7/12/06

MFUMO IKOLOJIA NI NINI?

Utangulizi
Kwa maelezo rahisi, mfumo ikolojia ni namna ya maisha katika eneo fulani ambapo viumbe wa aina mbali mbali ikiwa ni pamoja na wanyama na mimea hutegemeana, aidha kwa chakula ama hifadhi au vyote kwa pamoja. Mfumo huu wa maisha hushirikisha viumbe wote waliopo katika eneo husika, kuanzia wale wakubwa wanaoonekana kwa macho hadi wale tusioweza kuwaona kwa macho. Mmoja wa wanasayansi wanzilishi wa nadharia hii ni mwanasayansi wa Uingereza Bwana Arthur Tansley (1871- 1955). Yeye ni kati ya watu ambao walifanya kazi kubwa sana ya utaifi katika kuweka utambuzi wa mifumo ikolojia. Tuchukue mfano wa kitu kama dimbwi la maji. Katika dimbwi, kunaweza kuwa na viumbe hai wa namna mbali mbali waliopo pale kama vile vyura, viluwiluwi, mbu, utando wa mwani, bakteria na viumbe wanaofanana na hao. Katika mfumo kama huu, unaweza kukuta kuwa viluwiluwi hula mwani, na vyura hula mbu wanaotafuta maeneo ya kutagia mayai katika dimbwi husika. Mbu nao huhitaji hifadhi katika dimbwi kwa mazalio yao. Ni kwa namna hii basi tunaona kuwa kunakuwa na kutegemeana kwa viumbe hai hawa, ikiwa wote hutaji dimbwi hili kwa namna mbali mbali. Jitihada zozote za mwanadamu katika kuliharibu dimbwi hili, ni kuharibu mfumo mzina na mustakabali wa viumbe hai waliopo pale.
Tupate mfano mwingine wa mfumo ikolojia. Tuchukue mfano wa msitu mdogo au kichaka. Katika kichaka kunaweza kuwa na viumbe kama panya, nyoka, bakteria, mimea mikubwa na midogo, mashimo, wadudu wa namna mbali mbali pamoja na minyoo. Katika mazingira kama haya, kwa namna moja au nyingine viumbe hai hawa watategemeana, aidha kwa hifadhi au chakula, au vyote. Kuondolewa kwa kiumbe kimoja katika mfumo huo no kuhatarisha mustakabali wa viumbe wengine ambao hutegemea kuendesha maisha yao kutokana na kiumbe huyo. Mfano, katika kichaka, kuondolewa kwa panya kunaweza kuwa na athari kwa nyoka ambao hutegemea panya kama chakula chao, Koundolewa kwa mimea kunaweza kuathiri wadudu ambao hutegemea mimea hio kwa hifadhi na lishe.

FAIDA ZA MFUMO IKOLOJIA
Kama tulivyoona katika mifano hiyo hapo juu, kuna uhusiano mkubwa sana kati ya kiumbe na kiumbe. Kutoweka kwa kiumbe mmoja kunaweza kuwa na athari kwa viumbe waliosalia katika mfumo huo. Katika mfumo huu mwanadamu hajasahaulika, na ndio chanzo kikuu cha athari zilizo nyingi katika mifumo ikolojia.

Faida
Husaidia uwepo wa viumbe mahali mbali mbali. Mfano nyuki huchavusha maua katika kujitafutia chakula chake (chavua) na hivyo hufanya maua yasitawi vizuri. Maua haya huzaa matunda ambayo ni chakula cha viumbe wengine ambao ni pamoja na wanadamu. Kwa hivyo basi, bila nyuki na jamii nyingine za wadudu kama vipepeo,hatuwezi kuwa na uchavushaji. Mfano mwingine, mimea hupumua hewa ya oksijeni ambayo ni muhimu sana kwa maisha ya wanyama, na hali kadhalika wanyama hupumua hewa ya kaboni dayoksaidi ambayo husaidia uhai wa mimea. Kwa hivyo basi, bila mimea wanyama hawana maisha, na bila wanyama mimea haiwezi kuishi. Ni katika mazingira haya basi kuna utegemeano wa viumbe hai, kwa hiyo kutoweka kwa kiumbe hai kimoja kunaweza kuwa na athari kwa viumbe hai wengine ambao kwa namna moja au nyingine hutegemea uwepo wa kiumbe hicho. Kuna mifano mingi sana ya kutegemeana kwa viumbe hai, ambapo nafasi hii haitoshi kuelezea kila kitu, isipokuwa tu tuelewe kuwa viumbe hai wanategemeana sana kwa kila hali.

WAJIBU WETU
Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunalinda viumbe hai kwa kila hali, ili tusiweze nasi kuathirika, kwani wao wakiathirika nasi twaathirika pia.

Je unachukua hatua gani kuhakikisha viumbe hai wanaokutegemea wanaishi salama?
Jadili...

No comments: