Utangulizi
Ukiacha matumizi mengine ya maji kama kunywa na
kumwagilia mashamba, maji pia yamekuwa yakitumika kuendesha mitambo ya kusagia
nafaka (hydro mills) na mitambo ya kuzalishia umeme (hydroelectric power).
Matumizi ya maji kwa kuendeshea mitambo ya kusagia nafaka bado yanaendelea kwa
baadhi ya maeneo (nimeona Tanga na Kilimanjaro), ingawa kwa uchache, lakini uzalishaji wa umeme kwa kutumia
nguvu ya maji bado unaendelea kwa kasi. Kwa mada hii nitazungumzia matumizi ya
maji kwenye kuzalisha umeme, hasa kwa mazingira ya Tanzania. Kwa muktadha huu
mifano yangu mingi pamoja na picha zitakazotumika kwenye makala hii zitakuwa ni
za mitambo iliyopo ndani ya nchi, ambako ni rahisi kwa msomaji wa makala hii
kuitembelea na kujifunza. Sitajadili kwa undani sana masuala ya kiufundi ya
mitambo hii, sio lengo la makala hii, lengo nataka nijenge uelewa wa kawaida tu wa msomaji
namna umeme unavyozalishwa kwa nguvu ya maji.
Namna uzalishaji
unavyofanywa
Ili kukokotoa kiasi cha umeme utakaozalishwa kwa kiasi
fulani cha maji, kuna masuala kadhaa ya kisayansi ya kuzingatiwa, ili kupata matokeo yanayotarajiwa. Kanuni
inayotumiwa katika kukokotoa kiasi cha umeme utakaozalishwa ni P=Q*H*g, ambapo P ni ufupisho wa Power (nguvu ya umeme unaozalishwa, katika kilowati ), H
ni ufupisho wa Head (utofauti wa kimo kutoka maji yalipochotewa kwenye banio, mpaka mtambo
wa uzalishaji ulipo) na ‘g’ ni ufupisho wa acceleration due to gravity
(mgandamizo utokanao na nguvu za asili). Ili umeme uzalishwe, maji hutekwa
kwenye banio (intake) na kuingizwa katika bomba lenye kipenyo maalum (penstock)
kulingana na wingi wa maji. Kisha maji hayo kusafiri kwenye bomba kwa shinikizo
la nguvu ya uvutano hadi kwenye turbine, ambayo huzunguka na kuzungusha
jenereta ambao ndio hasa hufua umeme. Kuna turbines ambazo zimeunganishwa na
jenereta moja kwa moja na nyingine zimeungwanishwa kwa kutumia mikanda maalum au giaboksi. Mambo mengine muhimu yanayozingatiwa kwenye kuzalisha umeme huu ni ufanisi wa mfumo mzima (water-to-wire efficiency).
Wingi wa maji (Q)
Wingi wa maji (Q) yatakayopita mtamboni na kuzalisha umeme hupimwa kwa kiwango cha lita kwa
sekunde (l/s) au meta za ujazo kwa sekunde (m3/s). Kupima ujazo wa
maji kunasaidia katika kukokotoa kiasi cha umeme utakaozalishwa. Mitambo
inayotumika kubadili nguvu ya maji (potential energy) kuwa nishati mwendo
(kinetic energy) ina nafasi yake kwenye kukokotoa wingi wa umeme unaozalishwa
pia.
Kimo (H)
Kwa muktadha wa makala hii, kimo ni tofauti ya mwinuko
kutoka usawa wa bahari, kutoka kwenye banio (intake) maji yanapochotwa
kuelekezwa mitamboni na sehemu ulipo mtambo wa kubadili nguvu ya maji kuwa
nishati mwendo. Hio utofauti hupimwa kwa meta ama futi. Aina mbalimbali za
mitambo huhitaji kimo tofauti tofauti, kama itakavyofafanuliwa kwa ufupi hapo chini.
Nguvu ya uvutano,
acceleration due to gravity (g)
Hii ni ile nguvu ya uvutano kati ya anga na ardhi,
ndiyo inayofanya jiwe lirudi chini ukilirusha kwenda angani. Katika mifumo
mifumo ya uzalishaji umeme ninayoongelea hapa, maji yakishachotwa katika banio (intake), huelekezwa katika
bomba lenye kubwa maalum, kulingana na wingi wa maji, hadi kwenye mtambo wa
kufua umeme (turbine), kwa nguvu hii ya asili (gravitational force), hivyo maji
hayahitaji kusukumwa na nguvu nyingine yoyote. Nguvu hii ndio inayosababisha
uwepo wa shinikizo la maji kwenye bomba,
kuelekea kwenye turbine. Ni nguvu ya muhimu sana kwenye uzalishaji umeme kwa
njia ya maji.
Aina za Turbines
Turbine (wengine huita mifuo) ni mitambo ya kuzalishia
umeme ambayo huzungushwa kwa nguvu ya maji. Mitambo hii imegawanyika katika
aina mbali mbali. Mgawanyiko huu unatoka na tofauti za wingi wa maji
yanahitajika kuzungusha mtambo husika, kimo na eneo mahalia. Mitambo hii
haifanani kwa ukubwa kutoka na tofauti nilizoelezea hapo juu (wingi wa maji na
kimo). Kwa mantiki hii basi, kila mtambo husanifiwa kutokana na mahali
unapoenda kufungwa na pia kutokana na wingi wa maji na tofauti ya kimo. Ni mara
chache mno kukuta mitambo inayofanana ukubwa.
Francis turbines
Ni aina maarufu ya mitambo kwa hapa kwetu, kutokana na
ufanisi wake mkubwa unaofikia hadi asilimia 96. Mitambo hii imekaa katika
muundo wa mzunguko (spiral) na huweza kufungwa wima (vertical) ama kwa ulalo
(horizontal). Mitambo hii haihitaji maji mengi sana, ila inahitaji kimo kikubwa ili
kuongeza ufanisi na kuzalisha umeme mwingi. Kwa hapa Tanzania mitambo hii imefungwa na shirika la Tanesco Lower
Pangani, eneo la Hale wilayani Muheza mkoani Tanga (megawati 68), Mbalizi
mkoani Mbeya (kilowati 340) na Uwemba mkoani Njombe (kilowati 843). Mtambo mwingine wa aina hii upo kijiji cha Mawengi, wilaya ya Ludewa mkoani Njombe. Huu unamilikwa na
taasisi ya LUMAMA na una uwezo wa kuzalisha kilowati 300 kwa turbine mbili.
Vertical Francis Turbine - Uwemba Njombe (3x281 kw)
Horizontal Francis Turbine - Mawengi, Ludewa (2x150 kw)
Pelton turbine
Aina hii ya mitambo pia ni maarufu kwa hapa kwetu na
imekuwa ikitumika kwa mitambo mikubwa na midogo. Mitambo hii inahitaji kimo kikubwa
sana na maji kiasi kidogo. Aghalabu pelton inakuwa na bomba (jet) kati ya mbili na tano za kupeleka
maji kwenye pangaboi zake. Lengo la bomba hizi ni kupunguza ama kuongeza matumizi ya maji kadri ya mahitaji. Pia, turbine hizi huhitaji mwendokasi mkubwa
sana ili iweze kuzalisha umeme. Kwa Tanzania, mitambo hii imefungwa na Tanesco
eneo la Kihansi (megawati 180), imefungwa na Parokia ya Kabanga, wilaya ya
Kasulu mkoani Kigoma (kilowati 100).
Pelton turbine - Kabanga/Kasulu- Kigoma (100 Kw)
Cross flow turbine
Kiujumla hii ni mitambo midogo na hutumika kuzalisha
umeme wa kiasi kidogo, mpaka kilowati 200. Hutumia maji mengi sana, kwa sababu
mingi huwa na kimo kifupi (low head). Kwa hapa Tanzania mitambo hii imefungwa maeneo
yafuatayo: Uwemba mkoani Njombe, (kilowati 100), Heri Mission Kasulu, mkoani
Kigoma (Kilowati 100) na Lugarawa, wilayani Ludewa mkoani Njombe (kilowati 140).
Cross-Flow turbine - Lugarawa-Ludewa (140 kw)
Cross-flow turbine - Uwemba-Njombe (100 Kw)
Turgo turbine
Utendaji wa mitambo hii hauna tofauti sana na pelton,
ila mara nyingi mitambo ya aina hii huwa na jeti moja tu ya maji yanayoelekea
katika pangaboi zake. Katika pita pita zangu za kujifunza nimekutana na mtambo
moja tu wa aina hii, uliopo eneo la Dindira, wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. Ni
mtambo wa zamani sana, ulifungwa mwaka 1959 na Wakoloni wa Kiingereza, kwa
ajili ya kiwanda cha chai cha Dindira.Kwa sasa mradi huu umesimama kufanya kazi kutokana na uchakavu wa mitambo.
Turgo turbines Dindira, Korogwe- Tanga (2x206 kw)
Pump turbine
Hizi aghalabu ni pampu za kusukumia maji, ambazo
zimegeuzwa kinyume na kufanya kazi kama turbine zingine. Zina ufanisi wa chini
sana, ndio sababu hazitumiki mara nyingi. Katika maeneo ambayo nimepita na
kujifunza, nimekuta zinatumika sana kusagia nafaka, kwamba, badala ya wahusika
kufunga jenereta ya kuzalisha umeme, wao wanafunga kinu cha kusagia nafaka. Mfano mmojawapo wa
pampu inayofanya kazi ya kuzalisha umeme ni ile iliyopo kijiji cha Kinko,
wilaya ya Lushoto mkoani Tanga (kilowati 9). Pampu nyingine imefungwa kijiji
cha Mavanga, wilaya ya Njombe mkoani Njombe (kilowati 100).
Pump turbine, Mavanga-Njombe (100 kw)
Pump Turbine, Kinko, Lushoto-Tanga (9 kw)
Kaplan Turbine
Mfumo wa turbine hii unafanana kiasi fulani na ule wa
Francis, ingawa utendaji kazi wake uko tofauti. Turbine za Kaplan zinatumia
maji mengi sana na kimo kifupi, tofauti na aina nyingine za turbine, hivyo huhitaji kimo kifupi
tu (wakati mwingine hata meta 2 tu), ili kuzalisha umeme. Mojawapo ya turbine
za aina hii kwa hapa Tanzania imefungwa katika mradi wa umeme wa Bulongwa, wilayanai
Makete, mkoani Njombe, kwa ajili ya kutoa huduma ya umeme kwenye hospitali ya
Misheni ya Bulongwa (kilowati 180). Turbine nyingine ya aina hii imefungwa
katika mradi wa umeme wa Udeka, katika kijiji cha Matembwe wilaya ya Njombe mkaoni Njombe (Kilowati 150).
Kaplan turbine, Udeka Matembwe - Njombe (150 kw)
Ulinzi katika mifumo ya
uzalishaji umeme kwa njia ya maji
Kama ilivyo katika mitambo mingine, mitambo ya
kuzalishia umeme inakuwa na ulinzi anuwai ili kuepukana na majanga mbalimbali
kama vile mmomonyoko wa udongo (erosion), maporomoko ya ardhi (landslides),
mafuriko (floods), mpasuko wa mabomba ya kusafirishia maji (penstock rupture) na
ongezeko la mwendokasi katika mitambo.
Kwa hiyo basi, ulinzi katika mitambo hii huanzia katika mabwawa ambako
maji yanachepushwa kuingia katika mabomba hadi yanaposafirishwa na kufika
mitamboni.
Ulinzi wa mabwawa na mabanio
dhidi ya mafuriko na maji ya ziada
Kwenye usanifu wa mabwawa na mabanio, huwa kuna mbinu
kadhaa za kupitisha maji yanayozidi kimo cha bwawa ama banio. Juu ya ukuta wa
bwawa kuna pengo linaloachwa makusudi ili kupitisha maji yanayozidi, na kubakiza maji
yanayohitajika tu. Pengo hili kwa Kiingereza kujulikana kama ‘spillway’. Pia,
spillway husaidia kupitisha maji ya ziada kunapokuwa na mafuriko. Lakini
mafuriko yakizidi, kuna mageti maalum ambayo hufunguliwa ili kupitisha maji ya
mafuriko, ili kulinda kingo za bwawa zisimomonyoke. Katika mitaro ya
kusafirishia maji, kunakuwa na sehemu maalum (spillway) za kupunguzia maji
yanayozidi uwezo wa mtaro husika. Hii pia husaidia kulinda mtaro dhidi ya
mmomonyoko wa udongo wakati wa mafuriko.
Hilo pengo linaloonekana katikati ya kingo mbili ndio spillway
Spillway ya kwenye mtaro wa kusafirishia maji
Ulinzi wa mabwawa na mabanio
dhidi ya magogo , wanyama na mawe
Kwenye mabanio ama mabwawa kuna uwezekano wa
kusafirishwa mawe, magogo, takataka za aina anuwai na wanyama, kutokana na kusombwa na maji kutoka kwenye
vyanzo ama njiani. Kusipokuwa na udhibiti madhubuti kwa vitu hivi, kuna
uwezekano mkubwa vikaingia katika mabomba ya kusafirishia maji (penstock) na
kuziba mtirirko wa maji, ama kufika hadi katika ‘turbine’ na kuziharibu. Kuna
hatua kadhaa zinazochukuliwa ili kudhibiti takataka hizi. Katika sehemu ya
banio, hutengenezewa mfumo wa chujio ama chekeche (grate/mesh) kwa ajili ya
kuchuja taka na kuzuia mawe na magogo kupita. Huu mfumo husaidia kulinda
mabomba na mitambo mingine katika mfumo mzima wa uzalishaji umeme kwa njia ya
maji.
Chujio ya takataka
Ulinzi wa bomba la
kusafirishia maji dhidi ya mpasuko (rupture)
Bomba la kusafirishia maji kutoka katika banio hadi
mtamboni huwa linakua na mgandamizo mkubwa, kutoka na kimo na wingi wa maji.
Lina namna mbali mbali za ulinzi. Kwanza, huwa maji yanayopitishwa katika bomba
huwa yamepimwa uwingi wake, na kunakua na valvu ya kudhibiti wingi huo (gate
valves). Pili, mabomba mengi hufukiwa ardhini pale inapobidi, ili kudhibiti
mgandamizo huo. Tatu, mabomba huwa na kifaa cha kupumulia (ventilator) ili
kukabiliana na shinikizo kubwa la maji pale valvu za kwenye turbine zinapokuwa
zinafungwa kwa matengenezo ya turbine au kama kuna uharibifu unaotokana na kukwama kwa kitu ndani ya turbine. Haya yote kusaidia kudhibiti bomba
lisipasuke. Ukiachilia mbali hio vent, mabomba hasa ambayo yako juu ya ardhi
huwekewa valvu za usalama, ili kupunguza mgandamizo utokanao na nguvu ya maji.
Nne, vizuizi dhidi ya mbinuko wa mabomba(anchors) huwekwa pia ili kuzuia bomba
lisipinde pale linapozidiwa na shinikizo kubwa la maji.
Hizo nguzo zilizoshikilia bomba ndio 'anchors' nilizongeelea hapo juu
Hilo bomba jeusi lilipindia kulia ndio 'vent'
Ulinzi wa mfumo mzima dhidi
ya kujaa matope na mchanga
Katika baadhi ya maeneo, hasa yale yenye shughuli
nyingi za kilimo karibu na bwawa ama banio, kunakuwa na kiwango kikubwa sana
cha udongo kinachosombwa na maji na kuingizwa bwawani ama katika banio. Kwa
mifumo midogo ya uzalishaji umeme, kunakuwa na dimbwi dogo la kutuamisha tope (desilting
basin)na kuacha maji yakiendelea na mtirirko kuelekea mtamboni. Pia katika
bwawa lingiine dogo (forebay) huwa valvu maalum ya kutolea mchanga na matope
pale yanapokuwa yamejaa. Lakini katika mfumo wa mabwawa makubwa kunakua na
kifaa kijulikanacho kama ‘dredger’ kwa ajili ya kupunguza mrundikano wa tope na
mchanga kwenye bwawa.
Desilting basin
Forebay - Kinko, Lushoto-Tanga
Ulinzi dhidi ya
kuzidi/kupungua sana kwa mwendokasi wa turbine (over speeding/under speeding)
Kidhibiti mwendo(governor)
Kunapokuwa na matumizi madogo sana ya umeme kule
unakotumika, husababisha turbine kwenda kasi kuliko kawaida. Iwapo kasi hii
haitadhibitiwa basi kuna uwezekano wa kuharibu mitambo. Hali kadhalika iwapo
umeme unatumika kupita kiwango husababisha turbine kuzunguka polepole sana,
hivyo kupunguza mwendokasi na ufanisi. Ili kudhibiti hali hizi mbili, kifaa
kiitwacho gavana (governor) kufungwa sambamba na turbine ili kudhibiti mwendokasi
wake kulingana na mahitaji. Kifaa hiki hupokea mawasiliano ya mwendokasi kutoka
kwenye turbine na kurekebisha mwendokasi huo kutokana na mahitaji ya umeme wakati
husika. Kazi kubwa ya kifaa hiki ni kudhibiti mtiririko wa maji kuingia katika
turbine kadri ya mahitaji. Mahitaji yakiwa makubwa, gavana kufungua zaidi
valvu, hali kadhalika matumizi ya umeme yakipungua gavana kupunguza maji. Hali
kadhalika, iwapo mtambo utasimama ghafla, kifaa hiki hufunga kabisa mtirirko wa
maji ili kulinda turbine.
Kidhibiti mwendo (governor), Uwemba - Njombe
Kidhibiti mwendo (governor), Heri Mission Kasulu-Kigoma
Electronic Load Controller
Kwa mitambo ya kisasa sana, kuna kifaa kingine
kijulikanacho kama “Electronic Load Controller”, ambacho hufanya tofauti na
gavana, na ni cha kisasa zaidi. Kifaa hiki hakidhibiti mtiririko wa maji kama
gavana, ila kinadhibiti frequency na umeme unaotumika. Kunapokuwa na matumizi
makubwa ya umeme, frequency hupungua, hivyo kifaa hiki hupeleka mawasiliano
katika jenereta na jenereta huongeza mwendokasi ili kuendana na matumizi. Kunapokua
na matumizi madogo sana ya umeme, kifaa hiki huelekeza umeme wa ziada katika
vifaa maalum (ballast load/dump load), ili frequency ibakie ile ile
iliyopangwa. Hii ballast load mara nyingi zinatumika heater hizi tulizozizoea
kutumia majumbani kuchemshia maji, ila hizi huwa na uwezo mkubwa sana.
Electronic Load controller, Kinko, Lushoto-Tanga
Hitimisho
Umeme uzalishwao kwa nguvu ya maji umekuwa msaada
mkubwa sana kwa maendeleo ya taifa, tangu enzi za mkoloni. Ingawa enzi za
mkoloni mitambo ilikuwa midogo sana kwa ajili ya kukidhi matumizi ya taasisi za
kidini na chache za umma, serikali ya Tanzania ilijikita na kujenga mitambo
mkubwa zaidi na kusafirisha umeme kwenye gridi ya taifa ili kusambaza nchi
nzima. Bado kuna vyanzo vingi sana vya umeme huu mbayo havijaendelezwa,
kunahitajika juhudi za kuviendeleza ili kuleta maendeleo karibu zaidi na
wananchi.