11/24/06

USHAURI KUNTU KWA WAMILIKI WA MABASI!

UTANGULIZI
U hali gani msomaji wa safu hii. Katika makala zilizopita, niliwahi kugusia kidogo suala la uchafuzi wa mazingira hasa kwa mabasi makubwa ya masafa marefu, kuhusu utupaji wa taka kwa abiria wanaokuwa wakiabiri katika mabasi hayo. Leo nitafafanua kwa undani kidogo jinsi ya kufanya, ili kuweza kukabiliana na uchafuzi wa mazingira hasa kwa wenye mabasi. Ni ushauri tu, wana haki ya kuuchukua ama kuuacha, ni hiari yao lakini ni muhimu sana kama watauzingatia.

MADA
Katika makala niliyodondoa hapo juu katika utangulizi, nilisema kwamba ni kawaida kwa mtu yeyote anayesafiri kwa mabasi makubwa ya masafa marefu kukuta mifuko ya plastiki ikiwa imezagaa njiani, kando ya barabara hizi kubwa. Aghalabu mifuko hiyo hupatikana maeneo ambayo huwa hayana watu. Sasa huwa tunajiuliza nani huwa anatupa mifuko hiyo? Jibu ni 'Wasafiri' ama abiria. Ni jambo la kawaida sana kukuta katika kila basi kubwa la masafa marefu lina hifadhi ya mifuko ya plastiki ndani. Aghalabu mifuko hii hutumika kuwakinga baadhi ya abiria ambao hutapika njiani, labda kutokana na ugonjwa ama misukusuko ya gari wawapo njiani. Sasa basi, mara abiria wanapokuwa wamemaliza kutapika, hutupa mifuko hii nje ya basi kupitia madirishani. Vitendi hivi huchangia sana kuchafua mazingira, kwani mifiko hii ya plastiki ina athari sana kwa mazingira.
Hali kadhalika, nilijadili kuwa dakika kumi ambazo wenye mabasi hutoa kwa abiria kwa ajili ya kula na kujisaidia huwa hazitoshi. Hii ni kwa sababu, abiria hutumia muda kama dakika tatu mpaka tano kutoka nje ya basi waendapo kula. Sasa basi abiria wa mwisho kutoka katika basi husika kwa maana hii atatumia dakika tano zilizobaki kujisaidia, kupanga msitari katika kuagiza chakula, kula na kama inawezekana kwenda katika duka kununua maji ya kunywa. Katika hali ya kawaida, utaona kuwa muda huu hautoshi hata kidogo. Kwa hiyo basi abiria walio wengi hulazimika kubeba chakula katika mifuko na kwenda kula ndani ya gari. Matokeo yake, masalia ya vyakula pamoja na mifuko hutupwa nje ya basi na kuhatarisha mazingira. Hali kadhalika, iwapo mtu mwenye ugonjwa wa kuambukiza kama kipindundupindu ama homa za matumbo atatapika katika gari na kutupa matapishi nje ya basi, kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kusambaza ugonjwa huo katika maeneo ambapo matapishi hayo yanakuwa yametupwa. Hii ni hatari sana, ingawa sote tunaonekana kama tunafumbia macho tatizo hili. Nilitoa wito kuwa tuwaige watunza hifadhi wa mbuga ya wanyama ya Mikumi, mkoani Morogoro, huwa wanajitahidi sana kutoa elimu kwa abiria pamoja na kusafisha uchafu wote utupwao mbugani hapo. Kuna matangazo mengi sana mbugani hapo, yakisisitiza kutotupa taka ovyo katika mbuga hiyo.

USHAURI
Kwanza,ni vyema kama katika kila basi kukawa na sehemu ya kutunzia taka, kwa maana ya kwamba taka zote katika basi husika zikusanywe na kuhifadhiwa katika buti ya basi. Mara wafikapo kituoni, watumishi wa basi husika inabidi watupe taka hizi katika ghuba za kutupia taka ama mahali pengine palipoandaliwa maalumu kwa ajili ya kuhifadhi taka. Si ustaarabu hata kidogo kutupa taka ovyo njiani. Pili, inabidi ila basi liweke matangazo kuwajulisha abiria kuwa ni marufuku kutupa taka nje ya basi. Matangazo haya yaende sambamba na msisitizo wa kuwa na sehemu ya kuhifadhi taka katika basi, kwani kama hakuna sehemu ya kuhifadhi taka katika basi, unakuwa vigumu kwa abiria kutekeleza amri hizo. Tatu, kuwe na matangazo katika vituo vya mabasi haya kila mkoa, yanayohusu usafi kwa abiria wanapokuwa wakisafiri na mabasi hayo. Katika makala hii nimesisitiza sana suala la mabasi makubwa kwa sababu ndio yenye kuchafua sana njia zetu pamoja na mzingira kwa ujumla. Nne, serikali itunge sheria kali za kuwabana wamiliki ma watumishi wa mabasi kutotupa taka ovyo njiani na kwamba wawe na sehemu maalumu ya kuhifadhi taka katika mabasi.

Mbona wenye ndege wameweza, kwa nini hawa wamiliki wa mabasi wanashindwa?
Jadili

No comments: