11/24/06

MALENGO YA MAENDELEO YA MILENIA - 2: LENGO NAMBA SABA

UTANGULIZI
Katika makala zilizopita niliongelea malengo ya milenia ambayo kwa ujumla wake yapo nane, pia niliahidi kujadili lengo namba saba kwa undani na wasaa huo ni sasa. Lengo hili kwa Kiingereza limeandikwa ‘Ensure Environmental Sustainability’. Kwa tafsiri yangu katika Kiswahili nasema ‘Kuzingatia Uendelevu wa mazingira’. Katika ufafanuzi wake, walioandika lengo hilo wanasema lazima tuingize suala la mazingira katika mfumo wetu wa maendeleo endelevu katika sera na mipango ya nchi zetu na kurejesha rasilmali katika mfumo wake wa asili. Hii ina maana ya kwamba katika suala zima la maendeleo, huwezi kukwepa suala la mazingira, ndio sababu likapewa umuhimu wa pekee katika muktadha wa malengo ya milenia. Kwa ujumla wake, mazingira ni vitu vyote vinavyomzunguka mwanadamu. Ni mara nyingi sana katika shughuli zetu za uzalishaji mali tumekuwa tukichukua rasilmali nyingi katika mazingira yetu bila kurejesha kwa kiasi Fulani kama ninavyofafanua hapa chini.

1. ARDHI
Ardhi ndio mama wa kila kitu kiasi kwamba wataalamu tukaamua kuiita ‘Mother nature’. Bila ardhi hakuna maisha. Tumekuwa tukichukua rasilmali nyingi sana katika ardhi, mara nyingine bila kuzingatia uendelevu wake. Tunachukua mimea, wanyama, maji na madini bila kuchukua tahadhari za kimazingira na kujali madhara yajayo baada ya hapo. Madini yaliyo mengi yanapatikana ardhini na namna pekee ya kuyapata ni kuyachimba toka humo ardhini yalimo. Lakini kwa utovu wetu wa nidhamu tunaacha kufukia mashimo na kurejesha sehemu ya mimea na wanyama walioondolewa mahali hapo kwa makusudi. Tunamkomoa nani? Kwa mtazamo wangu sidhani na sipendi kuamini kuwa tunakuwa hatufahamu tunachokifanya. Matokeo ya madhara haya tunayapata hapa hapa, kwani kumekuwa na upungufu wa maji maeneo mbali mbali duniani, kwani katika shughuli zetu tunaharibu mzunguko wa maji. Pia kumekuwa na upotevu wa viumbe hai sehemu nyingi tu. Kwa kawaida ardhi, mimea na maeneo yenye unyevu yapatapo joto na mwanga wa jua hupumua.Katika kupumua huku mvuke huo huenda angani na kuganda na kufanya mawingu ambayo baadaye hurudi ardhini kama mvua, theluji, barafu na mzunguko huendelea. Sasa basi iwapo sehemu fulani ya mzunguko huu itaathirika kwa namna moja au nyingine basi athari hizi zitasambaa hata katika sehemu nyinginezo za mzunguko huu. Hivi ndivyo mfumo mzima ulivyo. Suala la kilimo pia ni la kuangaliwa. Kumekuwa na matumizi makubwa sana ya mbolea za viwandani katika shughuli za kilimo, hasa katika nchi zinazoendelea. Mbolea hizi,kwa namna moja au nyingine zinachosha sana ardhi, kiasi kwamba baada ya muda fulani ardhu husika inakuwa haina uwezo tena wa kuzalisha mazao mengi kama mwanzo. Wao wenyewe wanaotengeza mbolea hizi wanazipiga vita kwa sasa, sasa sijajua wanamtengenezea nani. Wameshajua kuwa zina madhara, hivyo wanataka kutumia mbolea asilia tu mashambani kwao. Kwa hiyo basi na sisi inabidi tubadilike na kutumia mbolea zinazotengenezwa kiasili kama samadi na mboji ili kulinda ardhi yetu. Licha ya mbolea, suala la kulima milimani ni la kuangaliwa, kwani husababisha mmomonyoko wa ardhi iwapo mvua itanyesha katika maeneo haya. Kuna tovuti kadhaa zimeelezea kinagaubaga suala hili pamoja na lile la kuzidisha idadi ya mifugo katika eneo dogo na kuzidisha madhara katika eneo husika, vitendo ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu ardhi na mazingira kwa ujumla. Kwa hiyo sitayaongelea kwa undani sana masuala haya. Inafaa tu kuyaachia majanga ya asili kama vile volkano na matetemeko ya ardhi yaharibu uasilia wa ardhi, na siyo sisi wanadamu kuiharibu kwa makusudi, kwani kwa kufanya hivyo tunajichimbia kaburi.

2. MAJI
Kumekuwa na kauli mbiu kuwa ‘Maji ni Uhai’. Hakuna ubishi katika hili, bila maji hakuna uhai. Lakini je rasilmali hii tunaitumiaje? Sidhani kama tunafanya juhudi za kutosha katika kuhakikisha kuwa tuna matumizi endelevu ya rasilmali hii. Kwanza, katika kilimo huwa tunatumia mbolea za viwandani. Mbolea hizi si zote huchukuliwa na mimea kwa ajili ya utengenezaji wa chakula. Sehemu ya mbolea hupotelea ardhini na kuchafua hifadhi ya maji katika miamba ijulikanayo kama ’aquifers’. Kitendo hiki kwa lugha ya kitaalamu hufahamika kama ’Leaching’. Hatuwezi kuona kwa macho kwa sababu kitendo hiki hufanyika chini ya ardhi, kwa hiyo huhitaji vipimo vya kitaalamu kujua madhara yake katika maji na maisha ya wanadamu kwa ujumla. Katika kilimo hicho hicho, dawa za kuulia magugu na wadudu waharibifu wa mazao mashambani pia huchangia madhara katika maji kwani dawa hizi mara nyingi huenda katika maji iwapo mvua itanyesha katika mashamba yaliyowekwa dawa hizi. Pili, maji ya bahari ndio yamekithiri kwa uchafu, na ndio humo humo tunapata samaki kwa ajili ya kitoweo. Maji machafu ya miji yote ambayo iko kando ya bahari huishia baharini, maji taka ya viwanda ambavyo hupakana na bahari hali kadhalika huishia baharini. Taka za sumu toka viwandani humwagwa baharini. Hali hii pia iko katika maziwa na mito, ingawa si kwa kiasi kikubwa sana kama baharini. Inasemekana kuwa kwa nchi zinazoendelea kama yetu, baadhi ya wavuvi hutumia mabomu katika shughuli zao za uvuvi. Kitendo hiki si tu kwamba kinaua mazalia ya samaki, bali pia ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa maji. Baruti itengenezayo mabomu ni kemikali yenye sumu, sasa basi iwapo itachangayikana na maji, basi sumu hizi huturudia sisi wenyewe aidha kwa kula samaki waliovuliwa kwa mabomu au kwa kunywa moja kwa moja maji hayo. Lakini kwa tamaa zetu za kupata pesa za haraka, tunasahau madhara ya muda mrefu kama haya na kuishia kushibisha matumbo yetu kwa uvuvi wa mabomu. Tatu, kuna ujenzi na kilimo katika vyanzo vya maji. Kama tunayofahamu, vyanzo vya maji ni muhimu kwa maisha yetu, kwa hiyo iwapo tunachafua hatumkomoi mtu, ila ni sisi wenyewe. Nimeliongelea kwa urefu sana suala hili katika makala zilizopita. Katika hali ya kawaida, inatakiwa tuyasafishe maji yaliyotumika majumbani na viwandani ili yaweze kutumika tena kwa shughuli nyingine, lakini tulio wengi hatuna utaratibu huu. Laiti kama tungezingatia suala hili basi uhaba wa maji kwa maeneo mbali mbali ingekuwa ni hadithi tu. Pia hatuna utaratibu wa uvunaji wa maji ya mvua, kwa maeneo mengi ya nchi zinazoendelea. Maji yanayopotea wakati wa mvua ni mengi sana, iwapo tungeyavuna na kuyahifadhi basi tungetatua suala la uhaba wa maji ambalo ni kubwa sana sehemu mbali mbali duniani. Nne, kama itakumbukwa, hivi karibuni wakati nchi ya Israeli ikiwa katika mgogoro na Lebanon, ilipasua kwa makusudi bomba la mafuta kando ya bahari na mafuta yote yaliyokuwa yanasafirishwa katika bomba hilo yakasambaa baharini na kuua viumbe wengi sana wanaotegemea maji hayo ya bahari. Hali hii ilileta usumbufu pia kwa vyombo vinavyosafiri majini katika maeneo hayo. Kitendo hiki ni cha kulaaniwa sana na kila mtu ambaye anajali usafi wa bahari na mazingira kwa ujumla, lakini cha ajabu hakuna hatua za kinidhamu zinazochukuliwa kukomesha tabia hii.


3. HEWA
Madhara ya uchafuzi wa hewa ni rahisi sana kusambaa kwa muda mfupi katika dunia hii. Hii inatokana na sababu kuwa hewa husafiri haraka sana hasa pale inapopata joto. Si ajabu basi iwapo hewa itachafuliwa katika bara fulani na madhara yakajiri katika bara lingine kwa muda mfupi sana. Tumesikia na kuona madhara ya uchafuzi wa hewa, hasa kuharibika kwa hewa ya ’ozone’. Niliongelea kwa kirefu suala hili katika makala zilizopita. Ikumbukwe kuwa kuna makubaliano yalifanyika katika mji wa Kyoto nchini Japan hasa kwa nchi tajiri, kuhusu kupunguza kiwango cha hewa zenye sumu toka viwandani kwenda angani. Hizi ni nchi za G8 zenye viwanda vingi na vikubwa ambavo huchafua sana hali ya hewa, hivyo ilikuwa ni hatua muhimu sana katika suala ziama la kutunza mazingira. Kama kawaida, Wamarekani hawakusaini mkataba huu wa makubaliano, kwa madai kwamba kusaini mkataba huo ni kukubali kuua uchumi wao ambao hutegemea sana viwanda hivyo. Wakaitwa tena nchini Afrika Kusini, wakakataa kwa mara nyingine tena kusaini mkataba huu. Kwa mara nyingine mwaka huu 2006, mwezi wa kumi na moja wamekataa tena kusaini mkataba huo na kurudisha nyuma kabisa juhudi za kupunguza uchafuzi wa hewa. Nchi nyingine zenye viwanda vingi kama Japan, Sweden, China, Ujerumani, Urusi na Denmark wameshaanza kupunguza kwa kiwango cha kuridhisha, uchafuzi wa hewa.

MIKAKATI ENDELEVU
Kuna mambo kadhaa ambayo yanapaswa kuzingatiwa iwapo tunataka kupata matokeo mazuri ya ya kile tunachokipanga.

SIASA DHIDI UTAALAMU!
Kwanza, tupunguze kama si kuacha kabisa kutatua matatizo ya kiufundi kwa mbinu za kisiasa. Pamoja na kwamba siasa inatawala maisha yetu ya kila siku, lakini si matatizo yote yanaweza kutatuliwa kisiasa. Suala la uchafuzi wa hali ya hewa ni la kiufundi, sasa iwapo tunataka kutatua suala hili kwa mbinu za kisiasa ni makosa makubwa sana kwani masilahi ya kisiasa ni ya muda tu. Matatizo kama njaa, ukosefu wa umeme, ukimwi, ukosefu wa maji, uharibifu wa rasilmali na ukosefu wa maadili ni matatizo ya kiufundi, hayapaswi kutatuliwa kisiasa. Yatatuliwe kiufundi kwani naamini kuna wataamu wengi tu wa utatuzi wa matatizo haya, wapewe nafasi. Umbumbumbu (au ni ubabe?) wa Marekani kukataa kusaini mkataba wa Kyoto wa kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa inatakiwa ukemewe na kila mtu anayependa maendeleo ya muda mrefu na si maslahi ya kisiasa. Nasisitiza tena kuwa siamini wala sifikiri kuwa Wamarekani hawajui wanachokifanya katika hili suala la Kyoto. Nina imani kuwa huenda suala hili likapewa umuhimu wa kipekee na wale waliochukua madaraka nchini humo hivi karibuni, tuvute subira.

MAZINGIRA KWANZA, PESA BAADAYE!
Pili, ningependa kuongelea suala la mirahaba ya madini. Kumekuwa na maelezo mbali mbali kutoka kwa wadau wa madini kuwa tunalipwa mirahaba kutokana na madini yanayochimbwa nchini mwetu. Ni sawa kuwa tunapata mirahaba lakini vipi maslahi ya uhai wa hapo baadaye? Kama nilivyoongelea hapo juu, tusiangalie suala la pesa ambalo ni la muda mfupi ila tuangalie matokeo ya kuacha mahandaki katika machimbo ya madini. Nini kitatokea katika miongo kadhaa ijayo iwapo hali itaendelea kuwa kama hivi? Nani ataathirika? Wanaochimba madini sasa kwa teknolojia za kisasa zisizojali mazingira na uhai wetu watakuwa wameshaondoka na faida na kutuachia mashimo ambayo hayatakuwa na msaada wowote kwa wakati huo ambao vizazi vitakavyokuwepo (huenda hata sisi ) vitakuwa havina maji wala miti. Tuige mfano wa hatua zilizochukuliwa katika kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira , kutokana na uchimbaji wa madini katika msitu wa Balangai wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Sipendi kuonekana naingilia masilahi ya baadhi watu katika jamii kwa kupinga uchimbaji wa madini, lakini naongelea suala hili katika muktadha wa kitaalamu zaidi. Watakaopenda kuongelea suala hili katika muktadha wa kiuchumi wanaruhusiwa pia. Unafikiri ni kwa nini hao wanaotaka kuchimba madini katika nchi yetu hawaendi nchi zingine zenye madini kama sisi? Suala ni kwamba nchi hizi wana sera na sheria endelevu sna kuhusu mazingira.

UTASHI WA KISIASA
Kutatua matatizo yanayoikabili dunia kwa sasa kunahitaji utashi wa kisiasa na si utatuzi wa kisiasa. Katika kutekeleza malengo ya milenia, kinachotakiwa zaidi ni utashi huu ninaouongelea, kwani kwa utashi matatizo haya yanatatulika kabisa. Mpaka sasa inasemekana kuwa hazijaonekana juhudi za makusudi katika kutatua matatizo yaliyoanishwa katika malengo ya milenia, kiasi kwamba huo mwaka 2015 wa matazamio huenda mengi kati ya malengo hayo yasiwe yametimizwa. Wewe masomaji wa makala hii pamoja na mimi inapaswa tutimize wajibu wetu katika kuyafanikisha malengo haya, kwani inawezekana kabisa kuyafikia.
Soma hapa kwa habari zaidi.