1/26/07

YA KALE NI DHAHABU: MGONGANO WA NADHARIA

UTANGULIZI
Kumekuwa na msemo kuwa 'Ya kale ni dhahabu', kwa maana ya kwamba mambo ya kale yana thamani na si mambo yote yanaweza kupitwa na wakati. Katika karne hii ya sayansi na teknolojia kumekuwa na mabadiliko sana katika maisha ya mwanadamu, kadri miaka inavyosonga. Teknolojia imetawala kila kitu, kiasi kwamba mambo mengi ya kale yanasahaulika. Maendeleo ya tekonojia yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, kwa sababu nyenzo nyingi tunazotumia kuyakabili mazingira yetu si rafiki wa mazingira. Katika tasnia hii ya sayansi ya mazingira kumekuwa na nadharia kadhaa ambazo zimekuwa zikielezea masuala mbali mbali. Katika mada hii, nitachambua mbinu za kienyeji za utunzaji a mazingira dhidi ya zile za kisasa, kwa kuangalia faida na hasara zake pamoja na namna ambavyo zinaweza kuunganishwa na kufanya kazi pamoja. Mbinu hizi zimejadiliwa na wataalamu anuwai, ingawa hakuna muafaka mpaka sasa, kwamba ni mbinu gani itumike.

MJADALA
MBINU ASILI ZA USTAWISHAJI MAZINGIRA
Miaka nenda rudi, watu mbali mbali wamekuwa wakitumia rasilimali katika mazingira yao kwa namna bora ambayo haimalizi rasilimali hizo ndani ya muda mfupi. Walitumia mbinu mbali mbali za asili kuhakikisha kuwa suala hili linafanikiwa, kama nitakavyoeleza hapa chini. Ni muda mchache sana uliopita ndipo wanasayansi wa kimagharibi wamegundua kuwa mbinu za kikale za utunzaji wa rasilimali zilikuwa na zimekuwa ni bora sana, kiasi kwamba kwa sasa wanafanya kila juhudi kuweza kiziweka katika mfumo wa kisayansi zaidi ama kuziunganisha na zile za kisasa. Mbinu hizi za kale ama za asili za utunzaji wa rasilimali hujulikana kwa Kiingereza kama “Traditional Environmental Knowledge Systems” ama TEKS kwa ufupi na zile za kisasa hujulikana kama “Modern Environmental Management Systems” ama kwa ufupi MEMS. Kwa sasa, kumekuwa na wataalamu mbali mbali ambao wanafanya utafiti katika maeneo ya asili kama vile vile barani Afrika, Amerika ya Kusini na Asia, kuona ni kwa namna gani wenyeji wa maeneo hayo wamekuwa wakitumia mbinu za kale katika kutunza rasilimali zao bila uharibifu mkubwa. Mimi binafsi nasema kwamba, watalaam wenzangu hawa wamefanya jambo zuri sana kuzitupia jicho mbinu hizi, ingawa wamechelewa sana. Nasema hivi kwa sababu tangu kuingia kwa ukoloni barani Afrika, Asia na Amerika Kusini karne ya kumi na tisa, mifumo mbali mbali ya jadi ilidharauliwa sana, na badala yake tukapandikiziwa mifumo tata na kandamizi ya kimagharibi ambayo aghalabu wazee wetu walikuwa hawaielewi sawasawa. Wazee wetu hawa ambao waliishi karne tajwa walikuwa na elimu ya mazingira wanayotoka, walijua kwa ukamilifu namna ya kuyakabili ingawa walikuwa na teknolojia duni kwa wakati huo. Kwa kiasi fulani, teknolojia hizi duni ndizo zilizosababisha wao wadumu na rasilimali hizi kwa muda wote huo, kwa sababu walikuwa hawawezi kuzimaliza kwa muda mfupi, kama ilivyo kwa misitu yetu sasa. Walijua aina za wanyama na mimea mbali mbali na uwingi wake, kasi yake ya kuzaliana na namna ya kuvitunza kwa vizazi vinavyofuata. Kwa hiyo basi, utafiti unaofanywa sasa na wataalamu mbali mbali duniani una lengo la kujua kwa undani hasa kwamba ni kwa namna gani hawa wazee wetu walifanikiwa kutunza rasilimali zao kwa wakati huo bila matatizo.
Miongoni mwa watafiti wenyeji wa maeneo asilia ambayo watafiti wanafanya utafiti wao wanataka kushirikishwa kikamilifu kuhusu mijadala mbali mbali, kwa sababu wao ndio wanaoyafahamu sana maeneo yao, hivyo uhusika wao una maana kubwa sana katika utafiti huo. Utafiti shirikishi ndio mbinu ndio suluhisho halisi la mafanikio ya utafiti huu, kwa maana ya kwamba ushirikishwaji wa wenyeji utasaidia sana kupatikana kwa mafanikio katika utafiti huu. Watu wengine nje ya jamii hio pia wanaweza kushiriki katika utafiti, ila msaada wao ni wa kiufundi zaidi kama vile kuchangia ushauri, utawala ama vifaa. Ikumbukwe kuwa lengo la utafiti wa mbinu hizi ni kuunganisha sayansi ya sasa na ile ya asili katika kulinda rasilimali za dunia hii kwa vizazi vijavyo.
Wenyeji asilia wa maeneo mbali mbali wana ujuzi wa jamii mbali mbali za wanyama na mimea katika eneo lao, hivyo wanajua kuwa ni mimea ipi inaliwa ama hailiwi na kwa sababu zipi, mimea ipi inatoa dawa za kumponya mwanadamu, mimea ipi ni sumu na ni sumu kali kiasi gani, mimea ipi inatoa mbao nzuri zaidi na kadhalika na pia kwa upande wa wanyama wanajua kuwa ni wanyama gani wa napaswa kuwindwa na wapi hawapaswi ama ni samaki wa aina ipi wanaliwa na wapi hawaliwi na kwa sababu zipi. Maarifa haya ndio hasa yaliyosababisha jamii hizi za wanyama na mimea vikawepo mpaka sasa, ingawa maendeleo ya sayansi na teknolojia yanasababisha upotevu wa rasilimali hizi.
Msisitizo wa MEMS umekuwa wa kihisabati zaidi katika utafiti huu, wakati ule wa wenyeji umekuwa wa kidhahania. Sasa basi wanasayansi wa kisasa wanatumia mbinu hiyo ili kujenga nadharia mbali mbali kwa ajili ya kuthaminisha rasilimali hizi na mabadiliko yake kadri muda unavyozidi kusonga mbele.

MIGONGANO YA NADHARIA HIZI
Kama nilivyodondoa hapo juu, nadharia za kisayansi zinatilia mkazo sana katika uthaminishaji wa rasilimali hizi ili kujenga nadharia za kisayansi (modelling) kwa ajili ya kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya rasilimali hizo. Kwa upande mfumo wa asili, wao wanatumia zaidi uelewa wao wa rasilimali hizo na si mbinu za kihisabati. Wao hugundua mabadiliko katika mfumo wa rasilimali kwa kulinganisha uwepo wake dhidi ya nyakati, kwa hiyo mbinu hii si ya kisayansi zaidi, ila huangalia uhalisia wa rasilimali husika. Tofauti ya pili ya mbinu hizi ni kwamba, mbinu za kiasili hutumia maadili na ujadi kwa kushirikisha miungu wa jadi katika kulinda rasilimali hizi, kwa maana kwamba miungu ndio huamua matumizi ya rasilimali hizi na ili kuweza kuzivuna basi lazima kuomba ruhusa kwa miungu hao ama kwa wawakilishi wao ambao ni wazee wa jadi. Mfano wa mbinu hii hutumika kutunza eneo la msitu wa Nyumbanitu wilayani Njombe mkoani Iringa na Ziwa Ngozi wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Mbinu hizi ama zinazofanana na hizi zimekuwa zikitumika katika maeneo mbali mbali hasa barani Asia na Afrika kwa karne kadhaa. Waumini wa nadharia hii huamini kuwa dunia ni kitu kinachoishi na viumbe wote wana uhusiano wa ukaribu na miungu wao, sasa basi kufanya uharibifu ama kufuja rasilimali hizo ni kwenda kinyume na maadili. Dhana hii inapingana na nadharia za sayansi ya magharibi katika ufafanuzi wa matumizi ya rasilimali. Waumini wa sayansi ya kimagharibi wao hutumia mfumo wa kihisabati wa uainishaji wa mimea na wanyama katika makundi mbali mbali ili kuweza kupata uelewa kwa undani zaidi na baadaye kutengeneza nadharia mbali mbali ili kuweza kujua maendeleo ya rasilimali hizo dhidi ya nyakati. Mfumo huu wa uainishaji ulianzishwa ulianzishwa na bwana Carl Linnaeus, mwanasayansi wa Sweden aliyeishi kati ya mwaka 1707- 1778. Nitamuongelea mtu huyu katika makala zijazo. Mgongano mwingine unatokana na tafsiri zisizo sahihi za lugha za asili kwenda katika lugha za kigeni, ambazo aghalabu ndio hutumika katika kuandika vitabu na machapisho mengine. Suala hili nalo lina athari sana, kwa kuwa wenyeji mara nyingi hawapati nafasi ya kuhariri kile ambacho kimeandikwa katika machapisho kutoka kwao.

UKALE DHIDI YA USASA
Karne zilizopita, ongezeko la watu halikuwa kubwa sana, hii ilitokana na sababu kadhaa. Kwanza, kulikuwa na magojnwa mengi ambayo yalikuwa yanaua sana watu na dawa zilikuwa haba ama hazikuwepo kabisa. Kwa hiyo basi ushindani katika rasilimali kaukuwa mkubwa kama sasa. Kutokana na kugundulika kwa dawa mbalimbali za kumtibu mwanadamu, ongezeko la watu limekuwa kubwa, hivyo ushindani katika matumizi ra rasilimali umekuwa mkubwa sana, kiasi kwamba mwanadamu amejikuta anavamia hifadhi za asili na maeneo mengine nyeti kwa kujitafutia chakula, dawa na makazi. Kuna mwanasayansi anaitwa Thomas Robert Malthus aliwahi kuiongelea nadharia hii, akihusisha ongezeko kubwa la watu lisiloendana na uzalishaji wa chakula, nitalitafutia suala hili makala ya pekee na kulifafanua. Pili matendo ya mwanadamu yamesababisha uharibifu wa mazingira, hasa ongezeko la joto na kupotea kwa baadhi ya mimea na wanyama. Sababu hizi na nyingine kadhaa ndizo zinawasukuma wanasayansi kwenda katika maeneo ya asili yasiyofikiwa kirahisi na teknolojia katika nchi zinazoendelea na kuongea na wenyeji. Lengo lao ni kujua kuwa, ni kwa namna gani maeneo hayo yamebaki hayajabughudhiwa pamoja na kukua kwa teknolojia? Madaktari hali kadhalika wanakutana na wataalamu wa asili katika kutafuta tiba za magonjwa mbali mbali, kwa kutumia mimea inayopatikana katika maeneo haya ambayo hayajaathirika na kazi za mikono ya wanadamu. Maeneo haya yamepewa uuhimu maalum, na yanalindwa na shirika la Umoja wa mataifa la elimu, utamaduni na sayansi (UNESCO). Kwa hiyo basi, elimu ya kale kuhusu mazingira si ya kudharauliwa hata kidogo, kiasi kwamba saa wataalamu wa utunzaji wa mazingira hawawezi kufanya kazi yao kwa mbinu za kisasa bila kushirikisha wenyeji.

UMUHIMU WA KUUNGANISHA MBINU HIZI
Kinachopiganiwa na wanasayansi wa kisasa ni kuunganisha mbinu za kikala na hizi za kisasa katika kutunza mazingira. Shida moja ni kwamba elimu hii ya asili haijaandikwa sana katika vitabu, inarithishwa tu toka kizazi kimoja hadi kingine na ndio udhaifu huu ambao wanasayansi wa kisasa wanatumia kuikandamiza elimu hii, wakidai kwamba wazee hawa wakifa basi wale wanaosalia wanapindisha ukweli. Pia, elimu ya kikale ya utunzaji wa mazingira haitumii kanuni na nadharia za kihisabati (mathematical proof and modelling) katika kutetea matunzo ya rasilimali hizi, hivyo wanakuwa hawana ushahidi wa kimaandishi kuthibitisha kile ambacho wanakitetea. Udhaifu huu nao pia umechangia sana sayansi hii mpya kudharau mbinu hizi za kale. Pamoja na udhaifu huu wa mbinu za kikale, wanasayansi wa kisasa wamegundua kuwa iwapo mbinu hizi za kikale zitarejewa na kuandikwa, basi kuna uwezekano mkubwa kuwa zikawa na manufaa kutunza rasilimali zetu, hasa ikizingatiwa kuwa maendeleo ya teknolojia ndio yanayosababisha kupotea kwa rasilimali tulizo nazo, pamoja na kubadili mifumo yake, kama vile kubadili mfumo wa kijenetiki wa rasilimali hizi.

UUNGANISHAJI WA MBINU HIZI UKOJE?
Kwanza, katika mfumo wa uainishaji wa rasilimali hizi ambazo kwa kiasi kikubwa ni mimea na wanyama kwa kutumia majina mawili yaani “Genus and species” (nimeshindwa kupata tafsiri ya Kiswahili ya maneno hayo), wanatumia majina ya asili na wakati mwingine majina ya maeneo ambapo rasilimali hizo zinapatikana. Mfano, kuna mimea yenye majina “Uluguruensis, ocotea usambarensis, Phrynobatrachus rungwensis, pterocarpus angolensis, garcinia kingaensis,cisticola njombe na kadhalika, huonyesha maeneo ya asili ambapo rasilimali hizi zinapatikana. Pia ni njia mwafaka ya kuheshimu na kuyathamini maeneo husika na kuyaenzi kwa utunzaji huu. Mbinu ya pili ni kukusanya taarifa nyingi kadri itakavyowezekana na kujaribu kuziunganisha na tafiti za kisayansi na nadharia zake pamoja na kufanya uwiano na ufananisho. Taarifa hizi zinaweza kuwa hadithi, hifadhi za vitu yva kale, masalia ama madhara ya eneo fulani dhidi ya kazi za mwanadamu na kadhalika, huwa zinasaidia sana katika utafiti, hasa kunapokuwa na utata. Tatu, serikali mbali mbali zimetunga sheria ambazo zinaendana na mazingira halisi ya eneo husika, wakifuatisha zile za asili. Hili nalo linasaidia kuunganisha mbinu hizi.

No comments: