2/3/07

GARI LA MIONZI YA JUA HILI HAPA!


UTANGULIZI

Kumekuwa na usemi kwamba *Tembea uone*. Usemi huu una maana kubwa, kwamba ukiwa mtembezi basi utaona mengi. Pia kuna usemi unaoambatana na huo, kwamba Mtembea bure si mkaa bure, huenda akaokota! Basi katika pita pita yangu hapa na pale, kwa maana ya kwamba nilikutana na habari njema kwa watu wanaojali matumizi endelevu ya nishati na upunguzaji wa hewa chafu duniani. Nilikuta gari moja zuri katika makumbusho, ambalo kwa mujibu wa watu niliowakuta hapo wanasema kuwa lilikuwa linaendeshwa kwa kutumia umeme wa mionzi ya jua. Sababu za kwa nini kwa sasa halitembei ni kwamba hali ya hewa si nzuri sana kuweza kuchaji betri za umeme wa mionzi ya jua kwa mahali hapo, huwa mionzi ya jua si ya kutosha kuchaji betri hadi kuwa na ujazo unaotakiwa.


GARI LENYEWE

Katika boneti la mbele kwa juu kuna moduli kadhaa za kufyonza mionzi ya jua na kuihifadhi katika betri zake sita ambazo huwa zinafunikwa na boneti (sehemu ambayo huwa na radieta, kwa magari yanayotumia mafuta). Betri hizi zimeunganishwa pamoja na kutengeneza umeme mkubwa. Umeme huu hutumika kuendesha mota ambazo ndio husababisha nishati ya mwendo ili gari hili liweze kwenda. Kwa upande wa nyuma, katika buti pia kuna moduli kadhaa ambazo hufanya kazi kama zile za mbele. Gari hili huweza kuendeshwa muda wa masaa sita bila betri kupungua nguvu, kwa wastani wa mwendo wa kilometa arobaini mpaka sitini kwa saa, kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa makumbusho hayo.


Binafsi nilifurahi sana kuweza kuona gari la ukubwa ule linaloendeshwa kwa kutumia mionzi ya jua, kwa sababu teknolojia hii ya kutumia mionzi ya jua kwa kuendesha mitambo si maarufu sana hapa duniani. Pia kuna magari madogo madogo mengi katika nchi zilizoendelea ambayo huendeshwa kwa kutumia betri za magari na mota, ambapo hayatumii mafuta, mara nyingi magari haya hutumiwa na walemavu wa miguu.Katika ulimwengu huu kwa sasa ambapo tunajadili ongezeko la joto duniani, ni bora tukafikiri kutumia magari ya namna hii kwa safari ambazo ni fupi fupi, ili kupunguza kiwango cha hewa chafu ambayo husababishwa na uchomaji wa mafuta katika mitambo mbali mbali.
Tufikirie dunia mbadala.


1 comment:

MTANZANIA. said...

Hongera na karibu sana katika uwanja huu wa kubadilishana mawazo.