UTANGULIZI
Hivi karibuni, yaani tarehe 15 Juni 2006, waziri wa fedha mheshimiwa Zakhia Hamdani Meghji aliwasilisha bajeti ya matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007 katika kikao cha bajeti cha bunge la Tanzania. Kama ilivyo kawaida, wengi wetu tulihamishia usikivu wetu Dodoma kusikiliza yale tuliyoandaliwa kwa mwaka wa fedha ujao. Kwa mtazamo wa wengi ni kwamba bajeti hii ina afadhali ukilinganisha na iliyopita, kwa kuwa imekumbuka maeneo mengi muhimu, kama vile kupunguza kodi katika mafuta, kuongeza ruzuku kwa pembejeo za kilimo na kuongeza mishahara ya watumishi. Ni mengi yanavutia katika bajeti ya mwaka huu, lakini kama ilivyo ada watu tunatofautiana katika mawazo. Kuna wanaopinga kuwa bajeti haijafanya lolote katika kumuinua mtu wa kipato cha chini. Maneno haya tumeyasikia mahali pengi hasa kutoka kwa wanasiasa maarufu, lakini ni haki yao kusema hivyo, kwani katiba inamruhusu kila mtu kutoa maoni yake kadri anavyotaka.
Kwa upande wangu, nilivutiwa na kipemgele cha kuongeza kodi katika mifuko laini ya plastiki, maarufu kama 'rambo' kutoka 15% hadi 120%, naunga mkono kodi hii, na ndio suala ambalo nimeliweka katika mjadala moto hapa mahali.
AINA ZA MIFUKO YA RAMBO
Mifuko ya rambo hutengenezwa kwa plastiki laini aina ya Low Density Polyethylene (LDP). Kuna mingine ambayo hutengenezwa kwa plastiki ngumu aina ya High Density Polyethylene (HDP), lakini hii si maarufu sana kama ile laini. Tofauti rahisi ya aina hizi za mifuko ni kwamba, mifuko laini haipigi kelele inapopapaswa na ile migumu hupiga kelele. Hii ndio tofauti rahisi na ya wazi ambayo mtu wa kawaida hutumia kutofautisha aina hizi. Lakini hata katika mfumo wa kikemikali, bidhaa zitumikazo kutengenezea aina hizi za mifuko hutofautiana. Tofauti hii ni kwamba, malighafi itumikayo kutengenezea mifuko laini haiwezi kurejeshwa katika hali yake ya awali kwa sababu wakati wa utengtenezaji wake, hufanyika badiliko la kikemia (chemical Change) badala ya badiliko la kiumbo (physical change) ambalo ni rahisi kugeuza na kutengeneza kitu kingine.
MATUMIZI
Ingawa kwa kiasi kikubwa matumizi hufanana, kuna tofauti ndogo ndogo. Mara nyingi mifuko laini ni midogo kwa muundo na myepesi, kwa hio haitumiki kubeba vitu vizito, tofauti na ile migumu ambayo hutumika kubebea vitu vizito. Kwa mfano, mara nyingi, watunza bustani za miti hutumia mifuko migumu katika kuotesha miti kwa kuwa hudumu kwa muda mrefu tofauti na ile laini ambayo huharibika ndani ya muda mfupi. Kuna matumizi ya aina mbali mbali ya mifuko hii kadri mtu atakavyotaka, na niliyotaja hapo juu ni baadhi tu.
ADHA ZA MIFUKO HII
Mifuko ya rambo imekuwa ikipigiwa kelele sana sehemu mbali mbali kuwa inachafua mazingira, kutokana na utaratibu wetu mbovu wa utupaji wa taka. Mifuko hii hupatikana kwa bei rahisi sana, na wakati mwingine hutolewa bure kabisa baada ya mtu kununua bidhaa. Mara nyingi mifuko hii huzagaa mahali pengi kutokana na kutoitupa katika mahali stahili. Suala hili limekuwa sugu, kwa nafikiri ndio sababu imeamua kupandisha kodi yake kutoka asilimia 15 hadi 120! (rejea Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2006/07 ukurasa wa 45). Hali kadhalika, mifuko hii mara nyingi hutumika kubebea vyakula kwa hiyo huwa na masalia ya vyakula wakati fulani. Ndege wa jamii mbali mbali, hasa jamii ya kunguru huiokota na kuisambaza kila mahali, katika harakati zao za kujitafutia riziki, kiasi cha kuleta kero. Vivyo hivyo, wakati wa mvua mifuko hii hukusanyika pamoja na taka nyingine na kuziba mitaro ya kupitisha maji taka. Hali hii husababisha maji kutuamac na kuleta harufu mbaya. Maji haya ni mazalio mazuri ya mbu waletao malaria. Ni maji haya haya ambayo yanaleta kipindupindu kisichoisha katika baadhi ya miji yetu. Mifuko hii imesambaa sana katika barabara zote kuu na kuchafua maeneo ya kando ya barabara hizo, hasa ziendazo mikoani. Hii ni kutokana na baadhi ya mabasi yasafirishayo abiria kutokuwa na utaratibu wa ukusanyaji wa taka katika mabasi yao, ili ziweze kutupwa mahali stahili. Mifuko hii, haiozi kirahisi ifukiwapo, hivyo husababisha usumbufu mara eneo husika linapotumiwa kwa matumizi mengine.
UTATUZI WA ADHA HIZI
Kuna namna nyingi sana endelevu za kuweza kukabiliana na suala zima la uchafuzi wa mazingira hasa suala la kutupa taka ovyo. Kwanza, inabidi tuwabane wasafirishaji wa abiria hasa wa masafa marefu, ambao kwa namna moja au nyingine hulazimika kusimama njiani ili kupata chakula. Hawa ndio chanzo kikuu cha kusambaa kwa mifuko laini njiani. Nasema hivi kwa sababu, muda wa dakika kumi hadi kumi na tano wanazotoa kwa ajili mapumziko na chakula hazitoshi, hivyo abiria hulazimika kunuua chakula na kula ndani ya gari na kutupa mifuko laini njiani, mara baada ya kumaliza kula. Tuwabane ili wawe na sehemu za kuhifadhia taka katika mabasi yao. Suala hili linawzekana, na linafanya kazi. Kama huamini, tembelea mbuga ya wanyama ya Mikumi, uone walivyo wakali kuhusu kutupa mifuko na na chupa za maji katika maeneo yao.
Suala lingine, ni kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira, hasa kwa watu wa mijini kuhusu namna ya kutupa taka ngumu mahali panapotakiwa. Inashangaza sana kuona kuwa watu hutupa mifuko laini na taka nyingine ngumu chini au pembeni ya pipa la taka wakati pipa liko hapo hapo. Hawa wanahitaji kuelimishwa kama si kuadhibiwa.
MIFUKO MBADALA
Pamoja na serikali kuchukua hatua katika kudhibiti usambaaji wa mifuko laini, kuna kundi kubwa la watu ambao wameona kuwa serikali haijawatendea haki kabisa. Baadhi yao ni wafanyabiashara waagizao mifuko hii toka nje ya nchi, na wasambazaji wao waliopo mahali mbali mbali hapa nchini. hata hivyo ningependa kutoa ushauri kwao, na kwa wengine. Ushauri huu ni kuwa, tuanze kutumia mifuko mbadala ambayo ni rafiki wa mazingira. Kwanza tutumie mapakacha. hii ni mifuko ya asili inayotengenezwa kwa makuti (majani ya minazi na michikichi). hufaa sana kubebea bidhaa za namna anuwai kama vile matunda, nazi viazi na kadhalika. ikifukiwa, mifuko hii huoza na kusababisha mbolea. Pili, tutumie bidhaa zinazotengenezwa kwa ukindu na mimea ya jamii yake. Hufaa saa kwa matumizi ya namna mbali mbali na tukiitumia tutakuwa tunakuza uchumi wa nchi kwa kuwaongezea kipato watengenezaji wake. tatu, tutumie mifuko ya karatasi za kawaida kama vile mifuko ya khaki. Mifuko ya namna hii huoza mara inapofukiwa (biodegradable), hivyo haiathiri mazingira. Pia kuna mifuko inayotengenezwa kwa nyuzi za 'Jute'. Jute ni malighafi itumikayo kutengeneza magunia. Mifuko hii ya jute ilikuwa maarufu sana siku za nyuma, kabla ya ujio wa rambo na ilikuwa na msaada mkubwa sana. Kwa sasa imeanza kurudi sokoni, kwa hiyo hatuna budi kuitumia kwa wingi. Kuna mifuko ya namna nyingi ambayo inaweza kutumika badala ya mifuko laini ya plastiki, ni suala la uamuzi na utashi tu.
Inawezekana kufanya mabadiliko. Je uko tayari?
Jadili.
5 comments:
Hongera Bwana Alex Mwalyoyo kwa kuanzisha Blogu ya Tanganyika yetu yenye mada moto moto ambazo zinahusu mazingira na maisha ya kila siku ya Mtanzania. Nimevutiwa sana na makala kuhusu mifuko ya plastiki, ung'oaji wa mianzi huko Iringa na habari za ramsar. Kimsingi makala zako ni za kiwango cha juu na za kuelimisha jamii ya kimataifa na siyo Watanzania tu. Kwa hiyo ili kuziongezea thamani jaribu kufanya yafuatayo; Jiunganishe na wana blogue maarufu kama Ndesanjo Macha mwenye blogu ya jikomboeblogspot.com ambaye vilevile huandika makala kwenye gazeti la Mwannchi kila Jumapili. Au Muhidin Isa Michuzi na blogu ya Issamichuzi blogspot.com
karibu sana Bw. Mwalyoyo (sijui jina hili ni la Mbeya au vipi), tuendelee kuaimsha jamii ya Kitanzania mtandaoni, mahali ambako mtu unajimwaga utakavyo, hakuna stori za kutupwa kapuni au kuchujwa.
Kwanza napenda kukukarisha katika Blogu nimefurahi kumbe wewe ni mmoja wa wasomaji wangu wa makala katika gazeti, nashukuru sana, pili kuhusu hii mada uliyokuja nayo mi nadhani kuna haja ya serikali kutafuta miundo mbinu mbadala itakayo fanya mifuko ya plastiki itoweke juu ya uso wa Tanzania.
Kadhalika nimefurahi sana kuona muelekeo wa Blogu yako kuhusu mambo ya mazingira, unajua mazingira yamo ndani ya maisha tuishio huwezi kufanya lolote bila kutaja mazingira.
Mazingira yapo katika maisha, mazingira yapo katika kila nyanja katika maisha ya binadamu.
Tupo pamoja karibu ndani ya ulimwengu wa Magazeti Tando
Jina la blog kwa kweli halitendi haki....kuzungumzia mazingira ya Tanzania chini ya jina Tanganyika.. sio sahahi kabisa!...
Sawa Bw Mwakanjuki. Nakubaliana na maoni yako, lakini hebu toa mawazo yako, tuweke jina gani hapao mahali?
Karibu sana
Post a Comment