FAHAMU
UMEME UTOKANAO NA PUMBA ZA MPUNGA NA MAGUNZI YA MAHINDI
UTANGULIZI
Najua
utashangaa sana kusikia kwamba pumba za mpunga au magunzi ya mahindi yanaweza
kuzalisha umeme na ukaendesha vifaa vyote unavyovijua wewe, ambavyo vinatumia
umeme, kama vile vinu vya kukoboa na kusaga nafaka, pasi, majiko ya umeme,
majokofu, taa, pangaboi n.k. Habari hii
ni ya kweli kabisa, na ni kazi ambazo nimekuwa nafanya kwa karibia nusu mwaka
sasa. Lakini pia umeme huu unaweza kuzalishwa hata kwa masalia makavu ya mazao mengine
kama vile pamba, korosho, tumbaku na nazi. Ili kupata umeme, lazima masalia
hayo ya mazao yawe makavu, angalau kwa asilimia 85 mpaka 90. Ili umeme
uzalishwe kwa kutumia masalia ya mazao, lazima kuwe na hatua kadhaa za
kipitiwa, kabla hatujapata umeme, kama ninavyofafanua hapa chini.
GASIFIER (TANURI LA KUCHOMEA PUMBA)
Hiki ni
kifaa (kama tanuri kubwa) kilichotengenzwa kwa chuma kigumu sana, ambacho hutumika kuchomea masalia ya mazao, katika
joto kubwa ambalo hufikia kiasi cha nyuzijoto zinazozidi 850. Katika uchomaji
huo, kiwango cha oksijeni kinachoingia katika tanuri hilo hudhibitiwa kwa kutumia tanki la maji ambalo lipo chini ya tanuri. Ni lazima kudhibiti kiwango cha oskijeni kinachoingia katika tanuri, ili pumba ziweze kuzalisha gesi inayowaka, kwa kufanya mwako usio kamili (incomplete combustion). Mchanganyiko wa hewa hizi zinazozalishwa katika mfumo huo ni
pamoja na Methane, Carbon dioxide, sulphur dioxide, carbon monoxide na mvuke. Baada
ya kuzalishwa, gesi hizo huchanganywa na maji katika mfumo maalum, ambapo
baadhi ya gesi hufyonzwa na maji, ikiwa ni pamoja na punje punje za pumba
zilizoungua. Gesi ya methane pamoja na carbon monixide kwa kuwa hazichanganyiki na maji basi huendelea na
safari kwenda kwenye hatua ya pili ya mchujo.
VENTURI
Huu ni
mfumo ambao hupokea gesi zenye joto kutoka kwenye cyclone, kisha hupooza gezi
hizo kwa njia ya maji na kuchuja gesi zisizotakiwa, ikiwemo mvuke, na kubakisha
methane na kiwango kidogo cha carbon monoxide kuelekea kwenye hatua ya nyingine ya mchujo. Masalia mengine katika hatua
hii ni pamoja na nta/lami (tar) ambayo hutengwa kwenye kifaa maalum ili isiendelee kwenye hatua za
uchujaji wa gesi unaofuata. Maji yaliyotumika kupoozea gesi huwekwa kwenye ndoo
maalum, kisha kurejeshwa katika tanki kuu ambao huhifadhi maji yanayotumika
mtamboni (tazama picha).
CYCLONE
Ni kifaa
chenye umbo la mviringo, ambacho hupokea gesi yenye joto kutoka kwenye venturi kwa lengo la kuipooza na kuondoa punje ndogo za pumba
iliyochomwa. Kwa jinsi ilivyotengezwa, punje punje za pumba hudondokea chini ya cyclone, pamoja na mvuke unaoendelea kupoa. Chini ya hii cyclone kuna valvu kwa ajili ya kutolea majimaji yatokanayo na mvuke uliopoa. Baada ya hatua hii, gesi husafirishwa hadi katika hatua
inayofuata, ambayo ni kwenye chujio ya kwanza.
CHUJIO YA
KWANZA
Chujio hii ni
ya umbo la mraba au mstatili, kwa ndani inakuwa
imegawanyika katika vyumba viwili, ambavyo vina uwazi kwa ndani, kwa ajili ya
gesi kupita, kutoka chumba kimoja kwenda katika chumba kingine. Chumba cha kwanza huwa kinawekwa mkaa, au pumba za mpunga zilizochomwa,
na chumba cha pili huwekwa pumba ambazo hazijachomwa. Kazi ya mkaa na pumba
hizi ni kunyonya mvuke, punje punje ndogo za pumba zinazokuja na gesi kutoka
kwenye cyclone. Chujio hii, kwa juu inakuwa na
dohani, ambayo hutumika kwa majaribio ya kuwasha gesi kuona kama imechujwa vya kutosha, kabla
haijapelekwa kwenye chujio ya mwisho na kwenye jenereta. Baada ya kuchujwa humu, gesi husafirishwa kwa bomba hadi katika
chujio ya pili. Chujio hii ya kwanza, kwa chini huwa na valvu ya kutolea maji, ambayo
aghalabu hutokana na mvuke uliopoa.
CHUJIO YA
PILI
Hii huwa ni
ya mviringo na kwa ndani upande wa juu huwa imewekwa kitambaa kigumu na pumba za mpunga zisizochomwa.
Kazi yake pia ni kuchuja zaidi gesi na kuondoa mvuke. Kwa upannde wa chini wa
chujio hii huwa na valvu pia, ya kuondolea maji yanayotokana na kupoa kwa
mvuke, utokanano na gesi ya joto inayopita hapo.
CHUJIO YA
TATU
Hii ina
umbo la mstatili na ni nyembamba kwa umbo. Kwa ndani, imetengezwa kwa vitambaa
viwili vigumu, ambavyo hutumika kuchuja gesi ili iweze kuingia katika jenereta.
Ni chujio ya mwisho katika mfululizo wa chujio hizi. Gesi ikishatoka katika
chujio hii huruhusiwa kuingia katika jenereta, kwa kutumia bomba la plastiki
lenye valvu maalum ya kuruhusu ama kuzuia gesi hii.
INJINI NA JENERETA
YA KUZALISHA UMEME
Injini
inayotumika kuendeshea jenereta ina ukubwa wa kilowati 32 na ina mzunguko wa
RPM 1500. Ijini hii huendeshwa kwa gesi iliyotokana na masalia ya mazao au
pumba za mbao. Gesi hii kabla haijachomwa katika injini huchanganywa na hewa
hii ya kawaida kwa kiwango cha 70/30. Hali kadhalika jenereta inayozalisha
umeme inakuwa na ukubwa wa kilowati 32, au wati 32,000. Kulingana na mahitaji,
injini na jereta inakweza kuwa chini ya hapo au juu ya hapo, ni matakwa ya
mhitaji kuamua ukumwa wa mfumo autakao. Jenereta hii inatosha kuzalisha umeme wa
kutumika kwa hadi nyumba 300 kwa vijijini, ambako matumizi ya umeme si makubwa sana. Kama nilivyoeleza hapo juu kwenye
utangulizi, vifaa vyote vya majumbani vinavyotumia umeme vinaweza kuendeshwa
kwa umeme huu.
HITIMISHO
Mitambo hii
ipo Tanzania, na imefungwa katika katika mikoa kadhaa na inazalisha umeme.
Mmoja umefungwa katika kijiji cha Nyakagomba, kata ya Nyakagomba wilaya ya
Geita vijijini, mkoa wa Geita (unatumia pumba za mpunga). Mtambo mwingine
umefungwa katika kijiji cha Kongwa, kata ya Mvuha, Morogoro vijijini (unatumia
pumba za mpunga). Mwingine umefungwa kijiji cha Malolo B, kata ya Malolo, wilaya
ya Kilosa, mkoa wa Morogoro. Mitambo mingine ambayo inaendelea kufungwa ipo kijiji
cha Mbaha, kata ya Mbaha wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, mwingine unafungwa kijiji cha
Kibindu, kata ya Kibindu, wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na mwingine unafungwa
kijiji cha Biro, kata ya Biro, wilaya mpya ya Malinyi mkoani Morogoro.
Gharama za mtambo huu, bila mfumo wa usambazaji umeme, kwa sasa ni dola elfu hamsini.
Nakaribisha maoni, ushauri na maswali.