UTANGULIZI
Magugumaji ni kati ya mimea inayosifika sana kwa kuzaliana hapa duniani, inayopatikana katika mazingira yenye maji kwa msimu wote, kama vile kwenye mito, ziwani,kwenye madimbwi, kwenye mitaro na miferejini.Unaweza kuvuna tani mia mbili za magugumaji kwa ekari moja tu! Ni mmea wa kijani ambao humea kwa kutambaa, hutoa maua ya rangi ya zambarau au hudhurungi na huweza kurefuka hadi kimo cha futi tatu. Mmea huu ni moja ya mimea ya jamii ya "Pickerelweed" au "pontederiaceae" (jamii ya magugu yanayostawi katika maji). Kwa jina la kitaalamu, mmea huu hufahamika kama 'eichhornia crassipes' na kwa Kiingereza hujulikana kama 'Water Hyacinth'.
ASILI YA MAGUGUMAJI
Takwimu za wataalamu wa elimu-mimea, zinaonyesha kuwa asili ya mmea huu ni katika nchi za kitropiki za Amerika ya Kusini, lakini kwa sasa mmea huu umesambaa katika mabara yote. Kwa nchi kama Marekani mmea huu ulisambaa kati ya mwaka 1884 na 1885 mjini Louisiana. Kuna mtu ambaye alikuwa katika mnada wa pamba katika nchi za Amerika ya kusini, akachukua mmea huu kama pambo la nyumba yake. Kwa kutojua, alitupa masalia ya mmea huo katika mto wa Mtakatifu Jones,baada ya kuzaliana sana kuliko alivyotarajia, na hatimaye mmea huo ukasambaa katika majimbo mengine ya Marekani. Kwa Afrika Mashariki, inasadikika kuwa mmea huu uliletwa enzi za ukoloni wa Waingereza, yaani kuanzia mwaka 1920, na hupatikana sana katika Ziwa Viktoria katika Mikoa ya Mara na Mwanza kwa upande wa Tanzania, na maeneo mengine yanayozunguka ziwa hili katika nchi za Kenya na Uganda.
MAZINGIRA YAKE
Magugumaji hustawi sana katika maji yaliyotuama, au yale yenye mwendo mdogo sana. Kama nilivyotaja hapo mwanzo, mmea huu hupatikana ziwani, mitoni, madimbwini, mitaroni na maeneo mengine oevu yanayofanana na hayo. Huweza kuota kwa kutawanya mbegu zake au kwa vikonyo vyake, na hutengeneza chakula chake moja kwa moja toka katika maji.
FAIDA NA MATUMIZI YA MAGUGUMAJI
Mmea huu una faida kadhaa, na huweza kutumika kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi. Mmea huu, kama nilivyotaja hapo juu, hupata chakula chake kutokana katika maji, hivyo basi, hutumika kuchuja maji taka na kuwa maji masafi kwa matumizi ya kubinadamu yasiyo ya moja kwa moja, kama vile kilimo cha umwagiliaji na ujenzi. Mfano mzuri unapatikana katika madimbwi ya maji taka ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo maji taka hukusanywa katika eneo moja na kuchujwa katika hatua mbali mbali kabla ya kusafishwa kwa matete na magugumaji, katika hatua za mwisho. Maji haya hutumika kumwagilia mpunga na mboga mboga, na pia hutumiwa na wanyama pori walio katika eneo hilo. Faida nyingine ya magugumaji ni katika kazi za sanaa za mikono. Nchini Kenya kwa mfano, kuna mradi ujulikanao kama 'Water Hyacinth Utilization Project' (WHUP), katika mwambao wa ziwa Viktoria, ambao hufanya matumizi endelevu ya magugu maji. Mradi huu hushughulika na utengenezaji wa vikapu, majamvi, kofia, meza, vivuli/viambaza, makaratasi, vitabu, karata, mikeka na vitu vingine muhimu kwa kutumia sehemu anuwai za mmea huu, kama vile maua, majani, shina na vikonyo. Kwa mfumo huu basi, mmea huu umesababisha ajira kwa watu wa maeneo hayo.
Ajira nyingine ya namna yake, ni kwa wale walioajiriwa katika udhibiti wa usambaaji wa magugu haya. Hawa huajiriwa ili kudhibiti magugumaji kusambaa ndani zaidi ya ziwa, kama tutakavyoona hapa chini.
ADHA ZA MAGUGUMAJI
Katika maeneo mengi duniani ambapo magugumaji hupatikana, mara nyingi huchukuliwa kama mmea usiotakiwa, ha hivyo kila juhudi hufanywa kuhakikisha kuwa mmea huu unaondoshwa. Shida kubwa ni kwamba, mmea huu huzaliana kwa kasi kubwa ya ajabu, kiasi kwamba juhudi kubwa pamoja na gharama huhitajika ili kudhibiti usambaaji huu wa kasi. Kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa mmea huu hustawi katika mazingira yenye maji, basi mmea huu ni adha kwa shughuli zote ambazo hufanyika katika maji. Mmea huu huzuia shughuli za uvuvi, hunasa katika panga boi za vyombo vya majini,huzuia uzamiaji na upigaji mbizi, huziba mabomba ya kusafirishia maji ya kuzalishia umeme na shida nyingine nyingi. Magugumaji husababisha utando mkubwa mfano wa jamvi katika maji, na kuzuia mionzi ya jua na hewa ya oksijeni kupenya chini ya maji, hivyo huzuia upatikanaji wa viumbehai wengine katika eneo hilo, hasa jamii ya mimea. Mazingira haya ya ukosefu wa oksijeni katika maji, yakichangiwa na utando mkubwa wa magugumaji hufanya maji yasitembee na hivyo kuwa mazalio makuu ya mbu waletao malaria. Ni sababu hizi hufanya watu wengi wayachukue magugumaji na kuchukua hatua za kuyatokomeza. Kuna kukinzana kwa kiasi kikubwa kwa mawazo katika suala zima la magugumaji.
Hapa ni kila mtu na mtazamo wake, watengenezaji wa samani huona yana faida, na watumiaji wengine wa maji huona kama ni bughudha tu!
UDHIBITI NA UTATUZI WA ADHA ZA MAGUGUMAJI
Kuna taasisi kadhaa ambazo hushughulika na udhibti wa ueneaji wa magugumaji. Pia kuna watu binafsi ambao hukerwa na maimea hii, hivyo huamua kuondoa kwa mikono. Kwa upande wa ziwa Viktoria, nchi zote tatu za Afrika Mashariki zina mipango endelevu ya kudhibiti kuenea kwa magugumaji, na kwa Tanzania na mradi wa LVEMP (Lake Victoria Environmental Management Project), ambao pamoja na mambo mengine hushughulika na usafi na ulinzi wa mazngira wa ziwa tajwa. Katika nchi nyingine zenye magugumaji, kuna wadudu wajulikanao kwa kitaalamu kama 'neochetina' ambao 'hupandwa' makusudi ili kula magugumaji. Hata hivyo, kiwango kikubwa cha kuzaliana cha magugumaji huzidi uwezo wa wadudu hao wa kuyala. Inasemekana pia kuwa samaki aina ya sangara ambao hupatikana kwa wingi katika ziwa Viktoria walipandikizwa kwa ajili ya kula magugumaji, lakini kasi yao ya ulaji inazidiwa kwa mbali na kasi ya ukuaji wa magugumaji. Kuna dawa za viwandani za kuulia mmea huu, lakini haishauriwi sana kuzitumia kwa kuwa nyingi kati ya dawa hizo si rafiki wa mazingira, na huua viumbe wengine waishio majini.Badala yake, mitambo ya kusaga magugumaji hutumika zaidi, hasa katika ufukwe wa ziwa hili kwa upande wa Kenya.
Ndugu msomaji wa makala hii, umeona faida na adha za magugumaji,japo kwa ufupi tu. Una mtazamo gani kuhusu mmea huu?
Jadili
No comments:
Post a Comment