7/31/07

SAFU ZA MILIMA YA USAMBARA

UTANGULIZI

Safu za milima ya Usambara ni sehemu tu ya safu za milima ya tao ya mashariki "eastern arc Mountains". Milima hii inaunganishwa na safu ya milima ya Udzungwa na Uluguru katika uhifadhi. Inasifika kwa kuwa na viumbe wengi wa namna ya pekee (endemic), kwa hiyo inapewa umuhimu mkubwa sana katika utunzaji wake na taasisi za kimataifa kama vile 'Critical Ecosystem Partneship Fund (CEPF), International Centre for Insect Physiology and Ecology (ICIPE) pamoja na 'Birdlife International'. Safu za milima hii zinaambaa ambaa toka Muheza, Korogwe hadi Lushoto katika mkoa wa Tanga.







Picha: Sehemu ya Msitu wa Kandelekampaa katika milima ya Usambara iliyoathiriwa kwa moto na kilimo, katika Kijiji cha Ndabwaa kata ya Malindi wilaya ya Lushoto


UMUHIMU WAKE
Safu za milima hii ni chanzo cha mito mingi sana, kama vile mto Zigi, mto Pangani na mto Umba, lakini sehemu kubwa ya misitu ya safu hizi imeharibiwa sana, hasa maeneo ya Lushoto na Korogwe, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu ambao kwa kiasi kikubwa hutegemea shughuli za kilimo na upasuaji wa mbao. Maeneo yaliyoathiriwa sana na shughuli hizi ni yale ya Usambara Magharibi, hasa wilayani Lushoto. Huku ndio sehemu kubwa sana ya misitu hii imefyekwa ama kuchomwa moto kabisa, hasa katika vijiji vya Ndabwa, Magamba na Lukozi. Kwa upande wa wilaya ya Muheza, angalau kuna matumaini, kwani misitu ya upande huu imetunzwa kwa kiasi cha kuridhisha. Ikumbukwe kuwa matunda na mboga mboga kutoka wilaya hizi hutoka katika mashamba ambayo ama yapo pembezoni mwa misitu hii ama yanapata maji yake toka katika misitu hii.



Picha Juu: Mto mkuzu, ambao hutoka katika milima ya Usambara. Mto huu ni tegemeo sana kwa wakazi wa vijiji vingi vya Lushoto kwa umwagiliaji na matumizi ya nyumbani.

Pichani: Kabichi ambazo hulimwa katika mashamba yaliyo katika safu za Milima ya Usambara

ELIMU YA MAZINGIRA
Kuna taasisi kadhaa ambazo zinajihusisha na kuelimisha jamii zilizo katika maeneo haya juu ya kutunza safu za milima hii, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha utalii rafiki wa mazingira (eco-tourism). Taasisi hizi ni kama vile Friends of Usambara Society (FOU), West Usambara Women Education (WUWE), Lushoto Youth Development Network na kadhalika. Hata hivyo bado juhudi zaidi zinahitajika katika kupunguza athari hizi.

6/13/07

NAFASI ZA UONGOZI KATIKA JUMUIYA YA WANABLOGU WA TANZANIA

OMBA NAFASI ZA UONGOZI
Ndugu msomaji wa blogu hii, kuna nafasi mbali mbali za uongozi zimetangazwa katika Jumuiya ya Wanablogu wa Watanzania. Unaruhusiwa kugombea nafasi yoyote, na si lazime uwe na blogu ili kupata nafasi hizo. Nafasi hizo zinazonadiwa ni za Mwenyekiti, Mhazini, Katibu na nyinginezo.

MAMBO YA KUZINGATIA
Tuma picha yako ukiambatanisha na wasifu wako, pamoja na sababu zinazokutuma kugombea na nafasi unayogombea. Ueleze ni kitu gani unataka kuifanyia Jumuiya katika kuikuza. Tuma maelezo yako kwa 'mijasayi@yahoo.com'.
Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea blogu ya Jumuiya 'http://blogutanzania.blogspot.com'

5/22/07

MWAKA MMOJA WA KUJADILI WATIMIA!

TOVUTI YATIMIZA MWAKA
Leo tarehe 22/05/2007 tovuti hii inatimiza mwaka mmoja tangu izinduliwe rasmi mwaka jana 2006. Tarehe kama hii mwaka jana ndipo makala ya kwanza ilibandikwa mahali hapa. Nakumbuka jinsi ilivyokuwa vigumu kuamua cha kuandika, lakini hatimaye mambo yakaenda vyema na mpaka leo naendelea kusimama.
Tangu izinduliwe rasmi mwaka jana, tuvuti hii imefanyiwa madiliko ya mwonekano mara tatu na bado itaendelea kuboreshwa kwa kuongeza mambo mapya ambayo kwa sasa yanaandaliwa.
Kimsingi mawazo ya kuanzisha blogu hii yalitokana na ushawishi mkubwa wa Mzee wa "Baragumu", ambaye ni swahiba wangu wa siku nyingi sana, tangu tukiwa tunasoma shule moja ya sekondari mkoani Iringa. Huyu ndiye aliyenishawishi kwa kiasi kikubwa kuanzisha tovuti hii na baadaye akafuatiwa na mwanablogu nguli, Mzee wa "Jikomboe". Pamoja na hawa pia kuna kundi kubwa sana la wanablogu wenzangu ambao naweza kuujaza ukurasa huu kama nitaamua kuwataja mmoja baada ya mwingine ambao wamekuwa wakitoa michango yao mbali mbali ya mawazo katika kuiboresha tovuti hii, hawa nao nawapa shukrani za pekee.
Nayathamini sana mawazo yenu na naomba tuendelee kushirikiana ili tuweze kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kuboresha mazingira yetu.
Naahidi kuendelea kuweka makala za kuzua mijadala ya kuboresha maisha yetu mahali hapa, na naomba tuendelee 'kujadili' kama kawaida yetu.

4/30/07

SAFISHA HAPA.....CHAFUA PALE!

UTANGULIZI

Ni suala la kawaida kukuta barafu/theluji katika miinuko ya maeneo mbali mbali ya nchi zilizo katika Tropiki ya Kansa, yaani nyuzi 23.26' kaskazini mwa Ikweta, hasa wakati wa majira ya baridi. Barafu/theluji huongezeka zaidi kama unazidi kuelekea kaskazini katika mzingo wa Aktiki (nyuzi 66.33'). Kwa wenyeji wa maeneo haya, huu ni msimu wa michezo ya wakati wa baridi kama vile kuteleza katika theluji na kutembea katika maji yaliyoganda (barafu). Lakini kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri kama baiskeli, magari, treni na ndege ni msimu usiopendeza sana. Kwa upande wa baiskeli, magari na ndege, ni msimu wa kubadilisha magurudumu. Magurudumu yanayotumika wakati wa kiangazi ni tofauti na yale yatumikayo wakati wa baridi. Tofauti yake ni kwamba magurudumu ya msimu wa baridi huwa na misumari midogo midogo katika uso wake, ili kuleta msuguano wa kutosha (friction) wakati chombo kinapopita katika barafu ama theluji. Bila magurudumu ya namna hii ni rahisi sana kwenda nje ya barabara kama kuna theluji, kwa sababu huwa inateleza sana. Theluji pia hujaa katika reli na kusababisha utelezi. Ni kawaida kwa maeneo haya kukuta vyombo vya kusafisha theluji barabarani kila asubuhi.

UONDOAJI WA THELUJI
Theluji ikishafagiliwa, hukusanywa mahali na kisha kuzolewa katika magari makubwa na kwenda kutupwa. Shida yake huanzia hapa, kwamba mara nyingi katika nchi hizi theluji hutupwa katika bahari ama maeneo mengine ambayo ni oevu. Iwapo kunakuwa na joto theluji hii huyeyuka na kuwa maji. Wanamazingira hawapendezwi na suala hili la kutupa theluji na barafu katika maeneo haya. Madai yao ni kuwa, mara nyingi theluji inayokusanywa mitaani huwa na takataka sana, kwa hiyo unapoikusanya na kwenda kuimwaga baharini ama maeneo mengine unakuwa unasababisha uchafu mahali hapo. Ieleweke pia kuwa theluji hii huweza kuambatana na mafuta yanayotumika kulainishia ama kuendeshea mitambo, hivyo kama itatupwa katika maeno yenye unyevu basi itasababisha kufa kwa viumbe hai ambao hutegemea maji hayo kwa maisha yao kama vile samaki na vyura. Hali kadhalika mafuta huganda katika mbawa za ndege wavuvi, hivyo hushidwa kuruka kujitafutia riziki zao na hivyo hufa kwa njaa.

SULUHISHO
Kutokana na malalamiko ya wanamazingira kuhusiana na uchafuzi huu, wazoaji wa theluji (hasa halmashauri za miji) wameamua kutupa theluji hii katika maeneo maalum yalitengwa kwa ajili hiyo (dump sites). Kwa hiyo maeneo hayo huwa ni maalum kwa ajili ya kumwaga theluji na barafu na uchafu unaoambatana navyo. Bado wanamazingira hawajaridhika na kitendo hiki, kwa sababu wanasema unatibu tatizo moja huku ukisababisha jingine la uchafuzi wa mazingira. imsingi barafu na theluji ni maji, na wanaomwaga wanajua kuwa wakati wa kiangazi huwa inayeyuka, suala linalogombaniwa hapa ni taka zinazoambatana na theluji ama barafu, kuwa ndizo zinazoleta madhara katika mazingira. Mpaka sasa bado kuna mgongano wa mawazo kuhusu nini kifanyike ili kutatua mvutano huu, tusubiri tuone matokeo yake.
Kwa upande wa nchi za Kitropiki hakuna tatizo la barafu, katika miji, ila suala la utupaji ovyo wa taka lipo na limeshamiri sana.

Barafu iliyokusanywa, ikisubiri kuzolewa na kwenda kutupwa!

4/12/07

FAHAMU MVUA ZA TINDIKALI

MVUA ZA TINDIKALI

UTANGULIZI

Katika makala zangu zilizopita, niliwahi kudokeza kidogo kuhusu mvua za tindikali, ama kwa Kiingereza ’Acid rains’. Leo nafafanua zaidi kuhusu mvua hizi, nikianzia na chanzo, madhara yake, namna ya kupima madhara yake na namna ya kupunguza mvua hizi.

CHANZO CHA MVUA ZA TINDIKALI
Kimsingi, mvua za tindikali husababishwa na chembe chembe nyevunyevu na zile kavu za baadhi ya gesi ambazo kwa pamoja huwa zinaelea angani. Chembe chembe hizi aghalabu ni tindikali ya salfuriki ama naitriki. Kuna vyanzo vikuu viwili vya tindikali hizi katika anga. Kwanza ni vyanzo vya asili ambavyo mwanadamu hana mamlaka navyo na hana namna ya kuvizuia, kama vile volkano na kuoza kwa mimea. Baadhi ya mimea inapooza huzalisha kiasi fulani cha tindikali, ambayo iwapo itakutana na maji basi huwa na madhara katika ardhi. Vivyo hivyo, kunapotokea mlipuko wa volkano, majivu pamoja na gesi kutoka katika volkano hizi huwa na chembe chembe za tindikali ambazo hupelekwa angani na kuelea. Kwa hiyo vitu hivi vikichanganyikana na maji au unyevu katika anga hufanya tindikali ambazo nimezitaja hapo juu.
Pili, viwanda vingi hasa vinavyozalisha nishati kwa kutumia tungamotaka hasa makaa ya mawe, mkaa na kuni huzalisha hewa nyingi sana za oksaidi za salfa na naitrojeni (SO2) na (NOx). Sasa basi, iwapo hewa hizi zitachangayikana na unyevu ulio angani pamoja na kemikali nyingine zinazoelea angani basi tindikali tajwa hapo juu na nyingine nyingi hutokea. Kuna wakati gesi hizi huweza kusafirishwa mbali zaidi kwa njia ya upepo na kuleta madhara mahali mbali kabisa na chanzo chake.

2H2O + 2SO2 + O2 → 2H2SO4 (dhaifu)
Hii ni tindikali ya salfuriki.

Mchanganyiko wa tindikali ya naitriki huwa kama ifuatavyo:
NO2 + OH· → HNO3 (dhaifu)

CHEMBE CHEMBE NYEVU
Kama nilivyodokeza katika aya za hapo juu, chembe chembe za hizi tindikali huweza kuwa nyevu ama kavu. Kwa upande wa chembe chembe nyevu, hizi huwa katika mfumo wa mvua, manyunyu, ukungu ama theluji. Sasa basi, iwapo upepo utapeperusha chembe chembe hizi mahali ambapo hali ya hewa ni ya unyevu, basi chembe chembe hizi hutua katika uso wa dunia kama mvua, ukungu, manyunyu ama theluji kulingana na hali ya hewa ya mahali husika. Sasa basi maji ya mvua ama ukungu ama manyunyu yaliyo na tindikali huwa na madhara kwa viumbe hai ambao wanatumia maji haya kwa namna moja ama nyingine. Makali ya athari ya tindikali hii hutegemena na kiasi cha tindikali kilicho katika maji haya, aina za udongo, wanyama na mimea inayotegema maji haya.

CHEMBE CHEMBE KAVU
Katika maeneo ambayo hali ya hewa ni kavu kabisa, kama ilivyo katika jangwa, chembe chembe za tindikali huweza kuchanganyika na vumbi ama moshi na kutua katika ardhi vikiwa katika hali ua ukavu hivyo hivyo. Vumbi ama moshi wenye tindikali hii huganda katika vitu mbali mbali kama vile mapaa ya nyumba, magari, madaraja, majengo na mimea. Sasa iwapo mvua kidogo tu itanyesha na kusafisha vitu hivi basi tindikali hii husambaa na kuleta madhara katika maeneo mbali mbali.

ATHARI ZA MVUA ZA TINDIKALI
Mvua za tindikali huchangia sana kuongeza sumu katika maeneo mbali mbali kama vile mito, maziwa na wakati mwingine husababisha mimea kupukutika ama kufa kabisa, kwa sababu tindikali hii huunguza majani na mashina ya mimea hii. Mvua hizi husababisha kuoza kwa mapaa yanayoezekwa kwa bati ama chuma na pia huathiri sana rangi za majengo. Gesi za oksaidi za salfa na naitrojeni pia huathiri uwezo wa kuona pamoja na kupumua kwa mwanadamu.

Athari Katika sehemu oevu
Sehemu oevu ni zile ambazo zina unyevu nyevu katika msimu wote wa mwaka kama vile mito, maziwa, madimbwi na ardhi oevu. Katika maeneo haya, mvua za tindikali huathiri wanyama na mimea ambavyo hutegema maji haya. Kwa kuwa maji haya yanakuwa na kiasi kikubwa cha tindikali kuliko uwezo wa viumbe hawa kuhimili, basi viumbe hawa hushidwa kuishi na hivyo hufa. Majani ya mimea katika maeneo haya hupukutika, kwa sababu tindikali hizi huunguza mimea hii na hivyo kuifanya kushindwa kusanisi chakula (photosynthesis).

Athari Katika Misitu
Kimsingi, jamii mbali mbali za mimea hutofautiana katika ustahimilivu wa madhara ya kimazingira. Mimea hutofautiana katika ustahimilivu wa ukame, baridi, joto kali, maji mengi (mafuriko), ukosefu wa mwanga na uharibifu mwingine. Hivyo basi, katika misitu ya namna mbali mbali, athari za tindikali hutofautiana. Ila athari za jumla za tindikali katika misitu ni kuchelewa kukua kwa mimea, kupukutika majani na kufa kabisa kwa mimea. Marekani, hasa katika misitu yake ya upande wa mashariki imeathirika sana na madhara haya ya kukauka kwa mimea, hasa maeneo yaliyo karibu na milima ya Appalachian. Hali kadhalika nchi kama Kanada, Urusi na nyingine za Ulaya ya Mashariki zimeathirika sana kutokana na mvua hizi za tindikali.

Athari Katika Rangi za Majengo, Magari na Metali
Rangi hutengenezwa kutokana na mchanganyiko wa kemikali mbali mbali. Hivyo basi, iwapo mvua za tindikali zitatua katika maeneo yaliyopakwa rangi huweza kubabua rangi hizi na kusababisha kitu kilichopakwa rangi kupoteza hadhi yake. Mfano, kama rangi ya gari itapukutika kutokana na tindikali hizi bila kupakwa tena, basi kutu itavamia na kuozesha gari husika. Hali kadhalika, metali za namna mbali mbali hupakwa ramgi ili kuchelewesha kutu, hivyo kama tindikali itaondoa rangi hizi basi kutu uweza kuathiri metali hizi. Mfano wa metali hizi ni katika madaraja, nguzo za chuma, sanamu za vyuma na mihimili mbalimbali. Athari hizi huenda kwa namna hii hii katika majengo mbalimbali yaliyopakwa rangi.

Athari za Uoni (visibility) kwa Mwandamu
Hapo juu nilidokeza kuwa gesi za oksaidi za salfa na naitrojeni husababisha madhara katika uwezo wa kutazama wa mwanadamu. Kunapokuwa na msongamano wa hewa hizi katika anga, mwanadamu hawezi kutazama mbali kwa sababu hewa hizi hufanya ukungu ambao huzuia kuona mbali. Athari za namna hii ni maarufu sana nchini China, hasa katika maeneo ambayo hutumia makaa ya mawe kuzalisha nishati kama vile katika jiji la Shanghai katika Jamhuri ya watu wa China.

Madhara mengine
Madhara mengine kwa mwanadamu ni kuwa, iwapo atavuta hewa hizi zinazosababisha mvua za tindikali katika mfumo wake wa hewa, basi huweza kuathiri uwezo wa mapafu kufanya kazi, hivyo huweza kuata magonjwa kama pumu na kansa.


UPIMAJI WA MVUA ZA TINDIKALI
Utambuzi wa mvua za tindikali hupimwa kwa kutumia skeli ya ‘pH’. Kipimo hiki pia hutumika kupima kiwango cha alkali ama besi katika ardhi na maji. Maji yaliyotakaswa (purified water) kwa kawaida huwa na kiwango cha 7.0 katika kipimo tajwa. Jinsi kipimo hiki kinavyofanya kazi ni kwamba, kuanzia katika kiwango cha 7 kushuka chini huashiria ongezeko la tindikali na kuanzia 7.5 hadi 14 huashiria ongezeko la alkali ama besi. Kwa hiyo kiwango cha 7 katika pH huchukuliwa kama ndio alama ya katikati kati ya alkali na tindikali.


NAMNA YA KUPUNGUZA MVUA ZA TINDIKALI
Kwa maneno rahisi mtu anaweza kufikiri kuwa namna rahisi ya kupunguza msongamano wa gesi zinazosababisha mvua za tindikali ni kupunguza moshi kutoka viwandani moja kwa moja. Hili si jambo rahisi sana namna hiyo kutokana na sababu mbalimbali. Nilieleza kuwa mojawapo wa vyanzo vya gesi hizo ni pamoja na nguvu za asili kama vile volkano na kuoza kwa mimea. Hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kuzuia volkano, sana sana ikitokea huwa tupewa maonyo ya kuiepuka kwa kukimbilia mahali salama. Hivyo basi, matukio kama haya yataendelea kusababisha mvua za tindikali. Hali kadhalika si rahisi sana kuzuia mimea isioze na kusababisha gesi hizi. Kuoza kwa mimea husaidia kuleta rutuba katika ardhi, kwa hiyo hili nalo hatuna mamlaka nalo sana. La muhimu hapa ni kupunguza matumizi ya makaa ya mawe, kwa kutumia vyanzo vingine safi vya nishati kama umeme wa jua na umeme wa nguvu ya maji. Suala hili lmekuwa gumu kutekelezeka kutokana na mgongano wa sera katika nchi mbali mbali. Lakini hata hivyo kuna matumaini katika kufanikiwa, kwa sababu sasa dunia imeamka na kuanza kuhangaikia kupunguza hewa zenye sumu katika anga. Mojawapo ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kutengeneza magari na mitambo mingine inayotumia mafuta yaliyochanganywa na mafuta ya mimea, (biodiesel).
Hali kadhalika, kumeanzishwa sheria kuwa, anayechafua zaidi anga kwa moshi wenye sumu na alipe zaidi kadri ya anavyochafua. Angalau sheria hizi zinafanya wachafuzi washituke kidogo na kuona kuwa wanahusika na uchafuzi huu.

Unaweza kusoma zaidi kuhusu mvua za tindikali hapa, hapa ama hapa.

3/15/07

UNAIFAHAMU NADHARIA YA r & k?

UTANGULIZI
Dhana hii ya r na k inaelezea mifumo mbali mbali ya maisha ya viumbe hai ambapo mifumo hii hufanya uwepo ama upotevu wa viumbe hivyo. Wataalamu wa mwanzo kuja na nadharia hii katika ikolojia ni mabwana Robert McArthur na Wilson mnamo mwaka 1967. Wao walifanya uchunguzi na kugundua kuwa katika maisha ya viumbe hai (kwa upande wao walifanya utafiti kwa mimea) kuna mfumo fulani wa urithi wa maisha ambao hutofautiana kati ya vinasaba vya mimea fulani na mingine. Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba, mimea kama magugu na miti hutofautiana katika mfumo wa maisha yake. Kwamba, magugu na nyasi hutumia sehemu kubwa ya chakula chao kuzalisha viumbe wengi zaidi wa jamii yao, ambao hata hivyo hawadumu kwa muda mrefu, wakati mimea mikubwa kama miti hutumia sehemu kubwa ya chakula chao katika ulinzi na kuongeza umri wa mimea ya jamii hiyo, hivyo kufanya mimea hii kudumu kwa muda mrefu. Hali kadhalika, kwa jamii za nyasi na magugu, pamoja na mimea mingine ya jamii hizo, huzaliana mara moja tu katika kipindi cha uhai wao, tofauti na mimea jamii ya miti ambayo hutoa mbegu karibu kila mwaka.
Kwa hiyo basi, kwa mujibu wa wasomi hawa, mimea ambayo inazaliana kwa wingi zaidi na haidumu sana inakuwa katika kundi la R, na ile inayozaliana kidogo kidogo na kudumu zaidi huwa katika kundi la K.

SIFA ZA VIUMBEHAI KATIKA KUNDI LA 'R'
Viumbe katika kundi hili huwa katika mazingira ambayo si stahimilivu na uwepo wake na kudumu kwake hutegemea uwingi wake. Nishati (inayotokana na chakula) inayotumika katika maisha ya kila kiumbe ni kidogo sana. Vizalia wengi zaidi huzaliwa katika kundi hili. Hukomaa kwa muda mfupi zaidi na huwa na maisha mafupi kwa ujumla. Jamii za mimea za kundi hili huzalisha viumbe mara moja tu kwa kila kiumbe na baadaya hapo hufa. Viumbe wa kundi hili la 'R' si stahimilivu wa athari za kimazingira kama vile mafuriko, moto, ukame na mashambulio ya wadudu waharibifu kama vile kuvu, nzige na viwavi.

SIFA ZA VIUMBEHAI KATIKA KUNDI NA 'K'
Viumbe katika kundi hili huwa katika mazingira stahimilivu na huweza kuvumilia athari kama vile ukame (kwa kupukutisha majani), huweza kuvuilia moto (kwa kuwa na magamba magumu), huweza kuvumilia mafuriko (kwa mimea kuwa mirefu zaidi), na inaweza kuwa na sumu ili kuzuia kuliwa na wanyama. Jamii za viumbe wa kundi hili wana maumbo makubwa, kama vile miti. Nishati inayotumika katika kuufanya mmea huu uwepo kwa muda mrefu ni kubwa sana na huzalisha viumbe wachache ambao hudumu kwa muda mrefu. Viumbe wa kundi hili pia huchukua kuda mrefu sana kukomaa na kuanza kuzaliana, na huzaa kwa zaidi ya mara moja. Ukichukulia mfano wa miti, huchukua miaka mingi hadi kuanza kuzalisha mbegu, na ikishaanza kuzaa basi huishi muda mrefu, kama haujakutwa na majanga ama kukatwa. Ni mara nyingi viumbe wa kundi hili huishi maisha marefu sana, kwa mfano kuna baadhi ya miti kama mibuyu na mininga ambayo huweza kuishi kwa zaidi ya karne tatu.
Lakini pamoja na kuwa na tabia zisizofanana, kuna wakati sifa za kundi moja huweza kukutwa katika kundi jingine pia. Kwa mfano, mimea jamii ya miti huishi kwa muda mrefu sana ukilinganisha na nyasi, na hivyo kuifanya iwe katika kundi K, lakini ni miti hiyo hiyo ambayo baadhi yake huzalisha mbegu nyingi sana na kuzisambaza mahali mbali mbali kwa ajili ya kuendeleza kizazi. Sifa hii ni ya kundi la R.

ULINGANIFU NA USHIRIKIANO WA KIMAZINGIRA
Pamoja na kuwa mimea tajwa hapo juu ipo katika makundi tofauti, huwa inafanya kazi moja ya kufanya uwepo wa mazingira bora kwa kila kundi. Kwa mfano, inapotokea janga kama volkano, huwa mimea na wanyama huathirika sana, kutegemeana na ukubwa wa tukio. Mara nyingi inapotokea maisha kuanza tena baada ya janga, mimea ya kundi R ndio huwa ya kwanza kuanza maisha, kwa kuzaliana upesi na kusambaa kwa haraka, na hivyo kutengeneza nafasi kwa ajili ya jamii nyingine za mimea katika kundi la K. Mfumo huu kwa kiingereza huitwa 'Ecological Succession' na ni mfumo unaopatikana mahali pengi sana duniani, kutokana na uharibifu ambao umetokea katika maeneo mbali mbali. Mimea inayozaliwa baada ya ile ya kwanza kuondolewa huitwa uzao wa pili, ama kwa kiingereza 'Secondary regrowth'.
Kwa hiyo basi, tunapoongelea suala zima la mazingira, ni lazima tuwe tunaangalia muingiliano kati ya kiumbe na kiumbe, kwa sababu mara nyingi huwa na uhusiano wa karibu. Kwa maana hiyo unapokata mti ambao kukua kwake hadi kukomaa huchukua si chini ya miaka 30, kama ilivyo kwa miti ya asili, ujue pia kuwa unaathiri na uwepo wa viumbe wengine ambao kwa namna moja hutegemea mti huo ama kwa kivuli, ama kwa kutunza maji au kwa namna nyingine yoyote ile. Fikiri kabla hujatenda!

3/9/07

TOVUTI INAFANYIWA MABADILIKO!

KUHUSU MUONEKANO WA TOVUTI

Ndugu msomaji wa makala zangu, kutokana na mahitaji ya wakati na kukua kwa teknohama, nimebadili muonekano wa tovuti hii, kwa hiyo kama unaivyoiona iko tofauti kimuonekano na ile ya mwanzo. Makala zake bado ni zile zile na nafikiri sasa nimepata uwanja mpana zaidi wa kuandika, tofauti na ile ya mwanzo ambayo ilikuwa na nafasi finyu sana, hata kuweka picha ilikuwa ni mizengwe. Muonekano wa tovuti hii umefanyiwa kazi na mimi mwenyewe, na bado kazi hiyo inaendelea, kwani ukiangalia viunganishi upande wa kulia wa tovuti bado havijapewa majina ya tovuti wakilishi. Kwa hiyo ndugu msomaji kama kutakuwa kuna mahali panaleta usumbufu ama viunganishi havikupeleki mahali unapotarajia, naomba weka maoni yako mwishoni mwa makala hii, na pia kama utataka maelezo zaidi kuhusu tovuti hii basi unaweza kuwasiliana nami kwa anuani pepe hii hapa.

2/5/07

TUTAENDELEA NA UBISHI HUU HADI LINI?


UTANGULIZI
Katika kukabiliana na ukweli, wanasayansi wa mazingira pamoja na watafiti wengine wameungana na sehemu nyingine ya jamii katika kuthibitisha kuwa mabadiliko yasiyo ya kawaida ya hali ya hewa ikiwemo ongezeko la joto duniani husababishwa kwa asilimia tisini na kazi za binadamu katika kujitafutia riziki. Asilimia kumi inayobaki inatokana na mabadiliko ya kawaida ya mwenendo wa dunia kama vile matetemeko ya ardhi na volkano. Ripoti ya tafiti za wanasayansi hawa kutoka maeneo mbali mbali hapa duniani imetolewa mwezi huu wa pili 2007. Ni kwa mara ya kwanza katika historia ya utawala wake, mwaka huu ambapo rais wa Marekani alitaja suala la uchafuzi wa hali ya hewa, napo alitamka kwa sekunde chache sana suala hilo hata bila kugusia undani wa tatizo lenyewe na wala hakufafanua atakavyofanya kukabili kadhia hiyo.


HALI HALISI
Kitakwimu nchi zilizoendelea ndio zinaongoza kwa kuchafua hali ya hewa, kutokana na moshi toka viwandani, zikiongozwa na Marekani. Kwa mujibu wa kitengo cha nishati cha serikali ya Marekani, takwimu zinaonyesha kuwa, hadi mwaka 1999, Amerika ya kaskazini (Marekani na Kanada) ndio walikuwa vinara wa kuchafua anga kwa hewa ya kaboni, kwa kiwango cha meta za ujazo milioni 1,720.4! Waliofuatia kwa uchafuzi ni nchi za Ulaya Magharibi, kwa kiwango cha meta za ujazo milioni 988.9. Viwango vya uchafuzi kwa maeneo mengine katika mabano ni Ulaya Mashariki (851.8), China (821.8), Asia (ukiondoa China na Japan, 700.8), Japan (296.7), Amerika Kusini (234.7), Mashariki ya kati (252.1) na Afrika (213.8). Takwimu hizi ni hadi mwaka 1999, na kwa sasa inaonyesha kwamba Marekani ndio inaongoza kwa uchafuzi ikifuatiwa na China. Pamoja na ukweli huu, inasikitisha kuona kuwa Wachina na Wamarekani ni kati ya watu wa mwisho kujadili athari za ongezeko la joto duniani, kwa sababu kuu kwamba iwapo watatakiwa kupunguza hewa chafu angani, basi viwanda vyao vingi vitadhoofika na hatimaye uchumi wao utayumba.

KILIO CHA DUNIA
Kutokana na mabadiliko haya ya hali ya hewa, kumekuwa na makongamano na mikutano kadhaa ya kimataifa katika kutafuta suluhu ya kudumu ya uchafuzi wa anga, kama nilivyowahi kuongelea katika makala zilizopita. Mojawapo ya mikutano hiyo ni ule uliofanyika katika mji wa Davos nchini Uswisi mwezi huu Februari. Mataifa makubwa yalikuwa yanajadili kuhusu biashara na suala la uchafuzi wa hali ya hewa likaibuka hapo. Katika mkutano huo pia, dunia ilimshangaa mkuu wa kampuni ya Nestle inayotengeneza vyakula, Bw Peter Brabeck-Letmathe aliposema kuwa suala la ongezeko la joto halina uzito wowote kwa sasa! Pia wakamshangaa mpinzani wa Bush kisiasa, Bw Al gore katika filamu yake ambapo anapinga suala la ongezeko la joto. Al Gore yeye anasema kuwa pesa zinazotumika sasa katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani kupitia makubaliano ya Kyoto (ambapo Marekani haijatia saini) zingetumika katika kuboresha mindombinu ya maji pahala mbali mbali! huyu alikuwa mgombea uraisi ambaye alishindwa na Bush mnamo mwaka 2000.
Sina uhakika kama hawa watu walimaanisha kile ambacho waliongea ama walikuwa wanatania, lakini kwa sababu ni wafanyabishara nadhani walimaanisha kuwa hawana mpango kabisa wa kukabili tatizo hili la ongezeko la joto. Sasa mimi ninauliza, ubishi huu tutaendelea nao hadi lini?
Unaweza kusoma habari zaidi a mkutano huo hapa, hapa na hapa.

2/3/07

GARI LA MIONZI YA JUA HILI HAPA!


UTANGULIZI

Kumekuwa na usemi kwamba *Tembea uone*. Usemi huu una maana kubwa, kwamba ukiwa mtembezi basi utaona mengi. Pia kuna usemi unaoambatana na huo, kwamba Mtembea bure si mkaa bure, huenda akaokota! Basi katika pita pita yangu hapa na pale, kwa maana ya kwamba nilikutana na habari njema kwa watu wanaojali matumizi endelevu ya nishati na upunguzaji wa hewa chafu duniani. Nilikuta gari moja zuri katika makumbusho, ambalo kwa mujibu wa watu niliowakuta hapo wanasema kuwa lilikuwa linaendeshwa kwa kutumia umeme wa mionzi ya jua. Sababu za kwa nini kwa sasa halitembei ni kwamba hali ya hewa si nzuri sana kuweza kuchaji betri za umeme wa mionzi ya jua kwa mahali hapo, huwa mionzi ya jua si ya kutosha kuchaji betri hadi kuwa na ujazo unaotakiwa.


GARI LENYEWE

Katika boneti la mbele kwa juu kuna moduli kadhaa za kufyonza mionzi ya jua na kuihifadhi katika betri zake sita ambazo huwa zinafunikwa na boneti (sehemu ambayo huwa na radieta, kwa magari yanayotumia mafuta). Betri hizi zimeunganishwa pamoja na kutengeneza umeme mkubwa. Umeme huu hutumika kuendesha mota ambazo ndio husababisha nishati ya mwendo ili gari hili liweze kwenda. Kwa upande wa nyuma, katika buti pia kuna moduli kadhaa ambazo hufanya kazi kama zile za mbele. Gari hili huweza kuendeshwa muda wa masaa sita bila betri kupungua nguvu, kwa wastani wa mwendo wa kilometa arobaini mpaka sitini kwa saa, kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa makumbusho hayo.


Binafsi nilifurahi sana kuweza kuona gari la ukubwa ule linaloendeshwa kwa kutumia mionzi ya jua, kwa sababu teknolojia hii ya kutumia mionzi ya jua kwa kuendesha mitambo si maarufu sana hapa duniani. Pia kuna magari madogo madogo mengi katika nchi zilizoendelea ambayo huendeshwa kwa kutumia betri za magari na mota, ambapo hayatumii mafuta, mara nyingi magari haya hutumiwa na walemavu wa miguu.



Katika ulimwengu huu kwa sasa ambapo tunajadili ongezeko la joto duniani, ni bora tukafikiri kutumia magari ya namna hii kwa safari ambazo ni fupi fupi, ili kupunguza kiwango cha hewa chafu ambayo husababishwa na uchomaji wa mafuta katika mitambo mbali mbali.
Tufikirie dunia mbadala.


1/26/07

YA KALE NI DHAHABU: MGONGANO WA NADHARIA

UTANGULIZI
Kumekuwa na msemo kuwa 'Ya kale ni dhahabu', kwa maana ya kwamba mambo ya kale yana thamani na si mambo yote yanaweza kupitwa na wakati. Katika karne hii ya sayansi na teknolojia kumekuwa na mabadiliko sana katika maisha ya mwanadamu, kadri miaka inavyosonga. Teknolojia imetawala kila kitu, kiasi kwamba mambo mengi ya kale yanasahaulika. Maendeleo ya tekonojia yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, kwa sababu nyenzo nyingi tunazotumia kuyakabili mazingira yetu si rafiki wa mazingira. Katika tasnia hii ya sayansi ya mazingira kumekuwa na nadharia kadhaa ambazo zimekuwa zikielezea masuala mbali mbali. Katika mada hii, nitachambua mbinu za kienyeji za utunzaji a mazingira dhidi ya zile za kisasa, kwa kuangalia faida na hasara zake pamoja na namna ambavyo zinaweza kuunganishwa na kufanya kazi pamoja. Mbinu hizi zimejadiliwa na wataalamu anuwai, ingawa hakuna muafaka mpaka sasa, kwamba ni mbinu gani itumike.

MJADALA
MBINU ASILI ZA USTAWISHAJI MAZINGIRA
Miaka nenda rudi, watu mbali mbali wamekuwa wakitumia rasilimali katika mazingira yao kwa namna bora ambayo haimalizi rasilimali hizo ndani ya muda mfupi. Walitumia mbinu mbali mbali za asili kuhakikisha kuwa suala hili linafanikiwa, kama nitakavyoeleza hapa chini. Ni muda mchache sana uliopita ndipo wanasayansi wa kimagharibi wamegundua kuwa mbinu za kikale za utunzaji wa rasilimali zilikuwa na zimekuwa ni bora sana, kiasi kwamba kwa sasa wanafanya kila juhudi kuweza kiziweka katika mfumo wa kisayansi zaidi ama kuziunganisha na zile za kisasa. Mbinu hizi za kale ama za asili za utunzaji wa rasilimali hujulikana kwa Kiingereza kama “Traditional Environmental Knowledge Systems” ama TEKS kwa ufupi na zile za kisasa hujulikana kama “Modern Environmental Management Systems” ama kwa ufupi MEMS. Kwa sasa, kumekuwa na wataalamu mbali mbali ambao wanafanya utafiti katika maeneo ya asili kama vile vile barani Afrika, Amerika ya Kusini na Asia, kuona ni kwa namna gani wenyeji wa maeneo hayo wamekuwa wakitumia mbinu za kale katika kutunza rasilimali zao bila uharibifu mkubwa. Mimi binafsi nasema kwamba, watalaam wenzangu hawa wamefanya jambo zuri sana kuzitupia jicho mbinu hizi, ingawa wamechelewa sana. Nasema hivi kwa sababu tangu kuingia kwa ukoloni barani Afrika, Asia na Amerika Kusini karne ya kumi na tisa, mifumo mbali mbali ya jadi ilidharauliwa sana, na badala yake tukapandikiziwa mifumo tata na kandamizi ya kimagharibi ambayo aghalabu wazee wetu walikuwa hawaielewi sawasawa. Wazee wetu hawa ambao waliishi karne tajwa walikuwa na elimu ya mazingira wanayotoka, walijua kwa ukamilifu namna ya kuyakabili ingawa walikuwa na teknolojia duni kwa wakati huo. Kwa kiasi fulani, teknolojia hizi duni ndizo zilizosababisha wao wadumu na rasilimali hizi kwa muda wote huo, kwa sababu walikuwa hawawezi kuzimaliza kwa muda mfupi, kama ilivyo kwa misitu yetu sasa. Walijua aina za wanyama na mimea mbali mbali na uwingi wake, kasi yake ya kuzaliana na namna ya kuvitunza kwa vizazi vinavyofuata. Kwa hiyo basi, utafiti unaofanywa sasa na wataalamu mbali mbali duniani una lengo la kujua kwa undani hasa kwamba ni kwa namna gani hawa wazee wetu walifanikiwa kutunza rasilimali zao kwa wakati huo bila matatizo.
Miongoni mwa watafiti wenyeji wa maeneo asilia ambayo watafiti wanafanya utafiti wao wanataka kushirikishwa kikamilifu kuhusu mijadala mbali mbali, kwa sababu wao ndio wanaoyafahamu sana maeneo yao, hivyo uhusika wao una maana kubwa sana katika utafiti huo. Utafiti shirikishi ndio mbinu ndio suluhisho halisi la mafanikio ya utafiti huu, kwa maana ya kwamba ushirikishwaji wa wenyeji utasaidia sana kupatikana kwa mafanikio katika utafiti huu. Watu wengine nje ya jamii hio pia wanaweza kushiriki katika utafiti, ila msaada wao ni wa kiufundi zaidi kama vile kuchangia ushauri, utawala ama vifaa. Ikumbukwe kuwa lengo la utafiti wa mbinu hizi ni kuunganisha sayansi ya sasa na ile ya asili katika kulinda rasilimali za dunia hii kwa vizazi vijavyo.
Wenyeji asilia wa maeneo mbali mbali wana ujuzi wa jamii mbali mbali za wanyama na mimea katika eneo lao, hivyo wanajua kuwa ni mimea ipi inaliwa ama hailiwi na kwa sababu zipi, mimea ipi inatoa dawa za kumponya mwanadamu, mimea ipi ni sumu na ni sumu kali kiasi gani, mimea ipi inatoa mbao nzuri zaidi na kadhalika na pia kwa upande wa wanyama wanajua kuwa ni wanyama gani wa napaswa kuwindwa na wapi hawapaswi ama ni samaki wa aina ipi wanaliwa na wapi hawaliwi na kwa sababu zipi. Maarifa haya ndio hasa yaliyosababisha jamii hizi za wanyama na mimea vikawepo mpaka sasa, ingawa maendeleo ya sayansi na teknolojia yanasababisha upotevu wa rasilimali hizi.
Msisitizo wa MEMS umekuwa wa kihisabati zaidi katika utafiti huu, wakati ule wa wenyeji umekuwa wa kidhahania. Sasa basi wanasayansi wa kisasa wanatumia mbinu hiyo ili kujenga nadharia mbali mbali kwa ajili ya kuthaminisha rasilimali hizi na mabadiliko yake kadri muda unavyozidi kusonga mbele.

MIGONGANO YA NADHARIA HIZI
Kama nilivyodondoa hapo juu, nadharia za kisayansi zinatilia mkazo sana katika uthaminishaji wa rasilimali hizi ili kujenga nadharia za kisayansi (modelling) kwa ajili ya kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya rasilimali hizo. Kwa upande mfumo wa asili, wao wanatumia zaidi uelewa wao wa rasilimali hizo na si mbinu za kihisabati. Wao hugundua mabadiliko katika mfumo wa rasilimali kwa kulinganisha uwepo wake dhidi ya nyakati, kwa hiyo mbinu hii si ya kisayansi zaidi, ila huangalia uhalisia wa rasilimali husika. Tofauti ya pili ya mbinu hizi ni kwamba, mbinu za kiasili hutumia maadili na ujadi kwa kushirikisha miungu wa jadi katika kulinda rasilimali hizi, kwa maana kwamba miungu ndio huamua matumizi ya rasilimali hizi na ili kuweza kuzivuna basi lazima kuomba ruhusa kwa miungu hao ama kwa wawakilishi wao ambao ni wazee wa jadi. Mfano wa mbinu hii hutumika kutunza eneo la msitu wa Nyumbanitu wilayani Njombe mkoani Iringa na Ziwa Ngozi wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Mbinu hizi ama zinazofanana na hizi zimekuwa zikitumika katika maeneo mbali mbali hasa barani Asia na Afrika kwa karne kadhaa. Waumini wa nadharia hii huamini kuwa dunia ni kitu kinachoishi na viumbe wote wana uhusiano wa ukaribu na miungu wao, sasa basi kufanya uharibifu ama kufuja rasilimali hizo ni kwenda kinyume na maadili. Dhana hii inapingana na nadharia za sayansi ya magharibi katika ufafanuzi wa matumizi ya rasilimali. Waumini wa sayansi ya kimagharibi wao hutumia mfumo wa kihisabati wa uainishaji wa mimea na wanyama katika makundi mbali mbali ili kuweza kupata uelewa kwa undani zaidi na baadaye kutengeneza nadharia mbali mbali ili kuweza kujua maendeleo ya rasilimali hizo dhidi ya nyakati. Mfumo huu wa uainishaji ulianzishwa ulianzishwa na bwana Carl Linnaeus, mwanasayansi wa Sweden aliyeishi kati ya mwaka 1707- 1778. Nitamuongelea mtu huyu katika makala zijazo. Mgongano mwingine unatokana na tafsiri zisizo sahihi za lugha za asili kwenda katika lugha za kigeni, ambazo aghalabu ndio hutumika katika kuandika vitabu na machapisho mengine. Suala hili nalo lina athari sana, kwa kuwa wenyeji mara nyingi hawapati nafasi ya kuhariri kile ambacho kimeandikwa katika machapisho kutoka kwao.

UKALE DHIDI YA USASA
Karne zilizopita, ongezeko la watu halikuwa kubwa sana, hii ilitokana na sababu kadhaa. Kwanza, kulikuwa na magojnwa mengi ambayo yalikuwa yanaua sana watu na dawa zilikuwa haba ama hazikuwepo kabisa. Kwa hiyo basi ushindani katika rasilimali kaukuwa mkubwa kama sasa. Kutokana na kugundulika kwa dawa mbalimbali za kumtibu mwanadamu, ongezeko la watu limekuwa kubwa, hivyo ushindani katika matumizi ra rasilimali umekuwa mkubwa sana, kiasi kwamba mwanadamu amejikuta anavamia hifadhi za asili na maeneo mengine nyeti kwa kujitafutia chakula, dawa na makazi. Kuna mwanasayansi anaitwa Thomas Robert Malthus aliwahi kuiongelea nadharia hii, akihusisha ongezeko kubwa la watu lisiloendana na uzalishaji wa chakula, nitalitafutia suala hili makala ya pekee na kulifafanua. Pili matendo ya mwanadamu yamesababisha uharibifu wa mazingira, hasa ongezeko la joto na kupotea kwa baadhi ya mimea na wanyama. Sababu hizi na nyingine kadhaa ndizo zinawasukuma wanasayansi kwenda katika maeneo ya asili yasiyofikiwa kirahisi na teknolojia katika nchi zinazoendelea na kuongea na wenyeji. Lengo lao ni kujua kuwa, ni kwa namna gani maeneo hayo yamebaki hayajabughudhiwa pamoja na kukua kwa teknolojia? Madaktari hali kadhalika wanakutana na wataalamu wa asili katika kutafuta tiba za magonjwa mbali mbali, kwa kutumia mimea inayopatikana katika maeneo haya ambayo hayajaathirika na kazi za mikono ya wanadamu. Maeneo haya yamepewa uuhimu maalum, na yanalindwa na shirika la Umoja wa mataifa la elimu, utamaduni na sayansi (UNESCO). Kwa hiyo basi, elimu ya kale kuhusu mazingira si ya kudharauliwa hata kidogo, kiasi kwamba saa wataalamu wa utunzaji wa mazingira hawawezi kufanya kazi yao kwa mbinu za kisasa bila kushirikisha wenyeji.

UMUHIMU WA KUUNGANISHA MBINU HIZI
Kinachopiganiwa na wanasayansi wa kisasa ni kuunganisha mbinu za kikala na hizi za kisasa katika kutunza mazingira. Shida moja ni kwamba elimu hii ya asili haijaandikwa sana katika vitabu, inarithishwa tu toka kizazi kimoja hadi kingine na ndio udhaifu huu ambao wanasayansi wa kisasa wanatumia kuikandamiza elimu hii, wakidai kwamba wazee hawa wakifa basi wale wanaosalia wanapindisha ukweli. Pia, elimu ya kikale ya utunzaji wa mazingira haitumii kanuni na nadharia za kihisabati (mathematical proof and modelling) katika kutetea matunzo ya rasilimali hizi, hivyo wanakuwa hawana ushahidi wa kimaandishi kuthibitisha kile ambacho wanakitetea. Udhaifu huu nao pia umechangia sana sayansi hii mpya kudharau mbinu hizi za kale. Pamoja na udhaifu huu wa mbinu za kikale, wanasayansi wa kisasa wamegundua kuwa iwapo mbinu hizi za kikale zitarejewa na kuandikwa, basi kuna uwezekano mkubwa kuwa zikawa na manufaa kutunza rasilimali zetu, hasa ikizingatiwa kuwa maendeleo ya teknolojia ndio yanayosababisha kupotea kwa rasilimali tulizo nazo, pamoja na kubadili mifumo yake, kama vile kubadili mfumo wa kijenetiki wa rasilimali hizi.

UUNGANISHAJI WA MBINU HIZI UKOJE?
Kwanza, katika mfumo wa uainishaji wa rasilimali hizi ambazo kwa kiasi kikubwa ni mimea na wanyama kwa kutumia majina mawili yaani “Genus and species” (nimeshindwa kupata tafsiri ya Kiswahili ya maneno hayo), wanatumia majina ya asili na wakati mwingine majina ya maeneo ambapo rasilimali hizo zinapatikana. Mfano, kuna mimea yenye majina “Uluguruensis, ocotea usambarensis, Phrynobatrachus rungwensis, pterocarpus angolensis, garcinia kingaensis,cisticola njombe na kadhalika, huonyesha maeneo ya asili ambapo rasilimali hizi zinapatikana. Pia ni njia mwafaka ya kuheshimu na kuyathamini maeneo husika na kuyaenzi kwa utunzaji huu. Mbinu ya pili ni kukusanya taarifa nyingi kadri itakavyowezekana na kujaribu kuziunganisha na tafiti za kisayansi na nadharia zake pamoja na kufanya uwiano na ufananisho. Taarifa hizi zinaweza kuwa hadithi, hifadhi za vitu yva kale, masalia ama madhara ya eneo fulani dhidi ya kazi za mwanadamu na kadhalika, huwa zinasaidia sana katika utafiti, hasa kunapokuwa na utata. Tatu, serikali mbali mbali zimetunga sheria ambazo zinaendana na mazingira halisi ya eneo husika, wakifuatisha zile za asili. Hili nalo linasaidia kuunganisha mbinu hizi.

1/5/07

MAISHA MBADALA

UTANGULIZI
U hali gani msomaji wa blogu yangu. Kwa leo nakuletea mambo mawili muhimu, hasa kuhusu suala zima la mazingira. Katika mapumziko ya Krismasi na mwaka mpya, nilifanikiwa kuzulu jiji la Copenhagen wao wanaita Kobenhavn, nchini Denmark, na kwa kweli nilifurahi sana.

MADA
MIFUO YA UMEME WA NGUVU YA UPEPO

Katika ufukwe wa bahari kwanza kabisa nilipokewa na msururu wa mifuo ya umeme inayoendeshwa kwa nguvu ya upepo, kwa kweli inaonyesha ni kwa jinsi gani hawa wenzetu wanajali suala la kupunguza ongezeko la joto duniani. Mifuo hii ni mingi sana nchini humu, na kuna watu wanadai kuwa inawezekana kabisa kuwa nchi hii ndiyo inayoongoza kwa kuwa na mifuo mingi ya umeme huu wa nguvu ya upepo.
Mitambo hii wao wameiweka katika ufukwe kwa sababu maalum, kwamba kandoni mwa bahari kuna upepo wenye nguvu sana kutokana na mawimbi ya bahari, kwa hiyo wakaona ni bora watumie nguvu hiyo katika kuzalisha umeme. Kwa upande wa kwetu sisi, bado tupo nyuma ya wakati kuhusu suala zima la kutumia nguvu ya upepo kuzalisha umeme. Tuna ufukwe mrefu sana katika bahari ya Hindi kuanzia Mtwara hadi Tanga, lakini bado hatujafanya matumizi sahihi ya ufukwe huu. Pia tuna maziwa makubwa matatu, nayo ni Tanganyika, Nyasa na Viktoria, ambapo pia ingewezekana kutumia fukwe zake kuzalisha umeme wa nguvu ya upepo, lakini hali si kama hivyo. Mpaka sasa bado sijajua kwa yakini sababu zinazotufanya tushindwe kutumia nguvu hii ya upepo kuzalisha umeme.

ADHA ZA MIFUO HII
Pamoja na hatua hii nzuri ya kuweka mifuo ya umeme, kumezuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanamazingira. Malalamiko haya yanadai kuwa mifuo hii ya umeme huwa inaharibu mandhari asilia ya eneo husika, kwa maana ya kwamba iwapo mifuo hii itawekwa mahali basi sura ya mahali hapo inabadilika, kwa sababu mifuo hii ni mikubwa sana. Kuna mifuo mingine huwa na kimo cha hadi kufikia meta mia moja kwenda hewani na huchukua eneo kubwa sana, kwa hiyo wanamazingira hawa hawajapendezwa kwa kiasi fulani na suala hili. Sababu ya pili ni kwamba, katika maeneo haya na mengineyo ambayo yana mifuo hii huwa kunakuwa na viumbe hai wengine kama ndege ambao huishi katika maeneao hayo, kwa hiyo basi ndege ambao huruka karibu na maeneo haya hupata ajali kwa kugongana na pangaboi za mifuo hii inapozunguka, hasa kunapokuwa na ukungu ama giza wakati wa mchana. Na kama nilivyodokeza hapo juu, mifuo mingi ipo katika fukwe za bahari na kama tunavyojua kuwa katika bahari na pembezoni mwake kuna ndege wavuvi kama batamaji, heroe, furukombe wavuvi, bundi wavuvi na kadhalika, basi ndege hawa wavuvi ndio ninaoongelea katika makala hii, kuwa wanagongana na pangaboi za mifuo hii.
Kwa hiyo pamoja na kwamba tunapata faida ya umeme kupitia mifuo hii, kuna hiyo tahadhari ambayo huwa tunapaswa kuizingatia, hasa tunapokuwa tunapanga mipango endelevu ya kuweka mifuo ya namna hii.

BAISKELI
Suala lingine ambalo ningependa kuliongelea kwa leo ni uwingi wa baiskeli katika jiji la Copenhagen. Kuna baiskeli nyingi sana hapa mahali hadi zinakuwa kero kwa wakati fulani. Kwa upande mwingine, uwingi huu unamaanisha kuwa kiasi kikubwa cha watu huwa wanatumia baiskeli katika safari fupi fupi za mjini hapa. Niliwahi kuliongelea suala hili katika makala zangu zilizopita, kuwa njia moja wapo ya kupunguza msongamano wa vyombo vya moto katika majiji makubwa kama hili ni kutumia usafiri wa kupunguza baiskeli kwa safari ambazo hazilazimu kutumia gari. Suala hili la kutumia baiskeli pia linasaidia kupunguza hewa zenye sumu kutokana na moshi magari. Inawezekana basi ikawa ni mkakati wa serikali katika kupunguza msongamano wa vyombo vya usafiri, kwamba wakasisitiza kutumia baiskeli kwa kiwango kikubwa kama ilivyo mahali hapa.




TUFANYE NINI?
Kwa kutumia mifano hii miwili inatakiwa tutoke na mtazamo mpya kuhusu suala zima la mazingira, kwa sababu kwa namna moja ama nyingine tusipojitahidi kuzuia ongezeko la joto duniani kuna hatari ya kupoteza asilimia kubwa ya viumbe wetu wa asili. Si suala geni kwa kusikia kwa walio wengi sababu kwa sasa tunasoma katika maandiko mbali mbali ya kumbukumbu za kihistoria kuwa hapo zamani kulikuwa na wanyama wanaitwa Dinosaurs na walitokomea kabisa katika uso wa dunia, kutokana na sababu anuwai, kwa hiyo na sisi kama hatutafanya juhudi za kuzuia hali hii basi kuna hatari kubwa sisi pamoja na viumbe wanaotuzunguka kutokomea kabisa katika uso huu wa dunia. Pamoja na kwamba kuna nguvu za asili kama matetemeko ya ardhi na volkano ambavyo huweza kubadili sura ya nchi na uoto wa asili, si vibaya kama nasi tutachukua hatua katika kudhibiti kile ambacho kipo ndani ya uwezo wetu kwa wakati huu. Mambo haya ni pamoja na kupunguza kiwango cha hewa chafu za viwandani, kupunguza kemikali katika maji ambayo huwa tunayamwaga katika bahari zetu, kupunguza kama si kuzuia kabisa utupaji ovyo wa masalia ya nishati nyuklia na la muhimi zaidi ni kupunguza matumizi ya madawa ya kilimo yenye sumu.
Inawezekana kufanya mabadiliko, tutimize wajibu wetu.