10/11/06

MAFUTA MBADALA

UTANGULIZI
Kumekuwa na kilio sehemu mbali mbali duniani kuhusu uchafuzi wa hewa pamoja na athari zake ambazo dunia imeanza kuonja makali yake. Kilio hiki kinatokana na kuongezeka kwa kiwango cha moshi wenye sumu katika anga, na kuharibu mfumo mzima wa hali ya hewa. Athari zaidi zinaonekana katika utando wa 'ozone', ambao umetobolewa na hewa hizi za sumu. Kazi ya utando huu ni kuzuia mionzi ya jua yenye athari kutufikia moja kwa moja na kutuathiri. Athari ambazo dunia inazipata kwa sasa ni pamoja na ongezeko la joto duniani na kupungua kwa kiwango cha barafu katika milima, kupotea kwa baadhi ya jamii za mimea na wanyama kutokana na ongezeko hili la joto, ongezeko la magonjwa kama kansa na magonjwa mengine ya ngozi. Pia kuna maeneo ambapo utando wa moshi wa viwanda na magari ni mkubwa na hivyo husababisha mvua za tindikali. Mvua hizi hutokana na kuongezeka kwa hewa ya salpha dayoksaidi katika anga. Hewa hii ikizidi angani na kuchanganyikana na maji au unyevu hutengeneza tindikali ya salfarasi 'sulphorous acid', na hii ina madhara sana kwa mimea na wanyama. Tindikali hii huunguza majani ya mimea na kwa wanyama husababisha magonjwa ya ngozi. Kwa nchi za Ulaya ya Magharibi wanafahamu sana madhara ya mvua hizi za tindikali, kwani zimeharibu sana uoto wa asili. Kutokana na sababu hizi basi, kumekuwa na hatua mbali mbali za kupunguza hewa chafu katika anga, na moja ya hatua hizo ni kutumia mafuta mbadala ya kuendeshea mitambo badala ya mafuta ya jamii ya petroli.

MAFUTA MBADALA NI YAPI?
Msisitizo wa kutumia mafuta yasiyo na madhara sana kwa mazingira umekuwa ukipata kasi kadri siku zinavyosonga. Nchi zilizoendelea zimekuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na uzalishaji mkubwa wa mafuta haya mbadala. Mafuta haya yanatokana na mimea kama mbono, miwa, michikichi, alizeti, maharage ya soya na mahindi. Kimsingi kila mmea una uwezo wa kutoa mafuta haya, kulingana na hali ya kiteknolojia iliyopo mahali husika. Mimea tajwa hapo juu, ukiacha miwa na mahindi, hutoa dizeli ambayo nchi zilizoendelea zinatumia kuendeshea mitambo ya namna mbalimbali. Miwa hutoa kimiminika kiitwacho 'ethanol' na hii kutumika sana kuendeshea mitambo pia. 'Ethanol' ni jamii ya pombe inayotengenezwa kwa njia ya mvukizo au mvuke. Kwa jina lingine rahisi hii ni 'gongo' ya kiwandani. Ni nyepesi sana na inashika moto haraka, hivyo wataalamu wameona inafaa kwa mitambo. Kumbuka kuwa karabai zinawashwa kwa mafuta ya jamii hii.

WAZALISHAJI WA MAFUTA MBADALA
Kwa upande wa 'ethanol', wazalishaji wakubwa kwa soko la dunia ni Brazili na Marekani na walianza karibu miaka ishirini iliyopita. Hawa wanazalisha bidhaa hii kutokana na makapi ya viwanda vya miwa. Pia nchi za umoja wa Ulaya ni wazalishaji wakubwa wa bidhaa hii. Kwa upande wa dizeli ya mimea, wazalishaji vinara ni Malaysia, China na Ujerumani. Malaysia ni mzalishaji wa kwanza wa mafuta ya mawese duniani, na dizeli wanayotengeneza inatokana na mawese. Wachina wanatengeneza 'ethanol' kutokana na mihogo na wanapata shehena kubwa ya mihogo hii kutoka Vietnam, Thailand na Indonesia.
Kwa upande wa Brazili, kuna magari milioni tatu yanayotumia ethanol! Wakati huo huo kuna magari milioni moja na laki tatu yanayotumia mchanganyiko wa petroli na ethanol.
(Chanzo cha takwimu: UNIDO/Berkeley BC Aprili 2006)

FAIDA ZA MAFUTA MBADALA
Mafuta haya hayatoi moshi wenye athari kwa anga, kwa kuwa hayana viambata vyenye sumu, kulinganisha na mafuta ya jamii ya petroli. Mafuta ya petroli huchanganywa na madini ya risasi 'lead' na hivyo yakitumika katika mitambo hutoa moshi wenye sumu katika anga.
Kwa kuwa mafuta mbadala hutokana na mimea, huongeza kipato kwa wakulima wa mazao yatoayo mafuta haya. Utengenezaji wa dizeli mbadala hauhitaji teknolojia za hali ya juu sana, tofauti na mafuta ya jamii ya petroli, hivyo hata nchi zinazoendelea zinaweza kumiliki mitambo ya kuzalishia mafuta haya.

TANZANIA NA MAFUTA MBADALA
Kumekuwa na tafiti mbalimbali zinazofanywa na watu na taasisi anuwai nchini Tanzania, kuhakikisha kuwa kunakuwa na maendeleo katika uzalishaji wa dizeli ya mimea. Baadhi ya taasisi zilizofanya utafiti wa mafuta haya ni pamoja na shirika la Msaada wa Kiufundi la Ujerumani (GTZ), Kampuni ya Kukuza Teknolojia (KAKUTE) ya Arusha na Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Mazingira Tanzania (TaTEDO). Kwa upande wa KAKUTE, wao wanafanya uzalishaji mdogo wa dizeli inayotokana na mbono, pamoja na kutengeneza sabuni zake.
Iwapo kutakuwa na msisitizo kwa watu binafsi, mashirika na serikali katika kuzalisha mafuta haya, basi tutaondokana na umasikini, kwa sababu bidhaa hii kwa sasa ina malipo mazuri katika soko la dunia. Nasema hivi kwa sababu tayarai nchini Tanzania tuna viwanda kadhaa vya miwa ambavyo hutoa makapi mengi ya kuweza kuzalisha ethanol na wakati huo huo mimea ya mbono husitawi hata katika maeneo yenye ukame.
Ni kitu kinachowezekana, ila inataka utashi!
Nafasi yako katika hili unaitumia kikamilifu?
Jadili!

No comments: