NADHARIA YA
CENTRE – PERIPHERY NA GESI YA MTWARA
Utangulizi
Kuna
nadharia anuwai za maendeleo, kwa kadri nilivyofundishwa na walimu wangu wa
somo la maendeleo (Development Studies). Na kila nadharia ina uzuri wake
na ubaya wake, lakini kinachoamua uzuri ama ubaya wa nadharia hizo ni
UTEKELEZAJI. Iwapo utekelezaji wa nadharia husika ni mbovu, hata nadharia iwe
nzuri kiasi gani lazima kutakuwa na mapungufu.
Nadharia ya Center Periphery /Core-Periphery
Nadharia
hii imekuwa ikitumika kwa muda mrefu kuelezea uwiano hasi wa maendeleo kati ya
nchi zilizoendelea na zile zilizo nyuma kimaendeleo. Mfumo huo umetumika sana na
wanazuoni kama Samir Amin, A.G. Frank na Emmanuel Walerstine katika maandiko yao
kwenye kuelezea maendeleo kwa mtazamo huo. Walijikita zaidi kwenye nadharia za za maendeleo za wafikiari wakuu kama Karl Marx. Kwa ufupi ni kwamba nadharia hii
inaelezea mfumo usio sawa unaotokana na ubepari, katika mgawanyo wa rasilimali
na maendeleo ya dunia. Nadharia hii inaongelea maendeleo ya “NCHI” na nchi, mie
nimeamua kuishusha na kuihusianisha na “MKOA” na mkoa.
Nina
uhakika kwamba serikali imeamua kutumia nadharia ya (Center-Periphery), kwa
hili la Mtwara. Tuna uhakika 100% kuwa gesi ipo Mtwara, na sehemu ya gesi hiyo
ndiyo inayotumika Ubungo kwenye uzalishaji wa umeme. Sasa, iwapo tujenge
mfuo wa umeme Mtwara na kuusafirisha kwa nguzo za msongo mkubwa kwenda sehemu
nyingine za Tanzania ni uamuzi mmoja, na iwapo tusafirishe gesi kwa bomba na
kuipeleka Dar kisha tujenge mfuo wa umeme hapo ni uamuzi mwingine. Maamuzi ya mfumo
upi utumike yapo mikononi mwa tuliowapa madaraka, wakisaidiana na wataalamu wa
mipango.
Nadharia ya (Centre-Periphery) ina mtazamo wa kwamba kuna
baadhi ya maeneo (iwe ni mkoa, majimbo, wilaya ama kata), ambayo kazi yake ni
kuzalisha malighafi na kupokea bidhaa zitonakazo na malighafi hizo. Haiwezekani
kuweka viwanda vya kuchakata malighafi hizo maeneo hayo, kwa sababu hayo maeneo
"YATAFAIDI". Nadharia hiyo pia inaelezea kwamba maeneo mengine «yamegeuzwa»
ni ya kuchakata kila malighafi, hata kama malighafi hiyo haitoki hapo. Haya ni maeneo
ya viwanda tu, hata kama gharama za kusafirisha malighafi za viwanda hivyo ni
ghali sana, kwa hiyo ajira zote zitokanazo na viwanda lazima "ZIWE HAPO
TU". Kwa mujibu wa nadharia hii hii, maeneo mengine ni kwa ajili ya
kuzalisha wasomi tu, ili kusaidia kuchakata na kuuza bidhaa na huduma
zitokanazo na bidhaa zilizochakatwa. Sijajua Mtwara iko sehemu ipi hapo katika
hiyo nadharia ya CENTER-PERIPHERY, kiasi kwamba serikali haitaki kujenga mifuo
ya umeme na kusafisha gesi Mtwara wala kujenga barabara za kufika maeneo hayo.
Picha nimetoa kwa Issa Michuzi
Kwa nini Mtwara wanalalamika?
Viwanda vingi vipo Dar Es Salaam, japo Dar Es Salaam
haizalishi malighafi zinazosindikwa na kuchakatwa katika viwanda hivyo. Kiwanda
cha Sigara kipo Dar, pamoja na kwamba tumbaku inatoka Rukwa, Mbeya, Tabora na
kwingineko. Viwanda vya kuzalisha juisi za matunda vipo Dar, japo matunda
yanatoka mikoa anuwai kama vile Tanga, Iringa, Morogoro, Mbeya na Pwani. Viwanda
vya mafuta ya kula vipo Dar, ilhali chikichi na alizeti zinazalishwa nje ya
Dar. Uwiano huu usio sawa ndio unaozua malalamiko kwenye jamii, kiasi cha
kuleta maandamano yasiyokoma. Nahusianisha uwiano huu usio sawa wa maendeleo na
nadharia tajwa na gesi ya Mtwara. Serikali imeamua kufuata njia ya
Center-Periphery kwa kuwanyima wananchi wa Mtwara fursa za ajira zitokanazo na
mitambo ya kuchakata gesi na kufua umeme. Nisingependa kuingia kwenye mjadala
wa kiasiasa zaidi kwenye hili, kwa sababu tayari wanasiasa wameshalijadili kwa
undani. Je wananchi wa Mtwara walishirikishwa kwenye kuamua kujenga mifuo ya
umeme Dar. Tujadili