6/28/06

UNAFAHAMU WALINZI HAI WA MAZINGIRA?

U hali gani msomaji wa blogu hii.
Katika mada ya leo, nataka kukufahamisha kitu muhimu sana katika suala zima la athari za uharibifu wa mazingira, na mustakabali wake katika viumbe hai. Nataka kuongelea kitu kinachitwa bioindicators. Mimi naita viashiria, (nitashukuru kama nitapata tafsiri ya kiswahili sanifu ya jina hilo)

UTANGULIZI
Hiki ni Kitu gani?
Hizi ni jamii za mimea au wanyama (wanyama ni pamoja na wadudu) ambazo huashiria uharibifu mazingira ya sehemu fulani, katika uso wa dunia. Viumbe hawa, huwa katika mfumo-ikolojia wa eneo fulani. Iwapo kunakuwa na mabadiliko katika hali ya mazingira ya mahali walipo, ambayo si ya kawaida, basi viumbe hawa huonyesha mabadiliko fulani, aidha katika mfumo wao wa lishe, maumbo, kibiolojia au wa kitabia. Kila kiumbe kina aina yake ya tahadhari ya uharibifu huu wa mazingira, iwe ni mimea au wanyama.

KAZI ZA VIUMBE HAO (BIOINDICATORS)
Viumbe hai hao wana kazi kubwa kadhaa katika suala zima la ulinzi wa mazingira. Kwanza, hutoa utambuzi wa uharibifu wa mazingira katika eneo fulani walipo. Pili, hutoa taarifa za uvamizi wa kitu ambacho si cha kawaida katika eneo husika kutokana na uharibifu ambao unatokea. Tatu, hutoa taarifa juu ya hali ya usafi wa mazingira wa eneo husika na nne, hutumika kufanya majaribio ya hali ya usafi wa maji, kama yamechafuliwa au la.

VIASHIRIA-MIMEA (PLANT INDICATORS)
Katika utafiti makini wa kisayansi, kuwepo au kutokuwepo kwa jamii fulani ya mimea katika maeneo fulani, huweza kutoa taarifa muhimu sana juu ya athari za kimazingira zinazotokea katika eneo hilo. Tuchukulie mfano wa mimea fulani midogo sana ya kijani "lichens", inayoota kama utando katika miamba na miti yenye unyevu nyevu . Hii mara nyingi hupatikana katika misitu. Mimea hii huweza kubadilika haraka sana iwapo kuna mabadiliko yasiyo ya kawaida katika msitu, kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, ukame na mfumo wa hali ya hewa ya msitu husika. Kutokomea kwa mimea hii katika eneo husika inaweza kuwa ni kiashiria cha hali tete ya uharibifu wa kimazingira kama vile uwingi wa hewa ya naitrojeni, madini ya oksaidi ya salfa au vichafuzi vingine vya jamii ya salfa.

VIASHIRIA-WANYAMA (ANIMAL INDICATORS)
Viumbe hai wadogo wadogo, wasioonekana kwa macho, huweza kuwa viashiria vya athari za mazingira, iwe ni katika maji au nchi kavu. Viumbe hawa wana uwezo wa kuzalisha protini mpya katika miili yao, ili kujikinga na athari mbaya za uharibifu wa mazingira, iwapo kunakuwa na vitu visivyo vya kawaida vinavyochafua mazingira yao. Protini hizi, huweza kuwa ni dalili za tahadhari, kuwa kuna uharibifu fulani katika mazingira walipo viumbe hao. Wanyama wengine hubadili matabaka ya miili yao, ili kujilinda na athari hizi. Hivyo basi, wataalamu wanapoona mabadiliko yasiyo ya kawaida katika maisha ya wanyama hawa, huweza kutambua uharibifu uliopo katika mazingira ya eneo husika na kuchukua hatua.

MATUMIZI YA VIASHIRIA HIVI
Kama tulivyoona hapo juu, viumbe hai viashiria hubadilika hali zao kunapokuwepo na mabadiliko katika mazingira walipo. Hata hivyo mabadiliko haya hutofautiana kati ya viumbe hawa. Mifumo hii ya kijenetiki, hutumika sana katika kutunza maliasili, kwa kujua mabadiliko katika hali za viumbe hai katika misitu. Ni rahisi kwa kiasi fulani kujua mabadiliko katika mifumo-ikolojia ya maeneo fulani kwa kutumia viumbe hawa. Uchafuzi wa maji pia huweza kugundulika kwa kutumia viumbe hai hawa, hasa kunapokuwa na madini kama 'cadmium au benzene' katika maji. Iwapo kunakuwa na madini haya katika maji, miili ya viumbe hai viashiria huwa na mabadiliko yasiyo ya kawaida. Madini haya si salama kwa matumizi ya binadamu.

Vyura, pia ni kati ya viumbe hai ambao hutumika mara kwa mara na wanasayansi katika kugundua athari za uharibifu wa mazingira. (kama una kumbukumbu nzuri, utakumbuka suala la vyura wa Kihansi Morogoro, walipoathirika kwa kukosa kiasi fulani cha maji ambacho ni muhimu kwa maisha yao, baada ya mradi wa umeme kutumia maji mengi kuliko kawaida). Kuna sababu kadhaa za mabadiliko ya maisha ya vyura, hasa kunapokuwa na uharibifu wa mazingira yao kwa namna fulani. Vyura hutaga mayai katika maji, hivyo muda wao mwingi huutumia katika maji. Hutaga mayai yaliyo wazi (nje) hivyo hutegemea maji kuyaangua. Wana ngozi ambayo kwa kiasi fulani hupitisha maji, hivyo huweza kuhisi mabadiliko mara moja. Ilishatokea pia katika Ziwa Manyara mkoani Manyara, kuwa kulikuwa na mabadiliko katika mtiririko wa maji. Mimea jamii ya mwani (algae) iliathirika, na ndege jamii ya korongo na heroe ambao hutegemea mimea hiyo kwa lishe yao pia waliathirika. Hii ni mifano michache tu, lakini kuna viumbe wa namna nyingi ambao hutumika kugundua athari za mazingira kwa maeneo mbali mbali hapa duniani.

TUFANYE NINI?
Hatuna budi kuangalia kwa makini shughuli zetu, ambazo nyingi ya hizo si rafiki wa mazingira, kama vile uchomaji wa misitu, uchimbaji na usafishaji wa madini kwa kutumia kemikali zenye athari kwa mazingira. Ni vizuri tukazalisha, lakini pia ni vema kuangalia mustakabali wetu na viumbe wengine ili tusiwaathiri na tusijiathiri sisi wenyewe. Viumbe hai viashiria, ni watoa taarifa wazuri wa athari tunazofanya, hivyo tuangalaie upya namna nzuri ya kutumia rasilimali zetu.

6/15/06

SERIKALI NA MIFUKO YA PLASTIKI "RAMBO"

UTANGULIZI
Hivi karibuni, yaani tarehe 15 Juni 2006, waziri wa fedha mheshimiwa Zakhia Hamdani Meghji aliwasilisha bajeti ya matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007 katika kikao cha bajeti cha bunge la Tanzania. Kama ilivyo kawaida, wengi wetu tulihamishia usikivu wetu Dodoma kusikiliza yale tuliyoandaliwa kwa mwaka wa fedha ujao. Kwa mtazamo wa wengi ni kwamba bajeti hii ina afadhali ukilinganisha na iliyopita, kwa kuwa imekumbuka maeneo mengi muhimu, kama vile kupunguza kodi katika mafuta, kuongeza ruzuku kwa pembejeo za kilimo na kuongeza mishahara ya watumishi. Ni mengi yanavutia katika bajeti ya mwaka huu, lakini kama ilivyo ada watu tunatofautiana katika mawazo. Kuna wanaopinga kuwa bajeti haijafanya lolote katika kumuinua mtu wa kipato cha chini. Maneno haya tumeyasikia mahali pengi hasa kutoka kwa wanasiasa maarufu, lakini ni haki yao kusema hivyo, kwani katiba inamruhusu kila mtu kutoa maoni yake kadri anavyotaka.
Kwa upande wangu, nilivutiwa na kipemgele cha kuongeza kodi katika mifuko laini ya plastiki, maarufu kama 'rambo' kutoka 15% hadi 120%, naunga mkono kodi hii, na ndio suala ambalo nimeliweka katika mjadala moto hapa mahali.


AINA ZA MIFUKO YA RAMBO
Mifuko ya rambo hutengenezwa kwa plastiki laini aina ya Low Density Polyethylene (LDP). Kuna mingine ambayo hutengenezwa kwa plastiki ngumu aina ya High Density Polyethylene (HDP), lakini hii si maarufu sana kama ile laini. Tofauti rahisi ya aina hizi za mifuko ni kwamba, mifuko laini haipigi kelele inapopapaswa na ile migumu hupiga kelele. Hii ndio tofauti rahisi na ya wazi ambayo mtu wa kawaida hutumia kutofautisha aina hizi. Lakini hata katika mfumo wa kikemikali, bidhaa zitumikazo kutengenezea aina hizi za mifuko hutofautiana. Tofauti hii ni kwamba, malighafi itumikayo kutengenezea mifuko laini haiwezi kurejeshwa katika hali yake ya awali kwa sababu wakati wa utengtenezaji wake, hufanyika badiliko la kikemia (chemical Change) badala ya badiliko la kiumbo (physical change) ambalo ni rahisi kugeuza na kutengeneza kitu kingine.

MATUMIZI
Ingawa kwa kiasi kikubwa matumizi hufanana, kuna tofauti ndogo ndogo. Mara nyingi mifuko laini ni midogo kwa muundo na myepesi, kwa hio haitumiki kubeba vitu vizito, tofauti na ile migumu ambayo hutumika kubebea vitu vizito. Kwa mfano, mara nyingi, watunza bustani za miti hutumia mifuko migumu katika kuotesha miti kwa kuwa hudumu kwa muda mrefu tofauti na ile laini ambayo huharibika ndani ya muda mfupi. Kuna matumizi ya aina mbali mbali ya mifuko hii kadri mtu atakavyotaka, na niliyotaja hapo juu ni baadhi tu.

ADHA ZA MIFUKO HII
Mifuko ya rambo imekuwa ikipigiwa kelele sana sehemu mbali mbali kuwa inachafua mazingira, kutokana na utaratibu wetu mbovu wa utupaji wa taka. Mifuko hii hupatikana kwa bei rahisi sana, na wakati mwingine hutolewa bure kabisa baada ya mtu kununua bidhaa. Mara nyingi mifuko hii huzagaa mahali pengi kutokana na kutoitupa katika mahali stahili. Suala hili limekuwa sugu, kwa nafikiri ndio sababu imeamua kupandisha kodi yake kutoka asilimia 15 hadi 120! (rejea Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2006/07 ukurasa wa 45). Hali kadhalika, mifuko hii mara nyingi hutumika kubebea vyakula kwa hiyo huwa na masalia ya vyakula wakati fulani. Ndege wa jamii mbali mbali, hasa jamii ya kunguru huiokota na kuisambaza kila mahali, katika harakati zao za kujitafutia riziki, kiasi cha kuleta kero. Vivyo hivyo, wakati wa mvua mifuko hii hukusanyika pamoja na taka nyingine na kuziba mitaro ya kupitisha maji taka. Hali hii husababisha maji kutuamac na kuleta harufu mbaya. Maji haya ni mazalio mazuri ya mbu waletao malaria. Ni maji haya haya ambayo yanaleta kipindupindu kisichoisha katika baadhi ya miji yetu. Mifuko hii imesambaa sana katika barabara zote kuu na kuchafua maeneo ya kando ya barabara hizo, hasa ziendazo mikoani. Hii ni kutokana na baadhi ya mabasi yasafirishayo abiria kutokuwa na utaratibu wa ukusanyaji wa taka katika mabasi yao, ili ziweze kutupwa mahali stahili. Mifuko hii, haiozi kirahisi ifukiwapo, hivyo husababisha usumbufu mara eneo husika linapotumiwa kwa matumizi mengine.

UTATUZI WA ADHA HIZI
Kuna namna nyingi sana endelevu za kuweza kukabiliana na suala zima la uchafuzi wa mazingira hasa suala la kutupa taka ovyo. Kwanza, inabidi tuwabane wasafirishaji wa abiria hasa wa masafa marefu, ambao kwa namna moja au nyingine hulazimika kusimama njiani ili kupata chakula. Hawa ndio chanzo kikuu cha kusambaa kwa mifuko laini njiani. Nasema hivi kwa sababu, muda wa dakika kumi hadi kumi na tano wanazotoa kwa ajili mapumziko na chakula hazitoshi, hivyo abiria hulazimika kunuua chakula na kula ndani ya gari na kutupa mifuko laini njiani, mara baada ya kumaliza kula. Tuwabane ili wawe na sehemu za kuhifadhia taka katika mabasi yao. Suala hili linawzekana, na linafanya kazi. Kama huamini, tembelea mbuga ya wanyama ya Mikumi, uone walivyo wakali kuhusu kutupa mifuko na na chupa za maji katika maeneo yao.
Suala lingine, ni kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira, hasa kwa watu wa mijini kuhusu namna ya kutupa taka ngumu mahali panapotakiwa. Inashangaza sana kuona kuwa watu hutupa mifuko laini na taka nyingine ngumu chini au pembeni ya pipa la taka wakati pipa liko hapo hapo. Hawa wanahitaji kuelimishwa kama si kuadhibiwa.

MIFUKO MBADALA
Pamoja na serikali kuchukua hatua katika kudhibiti usambaaji wa mifuko laini, kuna kundi kubwa la watu ambao wameona kuwa serikali haijawatendea haki kabisa. Baadhi yao ni wafanyabiashara waagizao mifuko hii toka nje ya nchi, na wasambazaji wao waliopo mahali mbali mbali hapa nchini. hata hivyo ningependa kutoa ushauri kwao, na kwa wengine. Ushauri huu ni kuwa, tuanze kutumia mifuko mbadala ambayo ni rafiki wa mazingira. Kwanza tutumie mapakacha. hii ni mifuko ya asili inayotengenezwa kwa makuti (majani ya minazi na michikichi). hufaa sana kubebea bidhaa za namna anuwai kama vile matunda, nazi viazi na kadhalika. ikifukiwa, mifuko hii huoza na kusababisha mbolea. Pili, tutumie bidhaa zinazotengenezwa kwa ukindu na mimea ya jamii yake. Hufaa saa kwa matumizi ya namna mbali mbali na tukiitumia tutakuwa tunakuza uchumi wa nchi kwa kuwaongezea kipato watengenezaji wake. tatu, tutumie mifuko ya karatasi za kawaida kama vile mifuko ya khaki. Mifuko ya namna hii huoza mara inapofukiwa (biodegradable), hivyo haiathiri mazingira. Pia kuna mifuko inayotengenezwa kwa nyuzi za 'Jute'. Jute ni malighafi itumikayo kutengeneza magunia. Mifuko hii ya jute ilikuwa maarufu sana siku za nyuma, kabla ya ujio wa rambo na ilikuwa na msaada mkubwa sana. Kwa sasa imeanza kurudi sokoni, kwa hiyo hatuna budi kuitumia kwa wingi. Kuna mifuko ya namna nyingi ambayo inaweza kutumika badala ya mifuko laini ya plastiki, ni suala la uamuzi na utashi tu.
Inawezekana kufanya mabadiliko. Je uko tayari?
Jadili.

6/13/06

UNG'OAJI WA MIANZI MKOANI IRINGA: NI SAHIHI?



UTANGULIZI
Ndugu wanablogu wenzangu, nimesoma makala ya Bw Johnson Mbwambo ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za mazingira Tanzania, ambayo ilitoka katika gazeti la Nipashe tarehe saba mwezi Juni. Ilinivutia na kunishitua kidogo, lakini nikaona niisome na kutoa maoni yangu kuhusu utaratibu mzima wa Serikali ya Mkoa wa Iringa kuhusu mpango wa kung'oa mianzi katika vyanzo vya maji. Yeye Bw Mbwambo ameandika makala kutokana na mahojiano aliyofanya na viongozi wa Mkoa wa Iringa juu ya uamuzi wa serikali na NGO katika mkoa wa Iringa, wa kutaka mimea jamii ya mianzi iliyo katika vyanzo vya maji ing'olewe, kwa kuwa si rafiki wa mazingira, kwa maana ya kwamba inakausha vyanzo vya maji. Ningependa kuongelea masuala machache muhimu katika makala yake hiyo isemayo "Operesheni ya kung'oa mianzi yapamba moto mkoani Iringa" .

MIANZI NI NINI?
Hii ni jamii ya mimea ambayo wataalamu wa elimu-mimea wameiweka katika kundi la majani yanayotoa maua, na si miti. Hii inatokana na jamii nyingi za mianzi kuwa na sifa za majani zaidi kuliko miti. Mianzi hupatikana duniani kote, lakini hutofautina kutokana na tofauti ya hali ya hewa ya sehemu mbali mbali. Mianzi ya kitropiki ni tofauti na ile ya nchi za baridi, hivyo hivyo mianzi ya sehemu kame ni tofauti na mianzi ya sehemu zenye unyevu wa kutosha. Mimea hii hupatikana katika jamii ya Bambuseae. kuna jamii 91 na aina zaidi ya elfu moja za mianzi kote duniani na kila aina ina sifa tofauti kulingana na mahali aina hiyo ilipo.Jamii za mianzi hutofautiana kwa urefu, kuna ile ambayo ikikua sana hufikia sentimeta chache hadi kukomaa, na ile ambayo hukua hadi kufikia urefu wa meta arobaini hadi kukomaa. Upana wa shina la muanzi hupishana sana kati ya jamii na jamii kutoka milimita moja hadi thelathini. Hata utoaji wa maua wa mianzi hutofautiana sana. Kuna jamii ambazo hutoa maua baada ya miaka 28 tu na ile ambayo hutoa maua baada ya miaka 120, (rejea Troup 1921) Synchronous'Gregarious' Flowering Species Table. Kuna jamii nyingi za mianzi ambazo hukua kwa wastani wa sentimeta 30 kwa siku (futi moja!), na baadhi ya jamii nyingine zimewekwa katika rekodi kwa kukua kwa wastani wa sentimeta 100 (mita moja!)kwa siku.
Kwa hapa Tanzania, mianzi hupatikana katika mikoa mingi sana,kama vile Tanga, Mbeya, Iringa, Ruvuma na Rukwa na kadhalika na matumizi yake pia hutofautiana kati ya mkoa na mkoa.


MATUMIZI YA MIANZI
Aina za matumizi hutofautiana kati ya sehemu na sehemu, na kati ya jamii moja na nyingine. Kwa wenzetu Wachina mianzi michanga huliwa na ile iliyokomaa hutumika kutengenezea karatasi, na vile vile hutumika katika matambiko yao kwa kuombea umri mrefu wa kuishi. Kwa Wahindi, mianzi ni alama ya urafiki wa heshima, kwa maana kwamba mtu kukirimiwa kwa bidhaa za mianzi (kama viti, vikombe nk) humaanisha urafiki. Mianzi hutumika kutengezea vyombo vya ndani, kama vile vikombe, nyungo, vikapu na matenga. Kwa Wanyakyusa na Wasafwa wa mkoani Mbeya, kuna vifaa vya kukamulia na kuhifadhia maziwa ambavyo huita 'kitana' au 'tana'.Mianzi hutumika kutengenezea viti, vitanda na meza, mianzi hutengeza madaraja, hujenga nyumba ambazo husilibwa kwa matope pamoja na vyoo. Mianzi hutumika kutengeneza mikongojo (fimbo za kutembelea) na bakora, hutumika kutengenezea mitumbwi pamoja na sakafu. Kuna jamii ambazo hutengeneza filimbi za mianzi (zipo katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Iringa na Rukwa). Mianzi hupandwa sehemu za makazi kama uzio.
Kwa ujumla kuna matumizi mengi mno ya mianzi, ambayo si rahisi kuyaeleza yote hapa.
Kibiolojia, mianzi ina faida yake pia. Husaidia kuzalisha hewa ya oksijeni, ambayo ni muhimu kwa maisha ya wanyama.

Mkoani Iringa mianzi ina matumizi ya aina yake. Kwanza mianzi michanga hutumika kutengenezea pombe maarufu ya 'Ulanzi' ambayo husafirishwa hadi mikoa jirani ya Ruvuma na Mbeya. Mianzi hii michanga hukatwa inapofikia kimo cha kuanzia futi mbili hadi nne na hapo huwekwa kifaa maalum chenye uwazi kwa juu kilichotengezwa kwa mwanzi pia. Kifaa hiki hugema utomvu wote toka katika mwanzi mchanga na kuuhifadhi> Utomvu huu baadaye huchachuka na kuwa pombe-ulanzi. Ni pombe maarufu sana makoani hapo. Pili, mkoa wa Iringa ni maarufu kwa ulimaji wa nyanya. Mianzi hutumika kutengenezea matenga ya kuhifadhia na kusafirishia nyanya kwenda sokoni.Tatu, mianzi hutumika kutengeneza mazizi ya mifugo, hasa maeneo ya vijijini, pia ni bidhaa muhimu sana ya ujenzi wa nyumba, hii ni sehemu zote, yaani mijini na vijijini.

MGONGANO WA MASLAHI
Amri ya serikali ya mkoa wa Iringa kwa upande fulani inaweza kuwa sahihi, hasa kama kuna ushahidi wa kutosha wa kuweza kutumika kuhalalisha uondoaji wa jamii hii ya mimea katika vyanzo vya maji. Sina uhakika kama amri hii inatekelezwa mkoani Iringa pekee au na maeneo mengine yenye mianzi katika vyanzo vya maji. Tukumbuke kuwa, miaka michache iliyopita kulikuwa na mjadala kuhusu miti jamii ya eucalyptus, kwamba ukuaji wake huhitaji maji mengi, hivyo jamii hii ya mimea ilikuwa hatari kwa vyanzo vya maji. Uondoaji wa miti hii ulileta migingano katika maeneo mengi ya nchi, hasa ikizingatiwa kuwa ni miti tegemeo kwa sekta nyingi sana, hasa viwanda. Miti hii (eucalyptus)ni nishati kuu katika mashamba na viwanda vya chai vilivyopo nchini, na pia ni tegemeo kwa TANESCO kwa kuwa hutengeneza nguzo za kusambazia umeme kwa kutumia miti hii. Miti hii ni nishati tegemeo katika kukausha tumbaku. Ni kwa sababu hizi na nyingine, ambazo zilifanya amri kwa watu, ya kuondoa miti hii iwe na malalamiko kutoka kila upande.
Ni ukweli kuwa mianzi mingi imepandwa katika sehemu zenye maji (ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji, kwa kuona kwangu mashamba mengi ya mianzi katika mikoa ya Iringa na Mbeya. Sijapata uhakika kama kweli mimea hii hukausha vyanzo vya maji, ndio sababu nasisitiza kuwa ni vizuri kukawa na ushahidi wa kutosha usio na mawaa kama vile machapisho ya kitaalamu, kabla ya 'kuisulubu' mimea hii muhimu. Kwa upande wa wadau ambao hutegemea sehemu ya mapato yao kutokana na mianzi(kama vile wagema na watengeneza matenga),inawezekana wakawa na mwitikio hasi, hasa kama hawajaelimishwa vya kutosha kuhusu athari za mianzi katika vyanzo vya maji. Hawa wataona moja kwa moja kuwa ajira yao inayoyoma.
Kwa upande wa serikali, wao ni watekelezaji wa sera zilizotungwa na bunge, ambazo aghalabu huwa za manufaa kwa jamii kwa ujumla. Hivyo basi, si ajabu kwa serikali kutekeleza sera ambayo inaonekana kuwa ina manufaa kwa wananchi wake. Kwa mtazamo huo, kama serikali imeona kuwa mianzi haifai kuwa katika vyanzo vya maji, basi haina budi kuiondoa mimea hiyo katika maeneo ya vyanzo vya maji ili kuwanusuru wananchi wake na baa la ukame (kama lililotokea miezi michache iliyopita).

UPANDAJI MITI MBADALA
Katika makala ya Bw Mbwambo, serikali imetaja na kupendekeza aina kadhaa za miti ambazo zitapandwa katika maeneo ya vyanzo vya maji na sehemu nyingine ambazo mianzi itaondolewa.Miti hiyo ni migunga, mizambarau na mivinje. Kuna jamii nyingine za miti ya asili ambazo zipo mkoani Iringa na zinafaa kupandwa katika vyanzo vya maji. Jamii hizi ni mikuyu (sycamore/fig tree) "ficus sycomorus", mivumo "ficus sur" ,albizia gummifera, mikoche "hyphaene compressa" na mingine mingi. Hii inafaa sana katika ulinzi wa vyanzo vya maji.

MUHIMU
Kama kweli serikali imepania kuondoa mianzi katika vyanzo vya maji, basi ni bora wananchi wakaelimishwa kuilinda miti mbadala, ili isije ikahujumiwa na wale walioondolewa mianzi yao, hili lipo na laweza kutokea.

Ndugu msomaji wa makala hii, ni nani yu sahihi katika suala hili? Ni serikali, au ni wananchi walioishi na mianzi hii kwa muda mrefu?
Jadili

6/12/06

ASILI, FAIDA NA ADHA ZA MAGUGU-MAJI

UTANGULIZI
Magugumaji ni kati ya mimea inayosifika sana kwa kuzaliana hapa duniani, inayopatikana katika mazingira yenye maji kwa msimu wote, kama vile kwenye mito, ziwani,kwenye madimbwi, kwenye mitaro na miferejini.Unaweza kuvuna tani mia mbili za magugumaji kwa ekari moja tu! Ni mmea wa kijani ambao humea kwa kutambaa, hutoa maua ya rangi ya zambarau au hudhurungi na huweza kurefuka hadi kimo cha futi tatu. Mmea huu ni moja ya mimea ya jamii ya "Pickerelweed" au "pontederiaceae" (jamii ya magugu yanayostawi katika maji). Kwa jina la kitaalamu, mmea huu hufahamika kama 'eichhornia crassipes' na kwa Kiingereza hujulikana kama 'Water Hyacinth'.

ASILI YA MAGUGUMAJI
Takwimu za wataalamu wa elimu-mimea, zinaonyesha kuwa asili ya mmea huu ni katika nchi za kitropiki za Amerika ya Kusini, lakini kwa sasa mmea huu umesambaa katika mabara yote. Kwa nchi kama Marekani mmea huu ulisambaa kati ya mwaka 1884 na 1885 mjini Louisiana. Kuna mtu ambaye alikuwa katika mnada wa pamba katika nchi za Amerika ya kusini, akachukua mmea huu kama pambo la nyumba yake. Kwa kutojua, alitupa masalia ya mmea huo katika mto wa Mtakatifu Jones,baada ya kuzaliana sana kuliko alivyotarajia, na hatimaye mmea huo ukasambaa katika majimbo mengine ya Marekani. Kwa Afrika Mashariki, inasadikika kuwa mmea huu uliletwa enzi za ukoloni wa Waingereza, yaani kuanzia mwaka 1920, na hupatikana sana katika Ziwa Viktoria katika Mikoa ya Mara na Mwanza kwa upande wa Tanzania, na maeneo mengine yanayozunguka ziwa hili katika nchi za Kenya na Uganda.

MAZINGIRA YAKE
Magugumaji hustawi sana katika maji yaliyotuama, au yale yenye mwendo mdogo sana. Kama nilivyotaja hapo mwanzo, mmea huu hupatikana ziwani, mitoni, madimbwini, mitaroni na maeneo mengine oevu yanayofanana na hayo. Huweza kuota kwa kutawanya mbegu zake au kwa vikonyo vyake, na hutengeneza chakula chake moja kwa moja toka katika maji.

FAIDA NA MATUMIZI YA MAGUGUMAJI
Mmea huu una faida kadhaa, na huweza kutumika kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi. Mmea huu, kama nilivyotaja hapo juu, hupata chakula chake kutokana katika maji, hivyo basi, hutumika kuchuja maji taka na kuwa maji masafi kwa matumizi ya kubinadamu yasiyo ya moja kwa moja, kama vile kilimo cha umwagiliaji na ujenzi. Mfano mzuri unapatikana katika madimbwi ya maji taka ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo maji taka hukusanywa katika eneo moja na kuchujwa katika hatua mbali mbali kabla ya kusafishwa kwa matete na magugumaji, katika hatua za mwisho. Maji haya hutumika kumwagilia mpunga na mboga mboga, na pia hutumiwa na wanyama pori walio katika eneo hilo. Faida nyingine ya magugumaji ni katika kazi za sanaa za mikono. Nchini Kenya kwa mfano, kuna mradi ujulikanao kama 'Water Hyacinth Utilization Project' (WHUP), katika mwambao wa ziwa Viktoria, ambao hufanya matumizi endelevu ya magugu maji. Mradi huu hushughulika na utengenezaji wa vikapu, majamvi, kofia, meza, vivuli/viambaza, makaratasi, vitabu, karata, mikeka na vitu vingine muhimu kwa kutumia sehemu anuwai za mmea huu, kama vile maua, majani, shina na vikonyo. Kwa mfumo huu basi, mmea huu umesababisha ajira kwa watu wa maeneo hayo.
Ajira nyingine ya namna yake, ni kwa wale walioajiriwa katika udhibiti wa usambaaji wa magugu haya. Hawa huajiriwa ili kudhibiti magugumaji kusambaa ndani zaidi ya ziwa, kama tutakavyoona hapa chini.

ADHA ZA MAGUGUMAJI
Katika maeneo mengi duniani ambapo magugumaji hupatikana, mara nyingi huchukuliwa kama mmea usiotakiwa, ha hivyo kila juhudi hufanywa kuhakikisha kuwa mmea huu unaondoshwa. Shida kubwa ni kwamba, mmea huu huzaliana kwa kasi kubwa ya ajabu, kiasi kwamba juhudi kubwa pamoja na gharama huhitajika ili kudhibiti usambaaji huu wa kasi. Kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa mmea huu hustawi katika mazingira yenye maji, basi mmea huu ni adha kwa shughuli zote ambazo hufanyika katika maji. Mmea huu huzuia shughuli za uvuvi, hunasa katika panga boi za vyombo vya majini,huzuia uzamiaji na upigaji mbizi, huziba mabomba ya kusafirishia maji ya kuzalishia umeme na shida nyingine nyingi. Magugumaji husababisha utando mkubwa mfano wa jamvi katika maji, na kuzuia mionzi ya jua na hewa ya oksijeni kupenya chini ya maji, hivyo huzuia upatikanaji wa viumbehai wengine katika eneo hilo, hasa jamii ya mimea. Mazingira haya ya ukosefu wa oksijeni katika maji, yakichangiwa na utando mkubwa wa magugumaji hufanya maji yasitembee na hivyo kuwa mazalio makuu ya mbu waletao malaria. Ni sababu hizi hufanya watu wengi wayachukue magugumaji na kuchukua hatua za kuyatokomeza. Kuna kukinzana kwa kiasi kikubwa kwa mawazo katika suala zima la magugumaji.
Hapa ni kila mtu na mtazamo wake, watengenezaji wa samani huona yana faida, na watumiaji wengine wa maji huona kama ni bughudha tu!

UDHIBITI NA UTATUZI WA ADHA ZA MAGUGUMAJI
Kuna taasisi kadhaa ambazo hushughulika na udhibti wa ueneaji wa magugumaji. Pia kuna watu binafsi ambao hukerwa na maimea hii, hivyo huamua kuondoa kwa mikono. Kwa upande wa ziwa Viktoria, nchi zote tatu za Afrika Mashariki zina mipango endelevu ya kudhibiti kuenea kwa magugumaji, na kwa Tanzania na mradi wa LVEMP (Lake Victoria Environmental Management Project), ambao pamoja na mambo mengine hushughulika na usafi na ulinzi wa mazngira wa ziwa tajwa. Katika nchi nyingine zenye magugumaji, kuna wadudu wajulikanao kwa kitaalamu kama 'neochetina' ambao 'hupandwa' makusudi ili kula magugumaji. Hata hivyo, kiwango kikubwa cha kuzaliana cha magugumaji huzidi uwezo wa wadudu hao wa kuyala. Inasemekana pia kuwa samaki aina ya sangara ambao hupatikana kwa wingi katika ziwa Viktoria walipandikizwa kwa ajili ya kula magugumaji, lakini kasi yao ya ulaji inazidiwa kwa mbali na kasi ya ukuaji wa magugumaji. Kuna dawa za viwandani za kuulia mmea huu, lakini haishauriwi sana kuzitumia kwa kuwa nyingi kati ya dawa hizo si rafiki wa mazingira, na huua viumbe wengine waishio majini.Badala yake, mitambo ya kusaga magugumaji hutumika zaidi, hasa katika ufukwe wa ziwa hili kwa upande wa Kenya.

Ndugu msomaji wa makala hii, umeona faida na adha za magugumaji,japo kwa ufupi tu. Una mtazamo gani kuhusu mmea huu?
Jadili

6/6/06

YAJUE MAENEO YA RAMSAR KATIKA TANZANIA (RAMSAR SITES)

Utangulizi
Maeneo ya Ramsar ni sehemu ya ardhi oevu duniani, (wetlands) ambayo yana umuhimu wa pekee duniani katika suala zima la uhifadhi wa mazingira. Ardhi oevu ni ile ardhi ambayo kwa msimu wote wa mwaka huwa na unyevunyevu. Jina hili "Ramsar" linatokana na mji wa Ramsar nchini Iran ambapo ndipo mkataba wa kutunza maeneo ya ardhi oevu duniani ulisainiwa, mnamo mwaka 1971. Kwa hiyo basi, mwaka 1971 ndipo yalipofanyika maamuzi ya kulinda maeneo ya ardhi oevu dhidi ya uharibifu, ili yaweze kutumika katika shughuli endelevu, kama vile vyanzo vya maji. Mpaka sasa, kuna mataifa 152 duniani yaliyotia sahihi mkataba huu wa kulinda ardhi oevu, ikiwemo Tanzania. Kuna maeneo tengefu 1608 ya Ramsar duniani yanayochukua ukubwa wa hekta milioni 140, kati ya haya Tanzania tuna maeneo manne tu, ambayo tutayaelezea hapa chini.


Nini umuhimu wa Maeneo haya?
Maeneo ya Ramsar yana umuhimu wa kipekee katika jamii. Kwanza, yana bioanuwai adimu sana hapa duniani ambazo aghalabu hupatikana maeneo hayo tu. Pili, ni vyanzo vikuu vya maji katika maeneo mengi diniani, hivyo, kama yakiharibiwa kwa shughuli za kibinadamu basi uhai wa viumbe hao adimu utatokomea pia. Maeneo haya ni chanzo kukuu cha nishati ya umeme, ambapo kwa namna moja au nyingine, mito inayozalisha umeme hutiririka kutoka katika nyingi ya ardhi hizi oevu. Chukulia mfano wa bonde la mto Rufiji, bonde hili huanzia katika milima ya Uporoto mkoani Mbeya na kusambaa katika mikoa mingine ya Iringa na Morogoro, ambapo kuna bonde la mto Kilombero ambalo ni maarufu kwa kilimo cha mpunga na ni moja ya maeneo tengefu ya Ramsar. Kwa mfano huu mmoja, nadhani tunaweza kuelewa japo si kwa undani, juu ya maeneo haya muhimu.

Maeneo Ya Ramsar Tanzania ni yapi?
Tanzania tuna maeneo manne tengefu, yaliyo chini ya mkataba wa Ramsar. Maeneo haya ni ardhi oevu ya Muyovozi katika mto Malagarasi-Kigoma (13/04/2000), ardhi oevu ya bonde la Ziwa Natron-Manyara (04/07/2001), bonde la mto Kilombero-Morogoro (25/04/2002) na bonde la Rufiji-Mafia hadi Kilwa-Pwani (29/10/2004). Katika mabano ni tarehe ambazo maeneo hayo yaliingizwa katika orodha ya maeneo tengefu ya Ramsar. Kwa hiyo, maeneo haya yanalindwa na mikataba ya kimataifa, ambapo hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uwindaji na ukataji miti.

Ni Sifa zipi zinatakiwa, ili Eneo liwe chini ya Mkataba wa Ramsar?
Kuna sifa kuu tisa zinazofanya eneo likubalike kuwa katika uhifadhi wa mkataba wa Ramsar. Sifa hizi zimegawanywa katika makundi manne tofauti, kwa hapa nitazichangaya zote.

1. Inatakiwa eneo oevu husika liwe na umuhimu wa kimataifa kwa kuonesha bioanuwai ambazo ni wakilishi, za kipekee, zisizopatikana mahali pengine popote ila hapo tu, iwe ni mazingira ya asili au ambayo hayajaribiwa uasili wake na liwe eneo ambalo liko katika sehemu stahili ya kijografia.

2. Eneo litahesabiwa kuwa na umuhimu wa kimataifa iwapo lina viumbe adimu ambao wapo katika hatari ya kutoweka kabisa toka katika uso wa dunia kutokana na muingiliano wa viumbe hai.

3. Ili eneo husika lihesabike kuwa na umuhimu w kimataifa, inatakiwa liwe lina viumbe hai (mimea na wanyama) ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza uanuwai wa kibiolijia (uasili)wa eneo husika.

4. Eneo litahesabiwa kuwa na umuhimu w kimataifa iwapo linasaidia upotevu/uwepo wa mimea/wanyama katika mzunguko mzima wa maisha ya viumbe hao (life cyles), au eneo ambalo linatoa ulinzi hao dhidi ya uharibifu, katika mazingira mbali mbali.

5. Iwapo eneo linatunza jamii ya ndege 20,000 kwa kawaida kwa wakati mmoja, basi hili litahesabiwa kuwa katika orodha ya maeneo tengefu.

6. Iwapo eneo linahifadhi asilimia moja ya aina za ndege kutoka jamii mbalimbali za ndege hao, litahesabiwa kuwa katika orodha hii.

7. Iwapo eneo lina hifadhi kiasi kikubwa cha jamii ya samaki wa asili (si wa kupandwa kama sangara wa Ziwa Viktoria) historia ya maisha ya samaki hao, mwingiliano wa jamii za samaki hao, ambao ni wakilishi wa eneo hilo oevu na ambaohangia utajiri wa bioanuwai duniani, litaignizwa katika orodha ya maeneo ya Ramsar.

8. Iwapo eneo ni chanzo kikuu cha chakula walacho samaki, sehemu ya kutagia/kuzaliana samaki, sehemu ya kupita ya samaki kwa ajili ya kutafuta mazalio au chakula, ambapo samaki hupategemea kwa maisha yao, basi eneo hilo litaingizwa katika orodha tajwa hapo juu.

9.Sifa hii inafanana sana na namba 6 hapo juu, lakini hii inahusika na wanyama kwa ujumla wake.

Kwa hiyo, ili eneo liwe katika orodha ya Ramsar, halina budi kuwa na moja kati ya sifa zilizoainishwa hapo juu, ingawa inatokea mara nyingine eneo moja kuwa na sifa kadhaa kati ya hizo.
Kwa sababu hizi basi, ilikuwa ni lazima kwa serikali kuwaondoa wafugaji katika ardhi oevu za Kilombero (Morogoro) na Mbeya) kutokana si tu na umuhimu wa kitaifa, bali kimataifa pia. Wafugaji na wakulima hawana budi kuelimishwa juu ya umuhimu wa maeneo oevu kwa maisha ya binadamu, badala ya kuyaharibu kwa kulima na kufugia makundi makubwa ya wanyama katika maeneo haya nyeti. Ni kwa sababu hizi ambapo serikali iliamua

6/5/06

SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI...TUNAJIFUNZA NINI?

Kila mwaka, tarehe tano Juni ni siku ya mazingira duniani. Watu katika nchi mbali mbali hapa ulimwenguni huadhimisha siku hii kwa namna mbali mbali, wengi aghalabu hufanya shughuli mbali mbali za utunzaji wa mazingira. Kwa hapa kwetu nchini, sherehe hizi huambatana na kufanya kazi za utunzaji mazingira, kama vile uokotaji wa taka mahali mbali mbali, upandaji wa miti sehemu za wazi na kadhalika. Lakini kwa upande mwingine, hapa nchini kwetu upandaji wa ,miti kitaifa hufanyika kila mwaka siku ya Januari mosi, yaani siku ya mwaka mpya. Nadhani hii tarehe imewekwa makusudi kwa sababu kwa maeneo mengi (kama si yote) hapa nchini huwa ni msimu wa mvua. Kwa hio, ili miti iliyopandwa iote vizuri, ni lazima ipate maji ya kutosha, kutokana na mvua hizi.

Ni kwa nini basi tunaadhimisha siku hii?
Nitaanza kwa kufafanua maana ya dhana hii ya "mazingira" . Mazingira, kwa ujumla wake, ni vitu vyote ambavyo humzunguka mwanadamu. Vitu hivi ni kama maji, miti, milima, mabonde, miamba na kadhalika. Tunaadhimisha siku hii kwa sababu nyingi. Sababu kubwa ni kwamba, bila mazingira, mwanadamu hawezi kuishi. Kwa hiyo mwanadamu hana budi kuboresha mazingira yake ili aendelee kuishi. Mwanadamu akiharibu mazingira, basi anaharibu uhai wake mwenyewe.
Kila mwaka kunakuwa na semina na makongamano sehemu anuwai hapa duniani, kwa ajili ya kujadili suala hili la mazingira kwa mapana yake, lengo kubwa ikiwa ni kuyaboresha. Mmoja wa mikutano hii maarufu ni ule uliofanyika katika mji wa Kyoto nchini Japan tarehe 11 Desemba mwaka 1997. Mkutano huu ulitengeneza mkataba wa kupunguza uchafuzi wa mazingirana ulianza kufanya kazi tarehe 16 Februari 2005, ambapo ulilenga kupunguza ongezeko la joto duniani, ambao ulifikia maamuzi magumu ya kupunguza uharibifu wa anga kwa kupunguza gesi zenye sumu kutoka viwandani. Mpango (mkataba) huu hufanya kazi kupitia chombo kijulikanacho kama "United Nations Framework Convention on Climate Change" (UNFCCC). Kumbuka kuwa Marekani haikutia sahihi mkataba huu, kwa kuogopa kuua viwanda vyake, ambavyo huzalisha gesi nyingi sana za sumu duniani. Chombo hiki ndicho hutoa mwongozo wa kiwango cha gesi za sumu zinazotakiwa kutolewa kutoka viwandani ili kutoharibu "ozone" ambayo ni kiwambo cha gesi ambacho huzuia mionzi ya jua yenye madhara kutufikia moja kwa moja toka angani. Mpaka sasa, nchi 163 zimeweka sahihi katika mkataba huu.
Mkutano huu wa Kyoto ulitanguliwa na ule wa tarehe 5 Juni mwaka 1992 katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil, ambao nao malengo yake yalikuwa ni kupunguza uharibifu wa mazingira na kutunza bio anuwai.

Hali ya mazingira ikoje hapa kwetu?
Hali ya mazingira yetu kwa ujumla ni mbaya, kwamba tunashindwa kuyatunza kwa kwa usahihi. Ni suala la kawaida kwa watu mbali mbali kulima na kujenga katika vyanzo vya maji, mbuga za wanyama na hifadhi za taifa. Ni kawaida kwa wenye viwanda kumwaga taka zenye sumu katika mito na vijito, na mifano hai ipo mingi tu. Ni kawaida kutupa ovyo chupa za maji tukishakunywa maji, na ni kawaida kujisaidia haja ndogo mahali palipoandikwa "USIKOJOE HAPA". Ni kawaida kwa watu kutupa taka chini pamoja na kwamba mahali hapo pameandikwa 'TUPA TAKA HAPA". Kwa nini? Kwa faida ya nani?Hatumkomoi mtu, ila ni sisi wenyewe tunajisababishia vifo vinavyoweza kuepukika kabisa. Tunapotiririsha maji ya sumu ya viwandani katika mito, ilhali tunavua samaki katika mito hiyo hiyo tunatarajia nini? Tunakatazwa kutumia zebaki katika kusafishia madini lakini hatuachi, kwa nini? Tunaharibu vyanzo vya maji na mito inakauka, tunakosa maji na umeme, hatuoni kuwa tunajinyima haki? Kwa nini? Ni viwanda vingapi vinachafua hali ya hewa kwa gesi za sumu? Hatuvifahamu viwanda hivi? Tumechukua hatua gani?
Je tunachukua hatua madhubuti katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira?
Jadili
Soma makala maalum ya siku ya mazingira hapa

HII INAWEZEKANA-TUWE NA UTASHI WA KISIASA!

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na misururu mirefu ya msongamano wa magari hasa katika jiji la Makamba (Dar es Salaam). Hii inatokana na ongezeko kubwa la watu pamoja na magari, lisiloendana na rasilmali za kuweza kuhimili ongezeko hili. Kwa maana hii basi, uwezo wa barabara zetu (carrying capacity), wa kuhimili tatizo hili ni mdogo sana. Na aghalabu misururu hii ipo katikati ya jiji na katika barabara zote kubwa za jiji hili. Hali hii inasababisha usumbufu kwa wananchi, hasa suala la kuchelewa kazini, kwa kutumia muda mrefu kusafiri umbali mfupi. Wagonjwa wa dharura mara nyingine hufia njiani kwa sababu ya kucheleweshewa matibabu kutokana na misururu hii. Ni suala la kawaida kukuta mtu anatoka kwake muda wa saa 12 asubuhi na kufika kazini kama saa 2.30 hivi, uchelewevu wote huu ukisababishwa na msongamano wa magari. Kumekuwa na midahalo mbalimbali katika vyombo vya habari, vyombo vya usafiri na katika vijiwe sehemu kadha wa kadha kuhusu adha hii, lakini sina uhakika kama midahalo hii inawafikia warasimu, ambao wanatakiwa kutatua tatizo hili. Ni kero kubwa kwa jiji hili, ingawa hatujaona nia thabiti ya wakubwa wa nchi hii ya kulidhibiti tatizo hili. Kuna nadharia kadhaa, ambazo zikifanyiwa kazi na na kuwekwa katika vitendo na warasimu zinaweza kabisa kupunguza, kama si kumaliza tatizo hili katika nchi hii.

1. Mipango Miji
Suala la kujaza ofisi zote katikati ya jiji, kwa mtazamo wangu naona si sahihi sana. Kwa mfano, asilimia kubwa ya wizara zote zipo Dar es salaam, tena katikati ya jiji, ukiachilia mbali wizara ya Mifugo na Tawala za mikoa na serikali za mitaa, ambazo zipo Dodoma. Sasa basi, wananchi ambao huwa na shida anuwai, hulazimika kujazana katika wizara hizi ili kutatuliwa shida zao. Sasa katika hali kama hii unafikiri misururu katikati ya jiji itaepukikaje? Suala hili laweza kutatuliwa kwa kuwa na majengo mengi nje ya jiji. Majengo kama Ubungo Plaza na Millennium Towers pale Kijitonyama yalistahili kujengwa mengi na iwe ni nje ya jiji, maeneo kama Mbezi, Kibamba, Boko, Bunju na Tegeta ili kupunguza msongamanao wa watu na magari. Kwa maana hii basi, kungekuwa na kupishana, kwamba mtu anaishi Magomeni na anafanya kazi Bunju na mwingine anaishi Kariakoo na kufanya kazi Mbagala, hivyo misururu isiyo ya lazima isingekuwepo jijini. Lakini kwa sasa hali ni kinyume chake, maghorofa mengi marefu hujengwa katikati ya jiji. Suala hili huongeza idadi ya ofisi na na watu na kufanya katikati ya jiji kuwa na watu wengi. Tujaribu kutumia nadhari hiyo, inawezekana kabisa kupunguza tatizo.

2. Uhamishaji wa miji mikuu
Suala hili liliwahi kufanyiwa kazi na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa kuanzisha mradi wa kuweka Makao makuu ya nchi pale mkoani Dodoma yaani Capital Development Authority (CDA). Sina uhakika na sababu zilizofanya mradi huu usiendelee kwa kasi, lakini kwa wataalam wa mipango miji wanajua ni nini Mwalimu alidhamiria kukifanya. Lengo la mradi kama huu, aghalabu huwa ni kupunguza msongamano usio wa lazima katika baadhi ya miji, kwa kusambaza huduma katka mikoa mbalimbali. Kuna baadhi ya nchi zimefanikiwa kutekeleza mipango kama hii. Nijeria ilihamisha makao makuu yake kutoka Lagos kwenda Abuja, Ivory Coast inahamishia makao yake makuu kutoka Abidjan kwenda Yamoussokrou na kadhalika. Hii inasaidia sana katika kupunguza misongamano isiyo ya lazima katika miji mikuu.
Nafikiri ni kwa sababu hii ambapo Mahakama Kuu na Benki Kuu za hapa kwetu zina kanda kadhaa katika mikoa mbali mbali. Lengo ni kupunguza misongamano na safari zisizo za lazima jijini Dar es Salaam.

3. Upandaji wa Pikipiki na Basikeli
Kuna haja ya kuwa na mipango endelevu ya kupanda pikipiki na basikeli kwa wingi, ili kupunguza uwingi wa safari za magari. hili linawezekana kama wananchi tutaamua kwa moyo mmoja kupanda basikeli kwa sehemu ambazo makazi yetu hayapo mbali na ofisi zetu. Kwa mfano unakuta mtu anaishi Mwenge Dar, na anafanya kazi Makumbusho au pale Sayansi. Huyu nae analazimika kukaa katika msururu wa magari na kuchelewa kazini ilhali kama angekuwa na basikeli, ingemchukua muda mfupi sana kufika ofisini kwake. Kuna ulazima wa kuwa na fikira mbadala katika suala zima la kupunguza msongamano usio wa lazima. Suala hihi la pikipiki na basikeli liende sambamba na kutembea, kwa maana kwamba kama mtu anaona sehemu yake ya kujipatia riziki haiko mbali na makazi yake basi ni bora akatembea ili kuepuka adha ya msongamano. Inawezekana!

4. Udhibiti wa Watu kukimbilia Mijini
Suala hili kwa kiasi kikubwa husababishwa na watu waliopo vijijini kukuta hawana huduma muhimu za jamii, na hivyo hujikuta hukimbilia mijini kutafuta huduma hizi kwa namna yoyote. Utoro huu ni mkubwa sana hasa kwa vijana, ambao huamua kukimbilia mijini baada ya kuhitimu masomo yao, kwa hisia kuwa mjini kuna kila kitu, kwa hiyo 'hakiharibiki kitu'. Ni kwa mtazamo huu wa vijana wa vijijini ambapo hujikuta wamejazana mijini na kukosa ajira na kuongeza msongamano usio wa lazima. Hii hufanya tuanze kunyang'anyana rasilmali chache zilizopo mijini, ikiwemo usafiri na makazi.
Utatuzi wa tatizo hili unawezekana iwapo tu warasimu watilia mkazo utekelezaji wa mahitaji muhimu ya watu wa vijijini kama vile shule bora, huduma za afya na maji.

Kwa ujumla, adha zilizoainishwa hapo juu zinaweza kutatuliwa iwapo tu kutakuwa na utashi wa kisiasa wa wananchi na serikali kwa ujumla katika kuzivalia njuga adha hizo. Masual haya yanawezekana na rasilmali za utekelezaji wake tunazo, wakiwamo watu, suala ni utashi wa kisiasa tu. Inawezekana!