6/28/06

UNAFAHAMU WALINZI HAI WA MAZINGIRA?

U hali gani msomaji wa blogu hii.
Katika mada ya leo, nataka kukufahamisha kitu muhimu sana katika suala zima la athari za uharibifu wa mazingira, na mustakabali wake katika viumbe hai. Nataka kuongelea kitu kinachitwa bioindicators. Mimi naita viashiria, (nitashukuru kama nitapata tafsiri ya kiswahili sanifu ya jina hilo)

UTANGULIZI
Hiki ni Kitu gani?
Hizi ni jamii za mimea au wanyama (wanyama ni pamoja na wadudu) ambazo huashiria uharibifu mazingira ya sehemu fulani, katika uso wa dunia. Viumbe hawa, huwa katika mfumo-ikolojia wa eneo fulani. Iwapo kunakuwa na mabadiliko katika hali ya mazingira ya mahali walipo, ambayo si ya kawaida, basi viumbe hawa huonyesha mabadiliko fulani, aidha katika mfumo wao wa lishe, maumbo, kibiolojia au wa kitabia. Kila kiumbe kina aina yake ya tahadhari ya uharibifu huu wa mazingira, iwe ni mimea au wanyama.

KAZI ZA VIUMBE HAO (BIOINDICATORS)
Viumbe hai hao wana kazi kubwa kadhaa katika suala zima la ulinzi wa mazingira. Kwanza, hutoa utambuzi wa uharibifu wa mazingira katika eneo fulani walipo. Pili, hutoa taarifa za uvamizi wa kitu ambacho si cha kawaida katika eneo husika kutokana na uharibifu ambao unatokea. Tatu, hutoa taarifa juu ya hali ya usafi wa mazingira wa eneo husika na nne, hutumika kufanya majaribio ya hali ya usafi wa maji, kama yamechafuliwa au la.

VIASHIRIA-MIMEA (PLANT INDICATORS)
Katika utafiti makini wa kisayansi, kuwepo au kutokuwepo kwa jamii fulani ya mimea katika maeneo fulani, huweza kutoa taarifa muhimu sana juu ya athari za kimazingira zinazotokea katika eneo hilo. Tuchukulie mfano wa mimea fulani midogo sana ya kijani "lichens", inayoota kama utando katika miamba na miti yenye unyevu nyevu . Hii mara nyingi hupatikana katika misitu. Mimea hii huweza kubadilika haraka sana iwapo kuna mabadiliko yasiyo ya kawaida katika msitu, kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, ukame na mfumo wa hali ya hewa ya msitu husika. Kutokomea kwa mimea hii katika eneo husika inaweza kuwa ni kiashiria cha hali tete ya uharibifu wa kimazingira kama vile uwingi wa hewa ya naitrojeni, madini ya oksaidi ya salfa au vichafuzi vingine vya jamii ya salfa.

VIASHIRIA-WANYAMA (ANIMAL INDICATORS)
Viumbe hai wadogo wadogo, wasioonekana kwa macho, huweza kuwa viashiria vya athari za mazingira, iwe ni katika maji au nchi kavu. Viumbe hawa wana uwezo wa kuzalisha protini mpya katika miili yao, ili kujikinga na athari mbaya za uharibifu wa mazingira, iwapo kunakuwa na vitu visivyo vya kawaida vinavyochafua mazingira yao. Protini hizi, huweza kuwa ni dalili za tahadhari, kuwa kuna uharibifu fulani katika mazingira walipo viumbe hao. Wanyama wengine hubadili matabaka ya miili yao, ili kujilinda na athari hizi. Hivyo basi, wataalamu wanapoona mabadiliko yasiyo ya kawaida katika maisha ya wanyama hawa, huweza kutambua uharibifu uliopo katika mazingira ya eneo husika na kuchukua hatua.

MATUMIZI YA VIASHIRIA HIVI
Kama tulivyoona hapo juu, viumbe hai viashiria hubadilika hali zao kunapokuwepo na mabadiliko katika mazingira walipo. Hata hivyo mabadiliko haya hutofautiana kati ya viumbe hawa. Mifumo hii ya kijenetiki, hutumika sana katika kutunza maliasili, kwa kujua mabadiliko katika hali za viumbe hai katika misitu. Ni rahisi kwa kiasi fulani kujua mabadiliko katika mifumo-ikolojia ya maeneo fulani kwa kutumia viumbe hawa. Uchafuzi wa maji pia huweza kugundulika kwa kutumia viumbe hai hawa, hasa kunapokuwa na madini kama 'cadmium au benzene' katika maji. Iwapo kunakuwa na madini haya katika maji, miili ya viumbe hai viashiria huwa na mabadiliko yasiyo ya kawaida. Madini haya si salama kwa matumizi ya binadamu.

Vyura, pia ni kati ya viumbe hai ambao hutumika mara kwa mara na wanasayansi katika kugundua athari za uharibifu wa mazingira. (kama una kumbukumbu nzuri, utakumbuka suala la vyura wa Kihansi Morogoro, walipoathirika kwa kukosa kiasi fulani cha maji ambacho ni muhimu kwa maisha yao, baada ya mradi wa umeme kutumia maji mengi kuliko kawaida). Kuna sababu kadhaa za mabadiliko ya maisha ya vyura, hasa kunapokuwa na uharibifu wa mazingira yao kwa namna fulani. Vyura hutaga mayai katika maji, hivyo muda wao mwingi huutumia katika maji. Hutaga mayai yaliyo wazi (nje) hivyo hutegemea maji kuyaangua. Wana ngozi ambayo kwa kiasi fulani hupitisha maji, hivyo huweza kuhisi mabadiliko mara moja. Ilishatokea pia katika Ziwa Manyara mkoani Manyara, kuwa kulikuwa na mabadiliko katika mtiririko wa maji. Mimea jamii ya mwani (algae) iliathirika, na ndege jamii ya korongo na heroe ambao hutegemea mimea hiyo kwa lishe yao pia waliathirika. Hii ni mifano michache tu, lakini kuna viumbe wa namna nyingi ambao hutumika kugundua athari za mazingira kwa maeneo mbali mbali hapa duniani.

TUFANYE NINI?
Hatuna budi kuangalia kwa makini shughuli zetu, ambazo nyingi ya hizo si rafiki wa mazingira, kama vile uchomaji wa misitu, uchimbaji na usafishaji wa madini kwa kutumia kemikali zenye athari kwa mazingira. Ni vizuri tukazalisha, lakini pia ni vema kuangalia mustakabali wetu na viumbe wengine ili tusiwaathiri na tusijiathiri sisi wenyewe. Viumbe hai viashiria, ni watoa taarifa wazuri wa athari tunazofanya, hivyo tuangalaie upya namna nzuri ya kutumia rasilimali zetu.

No comments: