6/13/18

FAHAMU BAYOGESI

Utangulizi
Bayogesi (biogas) ni kitu gani?

Bayogesi ni mchanganyiko wa gesi inayoundwa na viasilia mbalimbali vinavyotengenezwa katika mazingira ya kutokuwepo hewa (oksijeni) ambayo asilimia kubwa ni gesi ya methane (CH4). Bayogesi ambayo aghalabu hutokana na kinyesi cha wanyama, masalia ya mimea na kinyesi cha binadamu inaweza kuzalishwa na kutumika kupikia na hata matumizi mengine kama vile kuendeshea mitambo mbalimbali. Matumizi ya gesi hii kwa mtu ambaye ana mifugo kama vile nguruwe, ng’ombe yanaweza kusaidia kuondokana na gharama za kununua nishati ya kuni, mkaa, umeme na hata gesi asilia inayochimbwa ardhini. Gesi hii inapunguza gharama za watumiaji wa vyanzo vingine vya nishati. Mfano, gharama za nishati ya umeme na gesi asilia ni ghali sana hasa kwa mtumiaji atakayedhamiria kutumia jiko la umeme au jiko la gesi lakini kwa gesi hii ya samadi mtumiaji itamgharimu muda wake tu kujaza samadi na maji kila siku na atakuwa hana malipo ya pesa kila mwezi kama itakavyomlazimu kulipia umeme na gesi asilia kila mwezi, na hata kuni ambazo watumiaji wengine hununua.

Mnyambulisho wa viambata Vya bayogesi

Kimsingi, bayogesi huwa na mchanganyiko wa gesi za aina mbalimbali, lakini inayopatikana kwa kiwango kikubwa ni gesi ya methane. Mgawanyiko huo kwa asilimia ni kama ifuatavyo:-

Methane (50%)

Carbondioxide (25%)

Naitrojeni (10%)

Sulphur dioxide ( 5%)

Haidrojeni (1%)

Gesi nyingine (9%)

Zingatia kwamba asilimia zilizooneshwa katika mabano zinaweza kubadilika kutokana na malighafi inayotumika kutengeneza bayogesi (samadi, majani, masalia ya chakula n.k.) na hali ya unyevunyevu wa malighafi hizo.

Uzalishaji wa bayogesi

Samadi ghafi inayotokana na kinyesi cha wanyama (kama vile kuku, nguruwe, ng’ombe na punda) kinaundwa na viasili vya Kaboni, Haidrojeni, Oksijeni Naitrojeni na Salfa. Viasili hivi hutengeneza sukari, mafuta na protini. Kinyesi au samadi humeng’enywa na bakteria ambao huvunjavunja kinyesi hicho kutoka katika hali ya protini, mafuta na sukari na kutengeneza muunganiko wa viasili ulio rahisi zaidi. Mmeng’enyo wa samadi (kinyesi) kwa kutokuwepo wa gesi ya oksijeni hutengeneza hewa ya ukaa (carbรณndioxide). Mmengenyo wa samadi bila ya uwepo wa oksijeni huzalisha gesi ya methane (CH4) ambayo ndio inayowaka hasa. Gesi hii itokanayo na kinyesi huzalisha kilojuli 5,200 hadi 5,800 kwa meta moja ya ujazo.

Bayogesi huweza pia kuzalishwa kutokana na masalia ya mimea, kama vile masalia ya zao la mkonge, masalia ya kakao au masalia ya kahawa baada ya kutolewa ganda na nje. Malighafi hizi zote huweza kuzalisha bayogesi iwapo zitachachushwa katika mazingira yasiyo na hewa (anaerobic condition).

Aina za Mitambo ya Kuzalishia Bayogesi

Kuna aina kadhaa za mitambo ya kuzalishia bayogesi, ambayo inapatikana Tanzania. Aina hizi ni kama ifuatavyo.

<!-Fixed Dome Biogas Digester (CAMARTEC/Hydraulic/Chinese)

Mitambo ya aina hii ilianza kutengenezwa nchini China kuanzia mwaka 1936 na ikasamabaa India mnamo mwaka 1937. Aina hii ya mitambo ya bayogesi hujengwa katika maumbo ya mviringo wa nusu duara, na huwa na sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza huwa ni sehemu ya kuchanganyia samadi na maji, sehemu ya pili ni ya kuchachushia, sehemu ya tatu huwa ya kuhifadhia gesi, sehemu ya nne ni ya kuhifadhia samadi ambayo imeshatumika kuzalisha gesi. Sehemu ya tano ni ile ya matumizi, yaani jiko au oveni, au jenereta.

Aina hii ya mitambo hujulikana sana kama CAMARTEC (kufuatia kusambazwa kwa wingi na kituo hiki cha kuhawilisha teknolojia za kilimo kwa ajili ya matumizi vijijini, kituo hiki kipo mkoani Arusha). Lakini pia, mpango wa serikali wa Miradi ya Gesi ya Samadi Dodoma (MIGESADO) ulijenga kwa wingi sana aina hii ya mitambo katika mkoa wa Dodoma. Shirika lingine linalohusika na ujenzi wa mitambo ya aina hii ni Shirika la Maendeleo na Uholanzi (SNV), lenye tawi lake mkoani Arusha. Nao wanajenga kwa wingi sana mitambo ya aina hii. Chanzo cha malighafi kwa mitambo hii ni samadi ya wanyama na kinyesi cha wanadamu.

<!-Floating Drum/Gobar Biogas Digester

Aina hii ya mitambo sio maarufu sana kwa hapa kwetu Tanzania. Mitambo hii hutengenezwa kwa kutumia matanki makubwa ya plastiki (ya kuanzia ukubwa wa lita 1000), yanayobebana. Tanki kubwa huwa linatangulia chini na ndilo ambalo huwa na malighafi kwa ajili ya kutengenezea gesi. Tanki dogo hubebwa na hili kubwa, na huwa jepesi kwa sababu linakuwa linabeba gesi, kwa hiyo huwa linaelea juu ya hili kubwa. Tanki hili dogo huwa na kitu kizito cha kulikandamiza kwa juu yake, ili lisiweze kutumbishwa na upepo uvumao. Malighafi inayotumika kuzalishia gesi kwa mitambo ya aina hii ni masalia ya chakula yatokayo majumbani na mahotelini



< 3.Vacvina Biogas Digester

Asili ya mtambo huu ni nchini Vietnam, na inapatikana nchini Tanzania. Aina hii ya mitambo huwa na sehemu kuu nne ambazo ni tanki la kuchanganyia samadi na maji, tanki la kuchachushia samadi na kuzalishia gesi, tanki la kuhifadhia samadi iliyokwishatumia, mirija ya kusafirishia gesi kwenda katika vihifadhio, vihifdahio vya gesi (karatasi za nailoni ngumu) na sehemu ya kutumia gesi (jiko, oveni au jenereta). Matanki ya mtambo huu hujengwa kwa matofali ya kuchoma na saruji au matofali ya mchanga na saruji. Vitako vyaa matanki haya hujengwa kwa zege, ili kuongeza uimara na kuhimili uzito wa mchanganyiko wa samadi na maji.

Picha hiyo hapo juu inaonesha matanki ya kuchachushia masalia ya mkonge kwa ajili ya kuzalishia bayogesi, katika kiwanda cha mkonge kilicho Hale mkoani Tanga


<!-4. Plastic Bag Biogas digester

Hii ni aina nyingine ya mitambo ya bayogesi ambayo inapatikana Tanzania. Uchachushaji wa malighafi kwa ajili ya kuzalisha gesi kwa kutumia mtambo huu hufanyika kwenye mfuko mgumu sana wa plastiki, ambao huwa na sehemu ya kuingizia mchanganyiko wa samadi na maji, na sehemu ya kutolea gesi kwwenda kwenye matumizi. Mfuko huu mgumu wa plastiki aghalabu hufukiwa ardhini ili kuulinda dhidi ya jua kali na kutoboka kutokana na shughuli za kibinadamu. Kwa aina hii ya mtambo, gesi huhifadhiwa katika sehemu ya juu ya mfuko huu, kabla haijasafirishwa kwenda kwenye matumizi. Mtambo huu ni wa gharama rahisi kidogo ukilinganisha na mingine ambayo imeorodheshwa hapo juu, kutokana na kutohitaji ujenzi unaohusisha matofali, zege ama saruji. Lakini shida yake ni kwamba mifuko hii haipatikani kwa urahisi hapa Tanzania, mara nyingi huagizwa kutoka nje ya nchi.



Picha: Vihifadhio vya bayogesi, kutoka katika mtambo wa Vacvina

Matumizi ya Bayogesi

Nishati katika Majiko

Bayogesi kutumika kama nishati katika majiko, kuendeshea mitambo kama vile magari na jenereta za kuzalishia umeme. Kwa Tanzania, bayogesi imekuwa ikitumika katika majiko maalum ya gesi kwa kupikia aghalabu na watu wenye mifugo ambao wana uhakika na upatikanaji wa samadi.


Picha: Majiko yanayotumia bayogesi

Nishati ya Kuendeshea Mitambo (mashine, magari, jenereta za kuzalishia umeme)

Bayogesi hutumika kuzalisha umeme. Mfano mzuri ni mtambo wa kuzalisha umeme ulio katika mashamba ya Katani Limited yaliyo katika mji wa Hale mkoani Tanga. Mahali hapo kuna jenereta ya ukubwa wa kilowati 150 kwa ajili ya kuzalisha umeme, ambayo huendeshwa kwa kutumia bayogesi. Kabla ya gesi kutumika katika mitambo, kwanza huchujwa kwanza katika chujio maalum lililo na kemikali za madini ya chuma, ili kuondoa gesi ya ‘hydrogen sulphide’ (H2S) ambayo huathiri sana mitambo kwa kusababisha kutu. Hali kadhalika, hewa ukaa (CO2) nayo huondolewa katika mfumo huu wa uchujaji huu, ili kufanya gesi ya methane iwe safi kabla ya kutumika katika mitambo husika. Kwa gesi inayotumika kuendeshea magari, yenyewe hupozwa kabisa na kuwa katika mfumo wa kimiminika, ili iwe rahisi kuhifadhiwa na kutumika. Magari ya namna hii yanapatikana nchini Sweden.


Picha: Jenereta ya kuzalisha umeme, inayoendeshwa kwa kutumia bayogesi. Ina ukubwa wa kilowati 150 na inapatika katika kiwanda cha mkonge cha Katani Limited, kichopo Hale Mkoani Tanga. Aliyesimama hapo kwenye jenereta ni Mhandisi Gilead Kissaka, meneja wa kiwanda .

Mbolea Itokanayo na Samadi Iliyokwishameng’enywa

Baada ya bayogesi kuzalishwa, masalia ya samadi ambayo huwa imemeng’enywa hutolewa nje ya tanki la kuchachushia mara samadi mpya inapowekwa katika tanki, kupitia chemba maalum ya kuingizia mchamganyiko wa samadi. Samadi iliyomeng’enywa hutumika kama mbolea ya kukuzia mimea. Inafaa sana kwa kustawisha mimea ya aina mbalimbali.









Kwa makala zaidi, bonyeza hapa na hapa

30 comments:

tntamb1 said...

Nimesoma blog yako hii na kufaidika sana.

Je unafahamu bei za mitambo ya biogas zilivyo hivi sasa hapa TZ?

Niliona bei za hapo nyuma, ambapo zikilinganishwa na za Asia, unakuta kwamba za kwetu ni mara tatu zaidi. Hivi hiyo inachangiwa na nini hasa?

Alex Mwalyoyo said...

Asante sana ndugu yangu kwa kutembelea jamvi hili, na pia nikushukuru kwa swali lako.

Bei za Mitambo ya Bayogesi
Bei za ujenzi wa mitambo ya bayogesi kwa sasa zinatofautiana kati ya aina moja ya mtambo na aina nyingine, hata kama mitambo hiyo ina ujazo unaofanana. Hii inatokana hasa utofauti wa teknolojia inayotumika kujenga mitambo hii. Mfano, kwa mtambo aina ya Camartec wa ujazo wa meta 12, huweza kugharimu shilingi milioni mbili na nusu hadi tatu, na mtambo wa aina ya Vacvina wa ujazo huo huo hugharimu kiasi cha milioni moja na laki mbili hadi milioni moja na nusu, hii ni kwa jijini Dar Es Salaam. Sababu ya tofauti hizi ni kwamba, mtambo wa Camartec unatimia matofali mengi zaidi kuliko Vacvina, kwa ujazo wa gesi unaofanana.

Ni kweli kabisa kwamba bei za ujenzi wa mitambo ya bayogesi kwa Tanzania zipo juu ukilinganisha na nchi za Asia. Unafuu huu kwa nchi za Asia (mfano Vietnam, Nepal, India, Bhutan, Cambodia n.k) unatokana na sera madhubuti za nchi zao katika kukuza na kuendeleza sekta ya nishati, hivyo bayogesi na nishati nyingine za kujadidika (renewables) zinatengewa fungu kubwa sana ukilinganisha na kwetu. Pili, serikali nyingi za Asia huwahamasisha wananchi wao kutumia teknolojia zinazozalishwa na wao wenyewe (kama vile taa, majiko na jenereta za bayogesi)kuliko kutumia zile ambazo huagizwa kutoka nje. Sula hili hupunguza gharama za ujenzi na uhudumiaji wa mitambo ya bayogesi!
Tusaidiane kuikumbusha serikali yetu kuwekeza katika miradi ya nishati jadidifu ili tupunguze bei za nishati hizi na hivyo kuongeza matumizi yake, hasa kwa wananchi wenye kipato cha chini, mijini na vijijini!
Asante!

kelly said...

nimependa sana maelezo yako..ningependa kufahamu jinsi ya kutengeneza mtambo mdogo tu kwa ajili yangu apa nyumbani.na pia kama unafahamu vikundi au chuo wanapo toa elimu hi..0716512719

HUNGU TV said...

KWA CHUO NENDA ARDHI UNIVERSITY SEST DEPARTMENT

Unknown said...

Hi, nashukuru sana kwa maelekezo mazuri kuhusu bayogesi. mimi nataka kujenga mtambo wa bayogesi ambao malighafi itakuwa ni kinyesi cha binadamu. Naomba msaada wa namna ya kuujenga kwa maana ya mahitaji (BOQ)na pia jinsi ya kujenga. ujazo uwe kuanzia mita za ujazo 6.
Napatikana kwenye E-Mail: kkuchibanda@yahoo.com na simu +255 784 499982,+255 767 499982
Nitashukuru sana

Unknown said...

Nashukuru sana kwa maelezo yako.jee nikitaka kujenga wangu binafsi wenye ujazo wa mita 4-5 natakiwa nifanyeje? Uwe unatumia kinyesi cha binadamu. Ninaweza kuunganisha na bomba zinzotoa uchafu wa kinyesi cha kila siku kutoka kwenye nyumba yangu? Naomba msaada wako tafadhali kupitia email khamish604@gmail.com au allyhrashid@gmail.com tafadhali

Unknown said...

Nashukuru sana kwa maelezo yako.jee nikitaka kujenga wangu binafsi wenye ujazo wa mita 4-5 natakiwa nifanyeje? Uwe unatumia kinyesi cha binadamu. Ninaweza kuunganisha na bomba zinzotoa uchafu wa kinyesi cha kila siku kutoka kwenye nyumba yangu? Naomba msaada wako tafadhali kupitia email khamish604@gmail.com au allyhrashid@gmail.com tafadhali

Alex Mwalyoyo said...

Ndugu zangu,
Nawashukuru kwa kutembelea blog yangu na kujifunza masuala mbalimbali. Nimechelewa kujibu baadhi ya hoja zetu kutokana na kubanwa na majukumu mbalimbali. Hata hivyo nitajibu hoja zote, nitaweka bandiko moja ambalo litajibu hoja hizo. Kwa wale mlioomba kutumiwa kwa barua pepe nitafanya hivyo. Kama kuna masuala mengine yoyote ambayo mnegependa kujua, yanayohusu mazingira, nishati jadidifu (renewable energy) na masuala yanayofanana na hayo, msisite kuuliza, nitayaweka tu humu. Asanteni sana

Unknown said...

He' jiko LA kupikia LA bio gas no majiko tofasuti name hay a tunayotumia majumbani ya gas za kawaida? Nijibu kwa SMS au e mail maana nimetengeneza kwa kutumia pipa gas inatoka lakini haiwaki, 0713381343. chaznewa@gmail
.com

Alex Mwalyoyo said...

Ndugu Charles Newa, unaweza tu kutumia majiko ya gesi ya kawaida tunayotumia nyumbani. Kikubwa ni kwamba 'ignition point' ya bayogesi iko chini kidogo, kwa hio inabidi uwashe gesi yako kwa kiberiti, tofauti na hizi za viwandani ambazo 'ignition point' yake iko juu sana, kiasi kwamba huna haja ya kutumia kiberiti kuwasha.

Unknown said...

Hongera saana kwa kutoa elimu hii ni vizuri kufanyia mapema hayo malekebisho ya kutumiwa kwenye email iwe rahisi kupata taarifa kutoka kwenye ukurasa huu wa TANGANYIKA YETU KWA wepesi

Alex Mwalyoyo said...

Ndugu Hassanal Mkwachu, nitumie email yako. Utakuwa ukipata notifications kila nikiweka bandiko.

Unknown said...

Nimefurahi Kwa elimu yako unayoitoa Kwa jamii juu ya biogas Mimi ninahitaj kutengeneza mtambowangu wa nyumbani wa ujazo wa mita 3 tafadhali sana nijibu kupitia fedrickdidas@gmail.com

Unknown said...

Nimefurahi Kwa elimu yako unayoitoa Kwa jamii juu ya biogas Mimi ninahitaj kutengeneza mtambowangu wa nyumbani wa ujazo wa mita 3 tafadhali sana nijibu kupitia fedrickdidas@gmail.com

witness B said...

Enter your comment...jamani ni ninauliza inachukua muda gani bio gas kuzalishwa baada kuweka katika mtambo

Unknown said...

flyimo@outlook.com

Unknown said...

Wapinyanauza hayo matanki

Torokoko said...

Hello habari ninaulizia namna ya kutumia umeme wa nyumbani kwa kutumia Biogas?
Zile generator zake ni bei gani na nitazipata wapi?
Naomba contacts kama ikiwezekana

Unknown said...

Nimefurahi sana kwa elimu nzuri niliyoipata hapa.Ninaomba tusaidie watunzi wa vitabu vyetu vya sayansi shule za msingi wanachanganya watoto wetu kwa kuandika kabonmonoksaidi badala ya kabondioksaidi

Unknown said...

Naitaji kupata mafunzo ni namna gana nawez tengeneza biogas at hom kwa kutumia. Ndooo

Robinson Gaston said...

Hongera ndugu kwa kazi nzuri ya kutupatia elimu hii ya nishati umeme wa bayogass,
Naomba kama itakupendeza utuandalie
Somo linalohusu namna ya kuitengeneza mtambo mdogo wa kuzalishia umeme wa nyumbani kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika Mazingira yetu, hii itatufaa Sana sisi tunaokaa Mashambani ambako umeme haufiki leo wala kesho. Kimsingi kama tungekua na uwezekano wa kupata nishati hiyo huku na kuifanya kazi hakika tungefanya mambo makubwa sana

Robinson Gaston said...

Hongera ndugu kwa kazi nzuri ya kutupatia elimu hii ya nishati umeme wa bayogass,
Naomba kama itakupendeza utuandalie
Somo linalohusu namna ya kuitengeneza mtambo mdogo wa kuzalishia umeme wa nyumbani kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika Mazingira yetu, hii itatufaa Sana sisi tunaokaa Mashambani ambako umeme haufiki leo wala kesho. Kimsingi kama tungekua na uwezekano wa kupata nishati hiyo huku na kuifanya kazi hakika tungefanya mambo makubwa sana

Robinson Gaston said...

0620126149

Anonymous said...

Nashukuru sana kwa mafundisho mazuri sasa nilikuwa naomba kama inawezekana kutengeneza video namna yakutengeneza BIOGAS kwakutumia kamtambo kadogo tu kanyumbani. Unaweza kunijulisha kupitia Gmail yangu simonampile@gmail.com

Anonymous said...

Nashukuru kwa ufafanuzi mzuri juu ya biogas, Mimi ni mfugaji mkubwa wa kuku wa kisasa nahitaj kuwa na mtambo je naweza kutumia kinyesi cha kuku? Nijibh kupitia email yangu ๐—ผ๐—ฑ๐—ฒ๐˜๐—ต๐—ฎ๐—ฟ๐˜„๐—ฎ๐—บ๐˜„๐—ฎ๐˜€๐—ฎ@๐—ด๐—บ๐—ฎ๐—ถ๐—น.๐—ฐ๐—ผ๐—บ.

Anonymous said...

Elimu nzr

Anonymous said...

Napenda kujifunza nanna yakutengeneza gesi pipa Lita 100 samadi kiasi gani maji kiasi gani ufungji kwenda jikoni

Anonymous said...

Mimi nilijaribu kuzalisha gesi kwa kutumia kinyesi cha nguruwe ikashindikana lakin ni Mara ya pili sasa nimejaribu kuzalisha gesi kupitia kinyesi cha ng'ombe na nimepata matokeo ya kuridhisha lakin sijajua kinyesi cha nguruwe kwanini nilifeli kuzalisha gesi...? Naomba msaada kwa hilo

Anonymous said...

Yonken115@gmail.com

Anonymous said...

Inasemekana katika bioges Kuna gesi ambayo inaozesha vyuma, ni ipi hiyo?