06/09/2017

UZALISHAJI UMEME UTOKANAO NA NGUVU YA MAJI (HYDROPOWER)


Utangulizi
Ukiacha matumizi mengine ya maji kama kunywa na kumwagilia mashamba, maji pia yamekuwa yakitumika kuendesha mitambo ya kusagia nafaka (hydro mills) na mitambo ya kuzalishia umeme (hydroelectric power). Matumizi ya maji kwa kuendeshea mitambo ya kusagia nafaka bado yanaendelea kwa baadhi ya maeneo (nimeona Tanga na Kilimanjaro), ingawa kwa uchache, lakini uzalishaji wa umeme kwa kutumia nguvu ya maji bado unaendelea kwa kasi. Kwa mada hii nitazungumzia matumizi ya maji kwenye kuzalisha umeme, hasa kwa mazingira ya Tanzania. Kwa muktadha huu mifano yangu mingi pamoja na picha zitakazotumika kwenye makala hii zitakuwa ni za mitambo iliyopo ndani ya nchi, ambako ni rahisi kwa msomaji wa makala hii kuitembelea na kujifunza. Sitajadili kwa undani sana masuala ya kiufundi ya mitambo hii, sio lengo la makala hii, lengo nataka nijenge uelewa wa kawaida tu wa msomaji namna umeme unavyozalishwa kwa nguvu ya maji.

Namna uzalishaji unavyofanywa
Ili kukokotoa kiasi cha umeme utakaozalishwa kwa kiasi fulani cha maji, kuna masuala kadhaa ya kisayansi ya kuzingatiwa, ili kupata matokeo yanayotarajiwa. Kanuni inayotumiwa katika kukokotoa kiasi cha umeme utakaozalishwa ni  P=Q*H*g, ambapo P  ni ufupisho wa  Power (nguvu ya umeme unaozalishwa, katika kilowati ), H ni ufupisho wa Head (utofauti wa kimo kutoka maji yalipochotewa kwenye banio, mpaka mtambo wa uzalishaji ulipo) na ‘g’ ni ufupisho wa acceleration due to gravity (mgandamizo utokanao na nguvu za asili). Ili umeme uzalishwe, maji hutekwa kwenye banio (intake) na kuingizwa katika bomba lenye kipenyo maalum (penstock) kulingana na wingi wa maji. Kisha maji hayo kusafiri kwenye bomba kwa shinikizo la nguvu ya uvutano hadi kwenye turbine, ambayo huzunguka na kuzungusha jenereta ambao ndio hasa hufua umeme. Kuna turbines ambazo zimeunganishwa na jenereta moja kwa moja na nyingine zimeungwanishwa kwa kutumia mikanda maalum au giaboksi. Mambo mengine muhimu yanayozingatiwa kwenye kuzalisha umeme huu ni ufanisi wa mfumo mzima (water-to-wire efficiency). 

Wingi wa maji (Q)
Wingi wa maji (Q) yatakayopita mtamboni na kuzalisha umeme hupimwa kwa kiwango cha lita kwa sekunde (l/s) au meta za ujazo kwa sekunde (m3/s). Kupima ujazo wa maji kunasaidia katika kukokotoa kiasi cha umeme utakaozalishwa. Mitambo inayotumika kubadili nguvu ya maji (potential energy) kuwa nishati mwendo (kinetic energy) ina nafasi yake kwenye kukokotoa wingi wa umeme unaozalishwa pia. 

Kimo (H)
Kwa muktadha wa makala hii, kimo ni tofauti ya mwinuko kutoka usawa wa bahari, kutoka kwenye banio (intake) maji yanapochotwa kuelekezwa mitamboni na sehemu ulipo mtambo wa kubadili nguvu ya maji kuwa nishati mwendo. Hio utofauti hupimwa kwa meta ama futi. Aina mbalimbali za mitambo huhitaji kimo tofauti tofauti, kama itakavyofafanuliwa kwa ufupi hapo chini.

Nguvu ya uvutano, acceleration due to gravity (g)
Hii ni ile nguvu ya uvutano kati ya anga na ardhi, ndiyo inayofanya jiwe lirudi chini ukilirusha kwenda angani. Katika mifumo mifumo ya uzalishaji umeme ninayoongelea hapa, maji yakishachotwa katika banio (intake), huelekezwa katika bomba lenye kubwa maalum, kulingana na wingi wa maji, hadi kwenye mtambo wa kufua umeme (turbine), kwa nguvu hii ya asili (gravitational force), hivyo maji hayahitaji kusukumwa na nguvu nyingine yoyote. Nguvu hii ndio inayosababisha uwepo wa  shinikizo la maji kwenye bomba, kuelekea kwenye turbine. Ni nguvu ya muhimu sana kwenye uzalishaji umeme kwa njia ya maji.

Aina za Turbines
Turbine (wengine huita mifuo) ni mitambo ya kuzalishia umeme ambayo huzungushwa kwa nguvu ya maji. Mitambo hii imegawanyika katika aina mbali mbali. Mgawanyiko huu unatoka na tofauti za wingi wa maji yanahitajika kuzungusha mtambo husika, kimo na eneo mahalia. Mitambo hii haifanani kwa ukubwa kutoka na tofauti nilizoelezea hapo juu (wingi wa maji na kimo). Kwa mantiki hii basi, kila mtambo husanifiwa kutokana na mahali unapoenda kufungwa na pia kutokana na wingi wa maji na tofauti ya kimo. Ni mara chache mno kukuta mitambo inayofanana ukubwa.

Francis turbines 
Ni aina maarufu ya mitambo kwa hapa kwetu, kutokana na ufanisi wake mkubwa unaofikia hadi asilimia 96. Mitambo hii imekaa katika muundo wa mzunguko (spiral) na huweza kufungwa wima (vertical) ama kwa ulalo (horizontal). Mitambo hii haihitaji maji mengi sana, ila inahitaji kimo kikubwa ili kuongeza ufanisi na kuzalisha umeme mwingi. Kwa hapa Tanzania mitambo hii imefungwa na shirika la Tanesco Lower Pangani, eneo la Hale wilayani Muheza mkoani Tanga (megawati 68), Mbalizi mkoani Mbeya (kilowati 340) na Uwemba mkoani Njombe (kilowati 843). Mtambo mwingine wa aina hii upo kijiji cha Mawengi, wilaya ya Ludewa mkoani Njombe. Huu unamilikwa na taasisi ya LUMAMA na una uwezo wa kuzalisha kilowati 300 kwa turbine mbili.
Vertical Francis Turbine - Uwemba Njombe (3x281 kw)

Horizontal Francis Turbine - Mawengi, Ludewa (2x150 kw)

Pelton turbine
Aina hii ya mitambo pia ni maarufu kwa hapa kwetu na imekuwa ikitumika kwa mitambo mikubwa na midogo. Mitambo hii inahitaji kimo kikubwa sana na maji kiasi kidogo. Aghalabu pelton inakuwa na bomba  (jet) kati ya mbili na tano za kupeleka maji kwenye pangaboi zake. Lengo la bomba hizi ni kupunguza ama kuongeza matumizi ya maji kadri ya mahitaji. Pia, turbine hizi huhitaji mwendokasi mkubwa sana ili iweze kuzalisha umeme. Kwa Tanzania, mitambo hii imefungwa na Tanesco eneo la Kihansi (megawati 180), imefungwa na Parokia ya Kabanga, wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma (kilowati 100).
                                          Pelton turbine - Kabanga/Kasulu- Kigoma (100 Kw)


Cross flow turbine
Kiujumla hii ni mitambo midogo na hutumika kuzalisha umeme wa kiasi kidogo, mpaka kilowati 200. Hutumia maji mengi sana, kwa sababu mingi huwa na kimo kifupi (low head). Kwa hapa Tanzania mitambo hii imefungwa maeneo yafuatayo: Uwemba mkoani Njombe, (kilowati 100), Heri Mission Kasulu, mkoani Kigoma (Kilowati 100) na Lugarawa, wilayani Ludewa mkoani Njombe (kilowati 140).
Cross-Flow turbine - Lugarawa-Ludewa (140 kw)

Cross-flow turbine - Uwemba-Njombe (100 Kw)

                                  Cross-flow turbine - Heri Mission, Kasulu-Kigoma (100 Kw)


Turgo turbine

Utendaji wa mitambo hii hauna tofauti sana na pelton, ila mara nyingi mitambo ya aina hii huwa na jeti moja  tu ya maji yanayoelekea katika pangaboi zake. Katika pita pita zangu za kujifunza nimekutana na mtambo moja tu wa aina hii, uliopo eneo la Dindira, wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. Ni mtambo wa zamani sana, ulifungwa mwaka 1959 na Wakoloni wa Kiingereza, kwa ajili ya kiwanda cha chai cha Dindira.Kwa sasa mradi huu umesimama kufanya kazi kutokana na uchakavu wa mitambo.

Turgo turbines Dindira, Korogwe- Tanga (2x206 kw)


Pump turbine
Hizi aghalabu ni pampu za kusukumia maji, ambazo zimegeuzwa kinyume na kufanya kazi kama turbine zingine. Zina ufanisi wa chini sana, ndio sababu hazitumiki mara nyingi. Katika maeneo ambayo nimepita na kujifunza, nimekuta zinatumika sana kusagia nafaka, kwamba, badala ya wahusika kufunga jenereta ya kuzalisha umeme, wao wanafunga kinu cha kusagia nafaka. Mfano mmojawapo wa pampu inayofanya kazi ya kuzalisha umeme ni ile iliyopo kijiji cha Kinko, wilaya ya Lushoto mkoani Tanga (kilowati 9). Pampu nyingine imefungwa kijiji cha Mavanga, wilaya ya Njombe mkoani Njombe (kilowati 100).
Pump turbine, Mavanga-Njombe (100 kw)

Pump Turbine, Kinko, Lushoto-Tanga (9 kw)


Kaplan Turbine
Mfumo wa turbine hii unafanana kiasi fulani na ule wa Francis, ingawa utendaji kazi wake uko tofauti. Turbine za Kaplan zinatumia maji mengi sana na kimo kifupi, tofauti na aina nyingine za turbine, hivyo huhitaji kimo kifupi tu (wakati mwingine hata meta 2 tu), ili kuzalisha umeme. Mojawapo ya turbine za aina hii kwa hapa Tanzania imefungwa katika mradi wa umeme wa Bulongwa, wilayanai Makete, mkoani Njombe, kwa ajili ya kutoa huduma ya umeme kwenye hospitali ya Misheni ya Bulongwa (kilowati 180). Turbine nyingine ya aina hii imefungwa katika mradi wa umeme wa Udeka, katika kijiji cha Matembwe wilaya ya Njombe mkaoni Njombe (Kilowati 150).

Kaplan turbine, Udeka Matembwe - Njombe (150 kw)


Ulinzi katika mifumo ya uzalishaji umeme kwa njia ya maji

Kama ilivyo katika mitambo mingine, mitambo ya kuzalishia umeme inakuwa na ulinzi anuwai ili kuepukana na majanga mbalimbali kama vile mmomonyoko wa udongo (erosion), maporomoko ya ardhi (landslides), mafuriko (floods), mpasuko wa mabomba ya kusafirishia maji (penstock rupture) na ongezeko la mwendokasi katika mitambo.  Kwa hiyo basi, ulinzi katika mitambo hii huanzia katika mabwawa ambako maji yanachepushwa kuingia katika mabomba hadi yanaposafirishwa na kufika mitamboni.

Ulinzi wa mabwawa na mabanio dhidi ya mafuriko na maji ya ziada

Kwenye usanifu wa mabwawa na mabanio, huwa kuna mbinu kadhaa za kupitisha maji yanayozidi kimo cha bwawa ama banio. Juu ya ukuta wa bwawa kuna pengo linaloachwa makusudi ili kupitisha maji yanayozidi, na kubakiza maji yanayohitajika tu. Pengo hili kwa Kiingereza kujulikana kama ‘spillway’. Pia, spillway husaidia kupitisha maji ya ziada kunapokuwa na mafuriko. Lakini mafuriko yakizidi, kuna mageti maalum ambayo hufunguliwa ili kupitisha maji ya mafuriko, ili kulinda kingo za bwawa zisimomonyoke. Katika mitaro ya kusafirishia maji, kunakuwa na sehemu maalum (spillway) za kupunguzia maji yanayozidi uwezo wa mtaro husika. Hii pia husaidia kulinda mtaro dhidi ya mmomonyoko wa udongo wakati wa mafuriko.

Hilo pengo linaloonekana katikati ya kingo mbili ndio spillway
Spillway ya kwenye mtaro wa kusafirishia maji


Ulinzi wa mabwawa na mabanio dhidi ya magogo , wanyama na mawe
Kwenye mabanio ama mabwawa kuna uwezekano wa kusafirishwa mawe, magogo, takataka za aina anuwai na wanyama, kutokana na kusombwa na maji kutoka kwenye vyanzo ama njiani. Kusipokuwa na udhibiti madhubuti kwa vitu hivi, kuna uwezekano mkubwa vikaingia katika mabomba ya kusafirishia maji (penstock) na kuziba mtirirko wa maji, ama kufika hadi katika ‘turbine’ na kuziharibu. Kuna hatua kadhaa zinazochukuliwa ili kudhibiti takataka hizi. Katika sehemu ya banio, hutengenezewa mfumo wa chujio ama chekeche (grate/mesh) kwa ajili ya kuchuja taka na kuzuia mawe na magogo kupita. Huu mfumo husaidia kulinda mabomba na mitambo mingine katika mfumo mzima wa uzalishaji umeme kwa njia ya maji.
                                          Chujio ya takataka
Ulinzi wa bomba la kusafirishia maji dhidi ya mpasuko (rupture)
Bomba la kusafirishia maji kutoka katika banio hadi mtamboni huwa linakua na mgandamizo mkubwa, kutoka na kimo na wingi wa maji. Lina namna mbali mbali za ulinzi. Kwanza, huwa maji yanayopitishwa katika bomba huwa yamepimwa uwingi wake, na kunakua na valvu ya kudhibiti wingi huo (gate valves). Pili, mabomba mengi hufukiwa ardhini pale inapobidi, ili kudhibiti mgandamizo huo. Tatu, mabomba huwa na kifaa cha kupumulia (ventilator) ili kukabiliana na shinikizo kubwa la maji pale valvu za kwenye turbine zinapokuwa zinafungwa kwa matengenezo ya turbine au kama kuna uharibifu unaotokana na kukwama kwa kitu ndani ya turbine. Haya yote kusaidia kudhibiti bomba lisipasuke. Ukiachilia mbali hio vent, mabomba hasa ambayo yako juu ya ardhi huwekewa valvu za usalama, ili kupunguza mgandamizo utokanao na nguvu ya maji. Nne, vizuizi dhidi ya mbinuko wa mabomba(anchors) huwekwa pia ili kuzuia bomba lisipinde pale linapozidiwa na shinikizo kubwa la maji.
Hizo nguzo zilizoshikilia bomba ndio 'anchors' nilizongeelea hapo juu

Hilo bomba jeusi lilipindia kulia ndio 'vent'


Ulinzi wa mfumo mzima dhidi ya kujaa matope na mchanga

Katika baadhi ya maeneo, hasa yale yenye shughuli nyingi za kilimo karibu na bwawa ama banio, kunakuwa na kiwango kikubwa sana cha udongo kinachosombwa na maji na kuingizwa bwawani ama katika banio. Kwa mifumo midogo ya uzalishaji umeme, kunakuwa na dimbwi dogo la kutuamisha tope (desilting basin)na kuacha maji yakiendelea na mtirirko kuelekea mtamboni. Pia katika bwawa lingiine dogo (forebay) huwa valvu maalum ya kutolea mchanga na matope pale yanapokuwa yamejaa. Lakini katika mfumo wa mabwawa makubwa kunakua na kifaa kijulikanacho kama ‘dredger’ kwa ajili ya kupunguza mrundikano wa tope na mchanga kwenye bwawa.
Desilting basin

Forebay - Kinko, Lushoto-TangaUlinzi dhidi ya kuzidi/kupungua sana kwa mwendokasi wa turbine (over speeding/under speeding)

Kidhibiti mwendo(governor)
Kunapokuwa na matumizi madogo sana ya umeme kule unakotumika, husababisha turbine kwenda kasi kuliko kawaida. Iwapo kasi hii haitadhibitiwa basi kuna uwezekano wa kuharibu mitambo. Hali kadhalika iwapo umeme unatumika kupita kiwango husababisha turbine kuzunguka polepole sana, hivyo kupunguza mwendokasi na ufanisi. Ili kudhibiti hali hizi mbili, kifaa kiitwacho gavana (governor) kufungwa sambamba na turbine ili kudhibiti mwendokasi wake kulingana na mahitaji. Kifaa hiki hupokea mawasiliano ya mwendokasi kutoka kwenye turbine na kurekebisha mwendokasi huo kutokana na mahitaji ya umeme wakati husika. Kazi kubwa ya kifaa hiki ni kudhibiti mtiririko wa maji kuingia katika turbine kadri ya mahitaji. Mahitaji yakiwa makubwa, gavana kufungua zaidi valvu, hali kadhalika matumizi ya umeme yakipungua gavana kupunguza maji. Hali kadhalika, iwapo mtambo utasimama ghafla, kifaa hiki hufunga kabisa mtirirko wa maji ili kulinda turbine.
Kidhibiti mwendo (governor), Uwemba - Njombe

Kidhibiti mwendo (governor), Heri Mission Kasulu-Kigoma


Electronic Load Controller
Kwa mitambo ya kisasa sana, kuna kifaa kingine kijulikanacho kama “Electronic Load Controller”, ambacho hufanya tofauti na gavana, na ni cha kisasa zaidi. Kifaa hiki hakidhibiti mtiririko wa maji kama gavana, ila kinadhibiti frequency na umeme unaotumika. Kunapokuwa na matumizi makubwa ya umeme, frequency hupungua, hivyo kifaa hiki hupeleka mawasiliano katika jenereta na jenereta huongeza mwendokasi ili kuendana na matumizi. Kunapokua na matumizi madogo sana ya umeme, kifaa hiki huelekeza umeme wa ziada katika vifaa maalum (ballast load/dump load), ili frequency ibakie ile ile iliyopangwa. Hii ballast load mara nyingi zinatumika heater hizi tulizozizoea kutumia majumbani kuchemshia maji, ila hizi huwa na uwezo mkubwa sana.

                                          Electronic Load controller, Kinko, Lushoto-Tanga


Hitimisho
Umeme uzalishwao kwa nguvu ya maji umekuwa msaada mkubwa sana kwa maendeleo ya taifa, tangu enzi za mkoloni. Ingawa enzi za mkoloni mitambo ilikuwa midogo sana kwa ajili ya kukidhi matumizi ya taasisi za kidini na chache za umma, serikali ya Tanzania ilijikita na kujenga mitambo mkubwa zaidi na kusafirisha umeme kwenye gridi ya taifa ili kusambaza nchi nzima. Bado kuna vyanzo vingi sana vya umeme huu mbayo havijaendelezwa, kunahitajika juhudi za kuviendeleza ili kuleta maendeleo karibu zaidi na wananchi.

10/05/2016

UMEME UTOKANAO NA PUMBA ZA MPUNGA AU MAGUNZI YA MAHINDI AU PUMBA ZA MBAOFAHAMU UMEME UTOKANAO NA PUMBA ZA MPUNGA NA MAGUNZI YA MAHINDI

UTANGULIZI
Najua utashangaa sana kusikia kwamba pumba za mpunga au magunzi ya mahindi yanaweza kuzalisha umeme na ukaendesha vifaa vyote unavyovijua wewe, ambavyo vinatumia umeme, kama vile vinu vya kukoboa na kusaga nafaka, pasi, majiko ya umeme, majokofu, taa,  pangaboi n.k. Habari hii ni ya kweli kabisa, na ni kazi ambazo nimekuwa nafanya kwa karibia nusu mwaka sasa. Lakini pia umeme huu unaweza kuzalishwa hata kwa masalia makavu ya mazao mengine kama vile pamba, korosho, tumbaku na nazi. Ili kupata umeme, lazima masalia hayo ya mazao yawe makavu, angalau kwa asilimia 85 mpaka 90. Ili umeme uzalishwe kwa kutumia masalia ya mazao, lazima kuwe na hatua kadhaa za kipitiwa, kabla hatujapata umeme, kama ninavyofafanua hapa chini.


GASIFIER (TANURI LA KUCHOMEA PUMBA)
Hiki ni kifaa (kama tanuri kubwa) kilichotengenzwa kwa chuma kigumu sana, ambacho hutumika kuchomea masalia ya mazao, katika joto kubwa ambalo hufikia kiasi cha nyuzijoto zinazozidi 850. Katika uchomaji huo, kiwango cha oksijeni kinachoingia katika tanuri hilo hudhibitiwa kwa kutumia tanki la maji ambalo lipo chini ya tanuri. Ni lazima kudhibiti kiwango cha oskijeni kinachoingia katika tanuri, ili pumba ziweze kuzalisha gesi inayowaka, kwa kufanya mwako usio kamili (incomplete combustion). Mchanganyiko wa hewa hizi zinazozalishwa katika mfumo huo ni pamoja na Methane, Carbon dioxide, sulphur dioxide, carbon monoxide na mvuke. Baada ya kuzalishwa, gesi hizo huchanganywa na maji katika mfumo maalum, ambapo baadhi ya gesi hufyonzwa na maji, ikiwa ni pamoja na punje punje za pumba zilizoungua. Gesi ya methane pamoja na carbon monixide kwa kuwa hazichanganyiki na maji basi huendelea na safari kwenda kwenye hatua ya pili ya mchujo.VENTURI
Huu ni mfumo ambao hupokea gesi zenye joto kutoka kwenye cyclone, kisha hupooza gezi hizo kwa njia ya maji na kuchuja gesi zisizotakiwa, ikiwemo mvuke, na kubakisha methane na kiwango kidogo cha carbon monoxide kuelekea kwenye hatua ya nyingine ya mchujo. Masalia mengine katika hatua hii ni pamoja na nta/lami (tar) ambayo hutengwa kwenye kifaa maalum ili isiendelee kwenye hatua za uchujaji wa gesi unaofuata. Maji yaliyotumika kupoozea gesi huwekwa kwenye ndoo maalum, kisha kurejeshwa katika tanki kuu ambao huhifadhi maji yanayotumika mtamboni (tazama picha).


CYCLONE
Ni kifaa chenye umbo la mviringo, ambacho hupokea gesi yenye joto kutoka kwenye venturi kwa lengo la kuipooza na kuondoa punje ndogo za pumba iliyochomwa. Kwa jinsi ilivyotengezwa, punje punje za pumba hudondokea chini ya cyclone, pamoja na mvuke unaoendelea kupoa. Chini ya hii cyclone kuna valvu kwa ajili ya kutolea majimaji yatokanayo na mvuke uliopoa. Baada ya hatua hii, gesi husafirishwa hadi katika hatua inayofuata, ambayo ni kwenye chujio ya kwanza.  
 

CHUJIO YA KWANZA
Chujio hii ni ya umbo la mraba au mstatili, kwa  ndani inakuwa imegawanyika katika vyumba viwili, ambavyo vina uwazi kwa ndani, kwa ajili ya gesi kupita, kutoka chumba kimoja kwenda katika chumba kingine. Chumba cha kwanza huwa kinawekwa mkaa, au pumba za mpunga zilizochomwa, na chumba cha pili huwekwa pumba ambazo hazijachomwa. Kazi ya mkaa na pumba hizi ni kunyonya mvuke, punje punje ndogo za pumba zinazokuja na gesi kutoka kwenye cyclone. Chujio hii, kwa juu inakuwa na dohani, ambayo hutumika kwa majaribio ya kuwasha gesi kuona kama imechujwa vya kutosha, kabla haijapelekwa kwenye chujio ya mwisho na kwenye jenereta. Baada ya kuchujwa humu, gesi husafirishwa kwa bomba hadi katika chujio ya pili. Chujio hii ya kwanza, kwa chini huwa na valvu ya kutolea maji, ambayo aghalabu hutokana na mvuke uliopoa.

 

CHUJIO YA PILI
Hii huwa ni ya mviringo na kwa ndani upande wa juu huwa imewekwa kitambaa kigumu na pumba za mpunga zisizochomwa. Kazi yake pia ni kuchuja zaidi gesi na kuondoa mvuke. Kwa upannde wa chini wa chujio hii huwa na valvu pia, ya kuondolea maji yanayotokana na kupoa kwa mvuke, utokanano na gesi ya joto inayopita hapo.

 

CHUJIO YA TATU
Hii ina umbo la mstatili na ni nyembamba kwa umbo. Kwa ndani, imetengezwa kwa vitambaa viwili vigumu, ambavyo hutumika kuchuja gesi ili iweze kuingia katika jenereta. Ni chujio ya mwisho katika mfululizo wa chujio hizi. Gesi ikishatoka katika chujio hii huruhusiwa kuingia katika jenereta, kwa kutumia bomba la plastiki lenye valvu maalum ya kuruhusu ama kuzuia gesi hii.
 

INJINI NA JENERETA YA KUZALISHA UMEME
Injini inayotumika kuendeshea jenereta ina ukubwa wa kilowati 32 na ina mzunguko wa RPM 1500. Ijini hii huendeshwa kwa gesi iliyotokana na masalia ya mazao au pumba za mbao. Gesi hii kabla haijachomwa katika injini huchanganywa na hewa hii ya kawaida kwa kiwango cha 70/30. Hali kadhalika jenereta inayozalisha umeme inakuwa na ukubwa wa kilowati 32, au wati 32,000. Kulingana na mahitaji, injini na jereta inakweza kuwa chini ya hapo au juu ya hapo, ni matakwa ya mhitaji kuamua ukumwa wa mfumo autakao. Jenereta hii inatosha kuzalisha umeme wa kutumika kwa hadi nyumba 300 kwa vijijini, ambako matumizi ya umeme si makubwa  sana. Kama nilivyoeleza hapo juu kwenye utangulizi, vifaa vyote vya majumbani vinavyotumia umeme vinaweza kuendeshwa kwa umeme huu.

 

HITIMISHO
Mitambo hii ipo Tanzania, na imefungwa katika katika mikoa kadhaa na inazalisha umeme. Mmoja umefungwa katika kijiji cha Nyakagomba, kata ya Nyakagomba wilaya ya Geita vijijini, mkoa wa Geita (unatumia pumba za mpunga). Mtambo mwingine umefungwa katika kijiji cha Kongwa, kata ya Mvuha, Morogoro vijijini (unatumia pumba za mpunga). Mwingine umefungwa kijiji cha Malolo B, kata ya Malolo, wilaya ya Kilosa, mkoa wa Morogoro. Mitambo mingine ambayo inaendelea kufungwa ipo kijiji cha Mbaha, kata ya Mbaha wilaya ya Nyasa  mkoani Ruvuma, mwingine unafungwa kijiji cha Kibindu, kata ya Kibindu, wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na mwingine unafungwa kijiji cha Biro, kata ya Biro, wilaya mpya ya Malinyi mkoani Morogoro.
 
Gharama za mtambo huu, bila mfumo wa usambazaji umeme, kwa sasa ni dola elfu hamsini. 
Nakaribisha maoni, ushauri na maswali.

18/01/2013

NADHARIA YA CENTRE – PERIPHERY NA GESI YA MTWARA


Picha nimetoa kwa Issa Michuzi

NADHARIA YA CENTRE – PERIPHERY NA GESI YA MTWARA

Utangulizi

Kuna nadharia anuwai za maendeleo, kwa kadri nilivyofundishwa na walimu wangu wa somo la maendeleo (Development Studies). Na kila nadharia ina uzuri wake na ubaya wake, lakini kinachoamua uzuri ama ubaya wa nadharia hizo ni UTEKELEZAJI. Iwapo utekelezaji wa nadharia husika ni mbovu, hata nadharia iwe nzuri kiasi gani lazima kutakuwa na mapungufu.  

Nadharia ya Center Periphery /Core-Periphery

Nadharia hii imekuwa ikitumika kwa muda mrefu kuelezea uwiano hasi wa maendeleo kati ya nchi zilizoendelea na zile zilizo nyuma kimaendeleo. Mfumo huo umetumika sana na wanazuoni kama Samir Amin, A.G. Frank na Emmanuel Walerstine katika maandiko yao kwenye kuelezea maendeleo kwa mtazamo huo. Walijikita zaidi kwenye nadharia za za maendeleo za wafikiari wakuu kama Karl Marx. Kwa ufupi ni kwamba nadharia hii inaelezea mfumo usio sawa unaotokana na ubepari, katika mgawanyo wa rasilimali na maendeleo ya dunia. Nadharia hii inaongelea maendeleo ya “NCHI” na nchi, mie nimeamua kuishusha na kuihusianisha na “MKOA” na mkoa.

Nina uhakika kwamba serikali imeamua kutumia nadharia ya (Center-Periphery), kwa hili la Mtwara. Tuna uhakika 100% kuwa gesi ipo Mtwara, na sehemu ya gesi hiyo ndiyo inayotumika Ubungo kwenye uzalishaji wa umeme. Sasa, iwapo tujenge mfuo wa umeme Mtwara na kuusafirisha kwa nguzo za msongo mkubwa kwenda sehemu nyingine za Tanzania ni uamuzi mmoja, na iwapo tusafirishe gesi kwa bomba na kuipeleka Dar kisha tujenge mfuo wa umeme hapo ni uamuzi mwingine. Maamuzi ya mfumo upi utumike yapo mikononi mwa tuliowapa madaraka, wakisaidiana na wataalamu wa mipango.

Nadharia ya (Centre-Periphery) ina mtazamo wa kwamba kuna baadhi ya maeneo (iwe ni mkoa, majimbo, wilaya ama kata), ambayo kazi yake ni kuzalisha malighafi na kupokea bidhaa zitonakazo na malighafi hizo. Haiwezekani kuweka viwanda vya kuchakata malighafi hizo maeneo hayo, kwa sababu hayo maeneo "YATAFAIDI". Nadharia hiyo pia inaelezea kwamba maeneo mengine «yamegeuzwa» ni ya kuchakata kila malighafi, hata kama malighafi hiyo haitoki hapo. Haya ni maeneo ya viwanda tu, hata kama gharama za kusafirisha malighafi za viwanda hivyo ni ghali sana, kwa hiyo ajira zote zitokanazo na viwanda lazima "ZIWE HAPO TU". Kwa mujibu wa nadharia hii hii, maeneo mengine ni kwa ajili ya kuzalisha wasomi tu, ili kusaidia kuchakata na kuuza bidhaa na huduma zitokanazo na bidhaa zilizochakatwa. Sijajua Mtwara iko sehemu ipi hapo katika hiyo nadharia ya CENTER-PERIPHERY, kiasi kwamba serikali haitaki kujenga mifuo ya umeme na kusafisha gesi Mtwara wala kujenga barabara za kufika maeneo hayo.


Picha nimetoa kwa Issa Michuzi

Kwa nini Mtwara wanalalamika?

Viwanda vingi vipo Dar Es Salaam, japo Dar Es Salaam haizalishi malighafi zinazosindikwa na kuchakatwa katika viwanda hivyo. Kiwanda cha Sigara kipo Dar, pamoja na kwamba tumbaku inatoka Rukwa, Mbeya, Tabora na kwingineko. Viwanda vya kuzalisha juisi za matunda vipo Dar, japo matunda yanatoka mikoa anuwai kama vile Tanga, Iringa, Morogoro, Mbeya na Pwani. Viwanda vya mafuta ya kula vipo Dar, ilhali chikichi na alizeti zinazalishwa nje ya Dar. Uwiano huu usio sawa ndio unaozua malalamiko kwenye jamii, kiasi cha kuleta maandamano yasiyokoma. Nahusianisha uwiano huu usio sawa wa maendeleo na nadharia tajwa na gesi ya Mtwara. Serikali imeamua kufuata njia ya Center-Periphery kwa kuwanyima wananchi wa Mtwara fursa za ajira zitokanazo na mitambo ya kuchakata gesi na kufua umeme. Nisingependa kuingia kwenye mjadala wa kiasiasa zaidi kwenye hili, kwa sababu tayari wanasiasa wameshalijadili kwa undani. Je wananchi wa Mtwara walishirikishwa kwenye kuamua kujenga mifuo ya umeme Dar. Tujadili

03/10/2012

Tanesco na ombi la maboresho kutoka kwa walaji (Consumers)

Utangulizi Ofisi ya mahusiano ya Tanesco imetoa tangazo (pichani) ikiomba maoni ya wateja kuhusu maboresho ambayo wanataka kuyafanya, ili kuongeza ufanisi wa shirika hilo. Shirika hili ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi, hivyo ufanisi wake ni nguzo muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wetu kwa ujumla. Ushauri Mimi ni mdau wa nishati katika taifa hili na pia ni mteja wa Tanesco. Kuna mada fulani (iko hapa) niliiweka katika blog hii siku za nyuma kuhusu matatizo yanayoisibu Tanesco na namna ya kupunguza kama si kuondoa kabisa matatizo hayo. Tanesco ina vitengo vitatu muhimu, ambavyo ni uzalishaji umeme (Generation), usafirishaji umeme (Transmission) na ugavi umeme (Distribution). Shida kubwa sana ya Tanesco ipo katika generation na distribution. Ningeomba watendaji wakuu (menejimenti na bodi)za shirika hili wazingatie ushauri niliowapa hata robo tu,watafikia hilo lengo wanalolitafuta. Ushauri wangu umewahi kutolewa na wataalamu wengine wengi tu akiwamo Januari Makamba. Lakini pia wasome (na ikiwezekana kutekeleza) mapendekezo ya ripoti iliyoandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu upotevu wa umeme. Ni hayo tu. Tuendelee na mjadala

12/10/2011

Jiunge na Harakati za Siku ya Blogu Duniani

Siku ya Blogu ni ipi?

Utangulizi
Ni tukio ambalo linawakutanisha waandishi na wamiliki wa blogu duniani kujadili kuhusu mada moja ambayo huwa imechaguliwa na kisha kuweka mada hiyo katika blogu zao anuwai. Siku hii ni tarehe 15 Oktoba ya kila mwaka na imekuwa ikiadhimishwa tangu mwaka 2007. Matukio ya siku hii huratibiwa na mtandao uitwao ‘Blog Action Day’ (http://blogactionday.org) .

Mada za Siku ya Blogu
Kwa miaka ya nyuma, mada zilizowahi kujadiliwa ni umasikini (ufukara), maji na mabadiliko ya tabianchi. Mwaka jana 2010 mada iliyokuwa imechaguliwa ilihusu maji, kwa hiyo wanablogu duniani kote tulishiriki katika majadiliano kwa njia ya mtandao kuhusu suala la maji, kwa upana wake. Binafsi, nimeandika mada anuwai kuhusu maji na mazingi (kwa kuwa ndiyo taaluma yangu ilikoegemea). Mwaka huu, siku ya blogu duniani imesogezwa mbele kwa siku moja ili kushabihiana na siku ya chakula duniani (tarehe 16 Oktoba), kwa hiyo mada kuu ya mwaka huu inahusu CHAKULA! Kwa maana hiyo basi, wanablogu mbalimbali duniani wataandika mada mbali mbali kuhusu chakula, iwe ni upatikanaji wake, uhifadhi, uandaaji, matumizi, uharibifu, maadili katika usindikaji, ulafi, uhaba na namna tunavyowezesha upatikanaji wa chakula kwa jamii zote duniani na kadhalika.
Unakaribishwa kushiriki katika majadiliano haya, pia unaweza kujisajili katika mtanda wa Blog Action Day katika anuani niliyoiweka hapo juu!
Ahsante sana.