5/26/06

JE UNAITHAMINI NA KUIPENDA TAALUMA YAKO?

U hali gani mpenzi msomaji wa blogu hii?
Ningependa kuongelea suala muhimu sana katika maisha yetu ya uanazuoni. Mwaka jana Desemba 30, 2005 wakati rais wetu anahutubia bunge la Jamhuri ya Muungano (wa Tanzania?) kwa mara ya kwanza, aligusia kwa uchungu sana suala la wanataaluma kutotumia ipasavyo taaluma yao, lakini yeye aliita "Kutukanisha Taaluma" Katika mfano mmojawapo, aliwatuhumu Mabwana (nafikiri na Mabibi) ardhi kuwa wanauza maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya michezo, ili yatumike kwa shughuli za ujenzi, wakati taaluma yao hairuhusu kufanya hivyo.
Ukiliangalia suala hili kwa undani, utaona ukweli wake, hasa ukifuatilia suala la migogoro ya ardhi katika Tanzania, wilaya ya Kinondoni ikiongoza. Inasemekana kuwa hakuna wilaya yenye migogoro mingi ya ardhi katika Jiji la Dar es salaam kama Kinondoni. Zingatia kuwa karibu asilimia kubwa ya nyumba za bei mbaya kwa jiji hili ziko kinondoni ukianzia na Mbezi beach, Masaki, Oysterbay, Kinondoni nk. Hili la watu wa ardhi ni kundi moja la 'watukanisha taaluma'.
Kundi jingine alilogusia Mheshimiwa Rais ni la wanasheria, ambao hujigamba kwa kujiita "Learned Brothers/Sisters". Hawa nao hawajambo kwa kusaini mikataba ya ajabu ajabu ambayo ni wengi wetu tunaifahamu na inatukera. Ni hawa hawa waliosaidia kupitisha kwa kishindo sheria ya takrima, ambayo, kwa sasa wanataaluma wasiokubali kutukanisha taaluma yao wamesema kuwa haifai. Hebu tujiulize, iweje msomi wa shahada kadhaa za sheria akatia sahihi ya kuipitisha sheria ambayo anajua (au hajui?) kuwa inakiuka katiba ya nchi? Utajiitaje msomi ikiwa huthamini elimu na maadili ya taaluma yako?
Kuna kundi jingine la wanataaluma wanaotukanisha taaluma yao. Hawa ni wale ambao waliruhusu ujenzi wa majengo marefu sana pale Jijini Dar, hasa Kariakoo bila majengo hayo kukidhi viwango vya kitaalamu vinavyotakiwa. Matokeo ya kutukanisha taaluma yao tunayaona sasa, ambapo majengo kadhaa yameamriwa kubomolewa, kwa kuwa hayakidhi viwango sahihi vya ujenzi. Ina maana kuwa kabla ya majengo haya kujengwa hayakukaguliwa kama yanakidhi viwango vinavyotakiwa? Hivi hawa nao wanaithamini taaluma yao?
Hivi, ni viwanda vingapi hapa Tanzania ambavyo vinazingatia usalama wa mazingira kwa kushughulikia taka zizalishwazo na viwanda hivi? Wataalamu wa Tathmini za Athari za Mazingira (EIA) mpo? Mnatumia taaluma yenu kama ipaswavyo? Mmeona rangi ya maji ya mto Kizinga pale Mbagala Mission? Na rangi ya mto Kiwira pale Ilima Rungwe ikoje? Mmechukua hatua gani?
Kuna mambo mengi sana ya kuongela kuhusu uhusika wetu katika taaluma zetu, lakini hasa tujiulize, ni kwa nini baadhi yetu 'tunatukanisha' taaluma zetu? Mpaka hapo, ni kwa nini vyeti vya elimu ya hawa watukanishaji taaluma isitiliwe mashaka? Je hayo ni matokeo ya "kudesa?" au kuzunguka mbuyu?
Ni kwa kiasi gani tunathamini taaluma zetu?
Jadili

2 comments:

John Mwaipopo said...

Mwalyoyo nimekupata ngoja nikupigie Baragumu pale kwangu ili wanablogu waje-ge kukusabahi. Hongera kwa kuanza kublogu. Kumbuka kukikolea ni kama addiction 'flan' hivi. Huachi ng'o.

Nimesha rejea bongo nitakutafuta. Pia waweza kunitafuta kwa kanamaba ka simu kalekale ka kuanzia Mlimani.

boniphace said...

karibu karibu kaka nitapita hapa baadaye kusoma makala hizi