11/27/06

EBPA- MFANO WA KUIGWA!

UTANGULIZI
EBPA ni ufupisho wa ’Environment- Based Poverty Alleviation’. Hii ni taasisi isiyo ya kiserikali ambayo kazi yake kuu ni ulinzi wa mazingira, lakini kwa namna ya pekee, kama ambavyo nitafafanua hapa chini. Taasisi hii ina makao yake makuu jijini Dar Es Salaam na inaongozwa na Bwana Charles Lugenga.

MALENGO YA TAASISI
Kwa mujibu wa Bwana Lugenga lengo kuu la taasisi hii ni kutunza mazingira kwa namna ya pekee, kwa kukusanya sehemu ya taka zilizotupwa na kutengeneza vitu vingine kwa matumizi mbali mbali. Taka ambazo hukusanywa kwa wingi ni kama makopo ya vinywaji baridi, makopo ya vinywaji vikali, chupa za maji pamoja na vizibo vyake, vitunza-takwimu (diskettes), kadi za simu zilizotumika, magurudumu machakavu ya magari, mifuko mikubwa ya nailoni (viroba) pamoja na nembo za bidhaa mbali mbali (labels) na kadhalika. Katika maelezo yake, Bwana Lugenga anasema kuwa pamoja na kwamba si rahisi kukusanya kila taka lakini angalau kwa kiasi fulani tunaweza kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kutumia tena, kupunguza ingi wa taka na kurejesha. Anasema kuwa katika taasisi yake wanatumia mfumo wa ‘R3’ yaani ‘Reduce, Reuse, Recycle’ kwa maana ya kupunguza ukubwa au uwingi wa taka, kutumia tena taka kwa matumizi tofauti na ya mwanzo na kurejesha. Anasema kwa mfumo huu, kiwango cha taka kinachotupwa katika mazingira yetu kinakuwa na athari kidogo sana, tofauti na iwapo kama taka hizo zingetupwa bila kupitia hatua hizo. Anafafanua kuwa, kwa mfano ukichukua makopo ya vinywaji ukayakata na kutengeneza mikoba ama vikapu hutumii sehemu zote za kopo ila sehemu ndogo tu. Sasa basi hapa umekuwa umepunguza ukubwa wa taka, kwa hiyo unakuwa umepunguza pia athari.

BIDHAA ZITOKANAZO NA TAKA
Kuna bidhaa mbali mbali ambazo EBPA wanatengeneza kutokana na taka. Bidhaa hizo ni mavazi kama makoti, mataji na kofia zilizotengenezwa kwa makopo ya vinywaji, nembo ama vitunza takwimu vilivyotumika na kadi za simu zilizotumika. Katika hali ya kushangaza Bwana Lugenga na taasisi yake wamejenga nyumba kwa magurudumu yaliyotumika katika jiji la Dar es Salaam katika eneo la Pugu. Kuhusu suala la nyumba hii ya magurudumu, anasema kuwa anafanya mawasiliano na watu wa Kitabu cha Kumbukumbu cha Guinness ili apate kuweka kumbukumbu ya nyumba hii kuwa ya kwanza ya aina yake kutengenezwa kwa magurudumu kuanzia chini mpaka katika paa. Pia ni kawaida kumkuta bwana Lugenga akiwa na ama mkoba au kikapu kilichotengenezwa kwa bidhaa tajwa hapo juu popote pale alipo, kwa hiyo hatengenezi bidhaa zake kwa maonyesho, ila kwa matumizi. Anasema kuwa, chupa za plastiki za maji ya kunywa huokotwa na kupelekwa katika kiwanda cha TIRDO kilichopo Msasani. Chupa hizi husagwa na kutumuka kutengenza bidhaa mbali mbali, na kuna wakati malighafi itokanayo na chupa hizi hupelekwa nje ya nchi ambako kuna soko zuri. Pia bidhaa kama madumu yaliyotumika hukusanywa na kupelekwa mahali hapo, husagwa na kurejeshwa viwAndani ambapo hutumika kwa kazi mbali mbali.


UREJESHAJI WA TAKA
Uwapo njiani kama unatokea Ubungo kwenda Mwenge kabla hujafika njiapanda ya kwenda Survey mkono wa kushoto, utakuta kundi la vijana wakiwa wamekusanya chupa za maji na bidhaa nyingine za plastiki. Licha ya mahali hapa, kuna maeneo mengine mengi tu ambapo vijana wamejiari katika ukusanyaji wa taka za namna hii. Bidhaa hizi hupelekwa katika Kiwanda cha kurejesha taka ambacho nimekitaja hapo juu. Nilitembelea kiwanda hiki mnamo mwezi Mei 2006 na kukuta bidhaa mbali mbali zikiwa katika hatua mbali mbali kuelekea katika urejeshwaji. Licha ya taka, bidhaa ambazo hazikutengezwa vizuri kutoka katika viwanda mbali mbali vinavyojihusisha na utengenezaji wa bidhaa za plastiki hupelekwa mahali pale ili kurejeshwa na kutengeneza bidhaa nyingine.
Inawezekana pia kuwa kuna taasisi mbali mbali zinazofanya kazi kama taasisi hii ya EBPA mahali mbali mbali nchini mwetu, ni vizuri iwapo tutawaunga mkono kwa namna anuwai ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kulinda mazingira.

Inawezekana, tutimize wajibu wetu

No comments: