8/31/06

TUJIFUNZE TOKA KWAO

UTANGULIZI
Mu hali gani wasomaji wa blogu hii?
Kama nilivyodokeza siku zilizopita, nipo kaskazini mwa dunia yetu, hususan nchini Norway. Kwa ujumla muda huu ndio majira ya joto yanamalizika kwa huku, muda si mrefu tutakabiliana na baridi na barafu.

HALI YA HEWA
Kwa kawaida, hapa mahali naambiwa na wenyeji kuwa mvua haina msimu maalum, inanyesha wakati wowote (nafikiri ni kwa sababu ya misitu mingi) na kuwa karibu na bahari. Kwa kawaida wakati wa baridi joto hushuka hadi nyuzi -28 hadi -32 kulingana na maeneo. Na kuna wakati fulani (kama sasa) jua linazama muda wa saa 2.30 hadi saa 3.30 usiku kwa saa za hapa. Na kuna maeneo ya kaskazini mwa nchi ambapo jua huwa halizami kabisa kwa baadhi ya miezi, kwa hiyo ni suala la kuangalia saa tu katika kufanya mambo yako. Kwa mfano, wakati nasafiri kwa ndege toka Uholanzi kwenda Oslo, ilikuwa saa 4 kasoro usiku na jua lilikuwa likiwaka!

UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Nchi hii ina watu milioni 5 tu na nadhani robo ya hawa ni wahamiaji, kwa hiyo maeneo mengi ni misitu na nyumba chache sana. Kwa maana hii basi, basi wengi hujazana katika miji mikubwa kama Oslo, Trondheim, Stavanger na Bergen, kwa hiyo uharibifu wa mazingira si kwa kiasi kikubwa. Hali kadhalika, nishati kubwa zitumikazo huku ni mafuta na umeme, ingawa kuni hutumika mara chache sana kwa ajili ya kuzalisha joto katika baadhi ya nyumba wakati wa majira ya baridi. Hata hivyo wengi hutumia mitambo ya kuzalisha joto itumiayo umeme. Ukataji miti upo, hasa miti ya kupandwa, kwa ajili ya kuzalisha mbao na bidhaa nyingine za namna hiyo, na ukiwa katika jiji hili utakutana na magari mengi tu ambayo yanapakia magogo kupeleka viwandani. Kwa ujumla, hawa watu wamedhibiti vumbi kwa kiasi kikubwa wakisaidiwa na hali ya hewa (mvua za mara kwa mara na misitu), tofauti na kwetu ambapo kuna vumbi kila karibu kila mahali. Kwa hapo Tanzania, naweza kufananisha mitaa ya huku na ile ya jiji la Dar es Salaam kama vile barabara ya Haile Selasie, Garden, Shaaban Robert na Magogoni, kwa maana ya kwamba njia zote zina lami, mpaka njia za waenda kwa miguu.
Kuna udhibiti mkubwa wa vyombo vya majini, hasa kuhusu umwagaji wa mafuta na taka nyingine. Kwa watu niliowahoji, wanasema kuwa kuna adhabu kali sana iwapo mtu atakutwa anatupa taka majini, kwa kuwa kuna maeneo mengi sana hapa mahali ya kukusanyia taka. Hata hivyo taka hizi hutengwa kulingana na aina zake, kwa maana ya kwamba, kunakuwa na mapipa kama matatu katika eneo moja. Haya hukusanya taka za namna mbalimbali kila pipa peke yake, yaani kuna pipa la makopo ya maji na bia, pipa la masalia ya vyakula na pipa la taka ngumu kama za plastiki. Pamoja na udhibiti huo bado kuna wavunja sheria vile vile, ambao hutupa taka mahali popote watakapo na hawajali lolote.

USAFIRI
Kuna mpangilio mzuri sana wa njia za usafiri hapa mahali, na hakuna misururu kama ile ya jiji kubwa hapo nyumbani. Kwa mfano, nyakati za asubuhi kunakuwa na treni katika njia (reli) zaidi ya kumi katika stesheni kuu ambazo husafirisha abiria kwenda miji mbali mbali katika kazi na nyingi ya hizi hupita chini ya ardhi kwa baadhi ya maeneo. Kila baada ya dakika zisizozidi 7 treni hutoka stesheni kuu kwenda mahali fulani. Kwa mfano, mimi naishi Oslo na nafanya kazi mji wa Lysaker, inanichukua dakika kama kumi na tatu tu kufika kazini, umbali kama wa kilometa 30 hivi. Hali kadhalika kuna treni zinazopita katikati ya jiji katika mitaa mbali mbali, hizi zenyewe ni kwamba, reli zake zimepitishwa katikati ya lami, kwa hiyo magari na treni huchangia njia. Hizi ni nyingi kuliko nilizotaja hapo juu. Hali kadhalika kuna mabasi mengi sana makubwa katikati ya jiji, yanayosafirisha watu kutoka na kuingia jijini Oslo. Naweza kusema hizi ndio dala dala za huku. Pamoja na uwingi huu, ukichanganya na magari binafsi hakuna misururu!

KWA NINI HAKUNA MISURURU?
Kwanza, mpangilio wa mji ni mzuri sana, kuna njia nyingi sana kwa hiyo haimlazimu mtu kupita njia moja na kuna njia nyingi ambazo hupita juu ya nyingine (fly overs) kama lilivyo daraja la Manzese, na kati ya hizi kuna nyingine ni ndefu kwa kilometa kadhaa. Hali kadhalika kuna barabara zipitazo katika mahandaki, nazo ni nyingi pia.
Pili, jiji la Oslo ni kwa ajili hasa ya makazi na ofisi chache muhimu. Kwa maana hiyo basi, viwanda vingi vipo nje ya jiji hili, ambapo huwalazimu wafanyakazi kusafiri toka jijini hapa kwenda nje ya jiji kikazi, kwa hiyo basi huu ni mfumo wa kwenda na kurudi (two way), tofauti na nyumbani, ambapo asubuhi na jioni misururu huwa ya namna moja (mara nyingi) hasa wakati wa kwenda na kurudi kazini.
Tatu, kuna kundi kubwa la watu ambao hutumia baiskeli kwenda kufanya kazi zao ndani na nje ya jiji. Na kusema kweli baiskeli ni nyingi mno hapa mahali (kama Tanga au Morogoro vile) hadi zinakuwa kero. Nafikiri ni nyingi kutokana na utambarare wa jiji na hali ya hewa ya baridi, kwa hiyo mtu hachoki sana. Hizi nazo husaidia sana kupunguza misururu barabarani (nilishawahi kuongelea suala hili katika baadhi ya makala zangu zilizopita).
Kuna mengi sana ya kuongelea lakini kwa leo naishia hapa.
Nitaendelea kutafiti mambo mengine zaidi na kuwajulisha.

Wao wameweza wana nini? Na sisi tushindwe kwa nini? Kuna nini katikati hapa?
Jadili.

No comments: