9/8/06

KIJANI, NJANO NA MAZINGIRA!

UTANGULIZI
Ndugu wasomaji wa blogu hii, leo naleta kwenu wazo jipya ama mjadala mpya. Kama kawaida yetu, ni jadi kuwa mtu akitoa wazo basi nasi tunapata wasaa wa kuchangia mawazo yetu, aidha kwa kuboresha ama kukosoa. Kwa hiyo basi, kwa leo nitaongelea rangi za kijani na njano, ambazo kwa siasa za nchi yetu si rangi ngeni hata kidogo, lakini leo ni siasa za kijani na njano katika upande wa mazingira.

MADA
Kwa wakereketwa wa siasa za nchi yetu, kijani na njano ni rangi za bendera ya chama tawala na pia ni mbili kati ya rangi nne za bendera ya taifa letu. Kwa ujumla rangi hizi kwa bendera zote mbili huwakilisha utajiri wa maliasili vikiwemo mimea, wanyama na madini yapatikanayo nchini mwetu. Huo ndio ufafanuzi uliowekwa yakini na serikali na chama kwa bendera hizo. Kwangu mimi, rangi hizi ni zaidi ya hapo, na humaanisha mambo mengine pia. Kwa wanachama wa chama tawala, wao huadhimisha kuzaliwa kwa chama chao kila mwaka tarehe tano mwezi wa pili. Aghalabu sherehe hizi huwa na shamra shamra nyingi zikiambatana na upokezi wa wanachama wapya na uzinduzi wa matawi mapya ya chama. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, chama tawala nchini mwetu kina idadi ya wanachama rasmi wasiopungua milioni tano, nje ya mashabiki. Si haba, kwa nchi ya vyama zaidi ya kumi vya siasa na watu milioni thelathini na tano.
Kwa maana hiyo basi, nafikiri katika shamra shamra hizi wanachama hawa hupata wasaa wa kubadilishana mawazo na kuelimishana. Ni bora pia wakaelimishana maana ya rangi za bendera za chama chao kama hawajaelezwa, hasa kwa wanachama wapya. Pia, ni bora wakaelimishwa matumizi sahihi ya rangi hizo.

WAZO
Iwapo kila mwaka katika tarehe tajwa hapo juu wanachama wangekumbushwa (au kuelimishwa?) namna ya kutunza ukijani popote pale walipo, basi katika suala zima la mazingira tungekuwa mbali sana. Hebu chukua mfano, kila mwanachama kati ya hawa milioni tano (acha mashabiki) alazimike kupanda miti miwili tu mahali panapostahili, katika kumaanisha ukijani wa bendera ya chama chake, basi kwa mwaka tunakuwa na miti milioni kumi! Si suala dogo wala porojo, na hii ni kwa siku moja tu kwa mwaka mzima. Ukichanganya na miti tunayopanda kila Januari, basi tungekuwa tunasikia kwa mbali sana suala la ukame na kukauka kwa vyanzo vya maji.
Lakini, hata si kwa kupanda miti, basi iwe ni kuokota taka na kuzihifadhi mahali panapostahili ili kutunza ukijani, nadhani bustani nyingi sana mijini zingekuwa kijani sana hadi sasa, badala ya kuzungushia uzio kila mahali penye bustani ili watu wasikanyage bustani zetu. Ni suala la elimu na utashi tu.

Kwani haiwezekani?
Jadili

No comments: