6/6/06

YAJUE MAENEO YA RAMSAR KATIKA TANZANIA (RAMSAR SITES)

Utangulizi
Maeneo ya Ramsar ni sehemu ya ardhi oevu duniani, (wetlands) ambayo yana umuhimu wa pekee duniani katika suala zima la uhifadhi wa mazingira. Ardhi oevu ni ile ardhi ambayo kwa msimu wote wa mwaka huwa na unyevunyevu. Jina hili "Ramsar" linatokana na mji wa Ramsar nchini Iran ambapo ndipo mkataba wa kutunza maeneo ya ardhi oevu duniani ulisainiwa, mnamo mwaka 1971. Kwa hiyo basi, mwaka 1971 ndipo yalipofanyika maamuzi ya kulinda maeneo ya ardhi oevu dhidi ya uharibifu, ili yaweze kutumika katika shughuli endelevu, kama vile vyanzo vya maji. Mpaka sasa, kuna mataifa 152 duniani yaliyotia sahihi mkataba huu wa kulinda ardhi oevu, ikiwemo Tanzania. Kuna maeneo tengefu 1608 ya Ramsar duniani yanayochukua ukubwa wa hekta milioni 140, kati ya haya Tanzania tuna maeneo manne tu, ambayo tutayaelezea hapa chini.


Nini umuhimu wa Maeneo haya?
Maeneo ya Ramsar yana umuhimu wa kipekee katika jamii. Kwanza, yana bioanuwai adimu sana hapa duniani ambazo aghalabu hupatikana maeneo hayo tu. Pili, ni vyanzo vikuu vya maji katika maeneo mengi diniani, hivyo, kama yakiharibiwa kwa shughuli za kibinadamu basi uhai wa viumbe hao adimu utatokomea pia. Maeneo haya ni chanzo kukuu cha nishati ya umeme, ambapo kwa namna moja au nyingine, mito inayozalisha umeme hutiririka kutoka katika nyingi ya ardhi hizi oevu. Chukulia mfano wa bonde la mto Rufiji, bonde hili huanzia katika milima ya Uporoto mkoani Mbeya na kusambaa katika mikoa mingine ya Iringa na Morogoro, ambapo kuna bonde la mto Kilombero ambalo ni maarufu kwa kilimo cha mpunga na ni moja ya maeneo tengefu ya Ramsar. Kwa mfano huu mmoja, nadhani tunaweza kuelewa japo si kwa undani, juu ya maeneo haya muhimu.

Maeneo Ya Ramsar Tanzania ni yapi?
Tanzania tuna maeneo manne tengefu, yaliyo chini ya mkataba wa Ramsar. Maeneo haya ni ardhi oevu ya Muyovozi katika mto Malagarasi-Kigoma (13/04/2000), ardhi oevu ya bonde la Ziwa Natron-Manyara (04/07/2001), bonde la mto Kilombero-Morogoro (25/04/2002) na bonde la Rufiji-Mafia hadi Kilwa-Pwani (29/10/2004). Katika mabano ni tarehe ambazo maeneo hayo yaliingizwa katika orodha ya maeneo tengefu ya Ramsar. Kwa hiyo, maeneo haya yanalindwa na mikataba ya kimataifa, ambapo hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uwindaji na ukataji miti.

Ni Sifa zipi zinatakiwa, ili Eneo liwe chini ya Mkataba wa Ramsar?
Kuna sifa kuu tisa zinazofanya eneo likubalike kuwa katika uhifadhi wa mkataba wa Ramsar. Sifa hizi zimegawanywa katika makundi manne tofauti, kwa hapa nitazichangaya zote.

1. Inatakiwa eneo oevu husika liwe na umuhimu wa kimataifa kwa kuonesha bioanuwai ambazo ni wakilishi, za kipekee, zisizopatikana mahali pengine popote ila hapo tu, iwe ni mazingira ya asili au ambayo hayajaribiwa uasili wake na liwe eneo ambalo liko katika sehemu stahili ya kijografia.

2. Eneo litahesabiwa kuwa na umuhimu wa kimataifa iwapo lina viumbe adimu ambao wapo katika hatari ya kutoweka kabisa toka katika uso wa dunia kutokana na muingiliano wa viumbe hai.

3. Ili eneo husika lihesabike kuwa na umuhimu w kimataifa, inatakiwa liwe lina viumbe hai (mimea na wanyama) ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza uanuwai wa kibiolijia (uasili)wa eneo husika.

4. Eneo litahesabiwa kuwa na umuhimu w kimataifa iwapo linasaidia upotevu/uwepo wa mimea/wanyama katika mzunguko mzima wa maisha ya viumbe hao (life cyles), au eneo ambalo linatoa ulinzi hao dhidi ya uharibifu, katika mazingira mbali mbali.

5. Iwapo eneo linatunza jamii ya ndege 20,000 kwa kawaida kwa wakati mmoja, basi hili litahesabiwa kuwa katika orodha ya maeneo tengefu.

6. Iwapo eneo linahifadhi asilimia moja ya aina za ndege kutoka jamii mbalimbali za ndege hao, litahesabiwa kuwa katika orodha hii.

7. Iwapo eneo lina hifadhi kiasi kikubwa cha jamii ya samaki wa asili (si wa kupandwa kama sangara wa Ziwa Viktoria) historia ya maisha ya samaki hao, mwingiliano wa jamii za samaki hao, ambao ni wakilishi wa eneo hilo oevu na ambaohangia utajiri wa bioanuwai duniani, litaignizwa katika orodha ya maeneo ya Ramsar.

8. Iwapo eneo ni chanzo kikuu cha chakula walacho samaki, sehemu ya kutagia/kuzaliana samaki, sehemu ya kupita ya samaki kwa ajili ya kutafuta mazalio au chakula, ambapo samaki hupategemea kwa maisha yao, basi eneo hilo litaingizwa katika orodha tajwa hapo juu.

9.Sifa hii inafanana sana na namba 6 hapo juu, lakini hii inahusika na wanyama kwa ujumla wake.

Kwa hiyo, ili eneo liwe katika orodha ya Ramsar, halina budi kuwa na moja kati ya sifa zilizoainishwa hapo juu, ingawa inatokea mara nyingine eneo moja kuwa na sifa kadhaa kati ya hizo.
Kwa sababu hizi basi, ilikuwa ni lazima kwa serikali kuwaondoa wafugaji katika ardhi oevu za Kilombero (Morogoro) na Mbeya) kutokana si tu na umuhimu wa kitaifa, bali kimataifa pia. Wafugaji na wakulima hawana budi kuelimishwa juu ya umuhimu wa maeneo oevu kwa maisha ya binadamu, badala ya kuyaharibu kwa kulima na kufugia makundi makubwa ya wanyama katika maeneo haya nyeti. Ni kwa sababu hizi ambapo serikali iliamua

1 comment:

Alex Mwalyoyo said...

MATUMIZI ENDELEVU YA MAENEO YA RAMSAR (RAMSAR SITES)

Nashukuru kwa swali zuri la Bwana Marcopolo. Kwa maainisho kadhaa ya masharti ya Ramsar, maeneo hayo yanaweza kutumika kwa shughuli endelevu kama vile utalii usioathiri mazingira (kama vile kupiga picha za kitaii),utafiti wa viumbe hai usioathiri mazingira, uchoraji ramani kwa kutumia vifaa vya GIS na matumizi mengine ya jinsi hiyo, la muhimu tu ni kwamba shughuli hizi zisiathiri viumbe na mazingira asili ya eneo husika. Kwa hiyo basi, serikali yoyote ambayo ina maeneo ya tengefu ya Ramsar, inaweza kuyatumia maeneo hayo kwa shughuli kama hizo.