7/31/07

SAFU ZA MILIMA YA USAMBARA

UTANGULIZI

Safu za milima ya Usambara ni sehemu tu ya safu za milima ya tao ya mashariki "eastern arc Mountains". Milima hii inaunganishwa na safu ya milima ya Udzungwa na Uluguru katika uhifadhi. Inasifika kwa kuwa na viumbe wengi wa namna ya pekee (endemic), kwa hiyo inapewa umuhimu mkubwa sana katika utunzaji wake na taasisi za kimataifa kama vile 'Critical Ecosystem Partneship Fund (CEPF), International Centre for Insect Physiology and Ecology (ICIPE) pamoja na 'Birdlife International'. Safu za milima hii zinaambaa ambaa toka Muheza, Korogwe hadi Lushoto katika mkoa wa Tanga.Picha: Sehemu ya Msitu wa Kandelekampaa katika milima ya Usambara iliyoathiriwa kwa moto na kilimo, katika Kijiji cha Ndabwaa kata ya Malindi wilaya ya Lushoto


UMUHIMU WAKE
Safu za milima hii ni chanzo cha mito mingi sana, kama vile mto Zigi, mto Pangani na mto Umba, lakini sehemu kubwa ya misitu ya safu hizi imeharibiwa sana, hasa maeneo ya Lushoto na Korogwe, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu ambao kwa kiasi kikubwa hutegemea shughuli za kilimo na upasuaji wa mbao. Maeneo yaliyoathiriwa sana na shughuli hizi ni yale ya Usambara Magharibi, hasa wilayani Lushoto. Huku ndio sehemu kubwa sana ya misitu hii imefyekwa ama kuchomwa moto kabisa, hasa katika vijiji vya Ndabwa, Magamba na Lukozi. Kwa upande wa wilaya ya Muheza, angalau kuna matumaini, kwani misitu ya upande huu imetunzwa kwa kiasi cha kuridhisha. Ikumbukwe kuwa matunda na mboga mboga kutoka wilaya hizi hutoka katika mashamba ambayo ama yapo pembezoni mwa misitu hii ama yanapata maji yake toka katika misitu hii.Picha Juu: Mto mkuzu, ambao hutoka katika milima ya Usambara. Mto huu ni tegemeo sana kwa wakazi wa vijiji vingi vya Lushoto kwa umwagiliaji na matumizi ya nyumbani.

Pichani: Kabichi ambazo hulimwa katika mashamba yaliyo katika safu za Milima ya Usambara

ELIMU YA MAZINGIRA
Kuna taasisi kadhaa ambazo zinajihusisha na kuelimisha jamii zilizo katika maeneo haya juu ya kutunza safu za milima hii, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha utalii rafiki wa mazingira (eco-tourism). Taasisi hizi ni kama vile Friends of Usambara Society (FOU), West Usambara Women Education (WUWE), Lushoto Youth Development Network na kadhalika. Hata hivyo bado juhudi zaidi zinahitajika katika kupunguza athari hizi.

1 comment:

mwandani said...

makala ya kuelemisha tena kwa picha. Ahsante.

mzee, kama unaweza kufika kwenye blogu ya Mjengwa kuna mjadala moto kabisa kuhusu mazingira - hasa kupotea kwa misitu sehemu za Iringa, kuna wanablogu wanajadili vikali sana huko. tafadhali pitia utupe ushauri.