3/15/07

UNAIFAHAMU NADHARIA YA r & k?

UTANGULIZI
Dhana hii ya r na k inaelezea mifumo mbali mbali ya maisha ya viumbe hai ambapo mifumo hii hufanya uwepo ama upotevu wa viumbe hivyo. Wataalamu wa mwanzo kuja na nadharia hii katika ikolojia ni mabwana Robert McArthur na Wilson mnamo mwaka 1967. Wao walifanya uchunguzi na kugundua kuwa katika maisha ya viumbe hai (kwa upande wao walifanya utafiti kwa mimea) kuna mfumo fulani wa urithi wa maisha ambao hutofautiana kati ya vinasaba vya mimea fulani na mingine. Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba, mimea kama magugu na miti hutofautiana katika mfumo wa maisha yake. Kwamba, magugu na nyasi hutumia sehemu kubwa ya chakula chao kuzalisha viumbe wengi zaidi wa jamii yao, ambao hata hivyo hawadumu kwa muda mrefu, wakati mimea mikubwa kama miti hutumia sehemu kubwa ya chakula chao katika ulinzi na kuongeza umri wa mimea ya jamii hiyo, hivyo kufanya mimea hii kudumu kwa muda mrefu. Hali kadhalika, kwa jamii za nyasi na magugu, pamoja na mimea mingine ya jamii hizo, huzaliana mara moja tu katika kipindi cha uhai wao, tofauti na mimea jamii ya miti ambayo hutoa mbegu karibu kila mwaka.
Kwa hiyo basi, kwa mujibu wa wasomi hawa, mimea ambayo inazaliana kwa wingi zaidi na haidumu sana inakuwa katika kundi la R, na ile inayozaliana kidogo kidogo na kudumu zaidi huwa katika kundi la K.

SIFA ZA VIUMBEHAI KATIKA KUNDI LA 'R'
Viumbe katika kundi hili huwa katika mazingira ambayo si stahimilivu na uwepo wake na kudumu kwake hutegemea uwingi wake. Nishati (inayotokana na chakula) inayotumika katika maisha ya kila kiumbe ni kidogo sana. Vizalia wengi zaidi huzaliwa katika kundi hili. Hukomaa kwa muda mfupi zaidi na huwa na maisha mafupi kwa ujumla. Jamii za mimea za kundi hili huzalisha viumbe mara moja tu kwa kila kiumbe na baadaya hapo hufa. Viumbe wa kundi hili la 'R' si stahimilivu wa athari za kimazingira kama vile mafuriko, moto, ukame na mashambulio ya wadudu waharibifu kama vile kuvu, nzige na viwavi.

SIFA ZA VIUMBEHAI KATIKA KUNDI NA 'K'
Viumbe katika kundi hili huwa katika mazingira stahimilivu na huweza kuvumilia athari kama vile ukame (kwa kupukutisha majani), huweza kuvuilia moto (kwa kuwa na magamba magumu), huweza kuvumilia mafuriko (kwa mimea kuwa mirefu zaidi), na inaweza kuwa na sumu ili kuzuia kuliwa na wanyama. Jamii za viumbe wa kundi hili wana maumbo makubwa, kama vile miti. Nishati inayotumika katika kuufanya mmea huu uwepo kwa muda mrefu ni kubwa sana na huzalisha viumbe wachache ambao hudumu kwa muda mrefu. Viumbe wa kundi hili pia huchukua kuda mrefu sana kukomaa na kuanza kuzaliana, na huzaa kwa zaidi ya mara moja. Ukichukulia mfano wa miti, huchukua miaka mingi hadi kuanza kuzalisha mbegu, na ikishaanza kuzaa basi huishi muda mrefu, kama haujakutwa na majanga ama kukatwa. Ni mara nyingi viumbe wa kundi hili huishi maisha marefu sana, kwa mfano kuna baadhi ya miti kama mibuyu na mininga ambayo huweza kuishi kwa zaidi ya karne tatu.
Lakini pamoja na kuwa na tabia zisizofanana, kuna wakati sifa za kundi moja huweza kukutwa katika kundi jingine pia. Kwa mfano, mimea jamii ya miti huishi kwa muda mrefu sana ukilinganisha na nyasi, na hivyo kuifanya iwe katika kundi K, lakini ni miti hiyo hiyo ambayo baadhi yake huzalisha mbegu nyingi sana na kuzisambaza mahali mbali mbali kwa ajili ya kuendeleza kizazi. Sifa hii ni ya kundi la R.

ULINGANIFU NA USHIRIKIANO WA KIMAZINGIRA
Pamoja na kuwa mimea tajwa hapo juu ipo katika makundi tofauti, huwa inafanya kazi moja ya kufanya uwepo wa mazingira bora kwa kila kundi. Kwa mfano, inapotokea janga kama volkano, huwa mimea na wanyama huathirika sana, kutegemeana na ukubwa wa tukio. Mara nyingi inapotokea maisha kuanza tena baada ya janga, mimea ya kundi R ndio huwa ya kwanza kuanza maisha, kwa kuzaliana upesi na kusambaa kwa haraka, na hivyo kutengeneza nafasi kwa ajili ya jamii nyingine za mimea katika kundi la K. Mfumo huu kwa kiingereza huitwa 'Ecological Succession' na ni mfumo unaopatikana mahali pengi sana duniani, kutokana na uharibifu ambao umetokea katika maeneo mbali mbali. Mimea inayozaliwa baada ya ile ya kwanza kuondolewa huitwa uzao wa pili, ama kwa kiingereza 'Secondary regrowth'.
Kwa hiyo basi, tunapoongelea suala zima la mazingira, ni lazima tuwe tunaangalia muingiliano kati ya kiumbe na kiumbe, kwa sababu mara nyingi huwa na uhusiano wa karibu. Kwa maana hiyo unapokata mti ambao kukua kwake hadi kukomaa huchukua si chini ya miaka 30, kama ilivyo kwa miti ya asili, ujue pia kuwa unaathiri na uwepo wa viumbe wengine ambao kwa namna moja hutegemea mti huo ama kwa kivuli, ama kwa kutunza maji au kwa namna nyingine yoyote ile. Fikiri kabla hujatenda!

1 comment:

Anonymous said...

Naona umetumia neno - ustaarabu hapo juu.Maoni yangu ni kwamba neno hili halifai linaonyesho kwamba sisi wa afrika ni watu wanaompa muarabu sifa nzuri licha ya kwamba yeye kama mchinchaji, aliwauwa mamilioni ya wa Afrika kwa dharau na bila majuto yeyote mpka waleo.Tovuti lako ni safi na inaelimisha vizuri kuhusu mambo magumu ya ikologia.Dosari niliyo ona ni utumiaji wa neno hilo pekeyake.Muarabu akiona kwamba unamtaja yeye na mila yake kuwa bora kuliko yale yako atazidi kututharao na kuto heshimu tamaduni asili yetu.Kama wa Afrika lazima tujipende, na tuonyeshe wageni wetu sifa zetu bora tunayojivunia. Naomba uliondoe neno hilo linalotokeza ujinga wetu wa kimapokeo ya ukoloni na uingize badala yake neno lingine linalo imarisha fahari yetu ya utamaduni.