6/13/18

MAWE YA ILULA YAZUA MJADALA

Hii ni picha ya eneo la Ilula, mkoani Iringa. Uharibifu wa mazingira umesababisha kilele cha mlima huo kukosa miti. Picha ya Maggid Mjengwa.


UTANGULIZIKaribu katika mjadala ndugu mwanablogu mwenzangu. Niweke wazi kwamba mjadala huu ni mwendelezo wa mada iliyoanzishwa katika blogu ya mwanakijiji Maggid Mjengwa kuhusu mawe yaliyopo katika eneo la Ilula. Mada yenyewe katika blogu hio inasema hivi, nanukuu Kuna mwanakijiji mwenzetu aliyefikiri, kuwa Iringa "IMEBARIKIWA" kwa mawe. Lakini, mlima huo na mingine ya hapa Iringa ilifunikwa na misitu kabla. Kinachoonekana hapo n i uharibifu wa mazingira. Miti yote imekatwa. Kuna vijana wa Iringa wanaokumbuka, kuwa hadi mwaka 1977, waliweza kupanda milima hiyo iliyokuwa na miti mingi. Walikwenda huko na kuwinda ngedere wakiwa na mbwa wao. Binafsi nakumbuka utotoni. Miaka ile ya mwanzoni mwa 70's nikiwa na baba yangu tulisafiri kwa basi la KAMATA toka Igawa Mbeya hadi Iringa. Hapo tulikaa siku kadhaa kwa ndugu yetu mmoja aliyeitwa Merere. Ndugu huyu aliishi Gangilonga, ilijulikana pia kama "Uzunguni". Naikumbuka Iringa iliyokuwa na miti mingi. Mawe hayo ya mlimani sikumbuki kama niliyaona. Nakumbuka Gangilonga yenyewe ilikuwa imefunikwa na miti mingi.Nilipofika tena Iringa miaka ya 90 nikamwuliza mwenyeji wangu nikikumbuka Gangilonga ya utotoni; " Hivi Gangilonga ni wapi ? Niliuliza. " Hapa ulipo ndio Gangilonga!" Alinijibu. Naam. Tunakaribisha mawazo kutoka kwenu, juu ya namna gani tunaweza "kuikijanisha" tena Iringa na hatimaye kuyafunika tena mawe hayo yanayoonekana. Mwisho wa kunukuu.
Kiungo cha mada hio ni http://mjengwa.blogspot.com/2007/08/baraka-au-laana.html
Mtazamo ninaouandika hapa ni wangu, hivyo niko tayari kusahihishwa, kushauriwa ama kukosolewa. Karibuni!

Wanakijiji wanataka huo mlima wa Ilula ufinikwe na mimea kama inavyonyesha picha hii. Inawezekana, tutimize wajibu wetu!
MJADALAUtangulizi huo hapo juu ndio uliozua gumzo na majadala mkali miongoni mwa wachangiaji. Wengi wa wachangiaji walianza na hitimisho kwanza, kuwa ni lazima mimea ipandwe mahali pale ili pawe na ukijani kama ilivyokuwa hapo mwanzo, kama ilivyoshuhudiwa na mmoja wa wanakijiji aliyepita mahali hapo miaka hiyo ya ’70. Shida ilikuwa ni namna gani ya kuanza ’kupakijanisha’ mahali hapo. Na ukiangalia picha hio kwa umakini utaona kuwa kando ya hizo nyumba chini ya huo mlima kuna miti na inaonyesha kuwa ina afya njema tu. Sina uhakika kuwa miti hiyo ni ya kupandwa ama ya asili (nitatembelea hapo mahali na kutoa jibu), lakini kuna dalili zote kuwa hapo mahali miti inasitawi.

HOJA
1. PENDEKEZO LA KUGAWA MITI KWA WANANCHI

Baadhi ya wanakijiji walishauri kugawa miche ya miti kwa wakazi wa Iringa mjini, vyuoni na kwa wanafunzi wote, ili ikapandwe katika mlima wenye mawe pale Ilula. Wazo hili ni zuri, ila kuna wakati huwa halifanikiwi. Suala la kugawa miche ya miti na kuwalazimisha watu kuipanda sio mara zote linafanikiwa. Suala hili linategemea sana mazingira ya eneo husika, mwamko wa watu wa eneo hilo na uhusiano wa mamlaka inayogawa miche na wananchi wa eneo husika. Mfano, kati ya mwaka 1981 – 2000, mradi wa ‘Soil Erosion Control and Agroforestry Project’ (SECAP) ulianzishwa na kuendeshwa katika milima ya Usambara, hususan wilayani Lushoto. Mradi huu ulikuwa la lengo la kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na nyasi katika maeneo mbali mbali ya milima hii ya Usambara. Katika baadhi ya vijiji wanavijiji walipewa miche ya miti na mbegu za majani ya kulisha mifugo, baadhi yao walitupa miche na mbegu hizo na kufanya mradi kutokuwa endelevu. Vijiji ambavyo nilivipitia mwezi Juni mwaka 2005 na walikiri kufanya hivi, (pengine kwa kutojua faida za mti kwa wakati huo) ni Boheloi, Yamba, Mazashai (kata ya Gare) na vijiji vya Mambo, Makose na Mamboleo (kata ya Mtae). Vipara vilivyo katika maeneo haya vinasikitisha sana, hasa ukizingatia kuwa kulikuwa na mradi mkubwa wa utunzaji wa mazingira kwa miaka takribani ishirini. Huu sio uzushi, ila ni hali halisi, kama kuna mtu anatoka maeneo tajwa ama amepita maeneo hayo na kuongea na wenyeji, anaelewa nini ninaongelea hapa. Kuna miradi kadhaa inayofanana na huo wa SECAP ilifanyika katika wilaya ya Mbeya, ambayo ilifadhiliwa na iliyokuwa 'European Economic Community-EEC sasa inaitwa 'European Commission'-EC, ilifanikiwa. Nitatoa makala ya miradi hii siku za baadae kidogo.

2. PENDEKEZO LA KUWA NA SIKU MAALUM YA KUPANDA MITI
Kuna wanakiji walipendekeza kuteuliwa kwa siku maalum ya kupanda miti. Tayari siku hii tunayo, kwani kila ufikapo tarehe mosi mwezi Januari kila mwaka kunakuwa na kampeni za kitaifa za kupanda miti. Ni miti mingi inapandwa katika siku hii na watu binafsi, mashirika, serikali na taasisi mbali mbali. Baada ya kupanda miti suala la ufuatiliaji kujua hali ya mimea hii huwa duni sana, kiasi kwamba mingi ya miti hii huwa inakauka kwa kukosa matunzo. Suala la kupanda miti halina ubaya wowote na ni wazo zuri sana. Lakini sasa, baada ya kupanda, ni nani anajipa shida ya kujua hali ya miti hii baada ya kampeni hizi? Mara nyingi tunapanda miti katika kampeni wakati wa mvua za masika, lakini ni nani anajipa shida ya kufuatilia miti hii mara baada ya mvua za masika kwisha? Nani anakuwa na uhakika kuwa mizizi ya miti hii inakuwa imeshika vyema na ina uwezo wa kufyonza maji sasawasawa wakati wa kiangazi? Ni miji michache sana ambayo hufanya ufuatiliaji wa miti hii mara baada ya kampeni hizi. Kiujumla inatakiwa kila mwananchi awe na mwamko wa kutunza mazingira ya eneo husika, badala ya kusubiri kampeni, ambazo aghalabu huwa ni za zimamoto ama za muda mfupi.

3. MJADALA WA UMILIKI WA ENEO HUSIKA
Niwe wazi kuwa sina uhakika kuwa ni nani anamiliki eneo la Ilula lililoachwa wazi bila mimea. Huenda ikawa ni eneo lililo chni ya mamlaka ya halmashauri ya manispaa, halmashauri ya kijiji ama serikali kuu. Tangu miaka ya nyuma hasa baada ya Azimio la Arusha la mwaka 1967, sehemu kubwa ya ardhi ya nchi yetu ipo/ilikuwa katika miliki ya serikali kuu. Hii inajumuisha pamoja na mambo mengine vitu vyote vilivyomo katika ardhi hiyo, kama vile maji, madini, mimea na wanyama. Ni hivi majuzi tu ambapo maeneo haya yameanza kumilikishwa kwa serikali za mitaa, zikiwemo serikali za vijiji. Suala hili la ardhi kuwa chini ya serikali kuu lilifanya watu kuvamia maeneo haya na kufanya wanachokitaka ikiwa ni pamoja na kuchukua rasilimali zilizomo kama vile kuchimba madini, kurina asali, kuwinda, kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, kupasua mbao na mara nyingine kuichoma moto. Ilikuwa ni ‘Tragedy of the Commons’, kwamba mali ya umma haina hasara. Mara nyingi madhara ya vitendo hivi yametupata hata tusiohusika, kwa hiyo ndio sababu inayotufanya tunapiga kelele. Suala la kuacha kila kitu chini ya serikali kuu siliafiki sana. Tunasema kuwa “Serikali ina mkono Mrefu”, sawa lakini mkono huu una kikomo na kuna maeneo ambayo huwa mkono huu wa serikali kuu hauwezi kufika. Waliowahi kufanya kazi vijijini ambako hata baiskeli hakuna wanaelewa ninachoongelea hapa. Kuna baadhi ya vijiji Tanzania havifikiki kwa magari wala baiskeli, kwa hiyo kusema serikali kuu itafika maeneo hayo na kutekeleza yale wananchi wanayotaka sio kweli. Lazima mambo mengine yaliyo ndani ya uwezo wa serikali za vijiji yaachwe chini ya mamlaka ya serikali za vijiji. Kwa hiyo basi, maeneo kama haya yakipewa umiliki binafsi wa serikali za vijiji yatatunzwa na kuheshimiwa, kwani huku vijijini ndiko serikali inakoanzia na ni wanavijiji ambao ndio waathirika wa kwanza wa moja kwa moja wa athari chanya na hasi za vitendo nilivyoongelea hapo juu, na wengine tunafuata. Kuna wanakijiji wameponda sana suala hili, lakini kamwe hii hainizuii mimi kuendelea kusimamia hoja hii kwa miguu yote. Hatuwezi tu kukurupuka leo na kwenda kupanda miti katika eneo husika eti kwa sababu mvua za masika zinanyesha, bila kujua mmiliki wa eneo husika na bila kujua ana mpango gani na eneo hilo. Huku ni kukurupuka. Naunga mkono suala la kupanda miti, lakini lazima tujue tunapanda miti katika eneo la nani, isije kuwa tunatafuta kesi kwa kuvamia eneo la mtu.

4. MBINU SHIRIKISHI
Pamoja na kwamba kumekuwa na mawazo mbadala kutoka kwa wanakijiji kuhusu hoja hii, lakini pia ina umuhimu wake kwa mazingira ya sasa. Watanzania wa leo huwa wanahoji kila suala, hata kama hawachukui hatua katika suala hilo, lazima wajue nini kinaendelea. Siafiki suala la kuwapita kando ‘by-pass’ wakaazi wa eneo husika. Watanzania wa leo ukiwalazimisha suala ambalo hawalitaki huwa wanasema hapo hapo! Wamebadilika! Kwa hiyo basi, iwapo tunataka kupanda miti eneo la Ilula lililothiriwa, lazima tuwashirikishe wananchi. Narudia kusema kuwa, waliokata miti kwa ajili ya kuni, mbao, ujenzi, uchomaji wa mkaa na kadhalika huenda hawakutoka mbali na hapo, kwa hiyo ni hao hao. Kwa hiyo basi, naunga mkono hoja ya wao kushirikishwa katika kuhuisha mimea ya eneo husika. Nilitoa mfano wa mradi wa “Communal Areas Management Programme For Indigenous Resources” (CAMPFIRE) ulio nchini Zimbabwe, kuwa walitumia mbini hii katika kutekeleza mradi huo na walifanikiwa, kwa nini na sisi tusitumie mbinu hii kama inawezekana? Soma zaidi hapa http://www.resourceafrica.org/documents/1993/1993_campfire_bg.pdf kuhusu mradi huu.
Mfano mwingine wa mbinu shirikishi katika utunzaji wa mazingira unaweza kuusoma hapa, 'http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/9/13/habari33.php' Kitendo cha kufanya mambo ambayo yatawaathiri wananchi hapo baadaye bila kuwashirikisha ni dharau na kinaweza kuleta madhara. Hali kadhalika kitendo hiki kinawaweka wananchi nje ya mradi husika, hivyo wanakuwa hawana uchungu na mradi huo. Ndio hapa vurugu inapoanza, ni katika hatua hii uwindaji haramu hutokea, uchomaji wa mkaa kinyemela hufanyika, ukataji miti bila vibali hutokea na vitendo vingine vinavyofanana na hivyo. Ushirikishwaji wa jamii “Local Level Planning” haukwepeki kwa suala kama la Ilula, kwa hiyo hatuna budi kulipa nafasi yake katika mchakato huu mzima wa kuhuisha eneo husika. Tukidhani kuwa wao hajui mbinu bora za kuhuisha eneo hili tutakuwa tunawakosea haki. Sio vibaya kama tutakumbuka malalamiko ya wananchi wakati wa ‘Operesheni Vijiji/sogeza’ ya miaka ya sabini. Je miradi yote iliyoanzishwa na serikali katika operesheni hii bado inafanya kazi?

5. UREJESHWAJI WA MIMEA ASILIA
Kwa sababu wataalamu wa kwanza na wa kuaminika kwa mtazamo wangu ni wanakijiji wa eneo husika, naamini wao ndio wanaojua ni miti ama mimea ya namna gani ilikuwa inastawi katika eneo husika. Kwa hiyo basi, iwapo wazo ni kurejesha mimea katika eneo husika, sio vibaya kama ile mimea ya mwanzo (original indigeneous species) ikapewa kipaumbele,ndipo mimea mingine hamiaji (exotic species)ipewe nafasi. Inawezekana mimea ya mwanzo isikubali katika eneo husika kulingana na ukubwa wa athari, lakini pia mimea vamizi ina athari zake, na huenda isistawi vyema. Inabidi tuwe makini na hili, kwani tusije kurudi kule kule, leo tunapanda miti na baadaye kidogo tunaambiwa tukate kwa sababu inahatarisha vyanzo vya maji. Hii yote inatokana na kukurupuka. Nadhani tunakumbuka vyema habari ya mikaratusi, kwamba ilipandwa kwa lengo jema kabisa lakini ‘wataalamu’ sijui wa namna gani wakasema miti hii inaharibu vyanzo vya maji. Hoja hii niliipinga wakati fulani bloguni hapa. Nisingependa sana turejee huku miaka kadhaa ijayo.

HITIMISHO
Hatima ya michango ya wanakijiji iwe ni kuhakikisha kuwa eneo tajwa linabadilika kutoka hali ya jangwa iliyopo sasa na kuwa mahali penye mimea. Lakini tisifanye suala hili kwa kukurupuka, kama ilivyo jadi ya Watanzania wengi, tutafeli. Narudia kusema kuwa kijiji (blogu) na wanakijiji kwa ujumla tuna lengo la kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili. Lakini utatuzi huu lazima uwe ‘credible’, vinginevyo tutakuwa tunatwanga maji katika kinu.
Nawasilisha.

MABADILIKO YA HALI YA TABIANCHI

UTANGULIZIMnamo tarehe 18 Septemba 2007, nilihudhuria semina kuhusu mabadiliko hasi ya tabianchi na madhara yake katika viumbehai na katika maisha ya mwanadamu kwa upekee. Semina hii ilifanyika katika jiji la Oslo, Norway na ilishirikisha wadau wa taaluma mbali mbali kama vile wanasosholojia, wahandisi, wasanifu, wanasiasa, wataalamu wa ardhi na maji na wataalamu wa mazingira, kwa kutaja wachache, kutoka mabara yote. Hakika ilikuwa ni semina nzuri sana, kwani kulikuwa na mijadala mikali sana hasa kuhusu namna ya kuyakabili masuala haya kwa undani na kwa mbinu zinazokubalika katika mazingira ya sasa. Tulipata wasaa wa kuangalia picha za video zilizopigwa nchini Kenya, Nepal, Norway na Uganda, na wahusika toka nchi hizi ndio walikuwa wazungumzaji wakuu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, kadri walivyoshuhudia toka katika nchi zao.


MADAMtoa mada Joseph Kones kutoka Kenya aliwasilisha ushuhuda wake wa mabadiliko ya hali ya hewa kutoka mahali alipozaliwa, eneo la Maasai Mara, lililo katika bonde la mto Mara. Ikumbukwe kuwa bonde hili limesambaa mpaka Tanzania, katika mbuga ya wanyama ya Serengeti. Akasema kwamba kati ya miaka ya hamsini na sabini kulikuwa na mvua za kutosha na zilikuja kwa msimu maalum. Kwamba, mvua za masika zilikuwa inanyesha kuanzia mwezi Machi hadi Mei na ndio msimu ambao wakulima walipanda mazao yao. Lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ya hivi karibuni, hali imekuwa sio hiyo tena, kwani kwa sasa mvua za masika hazina msimu maalum kwa eneo hilo, ambalo kwa sasa linakabiliwa na ukame wa mara kwa mara. Pia mvua zinazonyesha katika eneo hilo kwa sasa hazina kiwango maalum kama zamani, kwamba zinaweza kuja nyingi na kusababisha mafuriko, ama zikaja chache na kutotosheleza mahitaji ya mimea, ama zisije kabisa katika msimu husika kiasi cha kusababisha ukame. Hali kadhalika, mtoa mada aliongelea suala la mbu waletao malaria, kwamba katika kipindi tajwa hapo juu kulikuwa hakuna mbu wa malaria katika eneo hilo, lakini kuanzia mwishoni mwa miaka ya themanini kumekuwa na malaria katika eneo hilo. Kutokana na ukame wa mara kwa mara, kumekuwa na baa la njaa ambalo husbabishwa na mazao kukauka kabla ya kukomaa, mifugo inakufa kutokana na kukosa malisho na kukauka kwa vyanzo vya maji kwa ujumla. Hali kadhalika, kumekuwa na ugomvi wa mara kwa mara kati ya jamii za wafugaji wa Kipsigi na Wamasai, kugombea malisho na maeneo ya kunyweshea mifugo yao. Kumekuwa pia na magonjwa yanayosambaa kwa njia ya maji, kama vile kichocho na homa za matumbo. Kumekuwa na uchafuzi wa mito na vyanzo vya maji, kutokana na wingi wa mifugo usioendana na uwezo wa vyanzo hivi kukidhi idadi hii ya mifugo. Akatoa wito kwa jumuiya za kimataifa pamoja na wadau wengine, kuangalia namna ya kuyaokoa maeneo haya kutokana na athari hizi.

Naye mtoa mada Frank Turyatunga (mwakilishi wa UNEP) kutoka nchini Uganda alikuwa na yake ya kusimulia kutoka nchini mwake. Alisema kwamba kuna mto unaotenganisha nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda. Mto huu enzi za miaka ya sitini na sabini ulikuwa hauathiriwi sana na mafuriko ya mara kwa mara, lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa sasa mto huo hufurika mara kwa mara na unamomonyoa kingo zake na kusababisha eneo kubwa la ardhi ya kumegwa na kusombwa na maji, na wakati mwingine mto huhama na kumega eneo la Uganda. Hali hii inasababisha Uganda kupoteza ardhi yake, kwani mto huu ni mpaka kati ya nchi hizi mbili, kwa maana hiyo kama mto unahama na kuelekea upande mwingine basi nchi nyingine hufaidi sehemu ya ardhi ambayo imehamwa na mto. Ikumbukwe kuwa eneo hili pa limegunduliwa kuwa na utajiri wa mafuta, kwa hiyo inaweza kuwa chanzo cha migogoro hapo baadaye. (Zingatia kuwa mto Songwe ulio kati ya nchi za Malawi na Tanzania una tabia ya namna hii, ya kuhama mkondo mara kwa mara kiasi cha kusababisha matatizo katika eno husika)

Mtoa mada Norbu Sherpa kutoka Nepal alikuwa na yake ya kuzungumza, hasa kutokana na athari za mafuriko ya mara kwa mara kutokana myeyuko wa barafu kutoka katika kilele cha milima ya Himalaya, unaochangiwa na ongezeko la joto duniani. Huyu alitoa ulinganifu wa athari kwa kufuata miaka, kama nilivyotaja hapo juu. Kwa ujumla mtoa mada huyu alilalamikia suala la kumegwa kwa ardhi kando ya kingo za mito, kiasi cha kuwalazimu wao kuhama maeneo hayo na kuelekea maeneo ambayo yana mwinuko zaidi, ili kujiepusha na athari za mafuriko hapo baadaye. Aliongelea suala la kusombwa kwa mazao, makazi na kupotea kwa maisha ya watu kutokana na mafuriko.

MJADALAShuhuda zilizojadiliwa hapo juu ndio zimekuwa kilio cha nchi nyingi duniani na athari hizi hata nchini mwetu zinaonekana waziwazi. Vimbunga vya mara kwa mara (1995), mafuriko (kumbuka el nino 1997/1998), ongezeko la magonjwa, ukame wa mara kwa mara (1993/1994) , (2005/2006) na ongezeko la joto ni baadhi tu ya athari za mabadiliko tajwa ya hali hewa. Ukiachilia ushuhuda wa uzoefu kutoka kwa wazee wetu na wakaazi wa maeneo mbali mbali, kuna mbinu za kisayansi za kupima mabadiliko haya hasi ya hali ya hewa na athari zake. Mbinu hizi zipo nyingi sana, ila nitagusia chache tu kwa ufupi. Mbinu hizi ni kama zifuatazo.

Ongezeko la JotoOngezeko la joto (mean annual temperature) hupimwa kwa kutumia vipimajoto vya satelaiti pamoja na vile vilivyo ardhini katika vituo vya hali ya hewa na kufanyiwa ulinganifu wa kitaalamu (modelling) kutoka wakati mmoja na mwingine ama kutoka mwaka mmoja na mwingine. Mfano, vipimo vya vilivyochukuliwa miaka ya arobaini hadi miaka ya sitini hulinganishwa na vile vinavyochukuliwa sasa na kukokotoa tofauti yake. Mara nyingi athari za ongezeko hili la joto ni pamoja na kuongezeka kwa myeyuko wa barafu ambapo husababisha mafuriko, kusambaa kwa magonjwa kama vile malaria na kukauka kwa vyanzo vya maji. Si ajabu basi tukisikia kuwa maeneo kama Kitulo, Makete, Mufindi ama Marangu hayakuwa na mbu waletao malaria katika miaka ya sitini na sabini lakini sasa kuna malaria!

Kupungua kwa kasi ama Kupotea kwa jamii za MimeaKuna baadhi ya mimea ambayo huwa inaathirika sana kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Upotevu huu hupimwa kulingana na wakati na kufanyiwa ulinganifu. Kwamba kwa mfano, kama mwaka 1930 kulikuwa na mimea 20 ya aina fulani katika meta moja ya eneo, na kwa sasa kuna mimea 8 ya jamii hiyo katika eneo hilo hilo la meta moja ya eneo, basi tunaweza kujua kwamba upotevu wa mimea ni kiasi gani kwa kufanya ulinganifu sasa, tangu eneo hilo lilipowekwa kumbukumbu ya mimea hiyo. Kwa sababu mimea na wanyama hushirikiana katika ikolojia na mfumo lishe, athari kwa mimea pia huleta athari kwa wanyama. Iwapo mimea mingi inakuwa imeondolewa katika eneo fulani , maji hayawezi kutunzwa ardhini, kwani mimea husaidia kutunza maji kwa kuzuia mionzi ya jua kutua moja kwa moja ardhini. Zingatia kwamba eneo tajwa linalofayiwa utafiti niliotaja hapo juu ni lile ambalo halijaathiriwa na shughuli za moja kwa moja za binadamu kama kilimo, ukataji miti na upandikizaji wa mimea mipya.

Mtawanyiko wa MajiKila eneo la ardhi duniani lina mtawanyiko wake maalum wa maji (surface run-off) kwa kila kilometa ya eneo. Kadri athari za kimazingira zinavyoongezeka ndio mtawanyiko huu hupungua ama kuongezeka. Kwa ufafanuzi ni kwamba, joto likichanganyikana na upepo huongeza kasi ya upumuaji (evaporation) ya mito na maziwa, hivyo kupunguza uwingi wa maji. Iwapo ongezeko hili ni la kudumu, basi na upungufu huu huwa ni wa muda mrefu. Hali kadhalika kwa maeneo yenye barafu, iwapo kutakuwa na ongezeko la joto, basi myeyuko wa barafu huwa ni wa kiwango cha juu na huenda ukawa ni wa kudumu hivyo kuongeza uwingi wa maji wa eneo husika, hasa wakati wa joto. Vipimo vya maji vya eneo husika ndivyo hufanyiwa ulinganifu kutokana na wakati na kutathmini athari zake.

Kutokana na athari hizi basi, kumekuwa na mwamko katika maeneo mbali mbali hapa duniani kuhusu namna bora ya kukabili athari za uharibifu wa mazingira na ongezeko la joto.
Tufanye nini basi ili kukabiliana na athari hizi? Nini kifanyike ili vyanzo vya maji visikauke? Tufanye nini ili mvua zije kwa wakati na za kutosha? Jadili.

JUMUWATA

Ndugu msomaji wa blogu hii, Jumuiya ya Wanablogu Tanzania (JUMUWATA) inakaribisha mchango wa mawazo yako wa namna ya kuiboresha.
Mchango wako unahitajika sana wewe mwenye blogu na hata usiye na blogu ilikujenga muelekeo uliochangiwa na wengi na sio kikundi cha watu wachache.Karibu uchangie, kosoa,kemea,shauri, ondoa, .... ilikupata muelekeo na jumuiya ya wanablogu Tanzania unayoweza kujivunia.Kama unablogu tunaomba uweke tangazo la kuwafahamisha watu kuhusu ombi la mchango wao wa mawazo hapa ili liwezekuwafikia watu wengi.
KARIBUNI WOTE!
Imetolewa na,
Uongozi wa JUMUWATA

KADHIA YA ONGEZEKO LA JOTO

Utangulizi
Kumekuwa na matukio mbali mbali yanayotokea mahali mbali mbali duniani kama kiashirio cha mabadiliko ya hali ya hewa katika uso wa dunia, ikiwemo vimbunga, mafuriko, ukame, kuongezeka kwa kina cha maji baharini, upotevu wa jamii za mimea na wanyama na kuyeyuka kwa barafu katika mzingo wa Aktiki ulio kaskazini mwa dunia. Haya ni baadhi tu ya matukio ambayo ni viashiria, kwamba inatupasa kucukua hatua za makusudi kukabili hali hii.

MADA
Kwa huku upande wa kaskazini mwa dunia, kumekuwa na malalamiko ya ukosefu wa theluji katika msimu mwafaka. Kwa kawaida, kwa tropiki ya Kansa msimu wa baridi huanza mwezi Novemba. Wenyeji wa huku huwa wanapenda sana kuteleza katika theluji na imezoeleka kila mara kwamba kila ifikapo mwezi Desemba basi kila mahali huwa na theluji ya kutosha kwa sababu joto huwa chini ya nyuzi sifuri, na kila mtu hufurahia hali hii. Lakini kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko yasiyo ya kawaida katika hali hii, kwamba kwa sasa inatokea kwamba ifikapo Desemba kunakuwa hakuna theluji kabisa na joto linakwa liko juu ya nyuzi sifuri. Kwa maana hiyo, msimu wa baridi umekuwa mfupi sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Wenyeji wanasema kuwa mabadiliko haya hasi yameanza hasa kuonekana kuanzia mwaka 1986 na kuendelea, na hali inazidi kuwa mbaya kadri miaka inavyozidi.
Kwa upande wa tropiki ya Kaprikoni, chini ya Ikweta, huku ndio huwa na ukame uliokithiri, kutokana na mabadiliko haya. Ikumbukwe kwamba mnamo mwaka 2005 kulikuwa na ukame ambao uliathiri sana upatikanaji wa maji, kiasi cha kusababisha matatizo katika uzalishaji wa umeme. Kwa mujibu wa baadhi ya tafiti za kitaalamu, hali hii huenda ikawa ni matukio ya kawaida iwapo nchi zinazoongoza kwa uchafuzi wa hali ya hewa hazitafanya juhudi za makusudi katika kupunguza hewa ya kaboni dayoksaidi itokayo katika viwanda vyao.
Inapaswa kila mtu ajivike majukumu ya kukabiliana na hali hii kwa kufanya yafuatayo.

1. Utunzaji wa Nishati
Kuzima vifaa vya umeme kama vile taa, pasi, runinga, majiko na feni ama viyoyozi iwapo kwa muda huo vinakuwa havihitajiki. Hii husaidia kupunguza matumizi ya nishati yasiyo ya lazima, hivyo kupunguza pia uzalishaji wa nishati husika.

2. Kutumia Usafiri wa Jumuiya
Iwapo kunakuwa hakuna ulazima wa kutumia usafiri binafsi, basi ni vyema kama tutatumia usafiri wa jumuiya kama vile mabasi, treni na meli kwa safari zetu mbali mbali. Kitendo hiki kitapunguza kiwango cha nishati kitumikacho na mitambo hii. Kitendo hiki kiende sambamba na matumizi ya baiskeli kwa safari fupi fupi ambazo hazimlazimu mtu kutumia gari ama pikipiki.

3. Utunzaji wa Maji
Tutumie maji tuliyonayo kwa kujibana. Hii itasaidia sana kupunguza matumizi yake, kiasi kwamba yale machache tuliyo nayo yanaweza kabisa kututosha. Pia ni vyema kama tutakuwa na utaratibu wa kusafisha maji yaliyokwisha kutumika, ili yatumike tena kwa matumizi mengine kama vile umwagiliaji wa mashamba na ujenzi.

Inawezekana, tutimize wajibu wetu.

HERI YA MWAKA MPYA 2008!

Nawatakia wasomaji wa blog hii Heri ya Mwaka mpya wa 2008.
Kila la heri kwa mwaka ujao, tuendelee kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi daima.
Maoni yenu nayaheshimu na nitayafanyia kazi ipasavyo.

"Happy New Year"

FAHAMU MBEGU ZA NYONYO/MBARIKA

Utangulizi

Mbarika ama nyonyo (castor seeds) ni mbegu za daikotiledoni ambazo zipo katika kundi la mbegu zitoazo mafuta, kundi moja na mbono kaburi (jatropha). Mmea wa nyonyo kitaalamu hujulikana kama 'ricinus communis'. Katika jamii nyingi za Kiafrika, mbegu za mmea huu zimekuwa zikitumika kutengeneza mafuta kwa ajili ya kulainisha ngozi za wanyama na kuwashia taa.
Mimea ya nyonyo ni sumu, kwa hivyo hailiwi na wanyama na husitawi maeneo mengi, hata yale yaliyo na ukame.

Picha: Mmea wa nyonyo/mbarika





Picha: Mbegu za nyonyo/mbarika, kabla hazijakomaa.

MATUMIZI

Mmea wenyewe hutumika kama uzio hai (live fence)
Katika baadhi ya jamii, majani ya mmea huu hutumika kukanda (massage) na kutibu maumivu yatokanayo na kuteguka.
Mbegu za nyonyo husagwa, huchemshwa na kuenguliwa mafuta. Mafuta ya nyonyo huweza kusafishwa katikaa mitambo ya kisasa na kutumika kuendeshea mitambo kama dizeli ya mimea (biodiesel). Pia hutumika kutengenezea mafuta ya kulanisha mitambo. Kumbuka kuwa mafuta ya kulainisha mitambo aina ya Castrol hutengenezwa kutokana na mmea huu.

MAGADI YA ZIWA NATRON NA MAZINGIRA -2

UtanguliziMnamo mwezi Juni mwaka 2006, niliwahi kuandika makala katika blogu hii kuhusu maeneo tengefu ya RAMSAR. Katika makala hiyo niliandika hivi :
”Maeneo ya Ramsar ni sehemu ya ardhi oevu duniani, (wetlands) ambayo yana umuhimu wa pekee duniani katika suala zima la uhifadhi wa mazingira. Ardhi oevu ni ile ardhi ambayo kwa msimu wote wa mwaka huwa na unyevunyevu. Jina hili "Ramsar" linatokana na mji wa Ramsar nchini Iran ambapo ndipo mkataba wa kutunza maeneo ya ardhi oevu duniani ulisainiwa, mnamo mwaka 1971. Kwa hiyo basi, mwaka 1971 ndipo yalipofanyika maamuzi ya kulinda maeneo ya ardhi oevu dhidi ya uharibifu, ili yaweze kutumika katika shughuli endelevu, kama vile vyanzo vya maji. Mpaka sasa, kuna mataifa 152 duniani yaliyotia sahihi mkataba huu wa kulinda ardhi oevu, ikiwemo Tanzania. Kuna maeneo tengefu 1608 ya Ramsar duniani yanayochukua ukubwa wa hekta milioni 140, kati ya haya Tanzania tuna maeneo manne tu. Maeneo haya ni ardhi oevu ya Muyovozi katika mto Malagarasi-Kigoma (13/04/2000), ardhi oevu ya bonde la Ziwa Natron-Manyara (04/07/2001), bonde la mto Kilombero-Morogoro (25/04/2002) na bonde la Rufiji-Mafia hadi Kilwa-Pwani (29/10/2004). Katika mabano ni tarehe ambazo maeneo hayo yaliingizwa katika orodha ya maeneo tengefu ya Ramsar. Kwa hiyo, maeneo haya yanalindwa na mikataba ya kimataifa, ambapo hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uwindaji na ukataji miti.”
Makala nzima inapatikana katika kiungo hiki: http://jadili.blogspot.com/2006_06_01_archive.html
HOJAKatika makala hii najibu hoja za mwandishi wa makala katika gazeti la Tanzania Daima la tarehe 29/01/2008 kama nilivyonukuu katika makala tangulizi hapo chini.
Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya Tanzania imekuwa na mazungumzo na kampuni ya Tata Chemicals ya India kuhusu uanzishwaji wa kiwanda cha usindikaji magadi katika eneo la Ziwa Natron, ambalo linalindwa na mikataba ya kimataifa, ambayo inazuia shughuli zozote za kiuchumi (ukiondoa utalii) ambazo zina athari kwa mazingira katika maeneo haya. Serikali ya Tanzania imeridhia mkataba wa Ramsar kuhusu ulinzi wa maeneo oevu, hivyo kutaka kulitibua eneo la ziwa Natron kwa kujenga kiwanda ni kukiuka mkataba huo.

HOJA YA MANUFAA YA MADINI
Mwandishi wa makala anasema kwamba madini ya nchi yetu hayajatunufaisha vya kutosha, kwa hiyo tunahitaji kuchimba magadi ili kujinufaisha kiuchumi. Sijaelewa mwandishi alimaanisha nini anapotaja ’madini’ na kuondoa magadi katika kundi la madini. Mimi nasema kwamba, hata magadi ni madini (sodium) ambayo huwepo katika mchanganyiko (compounds and mixtures) mbali mbali ambapo katika taaluma ya kemia yana alama (Na). Sasa basi magadi haya ya ziwa Natron yaweza kuwa ”Sodium Sulphate” (NaSO4), ”Sodium Carbonate” (NaCO3) , ”Sodium Chloride” (NaCl), Sodium Bisulphate NaH(SO3)2 ama Sodium Bicarbonate NaH(CO3)2, na kadhalika. Kwa hiyo aelewe kwamba kama kuna malalamiko ya kimazingira ama ya kipato kidogo kutokana na madini basi magadi hayawezi kabisa kuwekwa kando, kwa sababu nayo ni madini kama nilivyoonyesha hapo juu. Sodium Chloride (chumvi tunayotumia), huchimbwa kule Uvinza Kigoma kwa wingi, je yamenufaishaje taifa kimapato? Anaweza kuanzia hapo kufanya upembuzi, ili kuweza kufikia mwafaka wa manufaa ya madini kwa ujumla.

HOJA YA KIPATOKwamba tunachimba magadi ili kukuza kipato cha taifa sio hoja sana kwa sababu Tanzania inaweza kutafuta vyanzo vingine vya mapato kufidia kile ambacho tutapoteza kutokana na kutochimba madini haya. Suala la mazingira lazima lipewe kipaumbele Iwapo tungekuwa tunaangalia suala la kipato, basi ule mradi wa kamba (prawns) wa kule Rufiji nadhani ungeendelezwa kwa sababu nao likuwa na kipato kizuri tu. Tusisubiri kupigiwa kelele na mataifa makubwa na kushtuka kwamba kweli mradi una athari. Mwandishi wa makala anasema kwamba iwapo tutachimba magadi hayo tunatarajia kuingiza dola milioni 800,000 kwa muda wote wa mradi huo. Hata kama itakuwa ni kwa mwaka, sidhani kwamba itakuwa busara kuchuuza mazingira kwa pesa ndogo namna hiyo. Ambacho haelewi hapa huyu mwandishi ni kwamba ukokotoaji wa mahesabu ya mradi huu hufanywa na mwombaji ama mwendelezaji wa mradi, kwa hiyo lazima avutie kwake ili kutupendezesha na kutushawishi. Katika mfano wake, anasema kwamba Kenya inazalisha magadi kwa wingi sana tangu mwaka 1910, ila fedha ziotokanazo na magadi hayo huwafaidisha Waingereza zaidi kuliko Wakenya! Lahaula! Sasa kama fedha za Wakenya zinawafaidisha Waingereza, je tuna uhakika gani kama hizi za kwetu ambazo tunatarajia kuzipata kutokana na kuchimba magadi hazitaishia kuwafaidisha Wahindi? Ni nani katika serikali kakaa kupiga mahesabu na kupata jibu kwamba ni kweli tutaingiza kipato hicho katika mfuko wetu?

HOJA YA AJIRAKwamba mradi huu utaleta ajira 500 za moja kwa moja na nyingine 2000 zisizo za moja kwa moja sio hoja yenye mshiko ambayo inaweza kusimama na kuhalalisha utoaji kafara wa eneo la ziwa Natron. Suala ni kwamba kuna vyanzo vingine vingi tu vya ajira ambavyo vikipewa kipaumbele vinaweza kuajiri watu zaidi ya hao 2500 kwa muda mrefu ambao watatokana na mradi huu. Kilimo hakijapewa kipaumbele, ingawa kinadaiwa kwamba ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Karibu kila mkoa katika Tanzania unalima zao fulani, je tumechukua hatua gani kuona kwamba kila mkoa unafaidika na kilimo hiki? Iwapo kila mkoa unalima, na chukulia kwamba kila mkoa unatoa wakulima bora 1000 tu katika maelfu ya wakulima wote, tutakuwa na jumla ya wakulima 26,000, yaani mara kumi ya waajiriwa wa huo mradi. Sasa kwa nini tusiendeleze hapa penye ajira nyingi zaidi? Uvuvi nao umesahauliwa. Ni chanzo kizuri sana cha mapato yenye uhakika kwa nchi yetu Tanzania ambayo imejaa maji yanayoruhusu uvuvi kila kona. Kuna Ziwa Nyasa, Tanganyika, Viktoria, Rukwa na kadhalika. Je tumechukua hatua gani kuhakikisha kwamba maji haya yanaajiri watu wa kutosha? Tuna bandari ngapi za kujivunia ambazo zinafanya kazi kwa kiwango cha kuridhisha? Hatujayatumia maji haya vya kutosha katika uvuvi,usafirishaji na matumizi mengine, kwa nini?


KANUNI ZA TATHMINI YA ATHARI ZA KIMAZINGIRA (EIA)
Ufafanuzi wa Mradi
Mpaka sasa, kwa mujibu wa taarifa za serikali, kampuni ya Tata Chemicals bado haijakamilisha suala zima la upembuzi yakinifu kuhusu mradi huu kuangalia kama una madhara ama la, kwa hiyo basi bado kufikia hatua ya kuuweka mradi huu wa magadi ya Ziwa Natron katika miradi salama kimazingira. Taarifa hiyo inapatikana katika tovuti ya baraza la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) katika kiungo hiki, Tangazo la NEMC. ”http://www.nemctan.org/publichearinglnatorn.doc”. Na kwa mujibu wa kanuni za EIA, iwapo mradi husika unazua ”kelele na manung’uniko” toka kwa jamii, basi hicho ni kiashiria kwamba mambo siyo sawia.


RIPOTI YA ”EIA”Binafsi nikiri kwamba, kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu sijaipata na sijaipitia ripoti ya tathimini ya athari za kimazingira ambayo imefanywa na kampuni husika inayoomba kibali cha kuchimba magadi. Pamoja na hayo kama eneo husika linalindwa na sheria za kimataifa, ripoti hii haitakuwa na maana sana kwa sababu tayari eneo la Ziwa Natron haliruhusiwi kuendelezwa kwa shughuli za kiuchumi kwa mujibu wa mkataba wa Ramsar, kwa sababu ya umuhimu wake kwa bioanuwai. Kwamba eneo hili lina ndege aina ya korongo wadogo ”Lesser Flamingo” ambao huishi maeneo hayo na kutegemea eneo hilo kwa maisha yao.

Kwa habari zaidi pitia hapa, hapa na hapaHuo ndio msimamo wangu kama mtaalamu wa mazingira.

MAGADI YA ZIWA NATRON NA MAZINGIRA -1

‘WANAOPINGA UCHIMBAJI MAGADI WANATUMIWA’
na Salehe Mohamed

SIKU chache baada ya wadau wa mazingira kupinga mpango wa Serikali kuchimba magadi katika Ziwa Natron, kumeibuka tetesi kuwa wadau wanaopinga mradi huo wanatumiwa na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo waliopo nchini Kenya.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, vinaeleza kuwa wafanyabiashara hao wanahofia endapo Tanzania itaanza kuchimba magadi kuna kila dalili watu wa Kenya nao wakaanza kudai eneo lao lenye madini hayo linalomilikiwa na Waingereza.
Wadau hao inaelezwa kuwa waligharamiwa safari ya kuja Dar es Salaam kupinga uanzishwaji wa mradi wa kuchimba magadi kwenye mdahalo ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), uliokuwa ukilenga kupata maoni ya wadau kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo.
Vyanzo hivyo vinasema fedha zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa magadi ni zaidi ya zile zinazopatikana katika sekata ya madini hivi sasa na Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani.
Viliendelea kubainisha kuwa watu wanaopinga uanzishwaji wa mradi huo kwa madai kuwa utasababisha mazalia ya ndege aina ya Lesser Flamingo (Korongo Wadogo) kupotea, hiyo ni danganya toto kwani nchini Kenya wanachimba na bila kuharibu mazingira ya ndege husika.
Korongo wadogo
Miongoni mwa wataalamu wa mazingira ambao wanapenda kuona mradi huo ukitekelezwa hapa nchini ni Dk. Boniface Mbiyu, ambaye alisema nchi za Kiafrika zimekuwa maskini kwa sababu ya kuwasikiliza wahisani ambao wana lengo la kuzinufaisha nchi zao.
Alisema kama Tanzania itaweza kuchimba madini hayo inakadiriwa kupata zaidi ya sh bilioni 600 ambazo ni zaidi ya fedha wanazozipata katika sekta ya madini na itakuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani.
Alisema Kenya ilianza kuchimba magadi tangu mwaka 1910 na hakuna madhara makubwa ya kimazingira kama ambavyo watu wamekuwa wakipewa taarifa tofauti kuhusu uanzishwaji wa mradi huo.
Kenya ni miongoni mwa makoloni yaliyokuwa yakitawaliwa na Uingereza na mpaka hivi sasa Waingereza bado wanamiliki eneo linatoa magadi hayo na wameweka vikosi vya kijeshi eneo hilo kwa kushirikiana na askari wa Kenya.
“Huu mradi utakuwa na thamani kubwa sana kwa Watanzania na itakuwa mkombozi wa kiuchumi kwani fedha zitakazopatikana ni zaidi ya zile za dhahabu, makaa ya mawe na almasi,” alisema Mbiyu.
Alisema ni vema Watanzania hasa watu wanaoishi katika eneo la jirani ambalo linatarajiwa kuchimbwa magadi wakawa makini na kuepuka ahadi ndogo ndogo pamoja na maneno ya watu wasiopenda maendeleo ya Tanzania kiuchumi.
Kauli hiyo ya Dk. Mbiyu inaungana na ile aliyoitoa Waziri wa Malisili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kuwa serikali haitasitisha mpango wake wa kuchimba magadi katika Ziwa Natron lililopo katika Mkoa wa Manyara pamoja na kelele kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka mradi huo usitishwe.

MAGADI YA ZIWA NATRON, MKOMBOZI WA UCHUMI TANZANIA
Salehe Mohamed

TANZANIA ni moja ya nchi zilizobarikiwa duniani kuwa na rasilimali nyingi lakini pia ni moja ya nchi zinazoongoza kwa umaskini, kwa sababu ya kutokuzisimamia vema.
Dhahabu, tanzanite, almasi, makaa ya mawe, mbuga za wanyama na vivutio vingi ambavyo kama vingetumika ipasavyo vingeweza kuiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tajiri zaidi duniani.
Madini ni miongoni mwa sekta ambazo kila kukicha imekuwa ikipigiwa kelele kuwa inawanufaisha zaidi wageni kuliko wazawa kutokana na mikataba iliyoingiwa na wazawa wasio kuwa na uchungu na rasilimali za nchi yao.
Hivi karibuni kumezuka mashindano ya hali ya juu kati ya watunza mazingira, jumuiya za kimataifa na Serikali ya Tanzania kuhusu azima ya Tanzania kutaka kuchimba magadi yaliyopo katika Ziwa Natron lililopo mkoani manyara.
Wadau wa mazingira na jumuiya ya kimataifa wanasema eneo hilo ni tengefu kwa ajili ya kuhifadhi ndege aina ya lesser flamingo ambao hupatikana katika maeneo machache hapa duniani na wapo hatarini kutoweka.
Wakati wahisani na wadau wa mazingira wakisema hayo, Tanzania imesema itaendelea na mradi huo kwani utasaidia kupunguza umaskini kwa wakazi wa eneo hilo na kukuza uchumi wa nchi.
Mpango wa Serikali ni kuchimba tani 500,000 kwa mwaka kwa muda wa miaka 200 na tayari Kampuni ya Tata Chemical ya nchini India inakamilisha taratibu za mwisho kabla ya kuanza kwa mradi husika.
Zaidi ya dola za Marekani milioni 800,000 zinakadiriwa kupatikana endapo mradi huo utafanya kazi vizuri kama ilivyopangwa pamoja na kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa watu wanaofanya kazi katika mradi husika.
Kampuni ya Tata Chemical ndiyo ambayo hivi sasa inaendesha mradi kama huo katika Ziwa Magadi lililopo nchini Kenya na kwa kiasi kikubwa wametambua faida ipatikanayo na magadi ndiyo maana wameamua kuja kuwekeza Tanzania.
Kampuni hiyo imeahidi kuajiri zaidi ya watu 500 katika ajira ya kudumu na zaidi ya watu 2,000 watapata vibarua huku nyumba zaidi zikitarajiwa kujengwa kwa ajili ya wafanyakazi.
Reli ya kutoka eneo la mradi mpaka Tanga kwa ajili ya usafirishaji tayari ipo katika mchakato wa ujenzi, umeme nao utafika mradini pamoja na barabara itakayopitika kipindi chote cha majira.
Kimsingi mradi huu utawanufaisha watu wengi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa ambapo ni watu wachache hunufaika na fedha zinazopatikana kutokana na utalii.
Magadi ni aina ya madini ambayo yanapatikana kwa wingi katika Ziwa Natron na asili yake ni kulipuka kwa Volcano hai ya Mlima Oldonyo Lengai uliopo katika Mkoa wa Manyara.
Magadi yana matumizi mengi kwa binadamu, yakiwemo kutengenezea karatasi, viwanda vya ngozi, kusafisha maji, dawa, vitu vya kulipuka na vingine vingi.
Inakadiriwa kuwa nishati ya petroli, madini ya tanzanite, makaa ya mawe na madini mengine yakijumuishwa pamoja hayawezi kufikia fedha itakayopatikana kutokana na uchimbaji wa magadi.
Kimsingi magadi kama yakitumika ipasavyo yanaweza kuiletea Tanzania faida kubwa zaidi kuliko inavyofikiriwa na watu wengi ambao kwa namna moja au nyingine wamekosa uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa madini haya kwa uchumi wa Tanzania.
Kenya ina eneo linalojulikana kama nchi ya magadi, ambayo yalianza kuchimbwa mwaka 1910 na hutoa zaidi ya tani 600,000 kwa mwaka na inakadiriwa hupata zaidi ya dola milioni 41, fedha ambazo huwafaidisha zaidi Waingereza.
Eneo yanapopatikana madini hayo hulindwa na vikosi vya Kenya na Uingereza, ambayo wakati ikitoa uhuru kwa watu wa Kenya iligoma kutoa eneo hilo kutokana na umuhimu wake.
Mwaka 2001 jumuiya ya kimataifa, hasa wanaojiita wana mazingira walipitisha makubaliano ya kulinda maeneo chepechepe na yenye viumbe ambavyo vinaweza kutoweka ikiwemo eneo hilo la Ziwa Natron.
Lesser flamingo ndio ndege ambao jamiii ya kimataifa inataka wasipotee katika eneo husika ilhali jumuiya hiyo haitazami namna Tanzania inavyoathirika kiuchumi kama haitachimba madini hayo.
Jumuiya hiyo inaonyesha nia ya kutoa shinikizo la kutoipatia Tanzania misaada ya kifedha kama Tanzania itaendelea na mradi wake wa kuvuna magadi katika Ziwa Natron.
Inataka ilete masharti kama ya Mto Nile ambapo nchi zinazozunguka mto huo hutakiwa kuwasiliana na Misri ndipo ziweze kuyatumia maji ya mto huo.
Mtaalamu wa mazingira, Dk. Boniface Mbiyu alielezea umuhimu wa Tanzania kuchimba madini hayo kwa kipindi hiki ni mkubwa zaidi kuliko vipindi vilivyotangulia kwani nchi haiwezi kuendeshwa kwa kutegemea misaada ya wahisani.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ili nchi ifaidike zaidi ni lazima kuwapo na mgawanyo mzuri wa rasilimali hiyo kabla ya kuingia mkataba na wawekezaji ili yasije yakatokea yale ya madini.
Alisema mwekezaji na Serikali wanapaswa wapate asilimia 40 katika mradi huo huku asilimia 20 ikienda kwa wakazi wa eneo la mradi ambao wana hofu ya kupoteza fedha wanazozipata kutoka kwa watalii.
Kuwapo kwa ndege hao kumekuwa kivutio kikubwa zaidi kwa watalii ambapo inakadiriwa zaidi ya dola za Marekani 500,000 hupatikana sambamba na wananchi wa Kijiji cha Ngarisero kunufaika kwa kuwatembeza watalii.
Marekani ni nchi ambayo magadi hupatikana lakini ni lazima yachimbwe mita 400/600 kwenda chini, tofauti na Tanzania ambapo hata jembe la mkono linamtosha mtu kuchimba magadi.
Urahisi wa uchimbaji magadi katika Ziwa Natron utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara hiyo ambayo inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kukua kwa uchumi wa Tanzania.
Uchimbaji wa magadi katika ziwa hilo ndiyo mwelekeo mwema wa kufanikisha malengo ya kukuza uchumi wa Tanzania na kutimiza azima ya serikali ya kuboresha maisha ya wananchi.

Chanzo cha habari hii: Gazeti la Tanzania Daima, 29/01/2008

Nitazijadili hoja hizi kwa undani.

BARAFU YA MLIMA KILIMANJARO

Mlima Kilimanjaro ni mrefu kuliko mlima wowote ule hapa barani Afrika ukiwa na urefu wa meta 5895 juu ya usawa wa bahari. Juu ya mlima huu pamefunikwa na barafu. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na tafiti mbali mbali zikieleza namna barafu hiyo inavyoyeyuka kwa kasi kutokana na ongezeko la joto duniani (nimewahi kuliongelea kwa kina suala hili katika makala zilizopita). Kwa sasa kumekuwa na juhudi mbali za makusudi za kupunguza athari hizi, huenda kukawa kuna mafanikio siku za baadaye kama tutashirikiana kutunza mazingira kuzunguka mlima huu.
Kibo na Mawenzi
Kilele cha Mawenzi
Kilele cha Kibo

WAPINGA KUCHIMBA MAGADI ZIWA NATRON

na Salehe Mohamed

LICHA ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Professa Jumanne Maghembe, kusisitiza dhamira ya serikali kuchimba magadi katika Ziwa Natron, wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi wameupinga mradi huo.
Wadau hao walitoa maoni yao jana jijini Dar es Salaam katika mdahalo wa kupata maoni kuhusu uanzishwaji wa mradi huo, ulioandaliwa na Baraza la Mazingira (NEMC), likihusisha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Wadau hao walisema athari za mradi huo ni nyingi kwa binadamu, ndege, wanyama na upo uwezekano mkubwa wa kukauka kwa ziwa hilo, kama ilivyotokea kwa wananchi wa Kenya, hivyo hawaoni sababu ya kuukubali mradi huo.
Mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya TATA Chemical ya nchini India, ambapo kila mwaka watakuwa wakichimba tani 500,000 na watajenga kiwanda cha kuandaa magadi kwa ajili ya kusafirishwa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Engaresero, ambapo mradi huo utajengwa, Christopher Ndurway, alisema wakazi wa kijiji hicho zaidi ya 5,000 na mifugo yao hawatakuwa na sehemu ya kwenda iwapo mradi utaanza kazi.
“Sisi hatukubaliani na uamuzi wa serikali wa kutaka kuchimba magadi, kwani kuna athari kubwa za kimazingira pamoja na sisi na mifugo yetu,” alisema Ndurway.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Deodatus Mfugale, alisema mradi huo utaharibu mazalia ya ndege aina ya Lesser Flamingo ambao wapo hatarini kutoweka.

Korongo Wadogo
Alisema kuanzishwa kwa mradi huo kunakiuka makubaliano ya kimataifa ambayo yanatamka eneo hilo ni tengefu kwa ajili ya viumbe hivyo.
Mdahalo huo ulitawaliwa zaidi na ubishani mkali baada ya mwakilishi wa NDC, Abdalah Mndwanga, kusema kuwa mwekezaji alibadili eneo la kujenga kiwanda na kusogea umbali wa kilometa 30 zaidi ya eneo la awali.
Mwakilishi huyo alikuwa katika wakati mgumu zaidi pale alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa athari za kimazingira zitakazopatikana baada ya mradi, huku yeye akijibu kuwa alielekezwa kutoa takwimu za kiufundi na si vinginevyo.
Joseph Ng’ida, alisema serikali inapaswa ifanye upya tathmini ya mradi huo badala ya kukurupuka, hatua ambayo inaweza kusababisha majuto siku za usoni.

WAZIRI KITUKO
Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Ana Maembe, alisema maoni ya wananchi hao yatafikishwa kwa Waziri Maghembe ambaye ndiye atakayetoa kibali cha kuruhusu mradi huo.
Maghembe ameshawahi kunukuliwa akisema kuwa watu wanaopinga mradi huo wana sababu binafsi na kama wanataka serikali iachane na mradi huo ni vema wakatoa fedha itakazopata serikali katika kipindi chote cha mradi.

Chanzo: Tanzania Daima 24/01/2008

INDIAN FIRM HALTS PLAN FOR SODA ASH PROJECT

By Orton Kiishweko
THE CITIZEN

An Indian company that was keen to invest $500 million (about Sh600 billion) in a soda ash project along Lake Natron in Manyara district has reportedly pulled out.

The firm, Tata Chemicals, announced it was putting on hold its plans for a soda ash extraction and processing plant at Lake Natron due to intense pressure by environmental lobbyists.

Mr Homi Khusrokhan, the firm's managing director, said his company has suspended the investment and will wait results of the final Ramsar Management Plan currently under preparation for Lake Natron.

We still wait for a report that is meant to put the investors and environmentalists concerns into consideration, he said.

However, a report published in the Hindustan Times, one of India's leading newspapers, quoted Mr Khusrokhan as saying the project was also facing a tricky situation that has something to do with a tedious environmental convention.

Environmentalists all over the world have opposed the project, saying Lake Natron, which is an important breeding ground for flamingos, would be destroyed if the company set up a factory. Their campaign forced the shelving of the first environmental impact assessment report that had cleared the Indian firm to invest.

Yesterday, Tanzanian authorities were, however, unaware of the planned suspension with Environment Minister Dr Batilda Burian and Tanzania Investment Centre (TIC) chief executive Mr Emmanuel ole Naiko saying they were yet to receive official information from the company.

Mr Ole Naiko said the suspension of the project may not be conclusive as an assessment report that will consider the interests of investors and conservationists was still being awaited.

The merits and demerits of the project are still being debated and a common understanding has not yet been reached as far as I know, Mr ole Naiko said.

Dr Burian told The Citizen that the Government has not approved the project, and was still assessing it to determine whether to endorse it or not.

As the Government, we are obliged to bring about sustainable social, economic and environmental development. This means that we can allow the project only after the merits and demerits of the whole scheme, she said.

Mr Khusrokhan, a key spokesperson for the project, admitted that it was clear now that the plant could not be sited at the lakeside because of the risks to the environment. Therefore, the original Environment and Social Impact Assessment should be treated as withdrawn, he said.

But Mr Gideon Nasari, managing director of the state-run National Development Corporation (NDC), has in the past said that they plan to shift the plant 35km (22 miles) from the lakeshore to help preserve flamingos, which are a major tourist attraction.
However, a UK-based environment group, Birdlife International and the Royal Society for the Protection of Birds, opposed this saying that shifting the project 35km from the lake would not mitigate the negative impact the project is likely to pose to lesser flamingos and the local community.
Twenty-four conservationists from East African countries, under the banner of Lake Natron Consultative Group recently , called on the Tanzanian government to halt the project, saying its a recipe for destruction of the lake and it inhabitants.

Conservationists also argued that the economic benefits of the plant are insignificant, compared with its long-term negative effects on the environment and the country's struggling tourism sector.

Their reports have indicated that Lake Natron is by far the most significant of only five sites in the world where lesser flamingos breed regularly and successfully. The breeding at Lake Natron accounts for 75% of all the world's lesser flamingos.
Their reports also say, that based on flamingo tourism alone, Lake Natron has a value of close to $12 million a year.

Chanzo: The Citizen, 23/05/2008

UTETEZI WA MRADI WA MAGADI UNAENDELEA...

Magadi ya Ziwa Natron changamoto ya uchumi
Na Amana Nyembo
MRADI wa uchimbaji magadi katika Ziwa Natroni, mkoani Arusha, ni moja ya miradi ya viwanda ambayo serikali imeipa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) jukumu la kuuendeleza kwa ubia na sekta binafsi.
Mbali na uchimbaji wa magadi, miradi mingine ni uchimbaji wa makaa ya mawe, umeme wa Mchuchuma na chuma cha Liganga - yote ikiwa Arusha.
Akizungumza hivi karibuni Dar es Salaam, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Gideon Nasari, anasema mradi huo utakuwa na faida kwa Watanzania, kinyume kabisa na madai ya wanaharakati kuwa utaharibu korongo (flamingoes), ndege maarufu waishio huko.
Nasari anasema mradi huo utasaidia kuvutia utalii na kuwafanya wananchi wa eneo hilo kufaidika zaidi na baadhi ya miundombinu itakayotengenezwa, kwani hauwezi kuharibu mazalia ya korongo. Wamelichunguza hilo baada ya kutathmini na kutilia maanani mawazo na hofu za wadau.
Kwa sababu waendelezaji wa mradi wameamua kuhamisha eneo la kiwanda lililopangwa kwenda kilometa 32 kutoka Natron na eneo oevu (ramsar site) upande wa mashariki wa ziwa hilo.
Kiwanda kitakuwa mbali na Natron, kwani mazalio ya korongo yapo upande wa kaskazini na kusini sehemu ambayo ndege hao hawatajua nini kinafanyika upande mwingine.
“Hakutakuwa na njia yoyote ya usumbufu kwa korongo hao muhimu na wazuri…si hivyo tu, lakini kuwapo kwa shughuli za wanadamu eneo hilo kutasaidia kuwafukuza wanyama wengine wanyemeleaji,” anasema.
Akizungumzia mfumo wa kemikali katika ziwa hilo, Nasari anasema magadi kutoka ziwani yatavutwa kwa pampu kilometa 32 hadi kwenye mtambo ambako asilimia 23 ya magadi itatolewa na yanayobaki yatarudishwa ziwani.
“Kiwango cha malighafi ya magadi (brine) kitakachovunwa kwa mwaka ni sawa asilimia 0.12 ya jumla ya magadi yote yatakayoingia ziwani kwa mwaka, na hakutakuwa na mabadiliko makubwa yatakayoharibu viumbe hai (cyanobackeria) ziwani humo.
Hata hivyo, anaeleza kuwa mradi huo katika kiwanda hautachukua maji kutoka vyanzo vyovyote vinavyopeleka maji ziwani, kwani mradi una mpango wa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vyanzo vingine vya maji safi na salama kwa ajili matumizi ya binadamu na kiwandani.
“Inatarajiwa kwamba kitachimbwa kisima chenye kina cha mita 100 umbali wa kilometa 30 kutoka ziwani bila kuharibu mfumo wa mazingira…ujenzi wa kiwanda hicho utawahakikishia wananchi maji safi na salama kwa matumizi yao na mifugo,” anasema.
Hata hivyo, mradi wa Ziwa Natron unakisiwa kugharimu dola milioni 450 za Kimarekani, gharama ambazo zinajumuisha kiwanda cha kusindika magadi, pia kijiji cha wafanyakazi wa kiwanda hicho na uimarishaji wa miundombinu na mifumo yake.
Anaeleza miundombinu hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Longido hadi Natron na reli ya Arusha kupitia Natron sehemu ya kiwanda.
“Kutakuwa pia na njia ya kusafirisha umeme kutoka Arusha hadi eneo la kiwanda, lakini pia upanuzi wa Bandari ya Tanga na uimarishaji wa reli ya Tanga hadi Arusha utafanyika,” anasisistiza.
Mradi wa magadi kwa kuanzia utazalisha tani 50,000 za magadi na baadaye kuongezeka hadi tani 100,000 kwa mwaka. Kutokana na kuwapo kwa kiwanda hicho, nafasi za ajira ya kudumu zinatarajiwa kupatikana 500 na nyingine ambazo si za kudumu ni nafasi 2,000.
Anasema mradi huo unatarajiwa kuingiza faida ya dola 300 kwa mwaka kutokana na mauzo ya magadi yanayotoka katika Ziwa Natron.
Kuhusu uharibifu wa mazingira katika eneo hilo, anasema shughuli zote zitakazofanyika kwenye mradi zitaongozwa kwa mapendekezo na maelekezo ya taarifa za tathmini ya kimazingira na kijamii (environmental and social Impact assessment) kama ilivyopitishwa na serikali ya Tanzania.
Anasema hiyo ina maana kila tahadhari itachukuliwa kuhakikisha hakuna uharibifu wowote wa mfumo mpana wa mazingira.
Nasari anafafanua kwamba wananchi waishio katika eneo la mradi watapata nishati ya umeme na hivyo kupunguza kasi ya ukataji miti, vilevile umeme utasaidia usambazaji wa maji safi na salama kwa wananchi wengi. Teknolojia itakayotumika kusamabaza maji pia itadhibiti uchafu wa maji taka, kwani itakuwa ya kisasa na wala haitachafua mazingira na kuhakikisha usalama watu.
Anasema NDC na Tata Chemicals Limited, kutoka India na waendelezaji wa mradi huo kwa makini wanazingatia umuhimu wa kuhifadhi mfumo mpana wa mazingira katika sehemu ya mradi, ndiyo sababu walipokea na kujumuisha mawazo na malalamiko ya wadau kuhusu taarifa ya mazingira
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0784 846907

Chanzo: Tanzania Daima, 8/7/2008

MMOMONYOKO KATIKA DARAJA



Picha zikionyesha mmomonyoko wa udongo katika daraja, eneo la Interchick katika barabara ya Bagamoyo, Dar Es Salaam. Mmomonyoko huu usipodhibitiwa unaweza kuleta athari katika daraja hili na barabara kwa ujumla.

NAFASI ZA MASOMO YA NISHATI

NAFASI YA MASOMO ya MTANDAONI- BURE
Ndugu msomaji wa makala katika blogu hii, kama wewe unajishughulisha na masuala ya nishati na mazingira unakaribishwa kusoma kozi ya masuala hayo ambayo inaitwa "Energy for Sustainable Development (E4SD)" au kwa Kiswahili "Nishati kwa Maendeleo Endelevu", kwa njia ya mtandao (e-learning), hivyo huhitaji kusafiri kwenda popote kusoma zaidi ya kuwa na mtandao wa intaneti karibu nawe. kozi hii ya masuala ya nishati na mazingira imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya 'International Institute for Industrial Environmental Economics' (IIIEE), United Nations Development Programme (UNDP), United Nations Development Programme (UNEP)na the Global
Network on Energy for Sustainable Development (GNESD).

MALENGO YA KOZI
Malengo ya kozi hii ni kutoa elimu kwa upana zaidi juu ya uhusiano uliopo kati ya masuala ya nishati na maendeleo endelevu kwa nchi zinazoendelea.

MUDA WA KOZI
Kozi hii itaendeshwa mtandaoni kuanzia tarehe 20/04/2009 hadi tarehe 14/06/2009 na maombi yatumwe katika anuani itakayotolewa hapa chini kabla ya tarehe 06/04/2009.

MAOMBI
Tuma Maombi yako ya Kushiriki kwa kutumia barua pepe iliyopo hapa chini kwa:
Project coordinator E4SD Online Course
International Institute for Industrial Environmental Economics (IIIEE)
Lund University, Sweden
Phone: 0046 46 222 02 55
Fax: 0046 46 222 02 10
Post: P.O. Box 196, 221 00 Lund, Sweden
E-mail: katsiaryna.paulavets@e4sd.org
Web: http://www.iiiee.lu.se
Web: http://www.e4sd.org

Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti yao katika www.e4sd.org

JIUNGE KATIKA SIKU YA BLOGU

Tarehe 15/10/2009 ni siku ya blogu duniani, ambapo mwaka huu mjadala unahusu mabadiliko ya tabianchi (Climate Change).
Katika blogu hii nimekuwa nikiandika mada mbalimbali kuhusu masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabia nchi na matumizi ya nishati mbadala, kwa hiyo siku hii ni mwafaka sana katika kupigia debe suala na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi!

Kwa habari zaidi unaweza kutembelea hapa

NIMERUDI JAMVINI

Ndugu wanablogu wenzangu, majukumu ya kila siku ya kikazi yalikuwa yamenizidi mno, kiasi kwamba iliniwia vigumu kuweza kusoma na kuandaa makala za kujadiliana nayi hapa jamvini. Hata hivyo 'Ubize' haujaisha, ila umepungua kiasi, kwa hiyo nitajitahidi sana kuja na makala kadhaa za nishati na mazingira, ambazo ndio fani ninazojitahidi kubobea nazo kwa sasa.
Nimekuwa nikipita katika blogu zenu kujifunza hili na lile kila ninapopata nafasi na kuacha ujumbe kwamba nimepita. Lakini pia nafarijika kwamba baadhi ya makala na picha ninazobandika hapa zinatumika mahali pengine na huwa wanakumbuka kushukuru chanzo hiki, kwa hiyo ujumbe wetu huwa unafika mahali pengi zaidi na unasomwa.
Bila shaka tutaendelea kuwa pamoja kuendeleza mijadala kwa ajili ya maendeleo yetu.

Asanteni kwa uvumilivu!

Mwalyoyo

FAHAMU BAYOGESI

Utangulizi
Bayogesi (biogas) ni kitu gani?

Bayogesi ni mchanganyiko wa gesi inayoundwa na viasilia mbalimbali vinavyotengenezwa katika mazingira ya kutokuwepo hewa (oksijeni) ambayo asilimia kubwa ni gesi ya methane (CH4). Bayogesi ambayo aghalabu hutokana na kinyesi cha wanyama, masalia ya mimea na kinyesi cha binadamu inaweza kuzalishwa na kutumika kupikia na hata matumizi mengine kama vile kuendeshea mitambo mbalimbali. Matumizi ya gesi hii kwa mtu ambaye ana mifugo kama vile nguruwe, ng’ombe yanaweza kusaidia kuondokana na gharama za kununua nishati ya kuni, mkaa, umeme na hata gesi asilia inayochimbwa ardhini. Gesi hii inapunguza gharama za watumiaji wa vyanzo vingine vya nishati. Mfano, gharama za nishati ya umeme na gesi asilia ni ghali sana hasa kwa mtumiaji atakayedhamiria kutumia jiko la umeme au jiko la gesi lakini kwa gesi hii ya samadi mtumiaji itamgharimu muda wake tu kujaza samadi na maji kila siku na atakuwa hana malipo ya pesa kila mwezi kama itakavyomlazimu kulipia umeme na gesi asilia kila mwezi, na hata kuni ambazo watumiaji wengine hununua.

Mnyambulisho wa viambata Vya bayogesi

Kimsingi, bayogesi huwa na mchanganyiko wa gesi za aina mbalimbali, lakini inayopatikana kwa kiwango kikubwa ni gesi ya methane. Mgawanyiko huo kwa asilimia ni kama ifuatavyo:-

Methane (50%)

Carbondioxide (25%)

Naitrojeni (10%)

Sulphur dioxide ( 5%)

Haidrojeni (1%)

Gesi nyingine (9%)

Zingatia kwamba asilimia zilizooneshwa katika mabano zinaweza kubadilika kutokana na malighafi inayotumika kutengeneza bayogesi (samadi, majani, masalia ya chakula n.k.) na hali ya unyevunyevu wa malighafi hizo.

Uzalishaji wa bayogesi

Samadi ghafi inayotokana na kinyesi cha wanyama (kama vile kuku, nguruwe, ng’ombe na punda) kinaundwa na viasili vya Kaboni, Haidrojeni, Oksijeni Naitrojeni na Salfa. Viasili hivi hutengeneza sukari, mafuta na protini. Kinyesi au samadi humeng’enywa na bakteria ambao huvunjavunja kinyesi hicho kutoka katika hali ya protini, mafuta na sukari na kutengeneza muunganiko wa viasili ulio rahisi zaidi. Mmeng’enyo wa samadi (kinyesi) kwa kutokuwepo wa gesi ya oksijeni hutengeneza hewa ya ukaa (carbóndioxide). Mmengenyo wa samadi bila ya uwepo wa oksijeni huzalisha gesi ya methane (CH4) ambayo ndio inayowaka hasa. Gesi hii itokanayo na kinyesi huzalisha kilojuli 5,200 hadi 5,800 kwa meta moja ya ujazo.

Bayogesi huweza pia kuzalishwa kutokana na masalia ya mimea, kama vile masalia ya zao la mkonge, masalia ya kakao au masalia ya kahawa baada ya kutolewa ganda na nje. Malighafi hizi zote huweza kuzalisha bayogesi iwapo zitachachushwa katika mazingira yasiyo na hewa (anaerobic condition).

Aina za Mitambo ya Kuzalishia Bayogesi

Kuna aina kadhaa za mitambo ya kuzalishia bayogesi, ambayo inapatikana Tanzania. Aina hizi ni kama ifuatavyo.

<!-Fixed Dome Biogas Digester (CAMARTEC/Hydraulic/Chinese)

Mitambo ya aina hii ilianza kutengenezwa nchini China kuanzia mwaka 1936 na ikasamabaa India mnamo mwaka 1937. Aina hii ya mitambo ya bayogesi hujengwa katika maumbo ya mviringo wa nusu duara, na huwa na sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza huwa ni sehemu ya kuchanganyia samadi na maji, sehemu ya pili ni ya kuchachushia, sehemu ya tatu huwa ya kuhifadhia gesi, sehemu ya nne ni ya kuhifadhia samadi ambayo imeshatumika kuzalisha gesi. Sehemu ya tano ni ile ya matumizi, yaani jiko au oveni, au jenereta.

Aina hii ya mitambo hujulikana sana kama CAMARTEC (kufuatia kusambazwa kwa wingi na kituo hiki cha kuhawilisha teknolojia za kilimo kwa ajili ya matumizi vijijini, kituo hiki kipo mkoani Arusha). Lakini pia, mpango wa serikali wa Miradi ya Gesi ya Samadi Dodoma (MIGESADO) ulijenga kwa wingi sana aina hii ya mitambo katika mkoa wa Dodoma. Shirika lingine linalohusika na ujenzi wa mitambo ya aina hii ni Shirika la Maendeleo na Uholanzi (SNV), lenye tawi lake mkoani Arusha. Nao wanajenga kwa wingi sana mitambo ya aina hii. Chanzo cha malighafi kwa mitambo hii ni samadi ya wanyama na kinyesi cha wanadamu.

<!-Floating Drum/Gobar Biogas Digester

Aina hii ya mitambo sio maarufu sana kwa hapa kwetu Tanzania. Mitambo hii hutengenezwa kwa kutumia matanki makubwa ya plastiki (ya kuanzia ukubwa wa lita 1000), yanayobebana. Tanki kubwa huwa linatangulia chini na ndilo ambalo huwa na malighafi kwa ajili ya kutengenezea gesi. Tanki dogo hubebwa na hili kubwa, na huwa jepesi kwa sababu linakuwa linabeba gesi, kwa hiyo huwa linaelea juu ya hili kubwa. Tanki hili dogo huwa na kitu kizito cha kulikandamiza kwa juu yake, ili lisiweze kutumbishwa na upepo uvumao. Malighafi inayotumika kuzalishia gesi kwa mitambo ya aina hii ni masalia ya chakula yatokayo majumbani na mahotelini



< 3.Vacvina Biogas Digester

Asili ya mtambo huu ni nchini Vietnam, na inapatikana nchini Tanzania. Aina hii ya mitambo huwa na sehemu kuu nne ambazo ni tanki la kuchanganyia samadi na maji, tanki la kuchachushia samadi na kuzalishia gesi, tanki la kuhifadhia samadi iliyokwishatumia, mirija ya kusafirishia gesi kwenda katika vihifadhio, vihifdahio vya gesi (karatasi za nailoni ngumu) na sehemu ya kutumia gesi (jiko, oveni au jenereta). Matanki ya mtambo huu hujengwa kwa matofali ya kuchoma na saruji au matofali ya mchanga na saruji. Vitako vyaa matanki haya hujengwa kwa zege, ili kuongeza uimara na kuhimili uzito wa mchanganyiko wa samadi na maji.

Picha hiyo hapo juu inaonesha matanki ya kuchachushia masalia ya mkonge kwa ajili ya kuzalishia bayogesi, katika kiwanda cha mkonge kilicho Hale mkoani Tanga


<!-4. Plastic Bag Biogas digester

Hii ni aina nyingine ya mitambo ya bayogesi ambayo inapatikana Tanzania. Uchachushaji wa malighafi kwa ajili ya kuzalisha gesi kwa kutumia mtambo huu hufanyika kwenye mfuko mgumu sana wa plastiki, ambao huwa na sehemu ya kuingizia mchanganyiko wa samadi na maji, na sehemu ya kutolea gesi kwwenda kwenye matumizi. Mfuko huu mgumu wa plastiki aghalabu hufukiwa ardhini ili kuulinda dhidi ya jua kali na kutoboka kutokana na shughuli za kibinadamu. Kwa aina hii ya mtambo, gesi huhifadhiwa katika sehemu ya juu ya mfuko huu, kabla haijasafirishwa kwenda kwenye matumizi. Mtambo huu ni wa gharama rahisi kidogo ukilinganisha na mingine ambayo imeorodheshwa hapo juu, kutokana na kutohitaji ujenzi unaohusisha matofali, zege ama saruji. Lakini shida yake ni kwamba mifuko hii haipatikani kwa urahisi hapa Tanzania, mara nyingi huagizwa kutoka nje ya nchi.



Picha: Vihifadhio vya bayogesi, kutoka katika mtambo wa Vacvina

Matumizi ya Bayogesi

Nishati katika Majiko

Bayogesi kutumika kama nishati katika majiko, kuendeshea mitambo kama vile magari na jenereta za kuzalishia umeme. Kwa Tanzania, bayogesi imekuwa ikitumika katika majiko maalum ya gesi kwa kupikia aghalabu na watu wenye mifugo ambao wana uhakika na upatikanaji wa samadi.


Picha: Majiko yanayotumia bayogesi

Nishati ya Kuendeshea Mitambo (mashine, magari, jenereta za kuzalishia umeme)

Bayogesi hutumika kuzalisha umeme. Mfano mzuri ni mtambo wa kuzalisha umeme ulio katika mashamba ya Katani Limited yaliyo katika mji wa Hale mkoani Tanga. Mahali hapo kuna jenereta ya ukubwa wa kilowati 150 kwa ajili ya kuzalisha umeme, ambayo huendeshwa kwa kutumia bayogesi. Kabla ya gesi kutumika katika mitambo, kwanza huchujwa kwanza katika chujio maalum lililo na kemikali za madini ya chuma, ili kuondoa gesi ya ‘hydrogen sulphide’ (H2S) ambayo huathiri sana mitambo kwa kusababisha kutu. Hali kadhalika, hewa ukaa (CO2) nayo huondolewa katika mfumo huu wa uchujaji huu, ili kufanya gesi ya methane iwe safi kabla ya kutumika katika mitambo husika. Kwa gesi inayotumika kuendeshea magari, yenyewe hupozwa kabisa na kuwa katika mfumo wa kimiminika, ili iwe rahisi kuhifadhiwa na kutumika. Magari ya namna hii yanapatikana nchini Sweden.


Picha: Jenereta ya kuzalisha umeme, inayoendeshwa kwa kutumia bayogesi. Ina ukubwa wa kilowati 150 na inapatika katika kiwanda cha mkonge cha Katani Limited, kichopo Hale Mkoani Tanga. Aliyesimama hapo kwenye jenereta ni Mhandisi Gilead Kissaka, meneja wa kiwanda .

Mbolea Itokanayo na Samadi Iliyokwishameng’enywa

Baada ya bayogesi kuzalishwa, masalia ya samadi ambayo huwa imemeng’enywa hutolewa nje ya tanki la kuchachushia mara samadi mpya inapowekwa katika tanki, kupitia chemba maalum ya kuingizia mchamganyiko wa samadi. Samadi iliyomeng’enywa hutumika kama mbolea ya kukuzia mimea. Inafaa sana kwa kustawisha mimea ya aina mbalimbali.









Kwa makala zaidi, bonyeza hapa na hapa

MKUTANO WA WALIOSOMA MALANGALI SEKONDARI - IRINGA

Kuna baadhi ya wenzetu waliona ni vema kuwa tuliosoma shule ya Sekondari ya Malangali tukutane mnamo tarehe 5/2/2011 saa tisa alasiri pale Chonya Bar Riverside, Ubungo Dar Es Salaam. Mfahamishe kila mmoja ambaye atakuwa na fursa.


Kwa mawasiliano:-


Faraja 0787 525 396


Mawazo Kibamba 0713 555 725




Karibuni sana




Picha: John Mwaipopo na mimi, tukifurahia jambo pembeni ya ukumbi wa mikutano wa shule, enzi tukisoma Malangali Sekondari. Picha hii ilipigwa mwaka 1997 .

Mgao wa Umeme, utaishaje?

Mgao wa umeme
Historia inaonesha kwamba mgao usio wa kawaida wa umeme kwa nchi yetu kwa miaka ya karibuni ulianza mwaka 1992, kufuatia ukame wa muda mrefu ambao uliikabili nchi kwa sehemu kubwa, ukizingatia kwamba kwa kipindi hicho, sehemu kubwa ya umeme uliokuwa ukitumika hapa nchini ilitokana na nguvu ya maji (hydropower) na mafuta mazito (Heavy Fuel Oil – HFO). Kwa kipindi hicho, umeme utokanao na gesi asilia ulikuwa bado haujaanza kuzalishwa kwa kuwa miundombinu ya uzalishaji na usafirishaji wa gesi ilikuwa haijajengwa.
Mahitaji makubwa ya umeme kwa sasa hayaendani kabisa na kasi ya uwekezaji katika miundombinu ya uzalishaji wa umeme, suala hili limesababisha kiwango kidogo cha umeme unaozalishwa kugawiwa kwa wateja wachache kwa muda fulani, hivyo kuleta kitu kinachoitwa mgao wa umeme. Kabla hatujaingia katika mjadala wa namna ya kuondokana na mgao, ni vema tukaangalia historia 'fupi' ya mgao wa umeme tulionao.
Nilichoandika hapa chini nimechukua kutoka katika vyanzo mbali mbali, ikiwemo katika machapisho ya shirika la Tanesco, makala za magazeti, makala za mtandaoni na mahojiano binafsi na watendaji wa shirika hilo na mahojiano na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati.
**************************************************************************
Historia Kidogo
Kati ya mwaka 1996 na 2006 kilikuwa ni kipindi cha ubinafishaji wa mashirika ya umma kwa nchi yetu. Katika kipindi hiki mashirika mbali mbali ya umma yaibinafsishwa kwa wawekezaji mabepari ili kuyaendeleza. Katika orodha ya mashirika ya kubinafsishwa, Tanesco ilikuwemo. Ili kuiandaa Tanesco kubinafsishwa, serikali 'Haikuwekeza' rasilimali katika shirika hili, hivyo vitu vya msingi kama vile miundombinu ya uzalishaji umeme, usafirishaji na usambazaji, kuajiri nguvukazi mpya kila mara havikufanyika. Vitu hivi ni vya msingi sana katika suala zima la uhai wa shirika.
Ikumbukwe kuwa katika kipindi hicho, uchumi wa nchi ulikua kwa kiwango cha asilimia 7 kwa mwaka na kiwango hicho kiliendana na uwekezaji mkubwa katika migodi, kampuni za simu, kukua kwa sekta ya ujenzi (wa majengo ya kibiashara), kufunguliwa kwa mashamba makuwa yenye viwanda vya kusindika mazao, na kukua kwa sekta ndogo na za kati kiuchumi (small and medium sized enterprises). Sekta hizi ni watumiaji wakubwa wa umeme, hivyo waliongeza idadi ya wateja wakubwa wa umeme. Hadi kufikia mwaka 2002, shirika hili lilikuwa halijabinafsishwa, na kama nilivyotaja hapo awali hakukuwa na uwekezaji mkubwa tangu mwaka 1996.

Ujio wa Net Group Solutions
Mnamo mwaka 2002 serikali iliamua kuliweka shirika hili chini ya menejimenti kutoka nchini Afrika Kusini (Net Group Solutions) ili kukusanya mapato ya wadaiwa wakubwa na kuliandaa shirika na kubinafsishwa. Kampuni hii ilifanya kazi katika shirika hili hadi mwaka 2006 ya kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa wakubwa kama vile taasisi za serikali, jeshi, serikali ya Zanzibar na viwanda vikubwa. Ufanisi wa utendaji wa kampuni hii bado unatiliwa mashaka na wadau wengi, kwani haikusaidia kuondoa matatizo yaliyokuwa yakikabili shirika la umeme. Hatimaye mnamo mwaka 2006, serikali iliamua kutolibinafisha shirika lake. Mpaka hapo ikawa miaka 10 imeshapotea, ndani ya kigugumizi cha ugumu wa maamuzi ya 'Tubinafsishe' ama 'Tusibinafsishe'?.

Uwekezaji mpya kwenye umeme
Baada ya mwaka 2006 ndipo zikaanza juhudi za uwekezaji katika miundombinu ya umeme, mpaka sasa. Kwa mujibu wa ripoti ya mwezi Januari ya Tanesco, mahitaji ya umeme ni kiasi cha megawati 833, na mpaka mwezi huo shirika lililikuwa likizalisha kiasi cha megawati 1006 kutoka vyanzo mbali mbali kama vile maji, gesi na mafuta mazito. Katika kiwango hicho cha uzalishaji, umeme unaopatikana muda mwingi ni megawati 650 tu, hivyo hautoshelezi mahitaji. Ongezeko la mahitaji kila mwaka ni kati ya megawati 100 na 120. Hadi mwezi Juni mwaka 2011 ni megawati 145 tu ndizo ambazo zimeingizwa katika gridi ya taifa, hivyo suala la upungufu wa nishati hii bado ni kitendawili.

Hatua za dharura za uzalishaji umeme
Kimbilio kubwa la serikali katika kutatua janga la mgao imekuwa ni suluhisho la muda mfupi, la kutumia mitambo ya dharura ya kukodi ili kuzalisha umeme. Mitambo hii ambayo hutumia mafuta mazito na/au gesi na hutugharimu pesa nyingi kama taifa hivyo kuzorotesha uchumi. Hili ni pigo kwa uchumi wetu ambao bado ni mdogo. Suluhisho hili la muda mfupi la uhaba wa nishati haliwezi kutupeleka mbali, zaidi ya kutuongeezea umasikini. Kiwango cha gesi kinachopatikana sasa kwa ajili ya uzalishaji umeme ni kidogo, kwa sababu ya ufinyu wa miundombinu ya usafirishaji wa gesi kutoka mahali inapozalishwa kisiwani Songosongo hadi mahali inapotumika, Dar Es Salaam. Hivyo, hata kama mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi itanunuliwa na kufungwa leo, bado hatuwezi kupata umeme kwa sababu tuna upungufu wa gesi ya kuendeshea mitambo hiyo.


Tufanyeje kuepukana na mgao?


Utashi wa kisiasa
Kwa hili, kwa mtazamo wangu, kwanza kabisa kunahitajika utashi wa kisiasa (political will) wa wale tuliowakabidhi jukumu la kutuondolea umasikini. Utashi wa kisiasa ndio unaofanya kuwe na kigugumizi au maamuzi ya wapi tuweke rasilimali nyingi na wapi tuweke chache kulingana na vipaumbele vyetu vya taifa. Hatujawekeza rasilimali za kutosha katika utatuzi wa muda mrefu wa janga la upungufu wa nishati, hasa umeme. Kwa ulimwengu wa dijitali tulio nao, suala la upatikanaji toshelevu wa nishati linatakiwa kuwa ni kipaumbele namba moja. Huwezi kuongelea kilimo cha kisasa cha kuongeza thamani ya mazao kupitia usindikaji, iwapo huna umeme wa kuaminika. Huwezi kuongelea suala la kukuza sekta ya madini iwapo huna umeme wa kuaminika. Huwezi kukuza viwanda iwapo huna uhakika na umeme. Hakuna mwekezaji atakayekubali kupoteza rasilimali zake kwa kuwekeza mahali ambapo umeme si wa uhakika.

Uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati
Binafsi, sijaona mipango MADHUBUTI na INAYOTEKELEZEKA kwa rasilimali tulizonazo, ya kufanya uwekezaji mkubwa katika suala la nishati, hasa kwenye nishati jadidifu. Mpango wa serikali wa hadi mwaka 2015 ni kuzalisha megawati karibia 3000 na kuingiza katika mfumo wa gridi ya taifa. Mipango hii inategemea sana hisani ya wafadhili na mikopo. Binafsi sio mchumi, lakini natilia shaka sana mpango huu, kwa sababu kama taifa hatujaweka jitihada za kutosha kutoka vyanzo vya ndani vya mapato kugharamia miradi hii. Nimesoma bajeti za serikali kwa mwaka 2010/2011 na 2011/2012, bado hakuna mipango madhubuti ya uwekezaji mkubwa kutoka vyanzo vya ndani, kwenye nishati. Kwa miaka ya hivi karibuni, uchumi wa dunia umeyumba sana, na bado mpaka sasa katika nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya Euro uchumi haujatulia. Umoja wa Ulaya pamoja na serikali ya Marekani ndio wafadhili wakubwa wa miradi mingi ya nishati nchini kwa sasa, hivyo mtikisiko katika uchumi wao unaweza kubadili mwelekeo wa sera zao, kutoka kufadhili miradi na kutoa mikopo kwa nchi zinazoendelea na kupelekea kuinuana wao kwa wao kiuchumi, kama wanavyofanya kwa uchumi wa nchi ya Ugiriki unaoyumba. Hili linawezekana. Iwapo hili la kubadili sera litatokea, basi uwekezaji katika miradi ya nishati kwa hapa nchini utayumba na hivyo kuathiri utekelezaji wa mpango wa megawati 3000. Lisemwalo lipo!

Kudhibiti Upotevu na wizi wa umeme
Kwa mujibu wa takwimu za Tanesco kwa mwaka 2010, zilizochapwa katika ripoti iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia (Electricity loss Reduction Study, June 2011) , upotevu wa umeme huligharimu shirika kiasi cha dola za Kimarekani milioni 72. Katika umeme wote unaozalishwa, asilimia 20 ya umeme wote haufiki kwa wateja (kwa mfano, kama zinazalishwa megawati 850, ina maana megawati 170 zinapotea kabla ya kufika kwa wateja). Hiki ni kiwango kikubwa sana cha upotevu. Katika upotevu huu, asilimia 25 inatokana na ubovu na/au uchakavu wa miundombinu na asilimia 75 inatokana na upotevu kwenye mauzo. Takwimu hizi zinasikitisha kwa sababu shida kubwa ya upotevu haiko kwenye miundombinu kama wengi tunavyotarajia, ila kwenye mauzo (udanganyifu na ukosefu wa uadilifu). Iwapo kuna utashi wa kisiasa, asilimia hizo 75 ambazo zinatokana na (mkono wa mtu) zinaweza kudhibitiwa kabisa. Hasara hiyo ya dola milioni 72 inaweza kudhibitiwa na kuongeza kipato katika bajeti ya taifa.

Udhibiti wa mikataba tata ya uzalishaji umeme
Kumekuwa na matatizo kwenye mikataba ya uzalishaji umeme inayosainiwa kati ya serikali na kampuni binafsi. Mikataba mingi imetokana na mpango wa dharura wa uzalishaji umeme, hasa kunapokuwa na shida ya mgao. Mikataba hii imetokana na maamuzi mabovu ya makusudi ya watendaji waliopewa dhamana ya kusaini mikataba hii kwa niaba yetu. Udhibiti wa mikataba mibovu unahitaji utashi wa kisiasa pia, kwa wale tuliowapa dhamana ya kudhibiti utendaji mbovu. Napendekeza kwamba kutungwe sheria (kama haipo), kwamba mikataba mikubwa, kama ile ya uchimbaji wa madini na uzalishaji mkubwa wa nishati, ipitie kwanza bungeni, na iwapo ina maslahi kwa nchi basi iidhinishwe na bunge kabla serikali haijatia saini kwa niaba yetu! Kwa mbinu hii, tutaweza kuwa na uzalishaji mkubwa wa umeme usio na mawaa, kwa kuwa kila kitu kitafanyika kwa uwazi kupitia wawakilishi wetu bungeni.

Hitimisho
Suala la umeme lina maslahi mapana kwa taifa, kiuchumi, kiusalama na kijamii, si la kulifanyia maamuzi ya mzaha na pupa. Uhaba wa umeme unaathiri uchumi wa nchi, kwani uzalishaji katika ofisi, mashamba na viwanda unategemea umeme. Mgao unaathiri sekta nyingine kama vile maji, ambayo husukuwa kwa pampu zitumiazo umeme, kutoka pale yanapotekwa kwenda pale yanapotumika. Tuchukue hatua madhubuti za kuepuka janga hili, kwa maendeleo ya taifa! Tutimize wajibu wetu!

Nimefungua mjadala, tuendelee kuelimishana.

Jiunge na Harakati za Siku ya Blogu Duniani

Siku ya Blogu ni ipi?
UtanguliziNi tukio ambalo linawakutanisha waandishi na wamiliki wa blogu duniani kujadili kuhusu mada moja ambayo huwa imechaguliwa na kisha kuweka mada hiyo katika blogu zao anuwai. Siku hii ni tarehe 15 Oktoba ya kila mwaka na imekuwa ikiadhimishwa tangu mwaka 2007. Matukio ya siku hii huratibiwa na mtandao uitwao ‘Blog Action Day’ (http://blogactionday.org) .

Mada za Siku ya Blogu
Kwa miaka ya nyuma, mada zilizowahi kujadiliwa ni umasikini (ufukara), maji na mabadiliko ya tabianchi. Mwaka jana 2010 mada iliyokuwa imechaguliwa ilihusu maji, kwa hiyo wanablogu duniani kote tulishiriki katika majadiliano kwa njia ya mtandao kuhusu suala la maji, kwa upana wake. Binafsi, nimeandika mada anuwai kuhusu maji na mazingi (kwa kuwa ndiyo taaluma yangu ilikoegemea). Mwaka huu, siku ya blogu duniani imesogezwa mbele kwa siku moja ili kushabihiana na siku ya chakula duniani (tarehe 16 Oktoba), kwa hiyo mada kuu ya mwaka huu inahusu CHAKULA! Kwa maana hiyo basi, wanablogu mbalimbali duniani wataandika mada mbali mbali kuhusu chakula, iwe ni upatikanaji wake, uhifadhi, uandaaji, matumizi, uharibifu, maadili katika usindikaji, ulafi, uhaba na namna tunavyowezesha upatikanaji wa chakula kwa jamii zote duniani na kadhalika.
Unakaribishwa kushiriki katika majadiliano haya, pia unaweza kujisajili katika mtanda wa Blog Action Day katika anuani niliyoiweka hapo juu!
Ahsante sana.