2/5/07

TUTAENDELEA NA UBISHI HUU HADI LINI?


UTANGULIZI
Katika kukabiliana na ukweli, wanasayansi wa mazingira pamoja na watafiti wengine wameungana na sehemu nyingine ya jamii katika kuthibitisha kuwa mabadiliko yasiyo ya kawaida ya hali ya hewa ikiwemo ongezeko la joto duniani husababishwa kwa asilimia tisini na kazi za binadamu katika kujitafutia riziki. Asilimia kumi inayobaki inatokana na mabadiliko ya kawaida ya mwenendo wa dunia kama vile matetemeko ya ardhi na volkano. Ripoti ya tafiti za wanasayansi hawa kutoka maeneo mbali mbali hapa duniani imetolewa mwezi huu wa pili 2007. Ni kwa mara ya kwanza katika historia ya utawala wake, mwaka huu ambapo rais wa Marekani alitaja suala la uchafuzi wa hali ya hewa, napo alitamka kwa sekunde chache sana suala hilo hata bila kugusia undani wa tatizo lenyewe na wala hakufafanua atakavyofanya kukabili kadhia hiyo.


HALI HALISI
Kitakwimu nchi zilizoendelea ndio zinaongoza kwa kuchafua hali ya hewa, kutokana na moshi toka viwandani, zikiongozwa na Marekani. Kwa mujibu wa kitengo cha nishati cha serikali ya Marekani, takwimu zinaonyesha kuwa, hadi mwaka 1999, Amerika ya kaskazini (Marekani na Kanada) ndio walikuwa vinara wa kuchafua anga kwa hewa ya kaboni, kwa kiwango cha meta za ujazo milioni 1,720.4! Waliofuatia kwa uchafuzi ni nchi za Ulaya Magharibi, kwa kiwango cha meta za ujazo milioni 988.9. Viwango vya uchafuzi kwa maeneo mengine katika mabano ni Ulaya Mashariki (851.8), China (821.8), Asia (ukiondoa China na Japan, 700.8), Japan (296.7), Amerika Kusini (234.7), Mashariki ya kati (252.1) na Afrika (213.8). Takwimu hizi ni hadi mwaka 1999, na kwa sasa inaonyesha kwamba Marekani ndio inaongoza kwa uchafuzi ikifuatiwa na China. Pamoja na ukweli huu, inasikitisha kuona kuwa Wachina na Wamarekani ni kati ya watu wa mwisho kujadili athari za ongezeko la joto duniani, kwa sababu kuu kwamba iwapo watatakiwa kupunguza hewa chafu angani, basi viwanda vyao vingi vitadhoofika na hatimaye uchumi wao utayumba.

KILIO CHA DUNIA
Kutokana na mabadiliko haya ya hali ya hewa, kumekuwa na makongamano na mikutano kadhaa ya kimataifa katika kutafuta suluhu ya kudumu ya uchafuzi wa anga, kama nilivyowahi kuongelea katika makala zilizopita. Mojawapo ya mikutano hiyo ni ule uliofanyika katika mji wa Davos nchini Uswisi mwezi huu Februari. Mataifa makubwa yalikuwa yanajadili kuhusu biashara na suala la uchafuzi wa hali ya hewa likaibuka hapo. Katika mkutano huo pia, dunia ilimshangaa mkuu wa kampuni ya Nestle inayotengeneza vyakula, Bw Peter Brabeck-Letmathe aliposema kuwa suala la ongezeko la joto halina uzito wowote kwa sasa! Pia wakamshangaa mpinzani wa Bush kisiasa, Bw Al gore katika filamu yake ambapo anapinga suala la ongezeko la joto. Al Gore yeye anasema kuwa pesa zinazotumika sasa katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani kupitia makubaliano ya Kyoto (ambapo Marekani haijatia saini) zingetumika katika kuboresha mindombinu ya maji pahala mbali mbali! huyu alikuwa mgombea uraisi ambaye alishindwa na Bush mnamo mwaka 2000.
Sina uhakika kama hawa watu walimaanisha kile ambacho waliongea ama walikuwa wanatania, lakini kwa sababu ni wafanyabishara nadhani walimaanisha kuwa hawana mpango kabisa wa kukabili tatizo hili la ongezeko la joto. Sasa mimi ninauliza, ubishi huu tutaendelea nao hadi lini?
Unaweza kusoma habari zaidi a mkutano huo hapa, hapa na hapa.

1 comment:

Unknown said...

moral values hapa duniani sasa hivi ni kama hazipo,sasa hivi kuna bessiness values au money values.hizo nchi zinazoongoza kwa kuchafua hali ya hewa ndio zinaongoza kwa uzalishaji wa sigara.idadi kubwa ya vifo katika nchi hizo husababishwa na magonjwa yanayosababishwa na uvutaji sigara.wanasiasa haohao,kwa kuogopa kushuka kwa mapato na kukosa support ya wafanyabiashara wakubwa wameamua kulifumbia macho tatizo hilo.nionavyo mimi,ubishi wa mataifa haya utaendelea mpaka pale kutakapoibuka mataifa yatakayojibunia mbinu nyingine ya kunufaika na uharibifu unaosababishwa na mataifa ya magharibi.watashindwa kuvumilia,wataanza kujadili wenyewe.