10/23/06

NISHATI NA MAISHA

UTANGULIZI
Kwa dhana, nishati ni ule uwezo wa kufanya kazi au kitu fulani. Kuna nishati za aina mbalimbali kama vile joto, sauti, mwendo, mwanga na kadhalika. Kuna uwezekano mkubwa sana wa kubadilinishati hizi kutoka aina moja kwenda nyingine kwa kutumia mbinu na vifaa mbali mbali. Kwa mada hii nitaongelea kwa ufupi sana nishati za mwanga na joto.

UMUHIMU WA NISHATI
Kwa maelezo rahisi ni kwamba hakuna maisha bila nishati. Nishati ni chanzo cha uhai wetu, kwani nishati ya mwanga kama ule wa jua hutusaidia kuona na kufanya mambo mbali mbali, hutuletea vitamini D na pia nishati hii husaidia usanisi wa chakula cha mimea, ambayo nasi tunaitegemea kwa chakula chetu. Nishati ya mwendo hutusaidia kujongea kutoka mahali fulani hadi pengine kwa muda mfupi sana kwa teknolojia ya leo na nishati ya joto hutusaidia kwa mambo mbali mbali kama vile kuivisha chakula chetu, kukausha mazao, kurekebisha hali ya hewa majumbani na kadhalika.
Kumekuwa na mwamko mahali mbalimbali hapa ulimwenguni kuhusu mustakabali wa dunia hasa katika suala nyeti la nishati. Mara nyingi dunia imekuwa ikitegemea mimea, madini (makaa ya mawe na nyuklia) na mafuta kama vyanzo vikuu vya nishati za namna mbalimbali.

KUNI NA MKAA
Katika mimea tunapata kuni na mkaa ambavyo kwa nchi kama Tanzania huchangia zaidi ya asilimia tisini ya mahitaji yote ya nishati kwa taifa. Hiki ni kiwango kikubwa sana, kwa hiyo juhudi za makusudi zinatakiwa ili kupunguza kiasi hiki. Kuni hutumika na mkaa kila mahali katika nchi zinazoendelea katika kufanyia kazi mbali mbali, kuanzia majumbani hadi viwandani. Kuni hutumika kuzalisha nishati ya joto katika viwanda vya chai na tumbaku, hutmika kupikia majumbani na matumizi mengine mengi tu. Kwa nchi zilizoendelea kuni hutumika kuchemshia maji, ambayo husambazwa majumbani kwa mabomba maalum kwa ajili ya kuzalisha joto wakati wa baridi. Ni nishati tegemeo sana kwa nchi hizi hasa wakati wa baridi, kwa kuwa kutumia mitambo ya umeme kuzalisha joto ni ghali kwa kiasi fulani.

MAKAA YA MAWE
Makaa ya mawe kwa miaka ya nyuma yalitumika moja kwa moja viwandani kuzalisha nishati za joto na mwendo kwa matumizi mbali mbali. Mpaka sasa kuna maeneo kadhaa hapa duniani ambapo makaa ya mawe hutumika kuzalisha nishati (kama vile mgodi wa makaa ya mawe kule Ilima/KiwiraMbeya). Makaa pia hutumika katika viwanda vya saruji katika kuzalisha joto la kuyeyushia mawe ili yasagwe na kuzalisha saruji. Lakini kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa, ikaonekana kuwa makaa si nishati rafiki wa mazingira yetu, hivyo kukafanyika mabadiliko makubwa sana ya kuiacha nishati hii kwa maeneo mengi. Lakini bado kuna nchi nyingi tu ambazo hazijaiacha nishati hii, ikiwemo nchi ya China ambayo inakuja juu katika maendeleo ya viwanda duniani. Mwelekeo na mkazo vikawa katika mafuta ya jamii ya petroli ambayo kwa sasa yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha ya mwanadamu.

MAFUTA YA PETROLI
Mafuta haya yanatumika kuendesha mitambo ya namna mbali mbali pamoja na ile izalishayo umeme, maarufu kama jenereta. Magari, ndege, meli, baadhi ya treni, huendeshwa kwa nishati hii pia. Kadri muda unavyosonga, nishati hii nayo imeonekana si rafiki wa mazingira kama inatumika katika mazingira ambayo si muafaka. Moshi unaotokana na mafuta haya yanapotumika katika mitambo huwa na athari sana katika mazingira, kwa kuwa huongeza kiasi kikubwa sana cha hewa ya kaboni dayoksaidi katika anga na kuharibu utando wa ozoni. Matokeo yake ni kuwa kunakuwa na ongezeko la joto katika uso wa dunia, na ongezeko hili limeleta athari nyingi sana katika sehemu mbali mbali hapa duniani (nilishaliongelea hili katika mada zilizopita). hio ni moja, lakini pili ni kuwa iwapo kunatokea ajali majini na chombo kinachosafirisha mafuta kikahusika, mafuta hutapakaa katika maji (na kawaida mafuta huelea majini) na kuathiri viumbe wanaoishi katika maji. Kwa viumbe kama samaki, hushidwa kupumua kwa kuwa mafuta huzuia hewa kutoka na kuingia katika maji. Kwa ndege wanaoshi kwa kutegemea uvuvi, mara wapakaapo mafuta haya katika shughuli zao za uvuvi hushidwa kuruka kwa kuwa mbawa zao hushikamana na kukakamaa hivyo kwa wakati fulani hufa. Kwa sasa kuna mikakati kwa nchi zilizoendelea, kuachana na utegemezi wa nishati hii, lakini itachukua muda sana, ingawa inawezekena (rejea makala iliyopita).

MAJI
Kwa miaka mingi nguvu ya maji imekuwa ikitumika kwa namna mbali mbali. Kwa upande wa nishati, maji yamekuwa yakitumika moja kwa moja kuendesha mitambo ya kusagia nafaka, na kwa upande wa Tanzania bado mifumo hii inafanya kazi mpaka sasa. Kwa mfano, katika kijiji cha Kisiwani wilayani Muheza Mkoani Tanga, kuna mtambo wa kusagia nafaka ambao kuendeshwa kwa nguvu ya maji. Kwa upande wa pili, kutokana na maendeleo ya kiteknolojia, maji yanatumuka kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme, na kwa sasa dunia imekuwa tegemezi kwa nishati hii kwa kiasi kikubwa. Hli si shwari sana kwa upande wetu Tanzania, kutokana na maji kutokuwa ya kuaminika na kutokuwa na mfumo mzuri wa urejeshaji maji katika mabwawa mara baada ya kuyatumia. Pia hali ya hewa hasa suala la ukame limekuwa kikwazo kikubwa kwa uendelezaji wa nishati hii. Miradi mikubwa ya umeme wa nguvu ya maji si rafiki wa mazingira, kwa kuwa hutumia maeneo makubwa sana kuhifadhi maji, kwa hio kunakuwa na uhamishaji wa watu na wanyama na mara kadhaa husababisha mafuriko kwa watu waishio kando yake iwapo milango ya bwawa itafunguliwa kupisha matengenezo, kwa kuwa maji hufunguliwa kwa wingi sana. Pia miradi hii hutumia maji mengi sana, kwa hio viumbe wengine ambao hutegemea maji hayo mbele ya mabwawa hawapati maji kwa uhakika (kumbuka suala la vyura katika mradi wa umeme-Kihansi).

NYUKLIA
Ni moja ya nishati mbadala katika kupunguza tatizo la nishati. Kwa sasa ni nchi zilizoendelea tu ndizo zina uwezo na mamlaka ya kutumia nishati hii, kwa kuwa ni ghali sana. Pia inadhibitiwa sana na shirika na nguvu za nishati la Umoja wa Mataifa liitwalo 'International Atomic Energy Agency' (IAEA), kwa kuwa ni nishati hii hii itumikayo kutengeneza silaha za maangamizi, kwa hio wanahofia kuwa iwapo inaachwa bila ya udhibiti basi inaweza kutumika kwa malengo mengine, na si uzalishaji wa nishati. Kwa sasa nchi kama Japan, Korea Kaskazini, India, Iran*, Marekani, Norway na Urusi zinatumia nyuklia kwa kuzalishia nishati. Nyuklia huhitaji uangalizi wa hali ya juu sana, kwa kuwa ikivuja ina madhara sana kwa mwanadamu na viumbe wengine. Ajali ya kuvuja kwa mitambo ya nyuklia ilishawahi kutokea katika mji wa Chernobyl nchini Urusi mnamo mwaka 1986 na kusababisha madhara makubwa!
*(Vinu havijaanza kufanya kazi Iran)

UMEME WA MIONZI YA JUA
Ni teknolojia mpya kwa kiasi fulani, na ni rafiki wa mazingira. Ni mfumo wa kuvuna mionzi ya jua na kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo maalum ijulikanayo kama 'Photovoltaics'. Uzalishaji wa umeme huu hutegemea sana uwepo wa mwanga wa jua na vihifadhi vya umeme huo kama betri. Umeme huu unafaa sana kwa mazingira yaliyo mbali na umeme wa gridi. Ni teknolojia ghali kwa kiasi fulani ingawa ni nzuri.

Kwa namna moja au nyingine tuendelee kujaribu kutafakari na kutafuta suluhisho la matatizo ya nishati yanayoikabili dunia, ili iwe mahali salama pa kuishi wanadamu.
Nafasi yako ni ipi katika hili?
Jadili!

10/11/06

MAFUTA MBADALA

UTANGULIZI
Kumekuwa na kilio sehemu mbali mbali duniani kuhusu uchafuzi wa hewa pamoja na athari zake ambazo dunia imeanza kuonja makali yake. Kilio hiki kinatokana na kuongezeka kwa kiwango cha moshi wenye sumu katika anga, na kuharibu mfumo mzima wa hali ya hewa. Athari zaidi zinaonekana katika utando wa 'ozone', ambao umetobolewa na hewa hizi za sumu. Kazi ya utando huu ni kuzuia mionzi ya jua yenye athari kutufikia moja kwa moja na kutuathiri. Athari ambazo dunia inazipata kwa sasa ni pamoja na ongezeko la joto duniani na kupungua kwa kiwango cha barafu katika milima, kupotea kwa baadhi ya jamii za mimea na wanyama kutokana na ongezeko hili la joto, ongezeko la magonjwa kama kansa na magonjwa mengine ya ngozi. Pia kuna maeneo ambapo utando wa moshi wa viwanda na magari ni mkubwa na hivyo husababisha mvua za tindikali. Mvua hizi hutokana na kuongezeka kwa hewa ya salpha dayoksaidi katika anga. Hewa hii ikizidi angani na kuchanganyikana na maji au unyevu hutengeneza tindikali ya salfarasi 'sulphorous acid', na hii ina madhara sana kwa mimea na wanyama. Tindikali hii huunguza majani ya mimea na kwa wanyama husababisha magonjwa ya ngozi. Kwa nchi za Ulaya ya Magharibi wanafahamu sana madhara ya mvua hizi za tindikali, kwani zimeharibu sana uoto wa asili. Kutokana na sababu hizi basi, kumekuwa na hatua mbali mbali za kupunguza hewa chafu katika anga, na moja ya hatua hizo ni kutumia mafuta mbadala ya kuendeshea mitambo badala ya mafuta ya jamii ya petroli.

MAFUTA MBADALA NI YAPI?
Msisitizo wa kutumia mafuta yasiyo na madhara sana kwa mazingira umekuwa ukipata kasi kadri siku zinavyosonga. Nchi zilizoendelea zimekuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na uzalishaji mkubwa wa mafuta haya mbadala. Mafuta haya yanatokana na mimea kama mbono, miwa, michikichi, alizeti, maharage ya soya na mahindi. Kimsingi kila mmea una uwezo wa kutoa mafuta haya, kulingana na hali ya kiteknolojia iliyopo mahali husika. Mimea tajwa hapo juu, ukiacha miwa na mahindi, hutoa dizeli ambayo nchi zilizoendelea zinatumia kuendeshea mitambo ya namna mbalimbali. Miwa hutoa kimiminika kiitwacho 'ethanol' na hii kutumika sana kuendeshea mitambo pia. 'Ethanol' ni jamii ya pombe inayotengenezwa kwa njia ya mvukizo au mvuke. Kwa jina lingine rahisi hii ni 'gongo' ya kiwandani. Ni nyepesi sana na inashika moto haraka, hivyo wataalamu wameona inafaa kwa mitambo. Kumbuka kuwa karabai zinawashwa kwa mafuta ya jamii hii.

WAZALISHAJI WA MAFUTA MBADALA
Kwa upande wa 'ethanol', wazalishaji wakubwa kwa soko la dunia ni Brazili na Marekani na walianza karibu miaka ishirini iliyopita. Hawa wanazalisha bidhaa hii kutokana na makapi ya viwanda vya miwa. Pia nchi za umoja wa Ulaya ni wazalishaji wakubwa wa bidhaa hii. Kwa upande wa dizeli ya mimea, wazalishaji vinara ni Malaysia, China na Ujerumani. Malaysia ni mzalishaji wa kwanza wa mafuta ya mawese duniani, na dizeli wanayotengeneza inatokana na mawese. Wachina wanatengeneza 'ethanol' kutokana na mihogo na wanapata shehena kubwa ya mihogo hii kutoka Vietnam, Thailand na Indonesia.
Kwa upande wa Brazili, kuna magari milioni tatu yanayotumia ethanol! Wakati huo huo kuna magari milioni moja na laki tatu yanayotumia mchanganyiko wa petroli na ethanol.
(Chanzo cha takwimu: UNIDO/Berkeley BC Aprili 2006)

FAIDA ZA MAFUTA MBADALA
Mafuta haya hayatoi moshi wenye athari kwa anga, kwa kuwa hayana viambata vyenye sumu, kulinganisha na mafuta ya jamii ya petroli. Mafuta ya petroli huchanganywa na madini ya risasi 'lead' na hivyo yakitumika katika mitambo hutoa moshi wenye sumu katika anga.
Kwa kuwa mafuta mbadala hutokana na mimea, huongeza kipato kwa wakulima wa mazao yatoayo mafuta haya. Utengenezaji wa dizeli mbadala hauhitaji teknolojia za hali ya juu sana, tofauti na mafuta ya jamii ya petroli, hivyo hata nchi zinazoendelea zinaweza kumiliki mitambo ya kuzalishia mafuta haya.

TANZANIA NA MAFUTA MBADALA
Kumekuwa na tafiti mbalimbali zinazofanywa na watu na taasisi anuwai nchini Tanzania, kuhakikisha kuwa kunakuwa na maendeleo katika uzalishaji wa dizeli ya mimea. Baadhi ya taasisi zilizofanya utafiti wa mafuta haya ni pamoja na shirika la Msaada wa Kiufundi la Ujerumani (GTZ), Kampuni ya Kukuza Teknolojia (KAKUTE) ya Arusha na Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Mazingira Tanzania (TaTEDO). Kwa upande wa KAKUTE, wao wanafanya uzalishaji mdogo wa dizeli inayotokana na mbono, pamoja na kutengeneza sabuni zake.
Iwapo kutakuwa na msisitizo kwa watu binafsi, mashirika na serikali katika kuzalisha mafuta haya, basi tutaondokana na umasikini, kwa sababu bidhaa hii kwa sasa ina malipo mazuri katika soko la dunia. Nasema hivi kwa sababu tayarai nchini Tanzania tuna viwanda kadhaa vya miwa ambavyo hutoa makapi mengi ya kuweza kuzalisha ethanol na wakati huo huo mimea ya mbono husitawi hata katika maeneo yenye ukame.
Ni kitu kinachowezekana, ila inataka utashi!
Nafasi yako katika hili unaitumia kikamilifu?
Jadili!

9/20/06

YAJUE MALENGO YA MAENDELEO YA MILENIA

UTANGULIZI
Ni mara nyingi tumesikia, ama kuambiwa kuwa kuna malengo ya milenia, lakini huenda si wengi wetu tunaoyafahamu malengo hayo. Ni malengo yaliyoafikiwa mnamo Septemba 8 mwaka 2000, jijini New York Marekani na kuazimia kuwa ifikapo mwaka 2015, basi hayo maazimio waliyopanga yawe yametekelezwa kwa kiasi fulani cha kuridhisha, kama si kuyatekeleza kabisa.
Kwa ujumla kuna malengo manane ambapo nitayaeleza yote kwa ufupi katika makala hii na kuelezea lengo namba saba katika makala yake ya kujitegemea. Nitafanya hivi kwa sababu si busara kuelezea lengo namba saba pekee wakati malengo mengine hayafahamiki. Vile vile ni kwamba kufanikiwa kwa lengo moja basi ni njia ya mafanikio ya kuyafikia malengo mengine pia. Malengo haya yamewekewa viashiria, kujua kama yanatekelezeka ama la! Tafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili ni yangu!

YAFUATAYO NI MALENGO YA MAENDELEO YA MILENIA
1. Kupunguza Umasikini Uliokithiri pamoja na Njaa
Ndani ya lengo hili kuna malengo madogo mawili. Kwanza ni kupunguza hadi kufikia nusu, kwa kwa idadi ya watu ambao wanaishi kwa chini ya kiwango cha dola moja kwa siku, kati ya mwaka 1990 na 2015. (Kwa wakati huu, dola moja ya Kimarekani ni karibu sawa na shilingi 1200 za Kitanzania). Pili, ni kupunguza kwa zaidi ya nusu kwa idadi ya watu wasio na chakula.

2. Elimu Ya Msingi Kwa Wote
Kuhakikisha kuwa hadi mwaka 2015 mahali popote pale, watoto, kwa maana ya wasichana kwa wavulana wawe na uwezo wa kuhitimu elimu ya msingi.

3. Kukuza Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Wanawake
Lengo ni kuondoa tofauti za kijinsia katika shule za msingi na sekondari hadi mwaka 2005 na katika nyanja zote kabla ya mwaka 2015.

4. Kupunguza Vifo Vya Watoto Wachanga
Lengo ni kupunguza kwa theluthi mbili, idadi ya vifo vya watoto walio katika umri wa hadi miaka mitano, kati ya mwaka 1990 na 2015.

5. Kuboresha Afya za Akina Mama
Lengo ni kupunguza kwa hadi robo tatu, idadi ya vifo vya wanawake wazazi, kati ya mwaka 1990 na 2015.

6. Kukabili Virusi Vya Ukimwi/Ukimwi na Magonjwa Mengine Makuu
Lengo la kwanza ni kupunguza na kuukabili Ukimwi na kubadili mwelekeo wake ifikapo mwaka 2015. Lengo la pili ni ni kukabili na kutokomeza malaria na magonjwa mengine makuu hadi kufikia mwaka 2015.

7. Kujihakikishia Uendelevu wa Mazingira
Hapa kuna malengo matatu madogo. Lengo la kwanza hapa ni kuingiza misingi ya maendeleo andelevu katika sera na mipango ya mataifa mbali mbali na kubadili mwelekeo na upotevu wa rasilimali. Lengo la pili ni kupunguza hadi nusu kwa idadi ya watu wasio na maji safi ya kunywa na huduma za maji taka. Lengo la tatu ni kuboresha makazi ya watu angalau milioni mia moja hadi kufikia mwaka 2020.

8. Kuanzisha Ushirikiano wa Kimaendeleo Duniani
Hapa kuna malengo mawili madogo. Kwanza, ni kujenga misingi ya utawala wa sheria na inayotabirika na isiyo na ubaguzi katika mifumo ya biashara na fedha. (Hii inahusisha pia kujifunga na misingi ya utawala bora, maendeleo na kupunguza umasikini, kitaifa na kimataifa). Pili, ni kuyapa kipaumbele mahitaji ya nchi masikini sana duniani (hii inahusisha kuondoa vikwazo katika masoko huru na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi. Pia kupunguza (ama kuondoa kabisa) madeni ya nchi hizi masikini na kutoa misaada kwa nchi ambazo zinaonyesha mwelekeo wa kuondoa umasikini).
Unaweza Kuyasoma zaidi Malengo hayo Hapa

Kwa hiyo ndugu msomaji wa makal hii, haya ndio malengo ya milenia yaliyoazimiwa mwaka 2000.
Katika makala ijayo, nitawaleteeni mjadala wa kiundani wa malengo kadhaa, tukianzia na lengo namba saba.

9/8/06

KIJANI, NJANO NA MAZINGIRA!

UTANGULIZI
Ndugu wasomaji wa blogu hii, leo naleta kwenu wazo jipya ama mjadala mpya. Kama kawaida yetu, ni jadi kuwa mtu akitoa wazo basi nasi tunapata wasaa wa kuchangia mawazo yetu, aidha kwa kuboresha ama kukosoa. Kwa hiyo basi, kwa leo nitaongelea rangi za kijani na njano, ambazo kwa siasa za nchi yetu si rangi ngeni hata kidogo, lakini leo ni siasa za kijani na njano katika upande wa mazingira.

MADA
Kwa wakereketwa wa siasa za nchi yetu, kijani na njano ni rangi za bendera ya chama tawala na pia ni mbili kati ya rangi nne za bendera ya taifa letu. Kwa ujumla rangi hizi kwa bendera zote mbili huwakilisha utajiri wa maliasili vikiwemo mimea, wanyama na madini yapatikanayo nchini mwetu. Huo ndio ufafanuzi uliowekwa yakini na serikali na chama kwa bendera hizo. Kwangu mimi, rangi hizi ni zaidi ya hapo, na humaanisha mambo mengine pia. Kwa wanachama wa chama tawala, wao huadhimisha kuzaliwa kwa chama chao kila mwaka tarehe tano mwezi wa pili. Aghalabu sherehe hizi huwa na shamra shamra nyingi zikiambatana na upokezi wa wanachama wapya na uzinduzi wa matawi mapya ya chama. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, chama tawala nchini mwetu kina idadi ya wanachama rasmi wasiopungua milioni tano, nje ya mashabiki. Si haba, kwa nchi ya vyama zaidi ya kumi vya siasa na watu milioni thelathini na tano.
Kwa maana hiyo basi, nafikiri katika shamra shamra hizi wanachama hawa hupata wasaa wa kubadilishana mawazo na kuelimishana. Ni bora pia wakaelimishana maana ya rangi za bendera za chama chao kama hawajaelezwa, hasa kwa wanachama wapya. Pia, ni bora wakaelimishwa matumizi sahihi ya rangi hizo.

WAZO
Iwapo kila mwaka katika tarehe tajwa hapo juu wanachama wangekumbushwa (au kuelimishwa?) namna ya kutunza ukijani popote pale walipo, basi katika suala zima la mazingira tungekuwa mbali sana. Hebu chukua mfano, kila mwanachama kati ya hawa milioni tano (acha mashabiki) alazimike kupanda miti miwili tu mahali panapostahili, katika kumaanisha ukijani wa bendera ya chama chake, basi kwa mwaka tunakuwa na miti milioni kumi! Si suala dogo wala porojo, na hii ni kwa siku moja tu kwa mwaka mzima. Ukichanganya na miti tunayopanda kila Januari, basi tungekuwa tunasikia kwa mbali sana suala la ukame na kukauka kwa vyanzo vya maji.
Lakini, hata si kwa kupanda miti, basi iwe ni kuokota taka na kuzihifadhi mahali panapostahili ili kutunza ukijani, nadhani bustani nyingi sana mijini zingekuwa kijani sana hadi sasa, badala ya kuzungushia uzio kila mahali penye bustani ili watu wasikanyage bustani zetu. Ni suala la elimu na utashi tu.

Kwani haiwezekani?
Jadili

8/31/06

TUJIFUNZE TOKA KWAO

UTANGULIZI
Mu hali gani wasomaji wa blogu hii?
Kama nilivyodokeza siku zilizopita, nipo kaskazini mwa dunia yetu, hususan nchini Norway. Kwa ujumla muda huu ndio majira ya joto yanamalizika kwa huku, muda si mrefu tutakabiliana na baridi na barafu.

HALI YA HEWA
Kwa kawaida, hapa mahali naambiwa na wenyeji kuwa mvua haina msimu maalum, inanyesha wakati wowote (nafikiri ni kwa sababu ya misitu mingi) na kuwa karibu na bahari. Kwa kawaida wakati wa baridi joto hushuka hadi nyuzi -28 hadi -32 kulingana na maeneo. Na kuna wakati fulani (kama sasa) jua linazama muda wa saa 2.30 hadi saa 3.30 usiku kwa saa za hapa. Na kuna maeneo ya kaskazini mwa nchi ambapo jua huwa halizami kabisa kwa baadhi ya miezi, kwa hiyo ni suala la kuangalia saa tu katika kufanya mambo yako. Kwa mfano, wakati nasafiri kwa ndege toka Uholanzi kwenda Oslo, ilikuwa saa 4 kasoro usiku na jua lilikuwa likiwaka!

UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Nchi hii ina watu milioni 5 tu na nadhani robo ya hawa ni wahamiaji, kwa hiyo maeneo mengi ni misitu na nyumba chache sana. Kwa maana hii basi, basi wengi hujazana katika miji mikubwa kama Oslo, Trondheim, Stavanger na Bergen, kwa hiyo uharibifu wa mazingira si kwa kiasi kikubwa. Hali kadhalika, nishati kubwa zitumikazo huku ni mafuta na umeme, ingawa kuni hutumika mara chache sana kwa ajili ya kuzalisha joto katika baadhi ya nyumba wakati wa majira ya baridi. Hata hivyo wengi hutumia mitambo ya kuzalisha joto itumiayo umeme. Ukataji miti upo, hasa miti ya kupandwa, kwa ajili ya kuzalisha mbao na bidhaa nyingine za namna hiyo, na ukiwa katika jiji hili utakutana na magari mengi tu ambayo yanapakia magogo kupeleka viwandani. Kwa ujumla, hawa watu wamedhibiti vumbi kwa kiasi kikubwa wakisaidiwa na hali ya hewa (mvua za mara kwa mara na misitu), tofauti na kwetu ambapo kuna vumbi kila karibu kila mahali. Kwa hapo Tanzania, naweza kufananisha mitaa ya huku na ile ya jiji la Dar es Salaam kama vile barabara ya Haile Selasie, Garden, Shaaban Robert na Magogoni, kwa maana ya kwamba njia zote zina lami, mpaka njia za waenda kwa miguu.
Kuna udhibiti mkubwa wa vyombo vya majini, hasa kuhusu umwagaji wa mafuta na taka nyingine. Kwa watu niliowahoji, wanasema kuwa kuna adhabu kali sana iwapo mtu atakutwa anatupa taka majini, kwa kuwa kuna maeneo mengi sana hapa mahali ya kukusanyia taka. Hata hivyo taka hizi hutengwa kulingana na aina zake, kwa maana ya kwamba, kunakuwa na mapipa kama matatu katika eneo moja. Haya hukusanya taka za namna mbalimbali kila pipa peke yake, yaani kuna pipa la makopo ya maji na bia, pipa la masalia ya vyakula na pipa la taka ngumu kama za plastiki. Pamoja na udhibiti huo bado kuna wavunja sheria vile vile, ambao hutupa taka mahali popote watakapo na hawajali lolote.

USAFIRI
Kuna mpangilio mzuri sana wa njia za usafiri hapa mahali, na hakuna misururu kama ile ya jiji kubwa hapo nyumbani. Kwa mfano, nyakati za asubuhi kunakuwa na treni katika njia (reli) zaidi ya kumi katika stesheni kuu ambazo husafirisha abiria kwenda miji mbali mbali katika kazi na nyingi ya hizi hupita chini ya ardhi kwa baadhi ya maeneo. Kila baada ya dakika zisizozidi 7 treni hutoka stesheni kuu kwenda mahali fulani. Kwa mfano, mimi naishi Oslo na nafanya kazi mji wa Lysaker, inanichukua dakika kama kumi na tatu tu kufika kazini, umbali kama wa kilometa 30 hivi. Hali kadhalika kuna treni zinazopita katikati ya jiji katika mitaa mbali mbali, hizi zenyewe ni kwamba, reli zake zimepitishwa katikati ya lami, kwa hiyo magari na treni huchangia njia. Hizi ni nyingi kuliko nilizotaja hapo juu. Hali kadhalika kuna mabasi mengi sana makubwa katikati ya jiji, yanayosafirisha watu kutoka na kuingia jijini Oslo. Naweza kusema hizi ndio dala dala za huku. Pamoja na uwingi huu, ukichanganya na magari binafsi hakuna misururu!

KWA NINI HAKUNA MISURURU?
Kwanza, mpangilio wa mji ni mzuri sana, kuna njia nyingi sana kwa hiyo haimlazimu mtu kupita njia moja na kuna njia nyingi ambazo hupita juu ya nyingine (fly overs) kama lilivyo daraja la Manzese, na kati ya hizi kuna nyingine ni ndefu kwa kilometa kadhaa. Hali kadhalika kuna barabara zipitazo katika mahandaki, nazo ni nyingi pia.
Pili, jiji la Oslo ni kwa ajili hasa ya makazi na ofisi chache muhimu. Kwa maana hiyo basi, viwanda vingi vipo nje ya jiji hili, ambapo huwalazimu wafanyakazi kusafiri toka jijini hapa kwenda nje ya jiji kikazi, kwa hiyo basi huu ni mfumo wa kwenda na kurudi (two way), tofauti na nyumbani, ambapo asubuhi na jioni misururu huwa ya namna moja (mara nyingi) hasa wakati wa kwenda na kurudi kazini.
Tatu, kuna kundi kubwa la watu ambao hutumia baiskeli kwenda kufanya kazi zao ndani na nje ya jiji. Na kusema kweli baiskeli ni nyingi mno hapa mahali (kama Tanga au Morogoro vile) hadi zinakuwa kero. Nafikiri ni nyingi kutokana na utambarare wa jiji na hali ya hewa ya baridi, kwa hiyo mtu hachoki sana. Hizi nazo husaidia sana kupunguza misururu barabarani (nilishawahi kuongelea suala hili katika baadhi ya makala zangu zilizopita).
Kuna mengi sana ya kuongelea lakini kwa leo naishia hapa.
Nitaendelea kutafiti mambo mengine zaidi na kuwajulisha.

Wao wameweza wana nini? Na sisi tushindwe kwa nini? Kuna nini katikati hapa?
Jadili.