cha barafu katika milima, kupotea kwa baadhi ya jamii za mimea na wanyama kutokana na ongezeko hili la joto, ongezeko la magonjwa kama kansa na magonjwa mengine ya ngozi. Pia kuna maeneo ambapo utando wa moshi wa viwanda na magari ni mkubwa na hivyo husababisha mvua za tindikali. Mvua hizi hutokana na kuongezeka kwa hewa ya salpha dayoksaidi katika anga. Hewa hii ikizidi angani na kuchanganyikana na maji au unyevu hutengeneza tindikali ya salfarasi 'sulphorous acid', na hii ina madhara sana kwa mimea na wanyama. Tindikali hii huunguza majani ya mimea na kwa wanyama husababisha magonjwa ya ngozi. Kwa nchi za Ulaya ya Magharibi wanafahamu sana madhara ya mvua hizi za tindikali, kwani zimeharibu sana uoto wa asili. Kutokana na sababu hizi basi, kumekuwa na hatua mbali mbali za kupunguza hewa chafu katika anga, na moja ya hatua hizo ni kutumia mafuta mbadala ya kuendeshea mitambo badala ya mafuta ya jamii ya petroli.

MAFUTA MBADALA NI YAPI?
Msisitizo wa kutumia mafuta yasiyo na madhara sana kwa mazingira umekuwa ukipata kasi kadri siku zinavyosonga. Nchi zilizoendelea zimekuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na uzalishaji mkubwa wa mafuta haya mbadala. Mafuta haya yanatokana na mimea kama mbono, miwa, michikichi, alizeti, maharage ya soya na mahindi. Kimsingi kila mmea una uwezo wa kutoa mafuta haya, kulingana na hali ya kiteknolojia iliyopo mahali husika. Mimea tajwa hapo juu, ukiacha miwa na mahindi, hutoa dizeli ambayo nchi zilizoendelea zinatumia kuendeshea mitambo ya namna mbalimbali. Miwa hutoa kimiminika kiitwacho 'ethanol' na hii kutumika sana kuendeshea mitambo pia. 'Ethanol' ni jamii ya pombe inayotengenezwa kwa njia ya mvukizo au mvuke. Kwa jina lingine rahisi hii ni 'gongo' ya kiwandani. Ni nyepesi sana na inashika moto haraka, hivyo wataalamu wameona inafaa kwa mitambo. Kumbuka kuwa karabai zinawashwa kwa mafuta ya jamii hii.

WAZALISHAJI WA MAFUTA MBADALA
Kwa upande wa 'ethanol', wazalishaji wakubwa kwa soko la dunia ni Brazili na Marekani na walianza karibu miaka ishirini iliyopita. Hawa wanazalisha bidhaa hii kutokana na makapi ya viwanda vya miwa. Pia nchi za umoja wa Ulaya ni wazalishaji wakubwa wa bidhaa hii. Kwa upande wa dizeli ya mimea, wazalishaji vinara ni Malaysia, China na Ujerumani. Malaysia ni mzalishaji wa kwanza wa mafuta ya mawese duniani, na dizeli wanayotengeneza inatokana na mawese. Wachina wanatengeneza 'ethanol' kutokana na mihogo na wanapata shehena kubwa ya mihogo hii kutoka Vietnam, Thailand na Indonesia.
Kwa upande wa Brazili, kuna magari milioni tatu yanayotumia ethanol! Wakati huo huo kuna magari milioni moja na laki tatu yanayotumia mchanganyiko wa petroli na ethanol.
(Chanzo cha takwimu: UNIDO/Berkeley BC Aprili 2006)

FAIDA ZA MAFUTA MBADALA
Mafuta haya hayatoi moshi wenye athari kwa anga, kwa kuwa hayana viambata vyenye sumu, kulinganisha na mafuta ya jamii ya petroli. Mafuta ya petroli huchanganywa na madini ya risasi 'lead' na hivyo yakitumika katika mitambo hutoa moshi wenye sumu katika anga.
Kwa kuwa mafuta mbadala hutokana na mimea, huongeza kipato kwa wakulima wa mazao yatoayo mafuta haya. Utengenezaji wa dizeli mbadala hauhitaji teknolojia za hali ya juu sana, tofauti na mafuta ya jamii ya petroli, hivyo hata nchi zinazoendelea zinaweza kumiliki mitambo ya kuzalishia mafuta haya.

TANZANIA NA MAFUTA MBADALA
Kumekuwa na tafiti mbalimbali zinazofanywa na watu na taasisi anuwai nchini Tanzania, kuhakikisha kuwa kunakuwa na maendeleo katika uzalishaji wa dizeli ya mimea. Baadhi ya taasisi zilizofanya utafiti wa mafuta haya ni pamoja na shirika la Msaada wa Kiufundi la Ujerumani (GTZ), Kampuni ya Kukuza Teknolojia (KAKUTE) ya Arusha na Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Mazingira Tanzania (TaTEDO). Kwa upande wa KAKUTE, wao wanafanya uzalishaji mdogo wa dizeli inayotokana na mbono, pamoja na kutengeneza sabuni zake.
Iwapo kutakuwa na msisitizo kwa watu binafsi, mashirika na serikali katika kuzalisha mafuta haya, basi tutaondokana na umasikini, kwa sababu bidhaa hii kwa sasa ina malipo mazuri katika soko la dunia. Nasema hivi kwa sababu tayarai nchini Tanzania tuna viwanda kadhaa vya miwa ambavyo hutoa makapi mengi ya kuweza kuzalisha ethanol na wakati huo huo mimea ya mbono husitawi hata katika maeneo yenye ukame.
Ni kitu kinachowezekana, ila inataka utashi!
Nafasi yako katika hili unaitumia kikamilifu?
Jadili!

9/20/06

YAJUE MALENGO YA MAENDELEO YA MILENIA

UTANGULIZI
Ni mara nyingi tumesikia, ama kuambiwa kuwa kuna malengo ya milenia, lakini huenda si wengi wetu tunaoyafahamu malengo hayo. Ni malengo yaliyoafikiwa mnamo Septemba 8 mwaka 2000, jijini New York Marekani na kuazimia kuwa ifikapo mwaka 2015, basi hayo maazimio waliyopanga yawe yametekelezwa kwa kiasi fulani cha kuridhisha, kama si kuyatekeleza kabisa.
Kwa ujumla kuna malengo manane ambapo nitayaeleza yote kwa ufupi katika makala hii na kuelezea lengo namba saba katika makala yake ya kujitegemea. Nitafanya hivi kwa sababu si busara kuelezea lengo namba saba pekee wakati malengo mengine hayafahamiki. Vile vile ni kwamba kufanikiwa kwa lengo moja basi ni njia ya mafanikio ya kuyafikia malengo mengine pia. Malengo haya yamewekewa viashiria, kujua kama yanatekelezeka ama la! Tafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili ni yangu!

YAFUATAYO NI MALENGO YA MAENDELEO YA MILENIA
1. Kupunguza Umasikini Uliokithiri pamoja na Njaa
Ndani ya lengo hili kuna malengo madogo mawili. Kwanza ni kupunguza hadi kufikia nusu, kwa kwa idadi ya watu ambao wanaishi kwa chini ya kiwango cha dola moja kwa siku, kati ya mwaka 1990 na 2015. (Kwa wakati huu, dola moja ya Kimarekani ni karibu sawa na shilingi 1200 za Kitanzania). Pili, ni kupunguza kwa zaidi ya nusu kwa idadi ya watu wasio na chakula.

2. Elimu Ya Msingi Kwa Wote
Kuhakikisha kuwa hadi mwaka 2015 mahali popote pale, watoto, kwa maana ya wasichana kwa wavulana wawe na uwezo wa kuhitimu elimu ya msingi.

3. Kukuza Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Wanawake
Lengo ni kuondoa tofauti za kijinsia katika shule za msingi na sekondari hadi mwaka 2005 na katika nyanja zote kabla ya mwaka 2015.

4. Kupunguza Vifo Vya Watoto Wachanga
Lengo ni kupunguza kwa theluthi mbili, idadi ya vifo vya watoto walio katika umri wa hadi miaka mitano, kati ya mwaka 1990 na 2015.

5. Kuboresha Afya za Akina Mama
Lengo ni kupunguza kwa hadi robo tatu, idadi ya vifo vya wanawake wazazi, kati ya mwaka 1990 na 2015.

6. Kukabili Virusi Vya Ukimwi/Ukimwi na Magonjwa Mengine Makuu
Lengo la kwanza ni kupunguza na kuukabili Ukimwi na kubadili mwelekeo wake ifikapo mwaka 2015. Lengo la pili ni ni kukabili na kutokomeza malaria na magonjwa mengine makuu hadi kufikia mwaka 2015.

7. Kujihakikishia Uendelevu wa Mazingira
Hapa kuna malengo matatu madogo. Lengo la kwanza hapa ni kuingiza misingi ya maendeleo andelevu katika sera na mipango ya mataifa mbali mbali na kubadili mwelekeo na upotevu wa rasilimali. Lengo la pili ni kupunguza hadi nusu kwa idadi ya watu wasio na maji safi ya kunywa na huduma za maji taka. Lengo la tatu ni kuboresha makazi ya watu angalau milioni mia moja hadi kufikia mwaka 2020.

8. Kuanzisha Ushirikiano wa Kimaendeleo Duniani
Hapa kuna malengo mawili madogo. Kwanza, ni kujenga misingi ya utawala wa sheria na inayotabirika na isiyo na ubaguzi katika mifumo ya biashara na fedha. (Hii inahusisha pia kujifunga na misingi ya utawala bora, maendeleo na kupunguza umasikini, kitaifa na kimataifa). Pili, ni kuyapa kipaumbele mahitaji ya nchi masikini sana duniani (hii inahusisha kuondoa vikwazo katika masoko huru na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi. Pia kupunguza (ama kuondoa kabisa) madeni ya nchi hizi masikini na kutoa misaada kwa nchi ambazo zinaonyesha mwelekeo wa kuondoa umasikini).
Unaweza Kuyasoma zaidi Malengo hayo Hapa

Kwa hiyo ndugu msomaji wa makal hii, haya ndio malengo ya milenia yaliyoazimiwa mwaka 2000.
Katika makala ijayo, nitawaleteeni mjadala wa kiundani wa malengo kadhaa, tukianzia na lengo namba saba.