6/5/06

HII INAWEZEKANA-TUWE NA UTASHI WA KISIASA!

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na misururu mirefu ya msongamano wa magari hasa katika jiji la Makamba (Dar es Salaam). Hii inatokana na ongezeko kubwa la watu pamoja na magari, lisiloendana na rasilmali za kuweza kuhimili ongezeko hili. Kwa maana hii basi, uwezo wa barabara zetu (carrying capacity), wa kuhimili tatizo hili ni mdogo sana. Na aghalabu misururu hii ipo katikati ya jiji na katika barabara zote kubwa za jiji hili. Hali hii inasababisha usumbufu kwa wananchi, hasa suala la kuchelewa kazini, kwa kutumia muda mrefu kusafiri umbali mfupi. Wagonjwa wa dharura mara nyingine hufia njiani kwa sababu ya kucheleweshewa matibabu kutokana na misururu hii. Ni suala la kawaida kukuta mtu anatoka kwake muda wa saa 12 asubuhi na kufika kazini kama saa 2.30 hivi, uchelewevu wote huu ukisababishwa na msongamano wa magari. Kumekuwa na midahalo mbalimbali katika vyombo vya habari, vyombo vya usafiri na katika vijiwe sehemu kadha wa kadha kuhusu adha hii, lakini sina uhakika kama midahalo hii inawafikia warasimu, ambao wanatakiwa kutatua tatizo hili. Ni kero kubwa kwa jiji hili, ingawa hatujaona nia thabiti ya wakubwa wa nchi hii ya kulidhibiti tatizo hili. Kuna nadharia kadhaa, ambazo zikifanyiwa kazi na na kuwekwa katika vitendo na warasimu zinaweza kabisa kupunguza, kama si kumaliza tatizo hili katika nchi hii.

1. Mipango Miji
Suala la kujaza ofisi zote katikati ya jiji, kwa mtazamo wangu naona si sahihi sana. Kwa mfano, asilimia kubwa ya wizara zote zipo Dar es salaam, tena katikati ya jiji, ukiachilia mbali wizara ya Mifugo na Tawala za mikoa na serikali za mitaa, ambazo zipo Dodoma. Sasa basi, wananchi ambao huwa na shida anuwai, hulazimika kujazana katika wizara hizi ili kutatuliwa shida zao. Sasa katika hali kama hii unafikiri misururu katikati ya jiji itaepukikaje? Suala hili laweza kutatuliwa kwa kuwa na majengo mengi nje ya jiji. Majengo kama Ubungo Plaza na Millennium Towers pale Kijitonyama yalistahili kujengwa mengi na iwe ni nje ya jiji, maeneo kama Mbezi, Kibamba, Boko, Bunju na Tegeta ili kupunguza msongamanao wa watu na magari. Kwa maana hii basi, kungekuwa na kupishana, kwamba mtu anaishi Magomeni na anafanya kazi Bunju na mwingine anaishi Kariakoo na kufanya kazi Mbagala, hivyo misururu isiyo ya lazima isingekuwepo jijini. Lakini kwa sasa hali ni kinyume chake, maghorofa mengi marefu hujengwa katikati ya jiji. Suala hili huongeza idadi ya ofisi na na watu na kufanya katikati ya jiji kuwa na watu wengi. Tujaribu kutumia nadhari hiyo, inawezekana kabisa kupunguza tatizo.

2. Uhamishaji wa miji mikuu
Suala hili liliwahi kufanyiwa kazi na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa kuanzisha mradi wa kuweka Makao makuu ya nchi pale mkoani Dodoma yaani Capital Development Authority (CDA). Sina uhakika na sababu zilizofanya mradi huu usiendelee kwa kasi, lakini kwa wataalam wa mipango miji wanajua ni nini Mwalimu alidhamiria kukifanya. Lengo la mradi kama huu, aghalabu huwa ni kupunguza msongamano usio wa lazima katika baadhi ya miji, kwa kusambaza huduma katka mikoa mbalimbali. Kuna baadhi ya nchi zimefanikiwa kutekeleza mipango kama hii. Nijeria ilihamisha makao makuu yake kutoka Lagos kwenda Abuja, Ivory Coast inahamishia makao yake makuu kutoka Abidjan kwenda Yamoussokrou na kadhalika. Hii inasaidia sana katika kupunguza misongamano isiyo ya lazima katika miji mikuu.
Nafikiri ni kwa sababu hii ambapo Mahakama Kuu na Benki Kuu za hapa kwetu zina kanda kadhaa katika mikoa mbali mbali. Lengo ni kupunguza misongamano na safari zisizo za lazima jijini Dar es Salaam.

3. Upandaji wa Pikipiki na Basikeli
Kuna haja ya kuwa na mipango endelevu ya kupanda pikipiki na basikeli kwa wingi, ili kupunguza uwingi wa safari za magari. hili linawezekana kama wananchi tutaamua kwa moyo mmoja kupanda basikeli kwa sehemu ambazo makazi yetu hayapo mbali na ofisi zetu. Kwa mfano unakuta mtu anaishi Mwenge Dar, na anafanya kazi Makumbusho au pale Sayansi. Huyu nae analazimika kukaa katika msururu wa magari na kuchelewa kazini ilhali kama angekuwa na basikeli, ingemchukua muda mfupi sana kufika ofisini kwake. Kuna ulazima wa kuwa na fikira mbadala katika suala zima la kupunguza msongamano usio wa lazima. Suala hihi la pikipiki na basikeli liende sambamba na kutembea, kwa maana kwamba kama mtu anaona sehemu yake ya kujipatia riziki haiko mbali na makazi yake basi ni bora akatembea ili kuepuka adha ya msongamano. Inawezekana!

4. Udhibiti wa Watu kukimbilia Mijini
Suala hili kwa kiasi kikubwa husababishwa na watu waliopo vijijini kukuta hawana huduma muhimu za jamii, na hivyo hujikuta hukimbilia mijini kutafuta huduma hizi kwa namna yoyote. Utoro huu ni mkubwa sana hasa kwa vijana, ambao huamua kukimbilia mijini baada ya kuhitimu masomo yao, kwa hisia kuwa mjini kuna kila kitu, kwa hiyo 'hakiharibiki kitu'. Ni kwa mtazamo huu wa vijana wa vijijini ambapo hujikuta wamejazana mijini na kukosa ajira na kuongeza msongamano usio wa lazima. Hii hufanya tuanze kunyang'anyana rasilmali chache zilizopo mijini, ikiwemo usafiri na makazi.
Utatuzi wa tatizo hili unawezekana iwapo tu warasimu watilia mkazo utekelezaji wa mahitaji muhimu ya watu wa vijijini kama vile shule bora, huduma za afya na maji.

Kwa ujumla, adha zilizoainishwa hapo juu zinaweza kutatuliwa iwapo tu kutakuwa na utashi wa kisiasa wa wananchi na serikali kwa ujumla katika kuzivalia njuga adha hizo. Masual haya yanawezekana na rasilmali za utekelezaji wake tunazo, wakiwamo watu, suala ni utashi wa kisiasa tu. Inawezekana!

No comments: